Sunday, 16 October 2016

Makosa ya Nyerere Yalitengeneza Nyufa Katika Utaifa - Abuu Moukhtar


Ni vigumu kuandika kwa lengo la kumkosoa mtu anayeheshimiwa na wengi kiasi cha kuitwa Baba wa Taifa la Tanzania na ambaye mengi mazuri ya nchi yetu – ikiwemo amani, umoja na mshikamano - vinatajwa kuwa vilitokana na uongozi wake mzuri ulioweka misingi imara ya utaifa  na maendeleo. 

Ni ngumu zaidi kama anayelengwa kukosolewa ameipa heshima nchi yetu huko kama mmoja wa kiafrika waliokuwa na uzalendo wa hali ya juu ambaye ukizungumzia  watu watano waliochangia kwa kiasi kikubwa ukombozi wa bara la Afrika kutoka mikononi mwa wakoloni huwezi kuacha kumtaja.

Ugumu wa kukosoa ni maradufu pale ambapo anayekosolewa yupo katika utaratibu wa kufanywa mtakatifu kupitia dini yake, tena kupitia harakati za kimataifa, kwa matendo yake makuu.

Ni ngumu zaidi kukosoa unapokusudia makala yako isomwe na watu wa wote kama uchambuzi huru usioegemea upande wowote na itoke katika kipindi ambacho watu wanakumbuka kifo cha muhusika kwa matamasha, mikutano, sherehe mbalimbali, huku wito ukitolewa kuwa tuzidi kumuezi kwani tulivyofanya sasa haitoshi!

Kazi ya kukosoa inakuwa ngumu zaidi  ikiwa mlengwa anakosolewa  kwenye mambo ambayo wengi wanaamini ndiyo mazuri yake, yaani ujenzi wa taifa (nation building). Licha ya hayo yote, lakini ntajaribu kukosoa, licha ya unyeti wa mada hii, na kukosoa bila kuingiza hisia zangu binafsi

Ujenzi wa Taifa
Kazi kubwa ya kwanza iliyofanywa na viongozi waasisi wa mataifa yetu ya kiafrika ilikuwa ni kujenga utaifa, kuwafanya watu wajisikie wamoja na washikamane bila kujali tofauti zao za makabila, dini, mahali wanapotoka na kadhalika. Ikumbukwe wakati wa ukoloni.
Katika nchi za Afrika ambako wazungu walitawala kwa sera ya wagawanye uwatawale (divide and rule) hii haikuwa kazi rahisi na ndiyo maana waliofanikiwa wanasifiwa mpaka leo – mmojawapo akitajwa kuwa ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania aliyeongoza nchi yetu kwa miaka 23 kuanzia 1961 hadi 1984 alipotangaza kung’atuka. 

Inasemwa kuwa shukran kwa uongozi wake Tanzania imekuwa ni nchi ya mfano kwa amani na utulivu.  Watu wake ni wamoja na wanapendana sana. Inaelezwa na kuaminika kuwa mafanikio haya hayakuja hivi hivi bali ni kwa juhudi za Mwalimu Nyerere.

Katika baadhi ya mikakati ambayo inatajwa kuwa Nyerere aliitumia katika kujenga utaifa ni pamoja na kufifisha nguvu za taasisi za kimila, kukuza lugha ya Kiswahili ambayo imekuwa kiunganishi cha watu wa makabila mbalimbali na pia kuwa na utaratibu wa lazima kwa vijana kwenda Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambako walichanganyika na kujifundisha uzalendo.

Udini - Dosari Katika Utaifa Wetu
June 14, 1995, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikutana na waandishi wa habari katika hoteli ya Kilimanjaro kuzungumzia mustakbali wa taifa wakati taifa likijipanga kuchagua rais wa awamu ya tatu baada ya miaka kumi ya mrithi wa Mwalimu, Ali Hassan Mwinyi.

Katika hotuba yake Mwalimu Nyerere alielezea Tanzania kama nyumba mpya na imara iliyojengwa lakini ilikuwa haijatikiswa na dhoruba yoyote kuthibitisha uimara wake.  Baaade ilipopitiwa na dhoruba na misukosuko, nyumba ikaanza kuonesha udhaifu na nyufa zikajitokeza. Kumbe haikuwa imara kihivyo! Tukatanabahi. 

Nyerere alisema nyufa zilizojitokeza baada ya Tanzania kutikiswa zilikuwa za ukubwa tofauti, nyingine katika dari, nyingine katika ukuta na nyingine hata katika misingi.  Katika hotuba ile Nyerere alikusudia kuzungumzia kuhusu nyufa hizo za kushughulikiwa na kutaja sifa ya mtu aliyestahiki kuongoza nchi wakati ule ili ashughulikie nyufa hizo.

Katika hotuba yake nyingine aliyoitoa  katika mkutano Mkuu wa CCM Dodoma mwaka 1995 ambapo alizungumzia nyufa mojawapo  inayoonekena katika nchi yetu: suala la udini.  Alisema: “Watu wameanza kuzungumzia udini. Tulikuwa hatuzungumzi mambo ya udini-udini katika nchi hii. hata kidogo.''

Aliongeza: “Tulikuwa hatujali dini ya mtu, alikuwa anaijua peke yake. Ilikuwa haiji katika akili yetu kwamba tunapompima mtu tumchague huyu, tumfanye rais au tumfanye nani tunauliza dini yake, hatuulizi hata kidogo. Dini inatuhusu nini sisi. Hiyo ndiyo Tanzania tuliyokuwa tunajaribu kuijenga. Sasa watu  wanazungumza dini, udini bila haya, bila aibu. Wanajitapa kwa udini. Tunataa mtuchagulie mgombea ambaye atatusaidia kuondoa mawazo haya ya kipumbavu katika nchi yetu.”

Swali muhimu ambalo Mwalimu Nyerere hakuhangaika kulitafutia majibu ni kuwa kwa nini hiyo zamani watu walikuwa hawazungumzi mambo ya udini na siku hizo zilizofuata udini ukaanza kuzungumzwa waziwazi bila aibu?

Mahusiano ya Kidini
Watu wanaoijua Tanzania watakubaliana nami kuwa hakuna jambo linalotishia utaifa wetu kama mahusiani kati ya mbili kuu na vilevile kati ya dini hizi na serikali. Kumekuwa na malalamiko hususan kutoka kwa Waislamu kuwa serikali, hususan ya awamu ya kwanza ilipendelea sana Wakristo na kuwaonelea Waislamu.

Kauli za malalamiko haya zinazungumzwa na viongozi wakubwa, wasomi, wenye ushawishi na wanaotegemewa katika jamii ya Waislamu, na kwa hivyo lipo kundi kubwa la Waislamu ambalo linaamini hivyo.

Si nia yangu kujadili ukweli wa kauli hizi lakini naamini ni kutokana na hatua ambazo serikali ilizichukua, (labda kwa nia njema) Mungu anajua zaidi kuhusu hilo,  ambazo zimepelekea malalamiko haya. Ni hatua za mbaya zinazodhihirisha makosa aliyoyafanya Mwalimu Nyerere katika mradi wake wa ujenzi wa utaifa.

Kwanza, kabla sijazungumza makosa mahususi ya Nyerere yaliyopelekea malalamiko haya na kauli za udini, nitaje kuwa kosa la ujumla la viongozi waasisi wa nchi zetu ambalo hata Nyerere alilifanya.  Kosa lenyewe  ni kuamini kuwa wangeweza kujenga utaifa kwa mabavu. Tatizo la mbinu hii ya ujenzi wa taifa ni kuwa mafanikio yake ni ya muda mfupi.

Akiondoka madarakani yule mtawala waliyemuoga aliyelazimisha hisia za utaifa wakati watu hawaridhiki na mambo fulani, na hakutaka kuwasikiliza, basi lile kundi linalohisi linaonelewa huamka na kuanza kulalamika. Ukiangalia njia alizotumia Nyerere kujenga utaifa, ilikuwa ni lazima hisia na malalamiko ya udini ambao Mwalimu Nyerere alikemea mwaka 1995 ilikuwa ni lazima yaibuke.

Utaifa wa Tanzania ulikuwa ni wa kulazimsisha, watu wakatii kwa sababu walimuogopa Nyerere. Hapa tunazungumzia kipindi ambacho tetesi zinasema kila penye watu kumi tambua kuwa kuna shushushu mmoja. Katika hofu hii iliyojengwa nani angethubutu kutoa madai yoyote na wakati mifano ya kilichowapata waliopinga Nyerere ilishadhihiri?

Kosa Mahususi la Nyerere
Kosa mahsusi alilolifanya Nyerere na serikali yake ni kuingilia mno mambo ya Waislamu, hususan pale serikali yake ilipoifutilia mbali jumuiya ya East African Muslim Welfare Society (EAMWS) na kuwaundia Waislamu wa Tanzania chombo kiitwacho ‘Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) iliyorithi mali za EAMWS mwaka 1968.

Wakati EAMWS ilikuwa ni taasisi iliyopiga hatua kubwa ya maendeleo, BAKWATA ya leo haina kikubwa cha kuonesha kimaendeleo tangu mwaka 1968.  Wakati baadhi ya taasisi za kidini leo hii zinashindana na serikali kuanzisha mashule, vyuo vikuu na hospitali; BAKWATA licha ya ukongwe wake imeishia kumiliki vizahanati na vishule vichache vya sekondari zinazoongoza kwa matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne na sita, tena vya kurithi kutoka EAMWS.

Kwa nini serikali ya awamu ya kwanza ilijiingiza katika kuingilia mambo ya Waislamu kiasi cha kusaidia kuwaundia chombo cha kuendesha mambo yao – chombo ambacho mwishowe kikageuka kuwa sumu kwa Waislamu? Hili lilikuwa kosa kubwa la Nyerere na ndiyo msingi wa malalamiko ya udini.

BAKWATA katika miaka ya uwepo wake imelalamikiwa mno. Zipo taarifa za ufisadi wa kutisha tangu enzi hizo ikiwemo kuuza mali za wakfu, matumizi mabaya ya mali za Waislamu, ufisadi wa misaada iliyotolewa kwa ajili ya Waislamu wote, kushiriki katika shughuli ambazo ni kinyume na maadili ya Uislamu nk. Mwenendo wa BAKWATA tangu ianzishwe ni aibu tupu.

Watetezi wa Nyerere na serikali yake wanaweza kusema yeye hakushiriki  katika uendeshwaji wa BAKWATA, lakini kwa kusaidia tu kuua EAMWS na kuunda BAKWATA, hawezi kukwepa lawama hususan ukizingatia kuwa sera yetu  imekuwa ni ‘serikali haina dini’. Ilikuwaje Nyerere aingie na kuwaamulia Waislamu taasisi ya kuwaongoza?

Katika moja ya hotuba zake, Nyerere aliwahi kukemea kuingizwa maswala ya dini katika sensa kwa hoja kuwa suala hilo haliihusu serikali, lakini je serikali inahusika vipi na Waislamu hadi iamue kuwaundia taasisi? 

Tatizo kubwa zaidi ni kuwa BAKWATA ilikuwepo yenyewe bila mshindani kwa miaka mingi ikidhibiti mambo yote ya Waislamu. Waislamu waliipoteza bure miaka yote ambayo BAKWATA ilikuwa ndiyo taasisi pekee lakini ikiwa ni chombo cha hovyo ambacho kilikuwa ni cha Kiislamu kwa jina tu na kikiongozwa na wale waliuooekana kutekeleza ajenda za serikali kwa Waislamu.

Tatizo aliloliunda Nyerere limeendelea kuwagharimu Waislamu mpaka leo. Awamu zilizofuata za serikali zimeendelea kuipa BAKWATA hadhi kuliko taasisi nyingine na kuifanya ndiyo msemaje mkuu wa Waislamu.
Labda Nyerere aliyafanya haya kwa hoja kuwa anajenga utaifa, lakini matokeo yake ameweka nyufa kubwa katika utaifa,  tena katika msingi, nyufa ambayo huenda inaendelea kukua kila uchao maana waliomrithi kwa kiasi kikubwa wamefuata utamaduni uleule uliojengeka.

Watu tunampenda sana Nyerere lakini ukweli nao usemwe pale alipokosea. Ni vigumu kuamini kuwa wakina Profesa Shivji hawaoni makosa haya ya Nyerere ili hata tunapomuadhimisha tuwe na hadithi nzuri ya maisha ya Nyerere yenye uwiano wa mabaya na mazuri – kama walivyo binadamu na viongozi wote. 

No comments: