Wednesday, 1 February 2017

BURIANI MWANA WA KARIAKOO KAMANDA MOHAMED ''CHICO'' AWADH NA ALHAAJ ABDALLAH TAMBAZA

Buriani Alhaaj Kamanda Chico
Na Alhaaj Abdallah Tambaza

JUA limekuchwa baada ya sala ya alasiri jijini Dar.

Waombolezaji mamia kwa mamia, wamejibanza chini ya vivuli vya miti ya miarobani iliyotapakaa kila upande wa makaburi haya ya Kisutu jirani kabisa na mabweni ya Chuo cha Biashara- CBE.

Kwenye vipaza sauti, ilisikika surat Yaasin, ikisomwa kwa pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu; ikafuatiwa na tarumbeta pamoja na milio ya bunduki yenye kupasua roho kwa mshindo wake mkubwa—puu…puu…puu!! 

Hivyo ndivyo alivyozikwa, Jumapili ya Januari 22, mwaka huu, kipenzi chetu, ndugu yetu, rafiki yetu, kamanda wetu na mwana Dar es Salaam kindakindaki; (mstaafu) Kamishna wa Polisi Msaidizi Mwandamizi (SACP), Alhaaj Dk. Mohammed Chico.

Kamanda Chico alifariki saa 7:00 usiku wa Jumamosi, Januari 21, 2017 na mara kulipokucha habari za msiba zikatapakaa kote nchini kwa kasi ya ajabu kabisa.

Wa kwanza kunishitua alikuwa ni Mzee Shamas Akil, kutoka maeneo ya Kigamboni aliyenipigia simu saa 12:00 asubuhi kabla hakujapambazuka sawasawa na kunipa kile alichokiita, ‘habari za mjini’.

“Abdallah eh! Ndugu yetu Chico ametutoka… sikuweza kulala tena tokea nipate habari hizi saa 8:00 usiku jana… tutafahamishana mipango ya mazishi In Shaa Allah,” alisema Ali Kobe (Kocha) rafiki wa karibu wa hayati Kamanda Chico.

Mussa Shaggow, ni Mweka Hazina wa Klabu ya Saigon, klabu ambayo hayati Dk. Chico pia ni mwanachama. Naye Nilipompigia simu kufahamu taratibu za mazishi alisema:

“…Nimefadhaishwa sana na kifo hiki… ni juzi tu mimi na wenzangu tulikwenda kumjulia hali baada ya kuwa kitandani kwa muda mrefu sana…msiba uko kwake Kijitonyama lakini sala ya jeneza itafanyika Msikiti wa Manyema kabla ya alasiri leo,”alinifahamisha.

Alhaaj Kamanda Chico, kama ilivyo kwangu mimi, alizaliwa na kukulia jijini Dar es Salaam maeneo ya Kariakoo na kupata elimu yake ya awali pale AgaKhan School, Upanga (sasa Shule ya Msingi Muhimbili).

Baadaye alijiunga kwa masomo ya Sekondari ya Shaaban Robert ya jijini Dar es Salaam pia. Alijiunga kwa mara ya kwanza na Jeshi la Polisi kitengo cha Marine kule Kigamboni akianzia ngazi za chini kabisa. Alijiendeleza mpaka kuwa na degree ya uzamivu (Phd) akiwa kwenye utumishi polisi.

Nimemfahamu almarhum Kamanda Chico yapata nusu karne sasa, tokea tulipojuana mara ya kwanza kwenye madrassa ya Maalim Mzinga & Sons pale kona ya Mafia na Sikukuu, Dsm tulikopelekwa na wazazi wetu kuanza kusoma elimu ya msingi ya Dini ya Kiislamu tukiwa vijana wadogo chekechea.

Chuo Cha Maalim Mzinga kama kilivyo hivi sasa Mtaa wa Mafia na Sikukuu
Haraka haraka, Chico na mimi tukawa marafiki kwa sababu sote tulikuwa tukienda pale madrassani tukiwa na baiskeli zetu ambazo tulikuwa tukiendesha kwa pamoja kwenye mitaa ya Kariakoo wakati wa kutoka chuoni, tukikimbizana na kufurahi pamoja tukila embe mbichi zenye pilipili tulizonunua kwa mzee maarufu wakati huo Mzee Melabon.

Kutokana na utundu na ubunifu wake aliouonyesha kutoka utotoni, Kamanda Chico, akiwa na umri mdogo sana aliweza kuandika kwa ustadi mkubwa jina lake M.A. Saiwaad, pembezoni mwa baiskeli yake kuonyesha umiliki wake.

Nilivutiwa sana na maandishi yale, nami harakaharaka nikamwomba aniandike jina langu A. Mohammed, kwenye baskeli ya kwangu ili twende sawa. 

 Mohammed Awadh Saiwaad, ndiyo jina halisi la almarhum Dk. Chico. Ili kumjua vizuri makuzi yake ni lazima msomaji uwe na uelewa mzuri kwanza wa Jiji la Dsm.

Wakati huo, mji wa Dsm ulijengeka kutoka Gerezani; Mission Qrts (maeneo ambayo watu wa dini ya Kikristo walipenda kuishi); Kariakoo, Kisutu, Mwembetogwa – sasa Faya –; Ilala na Magomeni Mapipa.

Watu wa wakati huo walikuwa wakipenda mpira, muziki, senema, siasa na mambo ya namna hiyo. Wale waliopenda sana kucheza mpira walijipachika majina ya wachezaji mashuhuri wa wakati huo (role models) wa hapa nyumbani ama nje. Majina yao hayo ya kujipachika (nicknames) au kupewa na marafiki, yamebaki kuwa sehemu ya utambulisho wao mpaka leo.

Kwenye siasa, yupo mzee wetu Mzee Kissinger pale mtaa wa Kongo, ambaye jina lake hasa ni Mzee Shekue, lakini watu hawalijui jina hilo ila wamelizoea lile alilopewa la waziri wa zamani wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Dk. Henry Kissinger, lilotokana na umahiri wake wa kujenga hoja.
Mzee Kissinger
Jina halisi Shekue

Kwenye soka, walikuwapo waliojiita kina Peter Oronge kutoka Kenya (Mwinyi Mussa), Springet golikipa wa England (Kitwana Juma), Mnyika wa Tabora (Rashid Mohammed), Dennis Law England (Jamil Hizam), Mussa Shaggow kutoka Unguja (Alhaaj Mussa Mohammed Khamis wa Saigon).

Klabu ya Sunderland (sasa Simba) wakati huo alikuwapo winga machachari akiitwa Salim Ali ‘Jinni’. Alipewa jina hili kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuruka juu kupiga vichwa mipira ya kona. Kwa ustadi ule watu walimfananisha na jinni.

Hayati Kamanda Chico, yeye tokea udogo wake akipenda sana ukakamavu na ubabe  wa Kimarekani. ‘Miondoko’ na mavazi yake kwa jumla yaliendana na mila na desturi za kimarekani.
Hiyo, ukichanganya na Kimombo kizuri alichokuwa akizungumza, alikuwa amekamilika. Jina likawa limetua mahala pake hasa. Ilikuwa ni kutokana na Wamarekani wa Kihispaniola (Spanish Americans), ndani ya senema zile za kizungu, majina ya Chico ndiko yakisikika.

Sheikh Hamid Jongo, ni Kadhi wa Mkoa wa Dsm na Imam Mkuu wa Msikiti wa Manyema hapa jijini. Akitoa wasifu kabla ya sala ya jeneza siku ile ya Jumapili ya msiba, alimwelezea marehemu kama mmoja wa watu wanaounda kikundi cha Ashabi L’yamini, kilichosheheni waumini wa Msikiti wa Manyema.
Sheikh Hamid Jongo
Picha ya 1988
Alimwelezea  Alhaaj Dk. Mohammed Chico namna alivyoweza kuishi, kusaidia, kujichanganya, kujumuika na kutoa michango mbalimbali katika jamii alimoishi kila alipokwenda kikazi na hapa Dsm kwao.

“…kila watu wana vijiwe vyao; Kamanda Chico naye alikuwa na cha kwake kilichojulikana kama Ashabi L’yamini ambacho kilikuwa na kawaida ya kufanya dua na kuombeana kheri pale nyumbani kwangu Tandika wiki mara moja…

“ Kwa mapenzi yake Kamanda Chico alipendekeza mkusanyiko ule uwe unahamahama kwenda nyumba nyingine pia na basi ikawa hivyo…mara nyingi ikawa inafanyika kwake Kijitonyama, ”Sheikh Jongo alisema.

Kwa hiyo msomaji, ili kufahamu vizuri hali ya maisha ya watu wa Dsm zama hizo ni lazima kwanza uelewe mazingira yake na vitu vilivyokuwa vinawaunganisha wakazi hata wakawa wakijuana na kupendana tofauti na ilivyo sasa—jirani yako nyumba ya pili humjui!

Eneo la Kisutu ndiko mwandishi huyu alikozaliwa na kwamba ndiko kulikokuwa na kitovu cha Dsm na watu wake. Kisutu kulikuwa na barabara moja tu kuu ikijulikana kama Wadigo street.
Nyumba yetu sisi ilikuwa hapo. Pamoja na watu wengine mashuhuri walioishi Digo street ni mpigania Uhuru maarufu Mzee Haidar Mwinyimvua. Huyu ndiye baba mzazi wa Sheikh Ahmed Haidar, Imam Mkuu wa Masjid Mwinyikheir pale, Kisutu Akiba.

Wengine ni babu yake marehemu Chiko Mzee Mohammed Mshihiri, aliyekuwa anaishi nyumba ya nne hivi kutoka kwetu yeye na mmoja wa wake zake, Bibi bint Said. Mzee Mohammed Mshihiri alimiliki (landlord) nyumba kadhaa jijini Dsm.

Wadigo street ilikuwa mita kama 10 hivi kutoka uzio wa makaburi ya Kisutu eneo ambalo lilizungukwa na miti mingi ya mivinje. Mwisho wa barabara kulikuwa na madrassa maarufu ya Sheikh Goma walikosoma wengi wa wakazi wa eneo hilo.

Watoto wa Mzee Mohammed Saiwaad (Mshihiri) ni Awadh, Said, Hemed na Abeid. Awadh Mohammed (babake  Chico), huyu alikuwa akifanya kazi sokoni Kariakoo akiwa agent mkubwa wa samaki wabichi kutoka Bagamoyo, Kunduchi, Mbweni, Ununio na Kigamboni.

Biashara hiyo ilimpa umaarufu na kumfanya awe na uwezo mkubwa kifedha akimiliki, pamoja na mambo mengine, nyumba kadhaa maeneo mbalimbali jijini.

Mzee Issa Aussi, yeye  ni mmoja wa wazee wakongwe wa jiji la kwetu la Dar es Salaam. Nilikutana naye na kuongozana naye kutoka makaburi ya Kisutu baada ya mazishi ya Dk. Chico. Nikataka kujua alimjuaje babake marehemu Mzee Awadh Mohammed?

“… Ah! Sipati kukwambia… alikuwa mtu mwema na mkarimu sana kupita kiasi…

“ Kwa kweli alinifanya niache kwenda kwake kununua samaki pale sokoni Kariakoo … kwa sababu kila mara alikuwa akinipa samaki bure… alikataa pesa kutoka kwangu;

“…Kutokana na namna watu walivyojuana na kupendana mzee yule alikuwa akiona picha ya babaangu mbele yake hivyo akawa anashindwa kuchukua pesa zile…

“…Sasa nikaona nitakuwa namtia hasara hivyo nikawa siendi kununua samaki kwake, badala yake nikituma mtu,”alisema kwa mshangao mkubwa Mzee Issa.

Kulia: Ally Sykes, Issa Ausi, Sheikh Ayub na Juma ''Spencer'' Abeid

Mzee Awadh Mohammed, alimudu kumsomesha mtoto wake Chico katika shule ya AgaKhan Dsm. Wakati ule wa ukoloni shule hiyo wakisoma watoto wa watu wenye uwezo, kipato na majina makubwa (elites) hasa wahindi wenyewe na Waarabu.

Kamanda Chico alisomea huko na hivyo kuwa na uwezo mkubwa sana wa kuzungumza lugha ya Kiingereza kwa ufasaha na madoido mingi tokea utotoni; tofauti kabisa na zile shule zetu sisi za ‘Kikayumbakayumba’ za Mchikichini na Mnazi Mmoja.

Sasa, kila mara ninapokumbuka (retrospect) hali hii, siachi kuichukia serikali dhalimu ya Kifalme ya Uingereza iliyokuja hapa kwa kisingizio cha kueneza umissionari kupitia kanisa lao la Ki-Anglikana (Mfalme wa Uingereza ndiye mkuu wa Kanisa la Anglikana duniani), ikawa imefanya ubaguzi wa namna ile katika utoaji huduma muhimu, ikiwamo elimu, afya na makazi.

Msomaji hebu zingatia, hapakuwapo na hospitali yoyote jijini Dsm kwa watu weusi (Muhimbili ilijengwa 1957) hadi pale zilipojengwa hospitali ndogo tatu (Magomeni, Ilala, Mnazi Mmoja) kwa msaada kutoka Ireland. Wazungu wakitibiwa European Hospital (sasa Ocean Road); wahindi Hindu Mandal, Burhani na AgaKhan Hospital.

Waafrika walitibiwa kwenye hospitali ndogo na mbaya tu; iliyojengwa na mhindi  mmoja Khoja kutoka Bagamoyo aliyekuwa karibu na waafrika. Sewa Haji Hospital, ilikuwa pale karibu na Kituo cha Kati cha Polisi (Central). Tiba hapo sana sana ni kufunga vidonda, kucheki kifua kikuu (msiwaambukize watawala) nk. Magonjwa mengine yote ni kufa huku unajiona.

Kuhusu elimu, shukrani nyingi ziwaendee walimu wale wa madrassa ya Maalim Mzinga & Sons na Al Hasnain Muslim School ya kina marehemu baba zake Sheikh Yahaya, Sheikh Hassan na Hussein Juma ndugu wawili mapacha kwa jitihada kubwa walizozichukua madrassani kwao, kurekebisha ile tofauti kwa kutoa elimu ya ziada ya kisekula katika masomo ya hesabu, kuandika na kusoma Kiingereza.

Kushoto Sheikh Hassan Juma na kulia ni pacha mwenzake Sheikh Hussein Juma

Elimu hii ya ziada ikatufanya sisi tuliokuwa tunasoma Mnazi Mmoja na Mchikichini kuwa na uwezo sawa au zaidi na wale wenzetu wengine na hivyo kufaulu katika viwango vya juu katika elimu na kwenye ajira, wakati na baada ya Mwingereza kuondoka.

Mtoto wa pili wa (Babu Chico) Mzee Mshihiri ni Said Saiwaad. Mzee Said Saiwaad alipata elimu yake pamoja na hayati babangu Mzee Mohammed Swaleh Tambaza katika Kitchwele Govt. School jijini Dsm, na baadaye wawili hao walijiunga na Shirika la Reli la Afrika Mashariki.

Ingawa babangu alikuja kuacha kazi Railways mapema, baada ya kutukanana na mzungu wakati huo wa ukoloni, Said Saiwaad yeye aliendelea hadi kufikia ngazi za juu kabisa katika shirika hilo kubwa la treni katika Afrika Mashariki.

Mwandishi huyu wakati akijiunga na Chuo Cha Usafiri na Usalama wa Anga (East African School of Aviation,  pale Wilson Airport, Nairobi, mwaka 1973, alimkuta marehemu Mzee Said Saiwaad akiwa na cheo cha Afisa Mkuu Ugavi wa Shirika la Reli Afrika Mashariki Ukanda wa Kenya (District Supplies Officer Railways -Kenya Region). Wakati ule tukiwa badobado kielimu; cheo kama hicho ni cha wazungu tu.

Mzee Said Saiwaad na mkewe Bi. Ajuza pamoja na watoto wao Abdallah, Omar, Safia, Nuru na Eshe walikuwa wakiishi eneo mashuhuri kabisa kule Lavington, Nairobi. Kila mara, nafasi ilipopatikana mwishoni mwa juma niliwatembelea kwao tukala na kunywa pamoja tukikumbuka nyumbani.

Baba mwingine mdogo wa Alhaaj Kamanda Chiko ni Hemed Saiwaad, aliyekuwa agent wa soda na muuza barafu kwa wingi jijini Dsm na vitongoji vyake; na wa mwisho Mzee Abeid yeye alikuwa msanii wa michezo ya kuigiza kwenye runinga na redio nyumba yake ilikuwa pale mtaa Rufiji Kariakoo karibu na hospitali ya Dk. Juma Mambo.

Tarika ya Dandarawi (kikundi cha kufanya dua za pamoja, dhikri mbalimbali na kumwomba Mwenyezi Mungu ina makao yake pale Msikiti wa Ijumaa Kitumbini, Dsm. Hii ni moja ya tarika kongwe jijini iliyoongozwa kwa kipindi kirefu na Almarhum Sherrif Juneid Imam Mkuu wakati ule.

Hayati Dk. Chico alikuwamo humu akifuata nyayo za waliomtangulia kwenye familia yao ambao wote walikuwamo kwenye Dandarawi. Kwa namna moja ama nyengine, tarika hii inafanana na ile ya Shaddhilly ya Sheikh Nurdin Hussein. 

Familia nyingine ambayo ni wafuasi wazuri wa Dandarawi ni ile ya Hayati Abdulwahid na Ali Sykes. Wengine ni Sheikh Muharram Swaleh Kitembe (babake Sheikh Mahdi) na Sheikh Haidar Mwinyimvua wa Kisutu na wanawe wote.

Kwa makusudi nimeelezea habari hizi za tarika ya dandarawi na Ashabi Lyamini, katika muktadha huu wa maisha ya Kamanda Chico ili kuonyesha ni kwa kiasi gani zimeweza kumbadilisha na kumjenga kiroho na kuwa mtu bora wa namna yake. Kule polisi Kamanda Chico alianzia ngazi ya kuruta wa kawaida jeshini hadi kuweza kufikia ngazi za juu kabisa za uongozi.

Kuelezea maisha na nyakati za Almarhum Dk. Chico ni safari ndefu. Huwezi hata ukijitahidi vipi kuyamaliza na kuyaelezea kwa ukamilifu wake yale mwanajamii huyu aliyoyaishi katika uhai wake – ni mengi mno!

Katika safari yake ya kikazi alipata kushika wadhifa wa RPC –Kamanda wa Polisi wa mikoa ya Kilimanjaro na Morogoro kwa muda mrefu. Kote huko alikopita ameacha athari ya uongozi uliotukuka. 

Marehemu Kamanda Chico alikuwepo kama mwanachama pale kwenye klabu maarufu ya Saigon tokea miaka ya mwanzo ya 60 hivi akitokea klabu yake ya mtaani ya Everton alikokuwa akicheza mpira pamoja na watoto wenzake akina Suleiman Jongo (mchezaji wa zamani wa Yanga), Jumanne Macimenti (Simba) na Ahmada Digilla.

Almarhum Chico amefanya mambo mengi katika kudumisha udugu wa wana Saigon hata pale alipokuwa nje ya Dsm kwenye transfer za kikazi, basi roho na akili yake ilikuwa pamoja na wenziwe.

Daima, kila palipofanyika hafla pale klabu utamwona hayati Chico—akiwa na kofia yake ya tarbush kichwani— akiwa mstari wa mbele akifanya hili ama lile, iwe kwenye kufuturisha ama Khitma za kurehemu waliotangulia, na bila shaka yeyote, kama ilivyo ada, jina la Dk. Mohammed Chico litakuwa miongoni mwa watakaorehemewa mwaka huu. 

Saigon ni kiungo muhimu kwa wakazi na wenyeji wa Dsm ikiwa haitofautishi dini, siasa ama Simba au Yanga. Pale utakuta watu wakijinasibisha na U-daresalama wao tu. Hali iliyofanya kuwa kimbilio la walio wengi.

Daima tutakukumbuka shujaa wetu na kamanda wetu, sisi nduguzo wazawa wa Dar es Salaam kwa kuonyesha mfano wa kuigwa kwa kujitoa muhanga kuchagua kulitumikia Jeshi la Polisi wakati vijana wengi wakiwa hawapendi kufanya kazi hivyo.

Msomaji hebu fikiri kama watu wote wangekataa kuwa mapolisi hali ya usalama kwa raia ingekuwaje? Ni kazi ya wito ambayo wale tu wenye moyo wa uzalendo wa kweli hupenda kuifanya ili amani na utulivu upatikane kwa watu wengine.

Kule Ulaya na Marekani, kama kijana atajitolea kuwa jeshini, basi familia anayotoka na jamii anamoishi kwa ujumla hujivunia mtu huyo. Picha zake akiwa kwenye uniform zake daima huwa zinaning’inia kwenye kuta za sebule kwenye nyumba za jamaa zake.

Kamanda Chico alikuwa na fursa nzuri ya kujiunga na biashara kutokana na uwezo wa kifedha ambao familia yake imeuonyesha tokea awali; ukiongeza na elimu yake aliyokuwa nayo angeweza kuwa mtu yeyote yule mwengine lakini alichagua kufanya hii kazi ya kijamii pamoja na misukosuko yake.

Kamanda Chiko amemwacha mkewe Bi. Barke, watoto wanne na wajukuu watano. Mtoto wake mkubwa SP Awadhi Chico, amefuata nyayo za babake, kwani amekuwako Jeshini Polisi siku nyingi na sasa ni Deputy Regional Crimes Officer Ilala Region.   

Tunamwomba Allah (sw) amghufirie madhambi yake na pepo ya firdaus iwe makazi yake.
Inna Lillah Waina Illayhi Rajiuun!
Simu: 0715808864/ 0628985862
Kushoto: Sheikh Manzi, Chico, Sheikh Ali


Kulia Mwinyikhamisi, Abdallah Mohamed Tambaza na Ibrahim



No comments: