[QUOTE="SHERRIF ARPAIO, post: 17805014, member: 25584"]Mkuu Mohammed Said kwa upeo huu uliotukuka ingefaa uwe visiting professor of african history kwenye medani Ya kimataifa
Naamini ulikuwa very close ma prof Mazrui, Haroub Othman na A M Babu kabla hawajafariki[/QUOTE]
Sheriff...
Hao uliowataja wote ni walimu wangu.
Mimi siwezi hata kuwabebea makubazi yao.
Tuanze na Prof. Mazrui.
Nilimpa jina na kumwita, ''My distant Professor,'' na yeye naamini alilipokea jina hili.
Hili ni jina ambalo nililoandika kwenye kitabu cha Abdul Sykes nilichompelekea
mwaka wa 1998 kilipotoka.
Kushoto: Balozi Dr. R. K. Dau, Dr. Harith Ghassany na Mwandishi |
Watu wawili ndiyo walioniunganisha na Mazrui - Balozi Dr. Ramadhani Kitwana
Dau na Dr. Harith Ghassany.
Kitabu changu nilimkabidhi Dr. Dau na yeye ndiye aliyempa mkononi kitabu hicho.
Prof. Mazrui akaniaandikia kunishukuru.
Baadhi ya maneno aliyoandika ni kuwa nimemfurahisha kwa kuonyesha nini Waswahili
wamefanya Tanganyika.
Ikawa mara moja moja tunaandikiana.
Mwaka wa 2003 kulikuwa na mkutano Kampala ambao Prof. Ali Mazrui alihudhuria na
mimi nilialikwa na niliwasilisha mada.
Dr. Ghassany akanituma nimfikishie salamu zake kwa Prof. Mazrui.
Sote tulikuwa tunakaa Kampala Nile Hilton na nilizifikisha salamu zile.
Prof. Mazrui alifurahi sana kuniona na kupokea salamu za Dr. Ghassany kutoka kwangu.
Prof. Mazrui alikuwa na Dr. Ghassany Michigan.
Kulia: Sal Davis, Mwandishi na Ali Kilomoni Tanga 2010 |
Prof. Mazrui nilimmaliza nilipomwambia kuwa mimi ni rafiki mkubwa wa Sal Davis.
Mazrui na Sal Davis ni ''ndugu wa ndugu,'' kama mwenyewe Sal anavyopenda kueleza.
Sal Davis alipopelekwa na baba yake, Shariff Salim Abdallah kwenda kusoma Manchester akiwa na umri wa miaka 17 mwaka wa 1957 alipokelewa na Prof. Mazrui na waliishi nyumba moja.
Lakini nilimwacha kinywa wazi nilipomweleza kuwa nimefika hadi kijijini kwao Takaungu, nje ya Mombasa na kuona msikiti wao na kisima cha msikiti ambazo kina takriban miaka 400.
Nilimfahamisha kuwa nina ndugu zangu akina Baamumin katika kijiji cha Mtondia ambao wao ni ''squatters'' katika ardhi ya akina Mazrui.
Nina mengi ya Prof. Mazrui lakini tuishie hapa.
Kushoto: Tamim Faraj, Prof. Ali Mazrui na Mwandishi Kampala 2003 |
Prof. Haroub Othman yeye kanisomesha khasa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ni mwalimu wangu kabisa.
Kumbukumbu aliyoniachia Prof. Haroub ni moja, ni siku tulipokutana pembeni ya Msikiti wa Ibadh na tukazungumza kuhusu kitabu changu ambacho ndiyo kwanza kilikuwa kimewasili nchini kutoka Uingereza.
Hii ilikuwa mwaka wa 1998.
Mwalimu wangu alikuwa amesawajika.
Alikuwa amesoma katika kitabu cha Abdul Sykes mambo mawili au matatu yaliyomshtua sana.
Hakuwa anayajua kabla.
Kwanza historia ya Abdul Sykes na mchango wa wazalendo wengine katika kuasisi TANU.
Prof. Haroub kama ilivyokuwa kwa walimu wengi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaa walikuwa wanaamini kuwa TANU iliasisiwa na Julius Nyerere na siasa za kudai uhuru hazikuwapo kabla yake.
Pili, mgogoro baina ya Waislam na Nyerere baada ya uhuru na yale niliyoandika kwa urefu kuhusu kutumika kwa vyombo vya dola dhidi ya masheikh wakati wa mgogoro ule.
Prof. Haroub akanieleza kuwa yeye alikwenda kwa Nyerere kumuona ili amsikilize nini maoni yake kuhusu yale ambayo mimi niliandika.
Prof. Haroub alimuomba Nyerere aandike na yeye ili dunia isikie na yale ya upande wake.
Alimuomba kuwa amjibu na Ali Muhsin Barwani kwa yale aliyoandika dhidi yake katika kitabu chake, ''Conflicts and Harmony in Zanzibar,'' (1997).
Ningeliweza kusema mengi kuhusu mwalimu wangu Prof. Haroub Othman lakini na tuishie hapa.
Mwandishi na Ahmed Rajab London, 1991
Abdulrahman Babu nilijulishwa kwake London na Ahmed Rajab na siku nzima tulishinda pamoja Brixton sisi watatu mimi nikijibu maswali yao kuhusu hali ya siasa Tanzania na uongozi wa Ali Hassan Mwinyi.
Nilizungumza mengi na Babu na nilimuuliza kuhusu yeye kuandika historia ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 na aliniambia kuwa ataandika In Shaallah.
Babu hakuandika historia ile kwa sababu ambazo nilikuja kuzijua baada ya miaka kumi takriban.
Hawa wote, Prof. Mazrui, Prof. Haroub Othman na Prof. Abdulrahman Babu, ni walimu wangu na ni miamba ambayo kwa kweli mie ni kichuguu mbele yao.
No comments:
Post a Comment