Wednesday, 25 January 2017

SIKU BAADHI YA MASHEIKH WAKUBWA WA AFRIKA YA MASHARIKI WALIPOMUOMBEA DUA ABBAS SYKES


Picha na Majina kwa hisani ya Sheih Aziz wa Dar es Salaam Saigon Club
Habib Umar bin Sumayt na Habib Ahmad bin Hussayn Ibn Shaykh Abi Bakr bin Salim walipomtembelea Balozi Abbas Sykes, nyumbani kwake, Mtaa wa Shaaban Robert 1962, baada ya kuweka jiwe la msingi la Masjid Kitumbini, Dar es Salaam. 

Baadhi ya majina ya waliomo katika picha hii ni kama ifuatavyo:
1. Shareef Abdulkader al-Juinaydi (DSM),
2.al-'Allamah al-'Arif Billah Habib Ahmad bin Husayn Ibn Shaykh Abi Bakr bin Salim (znz); 3. Balozi Abbas Syks (DSM);
4. al-Allamah al-'Arif Billah Habib Umar bin Ahmad bin Sumayt (znz);
5. al-'Allamah al-Fadhil Shaykh Hassan bi 'Amier (znz) Mufti wa Tanganyika;
6. al-'Allamah Habib Hamid Mansab Ibn Shaykh Abi Bakr bin Salim (znz);
7; al-'Allamah Sayyid Ali Badawi (Lamu-znz);
8. al-'Allamah Maallim Sa'id bin Ahmad (Mombasa);
9. al-Akh Muhammad 'Alwi Bu Numay (znz);
10. al-Akh Abdulwahhab (DSM) presidant of Arab Association Tanganyika;
11. Shaykh al-Fadhil Abdulkader Ba'Abbad (DSM).
12. Shaykh Qasim bin Jum'a Darwesh (DSM).

Nyuma al-Allamah al-'Arif Billah Habib Umar bin Ahmad bin Sumayt ni Ali Mwinyi Tambwe katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika na mstari wa mbele waliochuchumaa wa tatu ni Zuberi Mtemvu.

Abbas Sykes katika ujana wake miaka ya 1950s

Balozi Abbas Sykes alipata siku moja kunihadithia kisa cha picha hii aliyopiga na masheikh wakubwa nyumbani kwake Sea View. Anasema siku hiyo ilikuwa mchana na yeye alikuwa yuko nyumbani hana hili wala lile. Mara anashtukia mlango unagongwa na Zuberi Mtemvu kasimama anamwambia kuwa amekuja na ugeni mkubwa wa masheikh wanataka kumuombea dua. Bwana Abbas anasema haraka akakimbilia chumbani kwake akavaa kanzu, koti na kofia kutoka nje kuwalaki masheikh wale na kuwakaribisha ndani. Balozi Sykes anasema ilipigwa dua nzito hapo ya kumuombea mafanikio katika kazi na maisha yake. Mwsaka ule wa 1962 anasema ndiyo kwanza alikuwa kachaguliwa na Julius Nyerere kuwa Regional Commiissioner wa kwanza Muafrika wa Jimbo la Mashariki.

Abbas Sykes na Mtemvu walikuwa watu waliokuwa wakielewana sana toka utoto wao na nyumba zao zilikuwa jirani licha ya Mtemvu kujiondoa TANU 1958 kufungua chama chake African National Congress (ANC). Abbas Sykes akiishi Mtaa wa Kipata (Sasa Mtaa wa Klesit Sykes) na Zuberi Mremvu mtaa wa Somali (Sasa Mtaa wa Omari Londo). Abbass Mremvu mtoto wa Zuberi Mtemvu kwa mama yetu Siti biti Kilungo alipozaliwa alipewa jina la Abbas na baba yake kwa heshima ya Abbas Sykes na urafiki na udugu uliokuwapo kati yao. Hii kanieleza mwenyewe Abbas Mtemvu. 

Abbas Sykes na Abbas Mtemvu
Kila ninapoiangalia picha hii hupata hisia ya siasa zilivyokuwa Dar es Salaam wakati wa kupigania uhuru na miaka michache baada ya uhuru na vipi mambo yalikuja yakabadilika. 

Katika picha hiyo kuna watu wamebeba historia ya uhuru wa Tanganyika mathalan Sheikh Hassan bin Amir, Zuberi Mtemvu, Sheikh Kassim bin Juma na Abbas Sykes mwenyewe.

Ingia hapo chini kuwasoma watu hawa:
http://www.mohammedsaid.com/2014/04/mchango-wa-mufti-sheikh-hassan-bin-amir.html
http://www.mohammedsaid.com/2016/12/zuberi-mtemvu-mpangaji-mikakati-watanu.html
http://www.mohammedsaid.com/2013/12/regional-conference-of-islam-in-eastern.html
http://www.mohammedsaid.com/2014/02/abbas-kleist-sykes.html

No comments: