Ofisi Ndogo ya Chama Cha Mapinduzi Patrice Lumumba Avenue |
Nina
hakika si wengi hata humo ndani ya CCM wamepata kusikia jina la Alexander
Tobias. Hawajapata kuisikia jina hili kama vile walivyokuwa hawajapata kusikia
majina ya wazalendo wengi walipigania uhuru wa Tanganyika. Tufatane katika kisa
hiki utakisikia kisa cha Alexander Tobias vile alikisaliti chama cha TANU hata
kabla hakijazaliwa.
Ilikuwa
mwaka wa 1987 niko ofisi ya Mzee Germano Pacha katika jengo la Biashara ya
Wazee Tabora nikiwa nimesindikizwa na wenyeji wangu wawili, Ali Salum Mkangwa
na Ilunga Hassan Kapungu. Ofisi hizi za wazee wa TANU zilikuwa takriban kila mkoa
khasa sehemu za mijini. Kazi yao kubwa ilikuwa kushughulika katika maduka yao
na bidhaa adimu kama vile mafuta ya kupikia, mchele, sukari na wakati mwingine
vitu kama sabuni nk. Hizi zilikuwa ni zile nyakati za hali ngumu sana ya uchumi
Tanzania kila kitu kiliadimika. Huyu Germano Pacha ni mmoja katika watu 17
waliounda pamoja na Mwalimu Nyerere chama cha TANU 1954. Nilikuwa niko katika
utafiti wa historia ya TANU na Sheikh Abubakar Mwilima aliniambia kuwa ni muhimu
nikamuhoji Mzee Germano Pacha kwani alikuwa anajua mengi katika historia ya
uhuru wa Tanganyika. Hakuwa Sheikh Mwilima peke yake aliyenipa ushauri huu.
Hassan Upeka aliyekuwa katika Idara ya Usalama ya TANU toka mwaka wa 1956 na
yeye pia alinishauri na kutia mkazo kuwa ni lazima niende Tabora nikazungumze
na Mzee Pacha. Alikuwa Mzee Germano Pacha ndiyo aliyonifahamisha kwa mara ya
kwanza kufukuzwa kwa kiongozi katika TAA wakati wa harakati za kudai uhuru wa
Tanganyika.
Mzee
Pacha anasema katika mkutano wa mwaka wa
1954 wa TAA mkutano ulioasisi TANU walimfukuza chama Alexander Tobias aliyekuwa
Katibu Mtendaji wa TAA Makao Makuu New Street kwa kosa la usaliti. Alexander
Tobias alichukua majalada ya TANU ya siri akawapa Waingereza kupitia idara yao
ya ujasusi Special Branch. Inasemekana Waingereza walimuhonga fedha nyingi kwa
kazi ile. Huyu Alexander Tobias alianza kazi pale New Street June 1953 wakati Mwalimu
Nyerere anachukua uongozi wa TAA. Alexander Tobias alikuwa mfanyakazi wa kwanza
kuajiriwa na TAA kama katibu wa kudumu pale Makao Makuu ya TAA. Uamuzi huu wa
kuwa na sekretariati pale Makao Makuu ulifanyika Nansio baada ya mashauriano kati
ya Abdul Sykes na Hamza Mwapachu wakati wanashauriana na wanafanya mipango ya
kumtia Nyerere katika uongozi wa TANU kupitia uchaguzi wa TAA wa April 1953.
Alexander
Tobias akaanza kazi June 1953 Nyerere akiwa Rais wa TAA na Abdul Sykes Makamo
wa Rais na hapo inaaminika ndipo alipodakwa na Special Branch na akawa sasa
anawapa siri za TAA na mwisho akawakabidhi majalada yenyewe. Ukipitia nyaraka
za Sykes za mwaka wa 1953 hiki ndicho kipindi ambacho TAA walikuwa wako
katika muendelezo wa mawasiliano na vyama vingine vya siasa nje ya mipaka ya
Tanganyika. Nimesoma barua kadhaa katika nyaraka za Sykes ambazo Alexander
Tobias alikuwa anaandika kwa niaba ya TAA kuiandikia serikali ya Kiingereza.
Katika barua hizo ziliyonivutia sana ni zile ya kumuombea ruhusa Ally Sykes kama kiongozi wa TAA kusafiri kwenda Lusaka, Northern Rhodesia kuhudhuria mkutano wa Pan African
Congress uliokuwa umeitishwa na Kenneth Kaunda akiwa kiongozi wa African
National Congress. Mkutano huu ulikuwa ujumuishe vyama vya siasa vilivyokuwa
Kusini ya Sahara kuzungumzia ukombozi wa nchi zao.
Ni wazi
Alexander Tobias kwa nafasi yake katika kipindi kile cha mpito kuelekea kuunda
TANU mwaka unaofuatia, alijua siri nyingi za chama na kwa kiasi kikubwa kwa usaliti wake aliwadhoofisha sana wazalendo wa TAA. Yale ambayo alifanya hakika ulikuwa ni
usaliti mkubwa ambao usingeweza kustahamilika ila yeye kufukuzwa chama na hicho
ndicho kilichofanyika siku ya kwanza tu katika mkutano wa TAA wa 1954. TANU
isingeweza kuwa na wanachama wasaliti wa mfano wa Alexander Thobias.
Nimekileta
kisa hiki baada ya kusoma katika mitandao ya kijamii kuwa kimepita kimbunga ndani ya mkutano wa CCM
Dodoma kinakumba wanachama waliokwenda kinyume na matakwa ya chama. Chanzo
kikiwa Uchaguzi Mkuu wa 2015. Baadhi wamefukuzwa chama, wengine wamepewa
karipio kali na wengine wamesamehewa. Ni
muhimu sana kwa chama kuijua historia yake. Bahati mbaya CCM haina historia
ukiacha ile ya kuundwa kwake mwaka wa 1977. CCM haina moja walijualo katika
historia ya TANU na ukombozi wa Tanganyika. Ndipo pale mwanzo nikasema
tufuatane ili tumjue msaliti Alexander Tobias. Ikwa huijui jana yako huwezi
ukaijua leo yako. Ndiyo leo hii bado tunapapasa kama vipofu katika mengi ambayo laiti tungeijua historia yetu bila shaka tungeijua na mila ya siasa zetu katika vyama vya siasa.
Alexander
Tobias aifukuzwa chama kwa usaliti dhahiri. Swali la kujiuliza ni hili. Hawa
waliofukuzwa CCM wamefukuzwa kwa usaliti? Kisa chao kinajulikana na kinatokana
na uteuzi wa nafasi ya mgombea urais katika CCM. Tofauti zao zilitokea hapa. Yawezekana
kweli msimamo wa kumuunga mkono huyu na kumpinga yule katika chama cha siasa ikawa kosa kiasi
kupelekea watu kufukuzana chama? Ikitokea mathalan Katibu Mtendaji wa CCM
akaiba majalada pale Makao Makuu Dodoma akayauza kwa wapinzani kama alivyofanya
Alexander Tobias 1953, kosa hili ni wazi ni la mwanachama kufukuzwa chama kwani
ni usaliti. Hili la wanachama kugongana katika uchaguzi wa nani apeperushe
bendera kugombea urais wa nchi kupitia CCM hukumu yake inahitaji utulivu wa
fikra.
Nampa pole ndugu yangu Ramadhani Madabida kwa yaliyomfika.
Nampa pole ndugu yangu Ramadhani Madabida kwa yaliyomfika.
Nakumbuka
kama jana vile siku nilipomuona Madabida katika TV akizungumza pale Lumumba akajaribu
kumnadi alyedhaniwa ni mgombea wake wa urais mbele ya vyombo vya habari. Mashaallah Madabida
ni mzungumzaji hodari anaejua kuchagua maneno yake kwa uzito unaostahili.
Madabida alizungumza vizuri sana hadi akafika kuinukuu Qur’an.
Zamani sana nilimuazima Madabida kitabu kinaitwa, ‘’Khrushchev Remembers.’’ Katika kitabu hiki utamu unakuja pale Stalin alipokufa na pakawa na ombwe zito na ombwe hilo likazua mvutano kati Nikita Khrushchev na Lavrenty Beria. Kati ya kambi mbili hizi ipi ichukue uongozi? Mwisho wa kinyang’anyiro kile mshindi alipatikana na damu nyingi ilibaki sakafuni.
Nawafananisha Madabida, Sophia Simba na wenzao waliofukuzwa pamoja na wale viongozi wa Chama Cha Kikomunisti cha Urusi waliopoteza maisha yao kwa kukimbilia kupanda jahazi lililokuwa liashapangiwa kuzamishwa.
Naamini Madabida anakikumbuka kitabu hiki na yale yaliyomfika Beria na wenzake.
Zamani sana nilimuazima Madabida kitabu kinaitwa, ‘’Khrushchev Remembers.’’ Katika kitabu hiki utamu unakuja pale Stalin alipokufa na pakawa na ombwe zito na ombwe hilo likazua mvutano kati Nikita Khrushchev na Lavrenty Beria. Kati ya kambi mbili hizi ipi ichukue uongozi? Mwisho wa kinyang’anyiro kile mshindi alipatikana na damu nyingi ilibaki sakafuni.
Nawafananisha Madabida, Sophia Simba na wenzao waliofukuzwa pamoja na wale viongozi wa Chama Cha Kikomunisti cha Urusi waliopoteza maisha yao kwa kukimbilia kupanda jahazi lililokuwa liashapangiwa kuzamishwa.
Naamini Madabida anakikumbuka kitabu hiki na yale yaliyomfika Beria na wenzake.
No comments:
Post a Comment