Sunday, 4 December 2016

BALOZI SEIF IDD NA SHAMBA LA BI FAUZIYA MAKALA YA MZANZIBAR MADHLUM ALIYEMSHITAKIA ALLAH

Displaying IMG-20161204-WA0200.jpg
Bi. Fauziya

Utangulizi
Bi Fauziya ni mjane wa Mwanamapinduzi Said Bavuai. Hivi karibuni ilisikika sauti yake kali katika mitandao ya kijamii ikizungumza na Makamu wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Idd akimshutumu kwa dhulma ya kumnyang'anya yeye na nduguze ardhi yao waliorithi kutoka kwa wazee wao. ''Video Clip,'' hii ilimsikitisha kila aliyeisikiza na inaonekana kila iliyomfikia aliirusha mbele ili ubaya wa kitendo hicho kiwafikie wengi. Kwa hakika kwa juma zima naamini sauti ya Bi, Fauziya ilisikika kote panaposemwa Kiswahili na kila pasemwapo Kiswahili Wazanzibari tupo wengi wakiwa waliuliwa ndiugu zao katika hayo mapinduzi na mali zao kuchukuliwa ikiwa mashamba au majumba au vyote kwa pamoja. Hapo chini ni ujumbe ulionifikia kutoka kwa mmoja wa Wazanzibari. Nimeona niiweke hapa ili tufaidike na maudhui yake. 

***

Sijaona kipya Bibi Fauziya anachokielezea  kunyakuliwa hilo shamba lao, itabidi ajirejeshe nyuma katika miaka 1964 na kuendelea namna Mashamba ya watu hata wakawaida kuchukuliwa na kugawiwa Eka 3 na wenye mashamba kubakishiwa eka chache kutokana na namba ya wanafamilia.

Watu wengine mashamba yao yalinyakuliwa kwa kuambiwa wazee wao hawakuja Zanzibar na mashamba, wengine wakahajir Zanzibar na msahamba yao kuchukuliwa, hio ndio spirit iliokuwa ya Mapinduzi kunyakua ardhi na kuzigawa wapendavyo na huyo mumewe Bi. Fauzia kati ya waliofanya hayo na kuyashabikia ajuwe hilo wala asijitie pambani hata kidogo.

Sijaona kipya ambacho Bi. Fauziya anachokizungumza isipokuwa labda kuwa kaolewa na Saidi Bavuai. Inafaa afahamishwe bibi huyu kuwa wenzake wamechukuliwa mashamba yao makubwa koliko hicho kikataa chake.

Unapokua hujanyeshiwa mvua utakaa kimya hata ukisikia walionyeshewa mvua wanalalama hutojua mvua ikimyeshea mtu huwa vipi, ikija kukunyeshea na wewe utaanza kutoa maneno ya kila namna.

Nimestaajabishwa sana kuona ‘’audio clip,’’ hii ya Bi. Fawziya kusambazwa kwa wingi na kama watu kumuonea huruma, huku wakisahau watu tele ambao mashamba yao halali, nyumba zao halali zimechukuliwa na kugeiwa watu bure na nyengine kuuzwa kwa bei ya chee.

Bi. Fauziya labda kwa watu wa tawheed watakuambia shukuru kwa tokeo hilo labda huo utakuwa ni utakaso na nyie mliokuwa sehemu ya kukaa na wenye kunyakua ardhi na mali za watu basi mnasafishwa.

Wamelia wengi huko nyuma na hawakusikilizwa vilio vyao, haya ndio tuyaitayo, Mapinduzi Daima, kwani ‘’daima,’’ mambo yatakwenda kwa sampuli hio.

Hao umoja wa Vijana wa CCM wakae kimya kama ni kweli wamesema hayo maneno hapo Kisonge, wajue fika siasa ya kunyakua ardhi za watu imetekelezwa kwa nguvu kuanzia 1964 na wengi wamechukuliwa ardhi zao na kumshtakia Allah, inafaa wajifunze dhana na siasa ya SMZ na BLM, tunaomba wawe kimya na wakae wapige vigelevigele na wamsifu Balozi kwa kazi nzuri aifanyao kutimiza malengo ya mapinduzi.

Ndugu msomaji msome Bi Fauziya hapo chini:

''Asslam Aleykum

Jina langu naitwa Fauzia Abdullah Saif Al Bahry. Mimi ni mjane wa Said Iddi BAVUAI, na nimeishi nae si chini ya miaka thalathini. Nimezaa nae nimejukuu nae, na nimemkalia mpaka EDA. Na mpaka leo naendelea kuwa mjane wa mzee BAVUAI. Ambae jana nimeshtushwa kusikia katika vyombo vya habari tunatangaziwa kwa jina la mdogo wangu Fadya. Na sijui kwa nini wasinitangaze mimi mkubwa wakamtangaza Fadya ambae ni mdogo na sisi tuko watatu Fauzia, Fadya na Firdaus lakini wametumia jina la mtu mmoja kuwa sisi wabadhirifu.



Hii lugha mimi ngeni kwangu kwa hakika siijui na hata sijui nini maana ya ubadhirifu nauliza nini maana ya ubadhirifu ? Sijui. Lakini nimefahamishwa kuwa ni wizi, kwaivo nakataa ile habari ilosema jana ambayo rikodi yake ipo na watu wamerikodi. Mimi nakataa si mwizi, siibi, sitoiba na sijamuibia mtu yeyote shamba la Kazole. Ni haki yetu tumerithi kwa wazee wetu, babaangu Abdallah bin Saif amefariki, Nassor bin Saif amefariki, na ami yangu Hemed bin Saif amefariki, na mali hii yetu. Mali tumerithi kwa wazee wetu.

Babaangu na ami zangu wamerithi kwa baba yao ambae amefariki toka 1930 na makaburi yake yapo pale pale kazole Muembe Amari, makaburi yapo ya mababu na ndugu na wazee walio tangulia mbele ya haki. Sijui ubadhirifu huu nimeufanya kwenye kitu gani? Kazole ni kwetu kazole nimeishi kazole nimekaa kazole naijua kwetu pakiitwa Muembe Amari. Tena mie mtu wa Kazole jirani yangu Kitope, jirani yangu Mahonda, jirani yangu Matetema. Shamba letu limepakana mpaka njia ya Mbaleni.

Hao walozuka leo wakasema lile ni shamba lao au sisi tumefanya ubadhirifu. Mh kama unataka kuchukua shamba chukua na kama unataka kuvunja kuta vunja lakini nakataa mimi na aila (familia) yangu sio wabadhirifu.

Mimi nimeolewa na mwanamme ambae ni kiongozi katika nchi sikumuona kufanya ubadhirifu, wala hajanifundisha ubadhirifu, wala kwetu sikuuona ubadhirifu. Niliona yeye (mume wangu) akifanya haki wizarani, maofisini, watu, makazini sijasikia yeye akifanya ubadhirifu wa aina yoyote. Yeye akisuluhisha na kutengeneza ndio hii siasa nilio ikuta wakati huo kwa hao waume walotuoa.

Huyo alochukua na kutoa amri ni Mh yuko katika ngazi ya juu na kajitangaza rasmi na maredio yote yanajua, TV pia. Hajasema siri. Zanzibar iniskie na Tanzania iniskie viongozi wa zamani wake zao wana nyanyaswa katika nchi hii. Wamesahau kila kitu.''
Chanzo : Kisiwandui





-9:04


No comments: