Thursday, 29 December 2016

SHEIKH ALI SALEH ALIIUNGA MKONO PALESTINA AKITUMIA MEMBARI YA MSIKITI WA KITUMBINI MIAKA YA 1940



Sheikh Ali bin Saleh
Picha kwa hisani ya Hamzah Rijal


Utangulizi
Hamzah Zubeir baada ya kusoma post. ''Liwali Ahmed Saleh na Sheikh Said Chaurembo,'' ameniandikia kufanya masahihisho kuhusu Sheikh Ali Saleh ambae nilimweleza kuwa alikuwa Muarabu. Naiweka hapa ujumbe alioniandikia ili sote tunufaike:

''Sheikh Mohamed Said Sheikh Ali bin Saleh hakuwa mwarabu, kama ndio unayomzungumza. Sheikh Ali bin Saleh ndio aliomchukua Mzee Ali Mwinyi na kumlea na alikuwa na ndugu yake akiitwa Rajab bin Saleh.

Sheikh Ali bin Saleh alikuwa mweupe kwa rangi yake na akivaa vilemba saa zote, kuna nyakati alikhitalifiana na jamaa zake wa Kingazija akajitenga nao na wengi hapo wakamnasibisha na Uarabu. Wengine wakimwita Bwana Ali mweupe. Yeye ndio aliokuja na Tarika ya Dandarawi. 

Sheikh Ali bin Saleh badaye alikuja akamkabidhi Mzee Ali Mwinyi Muslim School.

Abdi Mout A. Ajmi ni babu yake mzaa mama.

Kwa asili Sheikh Ali bin Saleh kwao Comoro ni mji wa Itsandaa, wenyewe wanajinasibu kuwa na root ya Yemen na hujita Sankule Arabiya''

ASALAAM ALAYKUM!

Sheikh Ali bin Saleh walikuwa ni ndugu watatu, wawili wanaume na mmoja mwanamke.

Rajab bin Saleh, Halima bin Saleh na Ali bin Saleh.

Halima bin Saleh ndio bibi yangu mzaa mama na yeye complexion yake sawa na Ali bin Saleh.

Hawa wote wamepata misingi ya dini na Rajab bin Saleh hakupata kwenda nje kusoma kasoma ndani kwa kina Sheikh Alamaa Burhani Mkele na wengine, katika Msikiti wa Jongeyani hapo Malindi alikuwa na darsa mbili mmoja ya watu wote na ya pili ni ya Wangazija wageni, wale Wangazija waliohamia Zanzibar bado hawakuwa wanakifahamu Kiswahili sawa, kwa hio akawa ana darsa na jamaa zake akitafsiri Qur'an kwa Kiarabu na Kingazija. Rajab bin Saleh alikuwa zaidi ni mcha Mungu na walikoseyana na Sheikh Ali Saleh akiwa anapenda mpira na mengine ya dunia na Sheikh Ali bin Saleh ndio Founder wa Young African Sports Club.

Sheikh Ali bin Saleh kaoa mara mbili katika maisha yake na kapata kwenye tumbo mmoja mwaname na mwanamke na tumbo jengine akapata mwanamke na wote watoto wake akawaita Fatma.


Sheikh Ali bin Saleh alikuw ana Command ya Kiarabu na akisoma sana magazeti yaliokuwa yakitoka Masri kama Al Manara na ndio zikawa Khutba zake za Ijumaa akizungumzia Palestine. Alikuwa akipinga ubeberu na hakuwa akificha hisia zake juu ya hilo.

Hapo chini nimenyambua sehemu za Sheikh Ali bin Saleh kutoka kitabu cha Abdul Sykes:

''Wakati ule Sheikh Ali Saleh Mwarabu vilevile kama alivyokuwa Liwali Ahmed Saleh, ndiyo alikuwa rais wa Al Jamiatul Islamiyya. Halikadhalika Sheikh Ali Saleh alikuwa ndiye imam wa Msikiti wa Ijumaa ukijulikana kwa jina maarufu, Msikiti wa Kitumbini. Jina hili lilitokana kwa kuwa msikiti wenyewe umejengwa sehemu iliyokuwa ikijulikana kama Kitumbini. Sheikh Ali Saleh alikuwa mtu shujaa asiyeogopa mtu. Wakati ule wa ukoloni bila woga wowote alikuwa akitoa khutba za hamasa katika sala ya Ijumaa akiunga mkono Waarabu wa Palestine dhidi ya uonevu wa Uingereza katika mgogoro wa Mashariki ya Kati. Mgogoro huu ingawa ulikuwa mbali sana na Tanganyika lakini ulikuwa mmoja wa migogoro iliyokuwa ikiitatanisha serikali kwa kuwa Waislam walikuwa wengi Tanganyika na waliona shida ya Waislam Palestine ni shida yao. Halikadhalika wakati ule kuliwa na suala la mitaala ya shule. Vitabu vya kiada vilivyokuwa vikitumika shuleni vilikuwa vimejaa propaganda za Ukristo dhidi ya Uislam. Katika vitabu hivyo Uislam ulionyeswa katika sura ya kuleta utumwa Afrika. Vile vile vitabu vilieleza kuwa Uislam ulienezwa kwa nguvu ya upanga. Sheikh Ali Saleh na Al Jamitul Islamiyya hawakukubaliana na uongo huo na hiyo ndiyo ikawa sababu ya mapambano baina yao na serikali. Serikali iliona Al Jamiatul Islamiyya ilikuwa sasa inajiingiza katika siasa. Serikali kutaka kuikomesha Al Jamiatul Islamiyya ikawa inatafuta sababu ya kuifunga shule.'' 

''Mkutano ule ulipendekeza jina la Ali Mwinyi Tambwe kushika nafasi ya Kleist. Sheikh Ali Saleh Imam wa Msikiti wa Kitumbini aliunga mkono uteuzi ule na Ali Mwinyi akashika wadhifa wa katibu wa Al Jamiatul Islamiyya  na akapewa maelekezo ya kuandika barua kwa PC. Ali Mwinyi alikuwa mfanyakazi wa serikali akifanya kazi katika ofisi ya Kabidhi Wasii. Ali Mwinyi hakumuandikia PC moja kwa moja, la hasha. Alikwenda kwa mwanasheria mmoja wa Kiasia, Rajabali Bhalo Verani akamuhadithia mkasa mzima uliopelekea kufungiwa kwa shule ya Waislam. Al Jamitul ilikuwa haina fedha za kumlipa lakini Verani akasema yeye ataichukua kesi ile bila ya malipo yoyote kwa kuwa ilikuwa kesi ya kudai haki kwa hiyo hakukuwa sababu ya kuwatoza watu wanaodhulumiwa. Verani akamuandikia PC na kumuamuru afungue shule ya Waislam katika saa arobaini na nane ama sivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Mara moja PC akauita uongozi mzima wa Al Jamitul Islamiyya ofisini kwake ili kujadili tatizo la kufungwa shule. Ali Mwinyi akenda kumueleza Verani kuhusu mwito wa PC. Verani akamuambia Ali Mwinyi kuwa amfahamishe PC kwamba, makubaliano yoyote yatakayofikiwa katika mazungumzo kati yake na uongozi wa Al Jamiatul Islamiyya shurti yaidhinishwe na yeye kama mwanasheria wa Al Jamiatul Islamiyya; na vilevile ajaribu kutafuta sulhu kati ya Wanubi na Wamanyema waliokuwa wamefarikiana na Wazaramo na Warufiji. Wanubi na Wamanyema, wote wakiwa kizazi cha pili cha wazee waliotoka Belgian Congo na Sudan walikuwa wamehasimiana na liwali wa Dar es Salaam, Ahmed Saleh. Wazaramo na Warufiji na watu wengine wakaisusia Al Jamiatul Islamiyya na kumuuunga mkono Liwali Ahmed Saleh. Kwa ufupi ugomvi huu ulikuwa mkubwa na Liwali Ahmed Saleh akajitahidi sana kumuangusha Sheikh Ali Saleh kutoka uongozi wa Al Jamiatul bila mafanikio.

Kulia Ali Mwinyi Tambwe, Oscar Kambona, wanne Ali Jumbe Kiro, Julius Nyerere na wa pili kushoto ni Mwalimu Sakina Arab (Picha hisani ya wajukuu wa Mwalimu Sakina Arab)
PC aliwaeleza wanachama wa Al Jamiatul Islamiyya kuwa amewaita ili wazungumze kuhusu kufungwa kwa shule na kupatanisha baadhi mbili zilizokuwa zimehasimiana kwa muda. PC alitaka kujua ni wanachama wapi wanalipa ada zao. Sasa ikawa baada ya mgogoro ule Wazaramo na Warufiji na watalamizi wao wakaacha kulipa ada zao za uanachama.   PC akawafahamisha kuwa kwa kutolipa michango yao basi wao si wananchama tena wa jumuiya ile; hata hivyo akawaeleza kuwa wanaweza kuendelea kuwa watayarishaji wa maulidi chini ya Liwali Ahmed Saleh na shule itaendeshwa na Wazulu, Wamanyema na Wanubi ambao uanachama wao haujasita kwa kutolipa ada. Baada ya hapo PC akafuta amri ya kuifungia shule. Shule ikakabidhiwa kwa Sheikh Ali Saleh aliyekuwa rais wa Al Jamitul Islamiyya, Kleist Sykes, Ali Jumbe Kiro, aliyekuwa mweka hazina, Ali Mwinyi Tambwe, katibu; Salum Abdallah, Ibrahim Hamisi, Hassan Machakaomo na Maalim Popo Saleh.'' 

Photo: HASSAN MACHAKAOMO
Kushoto ni Hassan Machakaomo

No comments: