Friday, 2 September 2016

KUTOKA AN-NUUR: KUHOJIWA KWA SHEIKH CHAMBUSO NA KUKAMATWA MASHEIKH TANGA

Utangulizi
Fuatilia ukurasa huu kuhusu taarifa za kuhojiwa na Polisi, Sheikh Rajab Ramadhani Chambuso imam, sheikh na mwalimu wa chekechea na shule ya Msingi ya Kiislam, Mabawa Tanga na pia mwalimu wa kusomesha Maarifa ya Kiislam katika Shule za Sekondari pamoja na kuhojiwa Sheikh Salim Barahiyan Mudir wa Tanga Muslim Youth wamiliki wa shule, hospitali, Kituo cha Radio ya Kiislam na taasisi kadhaa zinazojishughulisha na maendeleo ya Uislam Tanzania...



Na Bakari Mwakangwale

HOFU imetanda Jijini Tanga, kufuatia Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwahoji baadhi ya Masheikh maarufu na viongozi wa Taasisi za Kiislamu Jijini humo.

Miongoni mwa Masheikh waliofikishwa kituo Kikuu cha Polisi na kuhojiwa ni pamoja na Sheikh Salim Barahiyanina Ustadhi Chambuso  Ramadhani.

Hata hivyo haijajulikana wamehojiwa kwa tuhuma zipi, huku Amir wa Baraza la Vijana wa Kiislamu Tanzania, Ustadhi Ahmed Kidege, yeye ametuhumiwa kwa uchochezi.

Akizungumzia hali hiyo, kwa njia ya simu kutoka Jijini Tanga, Ustadhi Hamisi Shemtoi, alisema kumekuwa na taarifa kwa muda mrefu kwamba kuna baadhi ya Masheikh na viongozi wa dini wanatafutwa na Polisi.

Alisema, kufuatia taarifa hizo, Masheikh wamekuwa wakielezana kwamba, wajiandae kisaikolojia kwani wakati wowote wanaweza kukamatwa.

Akizungumzia kukamatwa Kwa Kiongozi wa Baraza la Vijana  wa Kiislamu Tanzania, Ust. Shemtoi, alisema Amir Kidege, alivamiwa na kumatwa na askari wanane, majira ya saa tano asubuhi Jumatatu wiki hii, akiwa ofisini kwake.

Alisema, baada ya kumatwa, aliwaomba maafande hao kutoa taarifa na kuruhusiwa ambapo alimpigia simu Ustadhi Shemtoi na kumeleza juu ya kukamatwa kwake na Polisi.

Alisema, baada ya kupokea taarifa hizo, ilimlazimu kwanza kuswali rakaa mbili za sunna, kwani alisema alifanya hivyo kumuomba Allah (sw) kutokana na hali ilivyo sasa kwani alijandaa kwa lolote dhidi yake katika ufuatiliaji huo.

Alisema, alishangaa baada ya kufika Polisi aliulizwa iwapo yeye ndiye Sheikh Chambuso, ambapo alijibu hapana, bali yeye ni Ustadhi Shemtoi, na kwamba amefika hapo kwa ajili ya kufuatilia kadhia ya kukamatwa kijana wake Ustadhi Ahmed Kidege.

Alisema, baada ya utambulisho huo, alikabidhiwa kwa Afande aliyejitambulisha kwamba ndiye kiongozi wa operesheni hiyo, na kwamba alielezwa kuwa wamemkamata kijana wake kwa ajili ya mahojiano ya kawaida, lakini kuna simu yake moja ameiacha ambayo inahitajika hapo Piolisi.

“Nililazimika kurudi hadi nyumbani kwake kuifuatilia hiyo simu ambayo alikuwa akiitumia ofisini kwake kisha niliisalimisha kwa kuwakabidhi.” Ameeleza Ustadhi Shemtoi.

Alisema, baada ya mahojiano na Polisi, walimwachia majira ya Magharibi, baada ya kumuwekea dhamana na kutakiwa kumrudisha siku ya Ijumaa (leo) majira ya saa mbili asubuhi kwa ajili ya kuripoti kituoni hapo.

Alisema, kwa mujibu wa fomu ya dhamana aliyojaza na kusaini imeonyesha kuwa anamdhamini Ustadhi Ahmed Kidege, kwa tuhuma za uchochezi.

“Lakini alipokuwa akihojiwa hawakumueleza kachochea nini, kamchochea nani wala eneo maalum alilotumia kuchochea, Msikitini, katika Kongamano au katika mitandao, lakini pamoja na yote hayo wamemwachia baada ya mahojiano ya masaa mawili.” Amesema Ust. Shemtoi.

Alisema, kikubwa wamechukua maelezo yake binafsi (CV) na kwa kuwa shughuli zake ni kufundisha mashuleni somo la Maarifa ya Uislamu (EDK), pia walitaka kujua analipwa na nani, ambapo aliwaeleza yeye anajitolea katika kazi hiyo.

Aidha, alisema wakati anaingia pale Kituo Kikuu cha Polisi, alikutana na Sheikh Salim Barahiyani, akiwa katika gari yake anatoka ambapo alimueleza kuwa anatoka ofisi za Uhamiaji, ambazo zipo hapo hapo Polisi.

Hata hivyo, badae kwa taarifa walizozipata ni kuwa Sheikh Barahiyani, alionekana tena hapo upande wa Polisi Makao Makuu, ambapo imeelezwa kuwa aliitwa kwa mahojiano na Jeshi la Polisi.

Alisema, mbali ya Sheikh Barahiyani, pia walikutana na Sheikh Chambuso Ramadhan, wakati yeye (Shemtoi) anapandisha akiwa na Ust. Kidege Ahmed, walimuona Sheikh Chambuso, akishushwa.

“Yeye hakukamatwa, alipigiwa simu akaenda mwenyewe na baada ya kuhojiwa wamezuia simu zake hapo Polisi.” Ameeleza Ust. Shemtoi.

Aidha, alisema Imamu wa Masjid Qubah, Barabara ya 15 Sokomjinga, Sheikh Ngaluba, naye alifuatwa na maafande wa Jeshi la Polisi, lakini hawakufanikwia kumkamata kwani hakuwepo katika eneo walilokusudia kumkamata.

Zaidi, alisema kwa siku ya Jumanne wiki hii amepata taarifa kuwa Amir wa Taasisi ya Dalur Hadith Ulumy,  ya Jijini humo Sheikh Ally Kiroboto, naye wamemkamata na kwenda kuhojiwa.

Imeelezwa kuwa hali hiyo imezidi kutia hofu wakazi wa Jiji la Tanga, wakizingatia kupotea kwa ndugu na jamaa zao katika mazingira ya kutatanisha, huku wakikosa taarifa kamili hata pale wanapokwenda katika vituo vya Polisi, Gerezani na hata katika Hospitali.

Kufatia matukio hayo, Jukwaa la Vijana wa Kiislamu Tanzania, limetoa tahadhari kwa Waislamu hususani vijana kuachana na mambo yanayotia shaka vyombo vya usalama, ikiwemo kutuma na kupokea jumbe (sms) zenye mashaka kupitia simu za mkono na mitandao ya kijamii.

  ***
Unaweza kusoma historia fupi ya Sheikh Rajab Ramadhani Chambuso katika juhudi zake za malezi ya watoto wadogo na vijana na katika kusomesha Uislam katika Mkoa wa Tanga...
Ingia hapo chini:


Nilipofika Tanga mwaka wa 1997 nikapata hamu ya kusoma Uislam lau kwa uchache wa kusoma. Sheikh Salim Barahiyan siku ya kwanza nilipofika darsani kwake Msikiti wa Ansar Barabara ya 20 nilimkuta anasomesha ''Riadh-Us-Saleheen.'' Kitabu kikubwa sana kwangu lakini nitafanyaje basi nikajiunga na mimi katika darsa.

Baadae nikajaelezwa kuwa nilikuwa kivutio cha aina yake katika darsa lile kwanza kwa mavazi yangu ambayo ndiyo nilikuwa navaa ofisini kwa hiyo kwa kuwa sikuwa na muda wa kwenda nyumbani kubadili kwa kuchelea kuchelewa darsa nilikuwa nikendanazo darsani hivyo hivyo.

Kwa wengi nilionekana mtu mtanashati na mtu wa kujipenda. Lakini zaidi lililovutia ni gari langu la kisasa nililokuwa ninagesha nje ya msikiti. Taratibu nikazoeleka pale darsani si kwa wanafunzi wenzangu bali hata kwa sheikh mwenyewe mwalimu wetu Sheikh Salim.

Sheikh Salim yeye ni kiongozi wa Ansar na Ansar wana namna yao ya uvaaji na kujiweka. Ikiwa kivazi ni kanzu au suruali basi lazima iwe juu ya kifundo na kisha lazima ufuge ndevu lau kama ni chache.

Haya yote ni katika mafunzo na suna ya Mtume (SAW). Bahati mbaya sana mimi sikuwa hata na moja katika hayo. Sivai suruali juu ya kifundo wala sifugi ndevu.

Ikawa sasa Sheikh Salim baada ya kudarsisha kwa muda akihisi kama wanafunzi wake tumechoka yeye husimama kidogo na kufanya maskhara ili wanafunzi wake turudishe nguvu za kumsikiliza.

Hapo Sheikh atanifanyia maskahara atasema, ''Sheikh Mohamed naona hicho kidevu chako kimekuwa cheupe kama ''bulb,'' au yai vile.''

Basi darsa zima litageuka kunitazama na sote tutaangua kicheko...

Sheikh Salim alinipenda sana na akanitia kwenye Bodi ya Shule na alikuwa akituita katika vikao akitupa na posho.

Mimi nililalamika kuhusu hizi posho lakini akanituliza akanambia, ''Sheikh Mohamed hebu nisikize, nyie huko makazini kwenu vikao vyote mnavyohudhuria mnalipwa, iweje hiki za shughuli za Kiislam ndiyo tusikulipeni?'' Sheikh Salim hakutaka kusikiliza chochote kuhusu sisi kukataa kupokea posho.

Sheikh Salim Barahiyan kafanya mengi katika kuwahudumia Waislam wa Tanga inataka ufike kwanza uione ofisi yake kisha utembelee taasisi zilizokuwa chini ya Ansar ndipo utaelewa kazi kubwa aliyofanya msomi huyu mwenye shahada mbili za Sharia moja kutoka Saudia na nyingine Pakistan.

Mwandishi alipokuwa mwanafunzi wa Sheikh Salim Barahiyan Tanga katika
miaka ya mwishoni 1990

No comments: