Bibi Titi alitolewa jela kwa msamaha wa rais hili halina shaka kwani ni rais
ndiye atoae msamaha huo.
Nyerere asingelimsamehe, Bi. Titi asingetoka kifungoni.
Nyumba zake Bi. Titi alirudishiwa na Rais Mwinyi na mimi nilikuwa mmoja
wa watu waliokwenda kwenye nyumba hiyo kuzungumzanae.
Nyumba hii ipo mkabala na Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Bi. Titi nakumbuka siku hiyo nilipokwenda kwake nilimkuta yeye na wajukuu
zake wanaangalia movie, ''Cinderella,'' katika TV na yeye akiwahadithia ile
movie akimwita Cinderella, ''Kisonoko.''
Kwa kauli yake Bi. Titi aliniambia kuwa Rais Mwinyi ndiye aliyemrejeshea ile
nyumba yake.
Hiyo ''bond,'' uisemayo haikupata kuwepo kama ilikuwapo basi ni wakati wa
kupigania uhuru lakini baada ya hapo palikuwa na upasi mkubwa baina yao.
Hili nimeligundua kwa Nyerere katika uhusiano wake na karibu na wengi sana
ambao alikuwanao wakati wa kudai uhuru.
Bi. Titi alipambana na Nyerere ile, ''nipe nikupe,'' ndani ya TANU NEC 1963
kisha kisha nyumbani kwa Nyerere 1968 na ugomvi wao mara zote hizo mbili
ni suala la EAMWS.
Safari hii ya pili Bi. Titi na Tewa Said Tewa walikwenda Msasani kumuona
Nyerere kumuuliza kwa nini anaachia vyombo vya dola vinapiga vita EAMWS.
Hii ilikuwa mwaka wa 1968 katikati ya kile kilichokuja kujulikana kama ''mgogoro
wa EAMWS.''
Labda turudi katika mazungumzo ambayo mimi nilikusudia kufanya na Bi. Titi.
Miadi ya kuonana na Bi. Titi alinifanyia Ally Sykes.
Wakati ule nilikuwa naandika kitabu cha Abdul Sykes na nilitaka kumhoji Bi.
Titi kuhusu historia ya TANU.
Si kama nilikuwa sina taarifa za Bi. Titi.
Nilikuwa na kila kitu chake lakini nilitaka kunogesha utafiti wangu kwa kumsikia
yeye mwenyewe alizungumza.
Bi. Titi alikataa kuzungumza kuhusu historia ya TANU lakini alinieleza kuwa yeye
hakuhusika katika njama za kutaka kupindua serikali.
Hata hivyo kama nilivyokwishaeleza Bi. Titi alikuja kueleza kwa kirefu ugomvi
wake na Nyerere kwenye mahojiano aliyofanya na gazeti la Rai mwaka wa 1994.
http://www.mohammedsaid.com/2016/12/mahojiano-swahiba-fm-miaka-55-ya-uhuru.html
No comments:
Post a Comment