Tuesday, 20 December 2016

TAMTHILIA YA BIBI TITI MOHAMED NA PROF. EMMANUEL MBOGO

Hapo chini ni kidokezo kaniandikia rafiki yangu Tamim Faraj kuhusu kitabu cha Bi. Titi Mohamed ambacho alikuwa kamaliza kukisoma na kimemgusa sana. Kaniandikia ili nami nikisome. Chini ya saa moja kitabu kikawa kimenifikia nyumbani na chini ya saa moja nyingine nikawa nimemaliza kuisoma tamthilia nzima ya Bi. Titi iliyoandikwa na Prof. Emmanuel Mbogo:

''Asalaam Aleykum,
Nimekisoma kijitabu (61 pages) cha tamthilia juu ya Bibi Titi - tiled: MALKIA BIBI TITI MOHAMED by Prof. Emmanuel Mbogo.

Ni kizuri.

Ni script iliyo capture vizuri a short history on the role of Bibi Titi katika kuupigania uhuru wa Tanganyika.  pazia la tamthiliya linafunguka jela ya Isanga alikofungwa Bibi Titi na kufungwa huko baada ya uhuru kupatikana.

Setting imepangwa kumuonesha  Bi Titi akiwa jela na daftari ambalo anaandika historia ya harakati za uhuru.

Zubeda askari jela baada ya kujua anachoandika Bi Titi, anamuomba kutumia historia aliyoiandika Bi Titi ili kuandaa igizo kwaajili ya kuazimisha sherehe za uhuru Disemba.

Anamueleza Bi Titi kawaida ya jela kufanya hivyo kila mwaka. Hivyo amamshawishi wafanye mchezo kwa mujib wa alichokiandika katika daftari lake na kumuomba Bi Titi ashiriki pamoja na wafungwa wenziwe.

Mwisho pazia linafungwa kwa Zubeda kurudishia daftari la na pia kumpa barua ya taarifa ya kutolewa gerezani.''


Tamim
***********************************************************************************
Kitabu kinaanza mwaka wa 1970 kwa kumuonyesha Bi. Titi akiwa Gereza la Isanga Dodoma, moja ya magereza magumu Tanzania. Kabla yake mwaka wa 1953 mwanasiasa mkubwa sana Tanganyika sehemu za Maziwa Makuu, Ali Migeyo alifungwa gereza hilo na Waingereza kwa kosa la kufanya mkutano wa siasa Kamachumu bila idhini ya serikali. Miaka 17 baadae mpigania uhuru Bi. Titi yuko kifungoni kwa kuhusika na kesi ya uhaini kutaka kuiangusha serikali aliyoipigania wakati wa kudai uhuru.



Akiwa hapo gerezani Bi. Titi anaandika historia ya uhuru wa Tanganyika na anaeleza ushirikiano wake na Nyerere wakati wakiwa katika ofisi ya TANU New Street. Bi. Titi anaeleza katika mswada wake,  anaoandika jela vipi yeye na wenzake walipita mtaa kwa mtaa kueneza TANU.

Kitu cha ajabu Gereza la Isanga wanamuomba Bi. Titi watumie historia yeke ile kufanya onyesho la historia ya uhuru wa Tanganyika.


Bi. Titi akiwa katika moja ya matawi ya TANU Dar es Salaam tawi hili lilikuwa Magomeni Mapipa nyumbani kwa Ali Msham Mtaa wa Jaribu 1955


Picha ya Mwandishi aliyopiga Viwanja Vya Mnazi Mmoja mwaka wa 1966 nyuma yake ni barabara iliyokuja kujulikana baadae kama Titi Street kwa kumuenzi Bi, Titi Mohamed na ukivuka barabara hiyo linaloonekana ni Soko la Kisutu maarufu  kama ''Soko Mjinga.''


Tamthilia hii ya Bi. Titi Mohamed ni kazi ya kupigiwa mfano kwani naamini hii ni tamthilia ya kwanza ambayo imejaribu kuhadithia historia ya TANU na historia ya uhuru wa Tanganyika kwa kuwataja wale ambao waliupigania uhuru wa Tanganyika. Kurasa za mwanzo Mwandishi anamleta Schneider Plantan akizungumza na Boi Selemani kuhusu TANU. 

Bwana Boi akimlalamikia Schneider kuwa mkewe Bi. Titi hatulii nyumbani kwa ajili ya shughuli za TANU kiasi imekuwa yeye ndiyo mfuaji wa nguo zake na mpishi wa chakula chake. 

Boi Selemani alikuwa dereva wa taxi. 

Schneider yeye ana historia ndefu katika siasa za Tanganyika. Yeye ndiye aliyesimama kidete kuwaleta vijana wasomi katika TAA ili kuwaondoa wazee waliokuwa wamechoka na kuifanya TAA isifanye siasa za maana kwa ajili ya ukombozi wa Tanganyika. 

Hii ilikuwa mwaka wa 1950. 

Sasa TANU ilipokuja kuasisiwa mwaka wa 1954 Schneider ndiye aliyemleta Bi. Titi katika TANU pamoja na wenzake akina Tatu Bint Mzee na wanawake wengine kuja kukipa nguvu chama. 


Kushoto ni  Tatu biti Mzee  Uwanja wa Ndege Dar es Salaam yuko Nyerere na Bi. Titi siku Nyerere anakwenda UNO kwa mara ya kwanza 1955

Tamthilia inaanza mwaka wa 1955 wakati Bi. Titi na wenzake wako katika hekaheka ya kuhamasisha wananchi kujiunga na TANU na wakati huo ndiyo safari ya Julius Nyerere kwenda UNO inatayarishwa. 

Boi katika mazungumzao yake na Schneider anatabiri kuvunjika kwa ndoa yake na mkewe Bi. Titi kwa ajili ya TANU na anamtupia lawama zote rafiki yake Schneider Plantan kwa kumpeleka mkewe TANU. 

Boi analalamika hadi kufikia kusema, ''Titi mwanamke wa Kiislam. Kasoma madrasa....Bibi Titi kapanda  jukwaani...hana baibui...''


Bi Titi Mohamed na Julius Nyerere wakihutubia wananchi Uwanja wa Jangwani 1955


Kulia ni Bi. Titi Mohamed, Clement Mtamila, Sheikh Suleiman Takadir, Julius Nyerere na nyuma ya Nyerere ni Maria
Nyerere, Rajab Diwani na John Rupia

Kitabu hiki, ''Malkia Bibi Titi Mohamed,''  ukikianza hukiweki chini hadi umekimaliza.

No comments: