Thursday, 1 December 2016

TAAZIA: BI. KHADIJA BINT KAMBA (1922-2016) MWANAMAMA MPIGANIA UHURU - MAKALA HISANI YA SAIGON GROUP

Bi. Khadija Bint Kamba
Mtaa wa Bi. Khadija Bint Kamba, Ilala

Anaitwa Hadija Bint Kamba, Bint mrefu mweusi mwenye umbo lililosadifu Unyamwezi, asili yake ni Tabora ndipo alipotokea baba yake na Kigoma ndipo wazazi wa mama yake walipotokea.

Ni kama ilivyo kwa familia ya Sykes, Bint Kamba alitoka katika familia mashuhuri jijini Dar es Salaam katika miaka ya 1950s. Aliingia katika harakati za ukombozi akiwa bint mdogo mwenye malengo tofauti kabisa na ya kipekee sana. Pamoja na kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukoloni tena akiuza roho kwani alikuwa ni bint pekee wa Kiafrika aliyeweza kujichanganya na Wazungu, hivyo aliweza kupata siri nyingi za wakoloni na kuwasaidia wapigania uhuru wasikamatwe na wakati mwingine wasidhurike. Alifanya kazi hii kwa siri kubwa sana, kiasi kwamba hakuwa akijulikana sana kwa watu hasa wanaharakati. Alikuwa mtu mwenye uwezo wa kipekee wa kutunza siri.

Mwaka 1955 akiwa na Bibi Titi na Bint Maftah walishirikiana kuunda Baraza la Wanawake Tanganyika ikiwa ni kikundi ndani ya TANU kilichokuwa kikitoa ushawishi kwa akina mama kuiunga mkono TANU.

Mwaka 1961 wakati wa Uhuru, Bint Kamba alikuwa ni mmoja wa timu iliyoundwa kubuni nembo ya Taifa (maarufu kama nembo ya ikulu ama nembo ya Adamu na Hawa ambayo mpaka sasa imeendelea kuwa alama kuu ya taifa (baadhi ya waandishi wanamtaja kuwa yule mwanamke anayeonekana kwenye nembo hiyo ndiye Bint Kamba)

Novemba 2 ya Mwaka 1962 Mwalimu Nyerere alipotangaza kuunda Umoja wa Wanawake wa Tanganyika  (UWT) Bint Kamba alikuwa ndio mpanga mikakati na mfumo wa uongozi wa UWT.
Pamoja na kushiriki katika mapambano ya kudai uhuru akiwa msiri mkubwa wa Mwalimu Nyerere, Bint Kamba hakuwahi kushika nafasi yeyote ya kisiasa kwa kugombea ama kuteuliwa. Baada tu ya nchi kupata uhuru Bint Kamba alieleza kuwa lengo lake limetimia na kwamba haitaji cheo chochote.

Mwaka 1985 katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Mwalimu Nyerere akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) pamoja na Baraza la Wazee wa Dar es salaam juu ya kung'atuka alimtaja mtu mmoja ambaye ni wa kipekee aliyeyashangaza maisha yake ya uongozi. Alimtaja Hadija Bint Kamba kuwa ni mwanamama na mpambanaji wa kipekee aliyeshiriki mapambano ya uhuru bila tamaa ya cheo. Mwalimu Nyerere alisema kuwa amekaa ikulu kwa miaka 25 na kila alipotaka kumteua, Hadija Bint Kamba aliendelea kubaki na msimamo wake kuwa hakupigania cheo bali alipigania haki na usawa...alitaka kuona Mwafrika anathaminiwa katika nchi yake na kwamba ametimiza lengo hilo.

Tangu Mwaka huo wa 1985, Mwalimu alimtangaza Bint Kamba kuwa ni, ''ShujaaAasiyevaa Nishani,'' na tangu wakati huo alishirikia vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Mikutano Mikuu yote akiwa ni mwalikwa mpaka pale umri ulipokuwa mkubwa na kumfanya ashindwe kuhudhuria vikao na mikutano hiyo.

BI. Hadija Bint Kamba amefariki jana tarehe 30 Novemba, 2016 akiwa ni miongoni wa waasisi waliobahatika kuishi kwa muda mrefu katika nchi huru ya Tanzania.

Bint Kamba amezikwa mchana wa leo tarehe 1 Desemba 2016 katika makaburi ya Kisutu yaliyopo jijini Dar es salaam.

Anakufa bila cheo lakini anazikwa kwa heshima ya kiongozi wa kitaifa, kwa msafara wa magari ya askari na viongozi wa CCM na Serikali kutoka mtaani kwake mtaa wenye jina lake Bint Kamba Street Ilala Bungoni mpaka Kisutu. Maraisi wastaafu, Katibu Mkuu wa CCM, Naibu Katibu Mkuu na viongozi  wengine wa CCM wakiongoza jeneza lenye mwili wake.

Anakufa bila utajiri  lakini anazikwa kwa hadhi ya bilionea.

HIVI NDIVYO ULIVYO MWISHO WA WATU WEMA...!!!
***
Mara tu nilipopata taarifa ya msiba huu katika Saigon Group niliandika maneno haya yafuatayo:

''Bi. Khadija Kamba katika sifa yake kubwa katika TANU ni yeye kukubali kutoka TANU kwenda Congress kama "mole," yaani mpelelezi. Hii ilimjengea uadui mkubwa na wenzake...bahati mbaya sana hizi ni katika historia zinazowatisha baadhi ya viongozi kwa hiyo historia ya mama yetu huyu haifahamiki vizuri wala haijaandikwa. Allah ampe kauli thabit.''
***
Nimepokea vilevile maneno kutoka kwa baadhi ya watu kuhusu msiba huu wa Bi. Khadija Bint Kamba:

''Uncle unatisha. Muandike Binti Kamba. Nadhani moja ya picha yake nzuri ni ile ya Ikulu na Nyerere wakati akiaga. CCM ilimjengea upya nyumba yake Bungoni. Namkumbuka huyu bibi akiishi Aggrey. Na wakati Kasanga Tumbo alipounda chama cha upinzani yeye na Issa Mtambo wakatangdaza kujiunga. Wakati huo Mtambo akiishi mtaa wa Pemba kwa mkwewe Bi Mwajuma Mlenda, ndugu yake Bi Maftaha.  Mtambo alikaa kibarazani na kuichana kadi ya TANU. Ilikuwa, ''shock,'' kwa wengi. Kisha rafiki yake Mwanjisi akaenda kumsihi, lakini wapi, akashikilia. Kumbe yote yale yalikuwa machezo! Inatisha!!!''
***
''Bi khadija Bint Kamba alizaliwa 1922  Tabora. Mama yake ni Muhombo. Kwao ni Ng'ambo Mbirani.  Baba yake ni Mzaramo wa Bagamoyo. Allah hakumjalia watoto. Lakini alikuwa ni mlezi mkubwa wa watoto wote wa nduguze. Ukihitaji historia yake nitafute. Mie ni Dada yangu upande wa umama. Na malezi yake yote yalikuwa kwa mjomba wetu marehemu  Khamis Mnubi pale Chemchem Mtaa wa Caravan siku hizi unaitwa Mtaa wa Uhuru.''
***
''Ni mama yangu bint Kamba hawa ndio kina mama wa mwanzo kabisa kujiunga na TANU akiwemo Bi. Baita wa Dodoma BI. Mtumwa wa Tabora, Bint Mrisho wa Tabora pia ni mama wa mwanzo katika TANU kwa ngoma yao ya Lelemama.''
***
[01/12, 10:57 p.m.] +255 717 423 353: Tumekuelewa Shekh Said
[01/12, 11:00 p.m.]
+255 717 423 353: Shekh Said huyu Bi Hadija hukumuandika hata ww katika    nakala zako sheikh ndio maana naona hata Tanzia kwa hisani ya Saigon.
***
[01/12, 11:41 p.m.] mohamedsaidsalum: Kuna tatizo sana kumtafiti "mole," yaani mpelelezi. Bi. Khadija baada ya 1958 hakuwa mwana TANU ila ni ''kibaraka msaliti.'' Uongozi wa juu kabisa ndiyo wakijua kuwa alikuwa katika kazi maalum. Sasa huyu anahitaji utafiti makhususi na CCM inawajibika sasa kuweka wazi hili jalada la mama yetu huyu tujue yote aliyofanya. Yuko, ''mole,'' mwingine iko siku nitamtaja huyu aliangamiza umma na mwenyewe alikereka sana mtu akimuuliza mchango wake katika historia ya Tanzania. Mimi nilifanya mahojianonae kwa yeye mwenyewe kuniita kupitia mwanae. Hili ni jambazi khasa la Waingereza.


No comments: