Friday, 17 February 2017

PROF. IBRAHIM NOOR SHARIF NA AHMED RAJAB

Prof. Ibrahim Noor Sharif akizungumza, Muscat Oman 2015

Ibrahim Noor: Msanii anayeutetea Uswahili

Ahmed Rajab



PROFESA Ibrahim Noor Sharif Albakry ni msomi, msanii, na mwandishi mwenye sifa nyingi. Wengi wanamjua kwa majina yake mawili ya mwanzo na kwa vitabu vyake kadhaa kuhusu lugha na utamaduni wa Kiswahili pamoja na maandishi yake ya historia na siasa. 
Mwandishi hupata taabu anapojaribu kuandika juu yake kwa sababu huwa hajui aanzie wapi.  Hiyo ndiyo shida niliyonayo hivi sasa, hapa nilipo, na si kwamba simjui kwa sababu nimefungua macho na kuanza kumuona yeye, wazazi wake, kaka yake, mdogo wake mwenye jina moja nami na nduguye wa kike. 
Lakini hapa nilipo, vidole  vyangu vinaponiwasha vikinihimiza nianze kugonga herufi za kumchora katika insha hii, sijui nianzie wapi.  Sijui ni Ibrahim Noor gani nimwandike. 
Mtu ni huyohuyo mmoja lakini ana sura zaidi ya moja.  Kila sura yake ina mng’aro wake na kipaji chake.  Kwa ufupi, amebobea kwa mengi.
Ibrahim Noor ni miongoni mwa wale wasomi wenye utundu wa kupenda kuiogelea kila bahari ya taaluma inayowakabili.  Ameweza kuwashinda wenzake kwa sababu hakuridhika kuiogolea bahari moja; na zaidi kwa kuwa ameweza kupiga mbizi, akachota alichokichota, katika kila bahari aliyoiogolea. 
Wenye kumjua kuwa amebobea katika ustadi wa lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Waswahili pengine hawajui  kuwa Ibrahim Noor pia ni gwiji wa sanaa na wenye kumjua kuwa ni msanii wa kupigiwa mfano pengine hawajui kwamba yeye pia ni mpiga picha mahiri.  
Mwenyewe anatafahari kwamba yeye ni mwalimu, kazi aliyoifanya kwa miaka zaidi ya 54 akianzia Kenya, Marekani na sasa Oman.
Nilikutana naye Jumanne iliyopita nje ya jengo la Kituo cha Utamaduni cha Chuo Kikuu cha Sultan Qaboos, mjini Muscat, Oman.  Kama kawaida yake alikuwa na uso mkunjufu, uliodhihirisha jinsi moyo wake ulivyo nadhifu kama ilivyokuwa kanzu yake na kilemba alichopiga.   
Hakuwa yule Ibrahim Noor wa shati na suruwali niliyezoea kumuona Unguja utotoni mwangu alipokuwa juu ya baiskeli akivikata vichochoro vya Mji Mkongwe.
Mavazi yake yalizidi kuupa haiba umri wake wa miaka 75 ingawa uso wake, sijui kwa miujiza gani, unaendelea kuusitiri uzee wake.  
Ibrahim Noor alizaliwa Unguja na alianza masomo ya dini kabla hajaingia skuli.  Qur’ani alisomeshwa na bibi mmoja aliyekuwa na chuo nyuma ya iliyokuwa sinema ya Majestic, Vuga.  
Alibahatika kufundishwa mambo ya fiqhi (ya sheria za Uislamu) na mmoja wa maulamaa wakubwa wa Zanzibar, Sayyid Alawy Abdulwahab Jamali Layl.  Bwana huyu alikuwa na darsa zake katika msikiti unaosimama hadi leo nyuma ya hiyo iliyokuwa sinema ya Majestic.  
Kwa masomo ya kizungu Ibrahim Noor alisoma skuli mbalimbali za msingi Unguja mjini (Mashimoni, Gulioni, Darajani na Holmwood), Pemba (Wete) na Unguja shamba (Donge).  Kwa vile mamake alikuwa mwalimu wa skuli alikuwa akimfuata kila alipokuwa akipata uhamisho kupelekwa ama Pemba au shamba Unguja.  
Mnamo 1957 aliingia skuli ya sekondari ya mambo ya ufundi ya Seyyid Khalifa Technical Secondary School, iliyokuwa Beit el Ras na ambayo baada ya Mapinduzi ya 1964 ikiitwa Nkrumah College. Alihitimu masomo ya sekondari 1961.
Ingawa skuli yake ya sekondari ilikuwa haisomeshi somo la sanaa aliinukia kuwa na mapenzi makubwa na fani hiyo.  Alizidi kuingiwa na hamu nayo alipokuwa akimuona mzee wake mmoja, Said Aboud, aliyekuwa daktari, akichora baada ya kuwaangalia wagonjwa wake. 
Ibrahim Noor alijisomesha sanaa mwenyewe na akafanya mtihani wa kuingia Chuo Kikuu cha Makerere kuendelea na masomo ya stashada ya sanaa.  Alifuzu mtihani na 1963 akahamia Kampala kuendelea na masomo.
Alipomaliza masomo Makerere 1967 na Zanzibar kukiwa kumoto kwa utawala wake wa mabavu na uvunjwaji wa haki za binadamu, Ibrahim Noor alihamia Kenya alikopata kazi ya kusomesha sanaa katika skuli mbalimbali za Nairobi na nje ya Nairobi.
Baadaye alibahatika kupata kazi ya kuwasomesha Kiswahili Wamarekani waliokuwa wamejitolea kwenda kufanya kazi Afrika ya Mashariki.  Akisomesha New York, Marekani. Kandarasi yake ilipomalizika alipata kazi nyingine ya kusomesha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Rutgers, New Jersey, huko huko Marekani. 
Alianza kuwa mhadhiri chuoni humo 1970 na kufikia 1989 aliteuliwa awe profesa kamili.  Chuo Kikuu cha Rutgers kilimpa fursa ya kuendelea na masomo yake na pia kusomesha katika idara mbili; idara ya mitaala inayohusu Afrika na idara ya sanaa. 
Katika chuo hicho ndiko alikofanya utafiti wa kina, anaoendelea nao, kuhusu historia ya Afrika ya Mashariki pamoja na kuhusu lugha na utamaduni wa Waswahili.  
Aliendelea kusoma katika chuo hicho cha Rutgers na 1983 alitunukiwa shahada ya udaktari wa Ilimu (Ed.D) na takhasusi yake ilikuwa Ilimu ya Sanaa.
Kitabu chake “Tungo Zetu”, kilichochapishwa 1988 na Red Sea Press,  hupitiwa na wasomi wengi wenye kufanya utafiti kuhusu mashairi ya Kiswahili.
Katika fani ya sanaa, Ibrahim Noor amezipitia nyanja mbalimbali tokea ule wa uchoraji, uchongaji, uchoraji wa kutumia rangi za mafuta na za maji, sanaa ya uchoraji kwa kutumia asidi (etching).  
Mitindo ya usanii wake pia ni ya aina kwa aina. Ukija kwenye dhahania ya usasa (modernist abstraction) utamkuta yuko, ukenda kwenye sanaa asilia ya kuandika hati (herufi) kwa nakshi (calligraphy) utamkuta kajaa tele.
Jumanne ya wiki iliyopita nilikwenda Chuo Kikuu cha Sultan Qaboos nilikomkuta Ibrahim Noor ili kuangalia Maonesho yaitwayo “Oman: Pepo ya Msanii, Edeni ya Mpiga Picha”.  
Maonesho hayo, yaliyozinduliwa Februari 6 na yatayoendelea hadi Februari 16, 2017, ni ya picha za sanaa alizozichora Ibrahim Noor pamoja na alizozipiga kwa kamera.  Kwa muda wa siku kumi ameupatia ulimwengu fursa ya kuushuhudia ugwiji wake katika fani hizo mbili. 
Oman aliyoiibua Ibrahim Noor katika maonesho hayo ni Oman inayolituliza jicho kwa kuangalia jamali ya maumbile ya nchi hii.  Ameyafanya majabali, miti, anga, bahari na mabonde yawe kama yanakukonyeza yakikutaka uyapapase. 
Sifa nyingine inayojidhihirisha katika sanaa ya Ibrahim Noor ni kwamba yeye ni mtu wa mahaba.  Hili ni jambo lililo dhahiri kwa kuziangalia tu picha zake kwani unaona wazi kuwa amezipiga au amezichora baada ya kuyaangalia kwa jicho la rehema mandhari yaliyomkabili.
Kwa hakika, mwenyewe anajigamba kwamba anaweza kumsomesha kwa muda usiozidi miezi miwili na nusu mtu asiyejua hata kukamata burashi ya kuchorea akawa mchoraji hodari.  Lakini anasisitiza lazima mtu huyo kwanza awe na mambo mawili: juhudi na mapenzi ya uchoraji.
Kuna funzo kubwa ambalo nadhani msanii huyu ameazimia kuwafunza Waomani wanapoyaangalia mandhari ya nchi yao.  Nalo ni haja ya kuhifadhi mazingira yao na kuutunza urathi wao.
Ibrahim Noor si msanii wa mwanzo aliyejaribu pia kuwa mpiga picha. Kumekuwako wasanii wengi kabla yake waliojaribu kuwa wapiga picha na kumekuwako pia na wapiga picha wengi waliojaribu kuwa wasanii wa uchoraji.  Sio wote waliofanikiwa kuwa mastadi wa fani zote mbili. Ibrahim Noor ni miongoni mwa wachache waliofanikiwa.
Anaweza kuiangalia mandhari iliyojaa mkorogo wa mambo lakini akaweza kupiga picha ya yale ayatakayo tu, mengine akayaacha kando.  Kwa hivyo, akiwa anapiga picha anakuwa kama anatunga insha. 
Anapoichora mandhari fulani anaweza, akitaka, akaongeza visivyoonekana katika mandhari hiyo.  Hapo pia huwa kama anatunga insha. 
Hali kadhalika, anaweza akakuchorea pundamilia ukawaona wametulia tuli, lakini ukiondoka ulipo ukarudi hatua moja au mbili nyuma ukawaona hao punda milia kana kwamba wamo mbioni. Huuibua mwendo na kasi za hao punda milia katika miraba yao wenyewe.
Binafsi wakati wote nilipokuwa nikiziangalia picha hizo za Oman, alizozichora au kuzipiga, akili yangu yote ilivuka bahari, ikatua Zanzibar na nikawa ninaiona nchi aliyozaliwa msanii huyu ikijisikitikia kwa kuwa hainaye Ibrahim Noor.  Kilichobakia kwao ni kitovu chake tu kilichozikwa chini ya ardhi yake. 
Ni wengine wenye kufaidika na ujuzi wake, elimu yake, maarifa yake na jasho lake.  Nchi yake iliyomsomesha haikumfaidi wala haikufaidika naye.  Yote ni kwa sababu ya siasa mbovu za ubaguzi za watawala wa Zanzibar tangu 1964. 
Ibrahim Noor si Mzanzibari peke yake aliyejikuta akiutumia ujuzi wake ugenini.  Wazanzibari kama yeye wametawanyika kote duniani. 
Oman nchi iliyoanza kuinuka tangu 1970 aliposhika ufalme Sultan Qaboos bin Said bin Taimur imeweza kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kwa msaada wa maelfu ya Wazanzibari waliosomeshwa huko walikozaliwa.
Siasa za Zanzibar ya leo ni moja ya mambo yanayomchemsha Ibrahim Noor na jina lake likawa maarufu katika mitandao ya kijamii ya Wazanzibari ambamo yeye hushiriki katika mijadala mbalimbali yenye kuhusika na mustakbali wa Zanzibar.
Utotoni mwangu simkumbuki kuwa ni mtu aliyejuhusisha na siasa.  Ndipo nilipomuuliza tulipokutana tena ni lini khasa alipoanza kuzivaa siasa. Alinambia kwamba ilikuwa 1970 ingawa alianza kuziingia taratibu bila ya kishindo kikubwa katika miaka ya mwisho ya mwongo wa 1960, alipokuwa mwanafunzi Makerere.  Alianza kwa kuwa na mwamko wa uzalendo wa kitamaduni (cultural nationalism).  
Si wengi wenye kujua kwamba yeye ndiye aliyekuwa mwanafunzi wa mwanzo aliyeandika kwa Kiswahili tasnifu ya stashahada ya sanaa alipokuwa Makerere.  Tasnifu yenyewe ilihusika na mashairi ya Kiswahili
Labda sifa kubwa aliyo nayo Ibrahim Noor ni kwamba yeye ni mtu wa watu.  Kwa vile ni mtu wa watu hana budi ila awe ni mwenye kuzipigania haki zao katika nyanja mbalimbali.
Anawapigania katika uwanja wa lugha yetu ya Kiswahili, katika medani ya historia kwa kujaribu kuinyosha historia anayohisi kuwa imepotoshwa kwa kusudi na anawapigania pia katika uwanja wa siasa kwa kuzitetea haki za wanyonge.  Mote humo anapigwa vita lakini haoneshi kuchoka.

No comments: