Si kwamba Waswahili wa Burundi zama za ukoloni
walijibagua na kujitenga mbali na elimu. La hasha! Waswahili walikuwa na elimu
ya kutosha zama hizo ukiwalinganisha na makabila
mengine. Walikuwa wanatumia herufi za Kiarabu (alphabet arabe) kwa kuandika Kiswahili
na walikuwa wanajuwa kupiga hesabu (calcul). Walikuwa na shule zao ambazo ni
madrasa. Walikuwa wakiandika tungo mbalimbali ikiwemo mashairi. Walitengwa kwenye
elimu kwa maksudi na ukoloni. Hasa ukoloni wa Wabeleji ambao uliwanyima wazi
Waswahili elimu mpya ya Kimagharibi na kuwapa Kanisa Katoliki umiliki pekee
(monopole) wa kuitoa elimu katika nchi.
Waswahili
walilalamika zama hizo wala hawakulala. Waliunda chini ya uongozi wa marehemu Sheikh
Amrani Juma taasisi iitwayo ASMARU (Association Scolaire Musulmane du
Ruanda-Urundi) yaani Taasisi ya Kielimu ya Waislam wa Ruanda-Urundi). Na
walipeleka malalamiko yao mbele ya Serikali na kuwambia nyiye ni wabaguzi, tunaomba
na sisi tupewe ruzuku (subventions) ili tujenge shule zetu na tuwalipe walimu
wetu waweze kuwafundisha watoto zetu bila kubadiliwa dini yao ya Uislam na
Kanisa ambalo ndio njia lilitumia kubadili imani za watoto baada kuona
limeshindwa kuwabadili watu wazima.
Ruzuku
hiyo iliombwa kwa sababu pesa hizo ni michango ya raia wanaipa Serikali kwa
kulipa kodi mbalimbali, na Waswahili walikuwa ni walipakodi wakubwa. Hata na
hivyo Serikali ya kikoloni ilikataa kuwapa chochote Waswahili, lakini la
kushangaza ikakubali kuwapa Waprotestanti ambao pia walilalamika. Waprotestanti
walipewa ruzuku ya 50,000 F (Franka elfu khamsini) ambazo zilikuwa nyingi sana
kwa zama hizo. Hatimaye Waswahili wakapiganisha huku na kule na kupata msaada
toka kwa ndugu zao Watanganyika na kujenga shule moja ya watoto wao ambayo ni
Jumuiya (Jina la Jumuiyatul Islamiyya fii Tanganyika).
Hiyo shule
ipo hadi leo Barabara ya Nane na ya Tisa Buyenzi. Alikuja kutoka Tanganyika
Mufti Hassan bin Amir kuzindua shule
hiyo. #WazeeWetuHawakuwaWazembe Mungu
awarehemu !
No comments:
Post a Comment