Utangulizi
Kalamu ya Mh. Ally Saleh haiandiki bali inazungumza. Siku zote ninapomsoma Alberto siishi kushangazwa na uwezo wa fikra zake na jinsi anavyojua kuchagua maneno ya kutumia kumfanya msomaji asiwe anasoma bali awe anasikiliza. Ndugu msomaji msikilize Mh. Ally Saleh akieleza mauaji yaliyoitia nchi yetu katika orodha ya dunia ya wananchi ambao waliuliwa kwa dhulma kuanzia Amristar India, Sharpaville na Soweto Afrika Kusini na Zanzibar.
MS
Mh. Ally Saleh Mbunge wa Malindi |
KUMBUKUMBU YA MAUAJI YA 26 - 27 JANUARI 2001
NA ALLY SALEH
Wakati naanza kutaka kuandika kumbukumbu hizi mwili umenisimka
mara kadhaa maana katika akili yangu tukio lile halitafutka. Si kwa kuwa
niliona chochote kile kwa macho yangu, la hasha, lakini nimeona zaidi kwa akili
yangu.
Kwa sababu ya maumble
yangu kila inapofika kuripoti matukio makubwa kama hili la Januari 26 na 27 au
kuzingirwa kwa Mtendeni, au kuzama kwa MV Spice Islander, mfumo wangu wa
utendaji huwa zaidi kukaa mbali na kukusanya taarifa na kuzituma, na kutoka
mara moja kwa mahojiano ya kimkakati.
Sikuwa naamini kuwa serikali
ingechukua hatua za kuua wananchi wake waliosema na kuweka dhamira kwa sababu
ya kuandamana kwa suala la haki. Suala hilo wengi wetu tutalisimamia hadi
mwisho wa uhai wetu, na baadhi yetu maandishi yetu yataendelea kupaza sauti zetu
hata tukiwa katika makaburi yetu na mifupa yetu imeshakuwa mchanga nalo ni
kuwa: CUF iliibiwa uchaguzi mwaka 2000 kama ilivyoibiwa 1995.
Na pia tutasimamia
ukweli kuwa CUF pia wameibiwa uchaguzi 2005, 2010 na wazi kabisa 2015 na ndio
maana kumbukumbu ya mauaji ya Janurari 26 - 27 itaendelea kuwepo kwa sababu
dhulma dhidi ya umma, CUF na Maalim Seif itaendelea.
Utawambiaje kwa mfano
wananchi wa South Africa wapuuze au waisahau kumbukumbu ya Sharpvile ambao
watoto wasio na hatia waliuuwa huko na baadae Soweto? Hivi itafutika vipi jambo
kama hilo? Utakuwaje binaadamu ukilifuta hilo? Na wengine wengi katika mataifa
yao wanayo mambo kama hayo.
Asubuhi ya Januari 26
haikuwa siku ya kawaida maana tuliamka na ukimya mkubwa sana kama ishara kuwa
mauaji makubwa yatafanywa kwa sababu ya kulinda madaraka ya mtu aliyepata
ushindi usio halali na kupewa nguvu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Nikiwa nyumbani
asubuhi na mapema nilisikia risasi ya kwanza ikilia kwa kutokea upande wa
Darajani mimi nikiwa Hurumzi. Watoto wangu Abdul-razak Shau na Dorid
Alberto wakaamua kutoka kiwenda kushiriki maandamano angalau
kwa maneno yao wakarushe mawe na mimi sikuwazuia.
Siku hiyo mbali na
kuishia barabarani askari waliojihami kwa silaha za kila aina waliingia mpaka
vichochoroni ambako milango yetu mingi ilitishiwa kuvunjwa.
Basi jinsi nilivyokuwa
nimejipanga nilikuwa nikipata ripoti kila baada ya dakika tano,na kwa kuwa
mbali na BBC nilikuwa naandikia pia Reuters, basi kila nikipata ripoti mpya
nilifanya, ‘’filing,’’ ama ya kuhojiwa upya au ya kuandika new piece.
Niliandika au
nilihojiwa mara nyengine huku nalia. Baada kama nilivyosema sikushuhudia kitu
lakini ripoti nilizopata zllikuwa, ‘’so graphic,’’ hata kwa kuhadithiwa utaweza
kuona kila kitu. Waliopigwa njiani, waliopigwa msituni, walioingiliwa
nakunajisiwa majumbani, waliokimbia wakiacha watoto au kuwafungia.
Hata hivi leo hasa
Pemba, watu waliokuwa watu wazima au watoto wana hadithi za maumivu makubwa ya
kuona, kuhisi, kusikia na yaliowakuta wenyewe
Mara baada ya tukio
hllo nilihojiwa na mashirika kadhaa ya haki za binaadamu na watafiti lakini
niliitwa kutoa mhadhara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambako nililia mara
kadhaa huku nikielezea yaliojiri siku mbili ambapo, “mvua ya risasi ilinyesha.”
Na bado nikaendelea
kupata maumivu ya kisaikolojia wakati kupitia mfuko mmoja wa Kimarekani
ulipotupa fedha mimi na Salma Said kupitia Zanzibar Journalists
Association kwenda kuwashawishi wanawake wa Pemba wajitokeze kutoa ushuhuda wao
juu yaliotokea kwenye Tume ya Uchunguzi ya Hashim Mbita.
Na ubabe wangu wote
ambao najidai ninao wallahi siwezi kurudia tulioambiwa na wahanga hao, itosehe
tu nikikwambieni kuwa “it was horrible experience.”
Wanawake hao walikwenda
kwenye tume hiyo kama walivyokwenda wengine wengi wa Unguja na Pemba. Cha
kusikitisha hakuna chochote Tume ilichokiona kwa maana ya nani wakuwajibishwa
na kwa hivyo Serikali haikutoa onyo, karipio, haikushtaki mtu yeyote kuanzia
askari mkubwa wala mdogo na kabisa kuhusu wanasiasa ambao ndio waliofanya
maamuzi ya kuzima maandamano hayo.
Kwa maana kuwa hata
baada ya watu 31 kufariki kwa hesabu ya serikali, watu kwa makundi kujeruhiwa
na wengine wakipata vilema na watu 4,000 kukimbilia ukimbizi Shimoni, Kenya na
Somalia hakuna alieguswa hadi hii leo, kama kwamba hawakufa binaadamu, hapakujeruhiwa
mtu.
Hii ndio kumbukumbu
yangu ya Januari 26 na 27, 2001 na ndio maana mara nyingi hupenda kuisema ili
wengine wajue jambo hili kubwa lilopita katika nchi yetu kwa sababu ya uamuzi
wa uhuru wa kuchagua.
Na miaka kadhaa mbele
bado uhuru wa kuchagua haupo na ndio maana CUF hawaoni sababu ya kutoendelea
kutafuta mamlaka kupitia kisanduku cha kura na wanashika ule msemo kuwa kama
yaliowafika hayo kwa kutaka sauti ya kura basi sasa, “They have got nothing to
lose but their chains” yaani hawana tena cha kupoteza zaidi ya minyororo yao.
Na ndio sababu kwamba
CUF ina wanachama imara, waadilifu na wasioyumba kwa sababu wanabakia na jukumu
la kusimamia matakwa ya waliojitoa muhanga, mbali ya wengi kwa maelfu
tulioshitakiwa kwa maelfu, tunaopigwa majumbani na kwenye baraza zetu hata leo.
Eti kuna watu hujitia
upofu wa kusema, "kila kitu wao , kila siku wao," kama kwamba hawajui
yote yaliowafka watu bila ya kosa zaidi tu kuwa mwanachama au shabiki wa CUF.
Kama kupandwa mbegu ya
CUF kudai haki yao ya kutawala kupitia kisanduku cha kura basi ilipandwa
Januari 26 - 27 na dalili za kufika dhamira hiyo zimeanza kujitokeza Oktoba 25,
2015 na kutujenga imani wengi kuwa sasa siku zinahesabika.
No comments:
Post a Comment