Thursday, 2 February 2017

ZILIKUWA NYAKATI ZA CHICO, NAT KING COLE, DEAN MARTIN, SAMMY DAVIS JR, SIDNEY POITIER…UKIPENDA SAL DAVIS NA HUSSEIN SHEBE



Baada ya kusoma taazia ya Abdallah Tambaza sina nguvu ya kuandika chochote kuhusu rafiki yangu Mohamed Awadh maarufu kwa jina la Chico. Taazia ya Abdallah mimi imenitia simanzi kiasi ya machozi kunilengalenga kila ninapopita sentensi moja kwenda nyingine sababu ni kuwa Abdallah alikuwa ananitajia mambo na watu niliokuwa nawafahamu na wengine tayari wameshatangulia mbele ya haki. Nikawa kama vile watu hawa nawaona tena. Miezi kama miwili hivi nilikutana na Chico Masaki akiwa amekaa na wajukuu zake ndani ya gari. Tulisalimiana kwa bashasha sana na wala haukunipikitikia kuwa ile ndiyo itakuwa mara yetu ya mwisho kuonana. Mazikoni Kisutu nimekutana na Abdallah kisha nikamuona na ndugu yake Mwinyikhamisi yeye ni mkubwa kwangu kwa umri na aliponiona tu Mwinyikhamisi anahangaika kusimama maana alikuwa kakaa chini miguu inampa tabu. Kila nikimzuia kunisimamia yeye ndiyo anashikilia kushika mkono wangu asimame tusalimiane. Namwambia, ‘’Ka Mwinyi starehe, starehe…’’ Wapi hanisikii anailazimisha miguu yake isimame anisalimie mimi  mdogo wake. Mapenzi na heshima iliyoje mkubwa kumsimamia mdogo. Hivi ndivyo wazee wetu walivyotufunza. Allah awarehemu.

Kulia ni Mwinyikhamis, Abdallah Tambaza na Ibrahim wote hawa ni ndugu
wakiwa katika khitma ya Dar es Salaam Saigon Club
Niko katika, ''keyboard,'' sasa naandika. Msiba wa Chico umetugusa wengi khawa vijana wa Dar es Salaam. Mwinyikhamis alikuwa mchezaji mpira wa sifa katika New Port Club wakati wa ujana wake. Leo Mwinyi hawezi kusimama. Inanijia mechi moja ambayo naamini iko katika kumbukumbu ya wenzangu wengi wa wakti ule. New Port imepangiwa kucheza na Brazil, timu ya wababe watu wakorofi wa sifa mji mzima unawafahamu kwa shari yao ingawa walikuwa na mpira mzuri wa wachezaji wa kusifika. New Port, club ya vijana waungwana, wastaarabu wanaocheza soka la kupendeza. Mashabiki wanajiuliza itakuwaje mpira huu leo na wahuni wale? 

Saa kumi jangwani pamefurika. Hii ni mechi ya kikombe mfano wa ''league,'' kwa sasa. Wakati ule vilabu vya mtaani villikuwa na nguvu na uongozi thabiti wa kuweza kuchezesha mechi nzuri zilizojaza watazamaji na kuibua gumzo mji mzima. Brazili kuna Kitwana (Victor Mature) mbabe wa sifa, Mrisho (Wanted) mbabe wa sifa, Abdallah Mkwanda (Inger Johannsson), mbabe pia, Suleiman Jongo (Rory Calhoun) mchezaji mpole na muungwana sana lakini anacheza timu ya wababe, Mohamed Ndava. Shamte Kobe (Bingwa wa Mieleka na ngumi), Hamisi (Marlon Brando), Sadiki Ngwira (Kitonsa), Salum Hussein (Livingstone Madegwa) mtoto wa Sheikh Hussein Juma ana boli safi sana.  Wengi katika hawa wametangulia mbele ya haki Allah awarehemu. New Port wanajua kuwa leo wanacheza meshi muhimu na watu washari na wababe wa mji. 

New Port, akina Mwinyikhamis na wenzake wametandaza boli staili ya TPC mpira unatembea kwenye majani na wanakwepa hila zote za ubabe hakuna kukunjana mashati. Brazil imefedheheka kwa sababu mechi imeishia sare na wababe hawakuweza kutamba. Hata hivyo New Port wametoka kwenye mechi ile hoi kama wamepigana round 15 na Muhammad Ali. Brazil usiku ule ule wamewafata New Port club kwao kudai wapewe siku ya mechi ya marudiano. Wamefika New Port wamepanda baiskeli zao na kuziegesha kwa vishindo. Wanatafuta shari ile waliyoikosa uwanjani.

Uongozi wa New Port walifanya kikao cha haraka na uamuzi ukawa hawataki kurudiana na Brazil, wahuni wale na wapewe ushindi. Asubuhi taarifa zimeenea Kariakoo nzima na pembezoni kuwa ile mechi ya marudiano haitakuwapo New Port wamekataa kucheza na wametoa ushindi. Brazil wakautangazia mji kuwa New Port wamejisalimisha. Hii ilikuwa 1965 au 1966 maana nakumbuka mimi nilikuwa niko shule ya msingi.

Msomaji nimekuletea kisa hiki kirefu upate kujua Dar es Salaam aliyokulia Chico na sisi sote wa uzao ule ilikuwaje.

Chico alikuwa mmoja wa wacheazaji wa Everton Club iliyokuwa Mtaa wa Narung’ombe si mbali sana na nyumbani kwao Mtaa wa Tandamti mtaa aliokuwa akiishi Mzee Mshume Kiyate rafiki mkubwa wa Mwalimu Nyerere na mmoja katika wazee wa Baraza la Wazee wa TANU lililoongoza harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika. Mtaa huu umebadilishwa jina na kuitwa Mshume Kiyate lakini sasa takriban mwaka wa ishirini kibao cha jina la Mshume Kiyate hakijawekwa kwa sababu ambazi si tabu kuzifahamu. Sasa hii Everton baada ya mtafaruku ndiyo ilikuja kuundwa Saigon na baada ya muda na uhasama wa muda mfupi Everton ilikufa na wote wakajiunga na Dar es  Salaam Saigon hii tuijuayo hivi sasa. Turudi kwa Chico. 

Chico alikuwa akicheza kama mlinzi na namkumbuka Chico kwa uchezaji wake wa ukakamavu, staili ikiitwa ''kikiri,'' Chico akicheza, ''halfback,'' na alikuwa, ‘’hard tackler’’ mchezaji aliyekuwa akiingia kufata, ''loose ball,'' anakumba mpira na mguu wako. Navikumbuka viatu vyake vya mpira alivyokuwa akivaa – ''Adidas Admire.'' Kulikuwa siku zile na aina mbili za viatu vya Adidas, ''Adidas Admire,'' na ''Adidas La Plata.'' Maarufu ambavyo wengi tukivaa ilikuwa ni ''La Plata.'' Hivi vilikuwa na njumu yaani, ‘’studs,’’ unyayo mzima wakati, ''Admire,'' njumu zilikuwa chache na zilikuwa za kufunga na ‘’spanner.’’ Chico alikuwa kijana, ‘’special.’’ Simkumbuki kijana yoyote katika timu zetu za mitaani aliyekuwa akivaa, ''Admire.''

Ndani ya uwanja Chico alikuwa nahodha mzuri. Yuko nyuma na mbele marehemu Jumanne Masimenti, Jalala, Oshaka (Mazola), Mashaka (Alfredo Di Stefano), Juma Abeid, Ali Kodo, Maufi wanashambulia sauti ya Chico itasikika akihamasisha kwa Kiingereza kisafi kilichonyooka mpira upelekwe goli la adui. Utasikia akipiga kelele, ‘’Push the ball forward,’’ ‘’Score,’’ au ‘’On him,’’ yaani asiachiwe mpira adui. Inawezekana hapo anamuhimiza Ahmada Digila (Danny Blachflour) au Khalid Fadhil (George Young) wapeleke mpira mbele. Chico uongozi na ukamanda alianza toka utoto hakuanzia katika Jeshi la Polisi. Kwa kweli tulikuwa tukisikia sauti hii mori ulikuwa unapanda na hakika tukiongeza juhudi katika kushambulia au kulinda goli. Huyu Ahmada alikuwa umri wangu. Yeye ni mtoto wa Sheikh Digila wa Mtaa wa Nyamwezi nyumba yake ilikuwa karibu na msikiti wa Makonde. Ahmada alipata elimu kubwa sana ya dini. Ahmada alikuwa na kasi ya ajabu katika kusoma Qur’an. Kwenye khitma yeye anawea kukumalizia juzuu hata tatu wewe moja hujakamilisha. Alikuwa ''midfielder,'' hodari katika vijana wa Saigon pamoja na Hassan (Gilbert Mahinya). Hassan Gilbert baadae alikuwa kuwa mtaalamu wa, ''Systems,'' katika moja ya mashirika ya umma na siku tulipokutana Mlimani City akiwa na mabinti zake wakubwa waliojipamba kwa hijab alinifahamisha kuwa amestaafu kazi baada ya kufikisha miaka 60. Nilpomfahamisha kuwa nami nami pia nishapumzika akanambia taarifa zangu anazo kwani alikuwa akinifuatilia huko Tanga nilipokuwa nafanyakazi. Nilifarajika kusikia hayo kuwa hata baada ya miaka ya kutengana wana Saigon walikuwa wakitaka kujua nani yuko wapi na anafanya nini.

Hivi ninavyoandika ni kama vile najiona niko Mnazi Mmoja tunafanya mazoezi na wakati mwingine tukijifunza kuachiana pasi za haraka za kuwazuga maadui. Namuona Ghalib Hamza, maarufu kwa jina la Guy. Chico juu ya ushujaa wake wa kuwakumba washambuliaji hathubutu kumfata Guy akiwa na mpira. Guy alikuwa hana kimo, mfupi lakini ana maungo kiasi. Kilichokuwa kikitutisha kwa Guy ni ile, ‘’ball control,’’ yake na ‘’dribbling skills,’’ angeweza kumzunguka Chico na hata kumtia harusi, yaani kupitisha mpira katikati ya miguu yake. Kulikuwa na Mohamed Ramadhani Kondo (Garincha), Rashid Vava mchezaji rafu club nzima tukimuogopa.  Wote wenzetu hawa wametangulia mbele ya haki. Naamini wasomaji vijana watapata tabu sana kuelewa haya majina niliyoyataja, hizi ''nicknames za akina Mazola, Di Stefano, Blanchflour. Hawa walikuwa katika wakati wetu wa miaka ya 1960 ndiyo wachezaji mpira maarufu wa vilabu tofauti vya Ulaya.

Chico alikuwa na baiskeli yake, ‘’sports’’ nyuma aliiandika, ‘’Thunderbird’’ na mwenyewe akiita baiskeli yake kwa jina hilo. Alikuwa anaipanda kwenda shule kavaa vizuri sana na kichwani kavaa, ‘’baseball cap.’’ Amechomekea shati lake jeupe alilolivalia T Shirt nyeupe ndani ndani na kiunoni amevaa, ‘’army belt.’’ Hii ilikuwa mikanda myeupe ya ‘’canvass,’’ yenye, ''buckle,'' ya fedha  au ''gold,'' inayong’aa. Mmarekani amekwishakazi. Vijana wote tuliokuwa tukijiona, ‘’fashionable,’’ tukivaa hivyo lakini Chico mwenzetu alitushinda kwa kuwa ilikuwa kama vile mambo yale yako katika damu yake. 

Nakikumbuka vyema chumba chake pale kwao. Kilikuwa nadhifu na alikuwa na ‘’record player,’’ yake na sahani za santuri nyingi za nyimbo mbalimbali za wanamuziki wa zama zile. Sasa hapo ndipo utakapotambua kuwa Chico alikuwa, ‘’special.’’ Mimi nilikuwa na ‘’record player,’’ yangu, ‘’Dansette,’’ imetengenezwa Uingereza, Sussex, nakumbuka ile label. Chico santuri zake zilikuwa ni Nat King Cole, Ray Charles, Dean Martin na wanamuziki mfano wa hao kama Sammy Davis na wengine. Muziki mgeni kwa wengi kwa wakati ule. Nyimbo alizokuwa akizipenda na akaniambukiza na mimi kuzipenda ni, ‘’Ramblin Rose,’’ na ‘’The Good Times,’’  zote za Nat King Cole. Hadi leo kila nikizisikia nyimbo hizi huwa nakumbuka utoto wetu katika mitaa ya Kariakoo.



Kushoto mstari wa mbele Hussein Shebe, Henin Seif, kulia wa pili ni Raymond Chihota, Hussein,
(pass) Mbaraka ''Bata'' picha ilipigwa mapema 1960

Miaka ya 1960 ilikuwa miaka ya patashika si Dar es Salaam tu bali dunia nzima na ndiyo maana Waingereza wakaipa jina miaka hiyo kuwa ni, ‘’Roaring 60s.’’ Dar es Salaam ilikuwa na mastaa wake wakivuma kama Hussein Shebe, Raymond Chihota na Henin Seif kuwataja wachache  katika Chipukizi Club, timu ya waimbaji vijana wakipigiwa muziki na The Blue Diamonds,  ''band,'' ya vikana wa Kigoa. Kulikuwa na Sammy Davis Jr Salim Hirizi akiimba nyimbo maarufu, ''Summer Time,'' kwa umahiri mkubwa.  Katika hawa waimbaji kubwa lao alikuwa Sal Davis. Siku Sal Davis alipokuja na Hussein Shebe Mtaa wa Tandamti kuwaamkia wazee wake Hussein nyumbani kwa kina Mohamed Jaggan ilikuwa gumzo la mtaa mzima na sisi ambao hatukuwapo kumuona Sal Davis tulisikitika sana. Uhuru wa Tanganyika uliingiza katika nchi mambo mengi kutoka Ulaya yaliyotuvutia sisi vijana. Huu ulikuwa wakati wa wazimu wa mambo mengi sana kutoka Marekani na Ulaya. Sote tukisukumwa na ujana tulikumbwa na wimbi hili. Haya ndiyo yalikuwa maisha ya sisi vijana katika Dar es Salaam ya miaka ile ya 1960 na Chico hakuweza kuliepuka wimbi hili kama vijana wengi walivyoshindwa.


Salum ''Sammy Davis Jr'' Hirizi kama alivyo hivi sasa

Sal Davis Katika Onyesho Ujerumani 1960s

Ilikuwa Chico ndiyo, ‘’alinijulisha,’’ mimi kwa Sidney Poitier na nikaanza kuingia kila senema yake ilipokuja mjini. Sidney Poitier katika miaka ile hakuwa maarufu kwa vijana wengi wa Dar es Salaam. Wengi wetu tulikuwa na John Wayne, Richard Widmark, Alan Ladd, Victor Mature, Marlon Brando na mfano wa hao na wala haikutupitikia kuwa tunaweza kwenda senema Empire, Avalon, Empress au Chox kuangalia senema, ‘’actor,’’ Mnegro kama Sidney Poitier au Jim Brown. Chico alikuwa, ‘’special,’’ yeye akimjua Sidney Poitier, Eartha Kitt na wengineo siku nyingi sana. Kuanzia hapo na mimi nikabadilika. Nakumbuka senema za Sidney Poitier alizokuwa akipenda kunihadithia kama ni kama ''Lilies of the Fied,’’ ‘’A Patch of Blue,’’ na nyingine nyingi.

Image result


Ujana haukawii kukimbia. Haukupita muda tukakua na ikawa lazima tukubali kuwa wakati wa mchezo umepita tunaingia ukubwani. Chico alitushangaza wengi alipojiunga na Jeshi la Polisi kwani si katika kazi ambazo, ‘’watoto wa mjini,’’ tulizipenda na kubwa ni kuwa kazi ya jeshi ilikuwa inahitaji kufanyakazi nje ya Dar es Salaam na wengi wakiona dhiki kuondoka mjini. Sasa hapa ndipo ninapotaka kuhitimisha kuwa Chico alikuwa, kwa kweli na kwa hakika kabisa alikuwa ‘’special.’’ 

Chico alijiunga na Jeshi la Polisi na aliitumikia nchi yake kwa uadilifu mkubwa. Alifanyakazi takriban kila mahali na kuacha jina lililotukuka. MIaka mingi baada ya sisi kutoweka hapa duniani, itakapokujaandikwa historia ya watoto wa Dar es Salaam na nini wamefanya katika taifa hili nina hakika Kamanda Chico jina lake litakuwa juu. 

Allah amlaze pema ndugu yetu Mohamed Awadh Saiwaad maarufu kwa jina la Chico aliloishi nalo utotoni hadi ukubwani. 

Mwandishi akiwa Viwanja Vya Mnazi Mmoja ambako Everton na kisha Saigon
walikokuwa wakicheza mpira. Nyuma ni barabara iliykuja kupewa jina la Bi. Titi 
Mohamed na ukivuka barabara hiyo ni Soko la Kisutu maarufu kwa jina la Soko 
Mjinga. Picha ilipigwa 1966

No comments: