Friday, 10 March 2017

TAAZIA: MUHAMMAD ALI MUHSIN

Muhammed Ali Muhsin
Muhammed Ali Muhsin Barwani
Tanga 2010

Huyo hapo juu ni Muhammed Ali Muhsin rafiki yangu toka mwaka wa 1999 nilipokutananae Muscat na kujulishwa kwake na baba yake Sheikh Ali Muhsin Barwani.

Alipofariki baba yake ambae mie alikuwa mzee wangu urafiki wangu na mwanae Muhammed ukazidi kupita kiasi. Muhammed amefariki leo Muscat.

Huenda si wengi wakamfahamu huku kwetu hivi sasa lakini yeye ni Mzanzibari.

Muhammad alikuwa mtu karim sana mwenye mapenzi na ndugu zake huku kwetu. Binafsi kwa miaka mingi nimepokea vitu vingi kutoka kwake kuanzia mashafu, juzuu, vitabu vya shule, nguo za watoto wadogo wa kike na kiume, vyerehani na kanzu akiniomba niwagaie ndugu zake huku Tanzania Bara.

Toka tumeanza ikiwa kazi ya mimi na yeye hadi akanambia sasa tushirikishe taasisi za Kiislam kazi hizi ili tutakapokuwa hatupo mambo yaendelee.

Mwezi uliopita kanipigia simu akanambia tujitayarishe kupokea shehena kubwa sana ya mashaf kwani wafadhili safari hii wameamua kuongeza nakala.

Ilikuwa katika harakati hizi za kutayarisha mipango hii ndipo nikapewa taarifa kuwa sahib yangu kalazwa Royal Hosptal, Muscat mgonjwa.

Usiku huu Muhammed amefariki na atazikwa kesho In Shaa Allah.

Allah ampe kauli thabit amsamehe madhambi yake na amtie peponi.
Kwake tumetoka na Kwake ni marejeo yetu.
Amin


Kulia: Muhammed Ali Muhsin, Abdallah Jabir na Mwamdishi
alipokuja kunitembelea Tanga 2010


Marhum Sh Mohammed Ali Mohsin Barwani Katika Friends Gathering ya mwanzo
nyumbani kwa Al Akh Sh. Ahmed Saif Rawahi 
10th January 2014







No comments: