Jaws Corner Mji Mkongwe ngome kuu ya CUF Picha ilipigwa na mwandishi siku ya uchaguzi 22 Oktoba 1995 |
Sheikh Amar nilikuwa Zanzibar siku ile ya kupiga kura tarehe 22 siku ya Jumapili Oktoba mwaka wa 1995. Mvua kubwa sana ilinyesha. Katika shajara yangu nimeandika mengi hadi majumuisho ya kura zote pamoja nä butwaa iliyogubika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kumtangaza mshindi.
Nikiangalia
nyuma leo naiona picha halisi ya viongozi wetu. Viongozi wetu bado
hawajabadilika wanaendelea kuishi katika ndoto na hofu za uchaguzi. Kwa
viongozi wetu uchaguzi ni jinamizi anaekuja na ndoto mbaya ya kutisha.
Election Calander Count Down iliyowekwa Jaws Corner wakati wa uchaguzi |
Wananchi
wa Zanzibar ndiyo waliosimama kwenye mstari toka 1995 hadi 2015 hawajatetereka
katika upigaji wao wa kura. Wamekuwa wakipiga kura ya ushindi kila uchaguzi na
matokeo ya kura zao wanayajua kwa hiyo uchaguzi hauwatii hofu. Waingereza
wangesema, "It is like a walk in the park." Yaani ni kama mtu ana
barizi kwenye bustani.
Zigo la
gunia la misumari yenye ncha kali wamejitwisha viongozi wetu vichwani mwao na
ukiwaangalia tu zile, "body language," zao zinafichua kila kitu.
Sambamba na hali hii wananchi wa Zanzibar wanazo namna zao za ajabu kabisa za
kujifariji na kujiburudisha kutokana na matatizo wayaonayo kwa viongozi wao.
Mara wanaweka kwenye mitandao ya jamii picha ya kinu cha umeme kilichokuwa Zanzibar nk. nk. Lakini kubwa Ijumaa kama ya leo wanaulizana Maalim Seif leo anaswali wapi? Allahu Akbar. Ikijulikana msikiti gani ataswali tayari ishakuwa adha. Hauna kuwahi jitahidi utakavyojitahidi jua utaswali nje juani. Wazanzibari wanawapenda sana viongozi wao...
Natamani
nikuwekeeni yale niliyoandika katika shajara yangu ukurasa wa Jumapili 22 Oktoba
1995 siku ya kupiga kura lakini natia natoa maana sheria ya mtandaoni imekuwa
kali kidogo. Unapoandika katika shajara uko faragha unajitanua upendavyo maana
unazungumza na nafsi yako...niliwaonesha wachapaji vitabu shajara zangu
wananitia hima niwaandikie kitabu kuhusu Zanzibar na matatizo ya uchaguzi.
Nawaambia
haya siwezi kuyasema hadharani maana ithibati yake ni mie nipate upande wa pili
na kwao huu ni muhali mkubwa. Wachapaji wao wanaangalia mauzo ya kitabu...si
rahisi leo viongozi wetu kukubali baadhi ya nema zilizopotea
Zanzibar...Wazanzibari wenyewe huzikumbuka neema hizi na kuziadhimisha kwa
kuweka picha mitandaoni kisha wakaomba dua.
Viongozi
wa Tanganyika wajitahidi sana wawajue Wazanzibari vinginevyo watakuwa siku zote
wanajikwaa na kungo'a kucha ya dole gumba.
No comments:
Post a Comment