Sheikh Rocket na bendera yake katika khitma ya Saigon Club 2010 |
Huyu wa Unguja alikuwa ni msafisha msikiti wa pale karibu na Ofisi ya Utawala Bora.
Mzee huyu akiondoka kwa meli bure, akarukia mabasi hadi
anaingia Sudan na Misri, kisha hupata usafiri wa meli kuingia Makka.
Alichokuwa nacho mkononi ni mkoba wake wa ukindu tu.
Rocket yeye alizidi, yeye kote alichonacho ni bendera
yake, na siku zote alikuwa wa mwanzo kufika kuliko ma group ya Watanzania.
Bahati mbaya zama zao
hakukuwa na mitandao ya kijamii kuweza kuzungumzwa.
Nimelipata jina la mzee wa Zanzibar jina lake ni Mzee
Zaidi, akisafisha Msikiti kwa kufyegia, kutia maji ya kunywa kwenye mtungi na
kupaka rangi Msikiti, alikuwa na yeye akitizamwa na watu wa kheri wasiokuwa
wakitaka kujulikana.
Katika mwambao huu wetu
iwe Unguja, Pemba, Bagamoyo, Mafia, Lamu, Tanga n.k. wametokea Masheikhe
wakubwa aidha wametokea waja wa kheri kama kina Mzee Zaidi na Sheikh Rocket.
Katika miaka ya 70 safari mmoja nilimshuhudia Rocket amekuja Msikiti Jibril,
mtu tuliokuwa tunamsikia tu, tukaambiwa alipofika siku yake ya kurudi Mrima, bandarini alipita tu na hakuna aliyemuuliza kwii, tiketi iko wapi na pasi ya
kusafiria iko wapi.
Waja wa Kheir huwezi
kuwaelezea, kuna mtu alipewa salamu kutoka Saudi kumpa Sheikh Rocket
aliojiuliza huyo mtu amejuana naye vipi na wakizungumza lugha gani?
Waja kama hawa huwezi
kujua daraja zao kwa Allah kwa namna walivyoiweka Akhera mbele na Dunia nyuma
ya migongo yao...
Kuna sheikhe wetu
mkubwa tu aliwahi kutuambia kuwa wao wamesoma na kujuwa lakini Ucha Mungu upo
kwa watu wa kawadia akatuambia kuna watu wanafunga Sunna ya Mtume Ayoub, siku
kufunga siku kula, siku takriban chini ya 172 kwa kuzingatia mwaka wa Kiislamu
kuwa na siku 354.
Watu hao ni wa kawaida
tu, nao hutoa sadaka kupindukia, ukimjaalia pesa na yeye hatokaa nayo ataigawa,
watu hao ni wa kawaida kabisa wapo lakini hatuna macho ya kuwajua na wao
walivyokuwa watu wa kawaida utajua ni mtu wa kawaida, ndipo marehemu Maalim
Aboud Maalim alipoambiwa asome dua na kupiga fatha alikataa akamuambia mzee
mmoja ambaye ni mtu wa kawaida akionekana mnyonge, mzee alikataa Maalim akasema
hatosoma dua mbele yake, aliposoma dua watu walistaajabu alivyokuwa anateremka
na kushusha vitu.
Kuna Mzee Rajab wa mtaa
wa Funguni hivi sasa ndipo ilipokuwepo Hoteli ya Bwawani, alisikia kuwa mwenye
kuadhini Miongo mitatu pasi kukosa kipindi pepo ndio itakuwa makazi yake, hakika
nafahamishwa kuwa watoto wadogo wa Mtaa wa Funguni wanaanza kufungua macho na
kuingia akili wakimsikia ana adhini kila kipindi, kazi zake zilikuwa hapo hapo,
akijua wakati wa Sala umeingia anakimbilia kuadhini, na kufa kwake alifia msikitini baada ya kusali sala ya asubuhi.
Kikwajuni mtaa wetu
alikuwepo Babu Haji kazi yake ilikuwa ni kuli, akiwacha mizigo na kukimbilia
kuadhini Msikiti wa Wireless.
Babu Haji alikuwa na hima ya kuadhini na pindipo
akifika msikitini ikawa kachelewa na kumeadhiniwa huwa mnyonge laysal kiyas.
Babu Haji inawezekana kuwa kaadhini kati ya miaka 40 au na zaidi.
Waja hawa wa kheri kwa
walivyokuwa watu wa kawaida basi nyakati zao walikuwa hawazungumziki ila sasa
ndio tunawzungumza Allah awajaalie pepo zenye mabustani mazuri mazuri na mito
inayoizunguka hizo Bustani.
Ameen.
Sheikh Rocket kwa heshima na taadhima akipokelewa viatu vyake katika khitma ya Saigon Club 2010 |
No comments:
Post a Comment