Wednesday 28 December 2016

LIWALI AHMED SALEH NA SHEIKH SAID CHAUREMBO


Mwangaza Oktoba 5, 1956


Utangulizi
Rafiki yangu Abubakar Shani kaweka katika group letu ''Kumbukumbu,'' kipande cha gazeti la Mwangaza la Oktoba 5, 1956 ikimuonyesha Liwali wa Dar es Salaam wa wakati ule Ahmed Saleh akiwa na Sheikh Said Chaurembo ambae alikuwa hakimu katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo akihukumu kwa mujibu wa sheria za Kiislam. Wote hawa wawili walikuwa watu maarufu na mimi katika utafiti wa kitabu changu, ''The Life and Times of Abdulwahis Sykes (1924 - 1968) The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika,'' wote nimekutananao katika nyaraza za Sykes na katika simulizi mbili. Simulizi ya kwanza kutoka kwa Tewa Said Tewa na ya pili kutoka kwa Ali Mwinyi Tambwe ambae yeye mwenyewe nimemkuta katika nyaraka hizo za Sykes. Naweka hapa chini yale niliyoandika kuhusu Liwali Ahmed Saleh  na nitahitimisha In Shaa Allah kwa habari za Sheikh Said Chaurembo:

''...Si mambo yote yalikwenda shwari katika kuiendesha shule ile. Mwaka 1940 Ahmed Saleh alichaguliwa kuwa liwali wa Dar es Salaam. Liwali Saleh alikuwa Mwarabu na alipenda mno madaraka na ukubwa. Yeye alitaka kila jambo la Al Jamiatul Islamiyya lianzie na kumalizikia kwake. Wakati ule Sheikh Ali Saleh Mwarabu vilevile kama alivyokuwa Liwali Ahmed Saleh, ndiyo alikuwa rais wa Al Jamiatul Islamiyya. Halikadhalika Sheikh Ali Saleh alikuwa ndiye imam wa Msikiti wa Ijumaa ukijulikana kwa jina maarufu, Msikiti wa Kitumbini. Jina hili lilitokana kwa kuwa msikiti wenyewe umejengwa sehemu iliyokuwa ikijulikana kama Kitumbini. Sheikh Ali Saleh alikuwa mtu shujaa asiyeogopa mtu. Wakati ule wa ukoloni bila woga wowote alikuwa akitoa khutba za hamasa katika sala ya Ijumaa akiunga mkono Waarabu wa Palestine dhidi ya uonevu wa Uingereza katika mgogoro wa Mashariki ya Kati. Mgogoro huu ingawa ulikuwa mbali sana na Tanganyika lakini ulikuwa mmoja wa migogoro iliyokuwa ikiitatanisha serikali kwa kuwa Waislam walikuwa wengi Tanganyika na waliona shida ya Waislam Palestine ni shida yao. Halikadhalika wakati ule kuliwa na suala la mitaala ya shule. Vitabu vya kiada vilivyokuwa vikitumika shuleni vilikuwa vimejaa propaganda za Ukristo dhidi ya Uislam. Katika vitabu hivyo Uislam ulionyeswa katika sura ya kuleta utumwa Afrika. Vilevilee vitabu vilieleza kuwa Uislam ulienezwa kwa nguvu ya upanga. Sheikh Ali Saleh na Al Jamitul Islamiyya hawakukubaliana na uongo huo na hiyo ndiyo ikawa sababu ya mapambano baina yao na serikali. Serikali iliona Al Jamiatul Islamiyya ilikuwa sasa inajiingiza katika siasa. Serikali kutaka kuikomesha Al Jamiatul Islamiyya ikawa inatafuta sababu ya kuifunga shule.

Al Jamiatul Islamiyya kwa wakati ule ilikuwa ikishughulika na kuendesha shule na kusoma maulidi ya kila mfungo sita. Ofisi ya liwali ilikuwa ikishughulika na mambo yote yaliyokuwa yanahusu sharia na mambo mengine ya Kiislam. Kwa miaka mingi maulidi yalikuwa na kamati yake maalum mbali kabisa na shughuli za ofisi ya liwali. Liwali Saleh hakupendezewa na mpango huu, yeye aliona kuwa kamati ya maulidi iwe chini yake. Liwali Saleh akaanza kutoa makosa jinsi maulidi yalivyokuwa yakisomwa na kusheherekewa. Alipinga mchanganyiko wa wanafunzi wa kike na wa kiume kuchanganyika na kupanda kwenye member na kusoma kasida. Jambo la kusikitisha katika mgogoro huu ni kuwa chanzo hasa cha kuwaleta wale wasichana kusoma mbele ya wazee wao ilikuwa ni kutafuta pongezi kutoka kwa wazazi. Al Jamiatul Islamiyya ilikuwa imenzisha shule ya wasichana wa Kiislam. Uongozi wa shule katika kutaka kuonyesha kazi nzuri iliyokuwa ikifanywa na shule iliona ifanye onyesho hilokama kivutio kwa wazazi. Katika fikra yao walonelea wawatoa watoto wale wa kike mbele ya wazazi wao waimbe kasda kuwadhihirishia kuwa shule ya watoto wa kike ipo na inaendelea. Kwa kufanya hivyo kwa nia njema kabisa ikawa Al Jamiatul Islamiyya imejipalia makaa.

Kwa kuzingatia sharia hasa, hiyo inaweza kuchukuliwa kuwa Liwali Saleh alikuwa sawa kutokana na mafundisho ya Kiislam, lakini ukitazama kwa mtazamo mwingine, unaweza ukasema kuwa wale walikuwa watoto wadogo wasiokuwa balehe na kwa hivyo basi kulikuwa hakuna ubaya wowote kwa wao kujitokeza mbele ya halaiki ya watu. Lakini ingawa kwa sura ya nje alionekana Liwali Saleh kama aliyekuwa mstari wa mbele katika kuipiga vita Al Jamiatul Islamiyya, ukweli ni kuwa ilikuwa ni serikali ya Kiingereza ndiyo iliyokuwa imemtuma. Al Jamiatul Islamiyya ilikuwa na nguvu sana na hili halikuipendeza serikali. Serikali iliona moja ya njia nzuri ya kuidhibiti Al Jamiatul Islamiyya ilikuwa kumpata kibaraka katika safu yake ya uongozi. Ahmed Saleh alikuwa mtu ambae Waingereza waliona angeweza kuwatumikia vyema na kwa utiifu mkubwa kuifanya kazi ile. Ilikuwa wazi kuwa Liwali Ahmed Saleh asingeweza kupata nafasi ya kuongoza Al Jamiatul Islamiyya kwa kuwa uchaguzi wa viongozi wake ulikuwa unafanyika kwa njia ya demokrasia na yeye hakuwa anapendeka pale mjini. Wanachama walikuwa wakipiga kura kupata vongozi wa jumuiya ile. Nafasi ya kuifungia Al Jamitul Islamiyya sasa ilikuwa imejitokeza katika mgogoro wa maulidi ile ya mwaka 1940. Siku ya pili yake baada ya wale mabinti wa Kiislam kusoma kasida mbele ya wazee wao, kikundi cha Wazaramo na Wamashomvi kilienda kwa District Commissioner wa Dar es Salaam, Mr. A.A. Pike kudai shule ifungwe kwa kuwa viongozi wa Al Jamitul Islamiyya walikuwa wamewadhalilisha mabinti zao na dini nzima ya Kiislam. Kundi lile likavamia shule wakaweka ulinzi milangoni huku wameshika mapanga na marungu wakidai shule ifungwe au sivyo damu itamwagika.  Ahmed Saleh kama liwali na kwa hiyo mtaalamu wa sharia akaunga mkono kile kikundi kilichokuwa kinadai shule ifungwe na serikali ikamuunga mkono Liwali Ahmed Saleh.

Al Jamiatul Islamiyya ikagawanyika katika kambi mbili hasimu. Kambi moja ikawa ni ile ya wale waliojulikana kama watu wa kuja, yaani ëwagenií. Hawa walikuwa Wamanyema, Wanubi na Wazulu wachache. Kambi nyingine ilikuwa ile ya wenyeji; Wazaramo, Wandengereko, Wamashomvi, Warufiji na watu wengine. Hawa walibaki katika ofisi zao New Street katika jengo la shule. Wenyeji ambao ndiyo walikuwa na wafuasi wengi walimuunga mkono Liwali Saleh na wakaanzisha Al Jamiatul Islamiyya ëAí. Kleist kwa ajili ya msimamo wake wa siasa hakuwa anapendeza katika macho ya serikali. Yeye akawa katika kundi la watu wa kuja, yaani wagenií. Kisingizio cha kuikomesha Al Jamiatul Islamiyya kikapatikana. Serikali ikafunga shule ili mzozo usizidi kukua na kuepuka kumwagika kwa damu.

Wanachama wa Al Jamiatul Islamiyya wakaitisha mkutano nyumbani kwa Mwarabu mmoja tajiri aliyekuwa na biashara ya kuuza duka, jina lake Baghwar aliyekuwa katika halmashauri ya Al Jamiatul Islamiyya kujadili kufungwa kwa shule. Kikao kile kiliamua kuwa katibu wa Al Jamitul Islamiyya, Kleist, aandike barua kwa Provincial Commissioner kulalamika kuhusu kitendo cha serikali kuifunga shule. Kleist alikuwa anapata mshahara mzuri sana miongoni mwa Waafrika waliokuwa wameajiriwa na Tanganyika Railways. Alihisi kuwa kwa yeye kuchukua hatua kama ile kungeweza kuhatarisha kazi yake. Alikuwa yupo karibu ya kustaafu kazi na alidhani kuwa kujitumbukiza katika jambo zito kama lile kungeweza kuhatarisha mafao yake ya uzeeni. Kwa kukataa kwake kuandika barua ile kwa PC, Kleist aliombwa ajiuzulu ukatibu wa Al Jamitul Islamiyya.

Mkutano ule ulipendekeza jina la Ali Mwinyi Tambwe kushika nafasi ya Kleist. Sheikh Ali Saleh Imam wa Msikiti wa Kitumbini aliunga mkono uteuzi ule na Ali Mwinyi akashika wadhifa wa katibu wa Al Jamiatul Islamiyya  na akapewa maelekezo ya kuandika barua kwa PC. Ali Mwinyi alikuwa mfanyakazi wa serikali akifanya kazi katika ofisi ya Kabidhi Wasii. Ali Mwinyi hakumuandikia PC moja kwa moja, la hasha. Alikwenda kwa mwanasheria mmoja wa Kiasia, Rajabali Bhalo Verani akamuhadithia mkasa mzima uliopelekea kufungiwa kwa shule ya Waislam. Al Jamitul ilikuwa haina fedha za kumlipa lakini Verani akasema yeye ataichukua kesi ile bila ya malipo yoyote kwa kuwa ilikuwa kesi ya kudai haki kwa hiyo hakukuwa sababu ya kuwatoza watu wanaodhulumiwa. Verani akamuandikia PC na kumuamuru afungue shule ya Waislam katika saa arobaini na nane ama sivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Mara moja PC akauita uongozi mzima wa Al Jamitul Islamiyya ofisini kwake ili kujadili tatizo la kufungwa shule. Ali Mwinyi akenda kumueleza Verani kuhusu mwito wa PC. Verani akamuambia Ali Mwinyi kuwa amfahamishe PC kwamba, makubaliano yoyote yatakayofikiwa katika mazungumzo kati yake na uongozi wa Al Jamiatul Islamiyya shurti yaidhinishwe na yeye kama mwanasheria wa Al Jamiatul Islamiyya; na vilevile ajaribu kutafuta sulhu kati ya Wanubi na Wamanyema waliokuwa wamefarikiana na Wazaramo na Warufiji. Wanubi na Wamanyema, wote wakiwa kizazi cha pili cha wazee waliotoka Belgian Congo na Sudan walikuwa wamehasimiana na liwali wa Dar es Salaam, Ahmed Saleh. Wazaramo na Warufiji na watu wengine wakaisusia Al Jamiatul Islamiyya na kumuuunga mkono Liwali Ahmed Saleh. Kwa ufupi ugomvi huu ulikuwa mkubwa na Liwali Ahmed Saleh akajitahidi sana kumuangusha Sheikh Ali Saleh kutoka uongozi wa Al Jamiatul bila mafanikio.

PC aliwaeleza wanachama wa Al Jamiatul Islamiyya kuwa amewaita ili wazungumze kuhusu kufungwa kwa shule na kupatanisha baadhi mbili zilizokuwa zimehasimiana kwa muda. PC alitaka kujua ni wanachama wapi wanalipa ada zao. Sasa ikawa baada ya mgogoro ule Wazaramo na Warufiji na watalamizi wao wakaacha kulipa ada zao za uanachama.   PC akawafahamisha kuwa kwa kutolipa michango yao basi wao si wananchama tena wa jumuiya ile; hata hivyo akawaeleza kuwa wanaweza kuendelea kuwa watayarishaji wa maulidi chini ya Liwali Ahmed Saleh na shule itaendeshwa na Wazulu, Wamanyema na Wanubi ambao uanachama wao haujasita kwa kutolipa ada. Baada ya hapo PC akafuta amri ya kuifungia shule. Shule ikakabidhiwa kwa Sheikh Ali Saleh aliyekuwa rais wa Al Jamitul Islamiyya, Kleist Sykes, Ali Jumbe Kiro, aliyekuwa mweka hazina, Ali Mwinyi Tambwe, katibu; Salum Abdallah, Ibrahim Hamisi, Hassan Machakaomo na Maalim Popo Saleh.

Baada ya Liwali Saleh kufanikiwa kuchukua uongozi wa Waislam ëwenyejií alihakikisha kuwa shughuli zote za Kiislam zinatendeka chini ya uongozi na maelekezo ya serikali ya kikoloni. Kwa ajili hii aliunda kamati yake ya Maulidi na Sala ya Idd yeye mwenyewe akiwa mwenyekiti wa kamati hizo. Liwali Ahmed Saleh alitumia kamati hizo kwa kujikomba kwa Waingereza. Katika kila hafla ya Kiislam ama iwe kwenye Baraza la Idd au Maulid, yeye alikuwa akiwaalika viongozi wa serikali Wazungu, kuja kutoa matamshi ya kukatisha tamaa harakati za Waislam za kupinga ukoloni kwa kuwaambia Waislam waache fujo na serikali ya kikoloni itawaletea maendeleo. Hali ilikuwa hivi hadi miaka ya 1950 mwishoni alipojiuzulu kutoka uliwali wa Dar es Salaam na harakati za kupinga ukoloni chini ya TANU zilipokuwa zimepamba moto.''




Kamati Ndogo ya Siasa Ndani ya TAA, 1951
Hakuna nyaraka zozote zinazoonyesha kama African Association ilikuwa imetayarisha mpango wa kushughulikia hali ya siasa.  Kuelewa mwelekeo wa siasa kama wakati ule inabidi mtu atazame mwenendo wa viongozi wa TAA na jinsi walivyokuwa wakiyashughulikia mambo tofauti yaliyokuwa yakiwadhili wananchi. Jambo la kwanza alilofanya Abdulwahid mara tu baada ya kuingia madarakani ni kuunda TAA Political Subcommittee (Kamati Ndogo ya Siasa ya TAA)  iliyomjumuisha yeye mwenyewe Abdulwahid, Sheikh Hassan bin Amir kama mufti wa Tanganyika; Dr. Vedasto Kyaruzi, Hamza Mwapachu, Said Chaurembo aliyekuwa liwali wa mahakama ya Kariakoo; John Rupia na Stephen Mhando. Kazi ya kamati hii ilikuwa ni kushughulika na masuala yote ya siasa katika Tanganyika. Kuundwa kwake ndiyo hasa ulikuwa mwanzo wa siasa za dhahiri katika Tanganyika na mwanzo wa harakati za kudai uhuru wa Mtanganyika.

No comments: