Wednesday, 8 March 2017

ALIKOTOKA PROF. LIPUMBA NA CUF 1995 - 2017



Huo hapo juu nii ukurasa mmoja kutoka shajara yangu ya mwaka wa 1995. In Shaa Allah tutarejea katika niliyoandika katika ukurusa huo miaka 22 iliyopita. Kwa sasa hebu tuangalia haiba ya siasa ya Prof. Lipumba ambae ndiye niliyemuandika katika ukurusa huo.

Nasoma katika mitandao ya kijamii kuwa Prof. Lipumba amekwenda Tanga na amepigwa pande na wananchi wa Tanga kiasi kuwa msafara wake unasindikizwa na ‘’convoy,’’ kubwa ya askari wenye silaha akapita Tanga wima kuelekea Pangani kufanya mkutano wake. 

Wanasema siku moja ni nyingi katika siasa sembuse miaka 22. 

Kuanzia mwaka wa 1995 hadi kufika leo mwaka wa 2017 miaka 22 imepita na kwa hakika ni miaka mingi kwa  Prof. Lipumba kiasi ya kuwa hapa nilipo nikiangalia nyuma najihisi kama Rip Van Winkle aliyelala miaka takriban 20 na  siku alipoamka akakuta kila kitu katika mji wake kimebadilika. 

Naamini Prof. Lipumba na yeye hakuwa mbali na fikra hizi nilizokuwanazo mimi kuwa imekuwaje hali ya siasa ikambadilikia kiasi hiki kuwa inahitaji nguvu za ziada kumuingiza Tanga wakati alikuwa akiingia Tanga na kutoka apendavyo na kupokewa na maelfu ya wananchi. 

Hakuna asiyejua kuwa alikuwa Prof. Lipumba ndiye aliyeitia nguvu CUF Tanga na Tanzania Bara kwa ujumla.

Sasa turudi katika ukurasa wangu wa shajara ambao picha yake iko hapo juu.

Ilikuwa Jumatano tarehe 18 Oktoba 1995 tuko katika harakati za Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi Tanzania. 

CUF mgombea wake wa urais Tanzania Bara ni Prof. Ibrahim Haruna Lipumba kijana msomi wa uchumi wa Princeton University Marekani. 

Vipi ghafla aliingia katika siasa kipindi kile ni kisa cha kujitegemea na iko siku In Shaa Allah tutakieleza. 

Siku hii ya Jumatano Oktoba 1995 katika shajara yangu niliandika maneno haya ambayo kwa wanaojua Kiingereza watayasoma hapo juu. 

Leo nikiangalia nyuma nashindwa kupata jibu ni kitu gani kilichonifanya mimi niwe naandika kwa Kiingereza badala ya lugha yangu Kiswahili. 

Tafsiri ya  maneno hayo ni hii hapo chini:

‘’Nimeondoka na basi. Nilipanga kwenda hadi Segera na kutoea hapo nipande basi linalotoka Dar es Salaam kwenda Tanga. Lakini tulipokuwa Korogwe, nikaona, ‘’convoy,’’ yetu ya kampeni inaingia Korogwe kwa hiyo nikashuka pale. Tulifanya mkutano hapo na baada ya mkutano nikaondoka na Tamim na Kassim katika Musso kuelekea Tanga. Prof. Lipumba alifanya mikutano miwili Muheza na Pangani.

Tulikusudia kutafuta mahali pa kuificha gari yetu. Tulipanga Rose Inn. CUF Tanga ina nguvu kubwa. Tulifanya mkutano mkubwa sana. Lipumba alinambia mkutano huu ulikuwa mkubwa kupita yote. 

Kushoto Prof. Lipumba, Shekue, Mama Ummy na aliyekuwa pembeni yake
ni binti yake Ummy

Kushoto Juma Duni Haji, Prof. Lipumba nyumbani kwa Mama Ummy Anzuani
ilipofanyika tafrija baada ya mkutano

Baada ya mkutano tulialikwa kwa Mama Ummy kwa chakula nk. Sikuweza kuamini macho yangu. Ule msafara na umma wa watu waliozunguka ile nyumba wakiimba wakati sisi tukiwa ndani tukikirimiwa. 

Nilipiga picha nyingi.

Mariam Shamte wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC akaja kuwahoji Juma Duni Haji na Prof. Lipumba. Jioni tulifanya mkutano na wazee kisha na wafanyabiashara.’’

Mariam Shamte wa Idhaa ya Kiswahili BBC akimhoji Juma Duni Haji
Rose Inn Tanga

Uwanja wa Tangamano ulifurika siku ile pomoni. 

Hapakuwa na hata nafasi ya mtu kuweka baiskeli yake. Siku ile Prof. Lipumba aliunguruma akawakumbusha watu wa Tanga historia yao na jinsi walivyopoteza kila kitu. Aliwauliza uko wapi mpira wa Tanga waliokuwa wakijivunia? Yuko wapi Shakila na taarab ya Tanga? Uko wapi mkonge na viwanda vilivyokuwa vikiwapa ajira watu wa Tanga?

Mkutano huu wa Tanga Uwanja wa Tangamano uliitia hofu kubwa CCM na haukupita muda Mwalimu Nyerere akafikaTanga katika juhudi ya kukinusuru chama chake na kumnusuru William Mkapa mgombea wa CCM asikose kura za Mkoa wa Tanga. 

Katika mkutano aliohutubia Mwalimu Nyerere Uwanja wa Tangamano, Mwalimu alionya kumwagika kwa damu nchini endapo Watanzania watapiga kura kwa misingi ya dini zao. 

Sijui kitu kipi kilimfanya Mwalimu Nyerere aseme maneno hayo. 

Yeye mwenyewe mwaka wa 1955 katika uwanja huo huo wa Tangamano alihutubia umma mkubwa wa wananchi mara ya kwanza alipokuja Tanga baada ya kuundwa kwa TANU na umma mkubwa kama ule uliokuja kumsikiliza Prof. Lipumba ulijazana pale kumsikiliza. 

Hakika hofu kubwa ilikuwa imewaingia CCM na waliweza kusoma nyakati katika kuta bila shida yoyote. 

Prof. Lipumba alikuwa ameamsha matumaini mapya kwa jamii iliyokuwa imetengwa na kubaki nyuma toka uhuru upatikane mwaka wa 1961.

Nimekaa na kurejesha fikra zangu mwaka wa 1995 ambako kwa mara ya kwanza Prof. Lipumba aliingia Tanga na kuuteka mji na kuanzia hapo CUF ikawa na nguvu kubwa Tanga, nguvu ambayo ilifikia kileleni katika uchaguzi wa mwaka wa 2015 kwa CUF kuchukua kiti cha ubunge Tanga Mjini na kuongoza katika serikali za mtaaa.

Leo watu wa Tanga hawataki kuiona sura ya Prof. Lipumba katika mji wao. Hakika siasa ni mchezo mchafu na kadri unavyokuwa mchezaji mchafu na ndivyo mchezo wenyewe unavyozidi kunoga.

Kushoto Juma Duni Haji, Prof, Lipumba na Mwandishi nyumbani kwa
Mama Ummy Tanga 1995
Mwandishi na Prof. Lipumba miezi michache kabla hajajiuzulu uongozi 2015




No comments: