Thursday 11 May 2017

TAAZIA: ALI MBARAK MAARUFU ALI BOBO BWANA WA WATU WA DAR ES SALAAM


Ali Mbarak (Bobo)

Waarabu wana msemo, ‘’Yule awatumikiae watu ndiye bwana wao.’’ 

Kwa muktadha wa msemo huu nathubutu kusema kuwa marehemu Ali Mbarak au Ali Bobo kama alivyojulikana kwa watu hakika ni bwana wa watu wote wa Dar es Salaam. 

Ali Mbarak amefariki leo usiku na kuzikwa L'Asr Makaburi ya Kisutu baada ya kusaliwa Msikiti wa Maamur.

Sidhani kama kuna kijana wa Ki-Dar es Salaam wa makamu yangu na chini kidogo ambae hakupata kumjua Ali Bobo.

Katika miaka ya 1970 alikuwa mmoja wa viongozi wa mpira  Cosmopolitan Football Club.

Ali Bobo alikuwa kila katika shughuli itakayofanyika Dar es Salaam akiwapo basi yeye atakuwa anawaandalia watu. 

Sikupatapo hata siku moja mimi binafsi kumuona kakaa kitako akiandaliwa na kula kama watu wengine.

Kazi hii ya uandazi akiifanya kwa ufanisi mkubwa huku akitabasamu. 

Ali Bobo si tu amuweke mtu na yeyote mahali pa kukaaa ili muradi kapata nafasi ya kukaa jamvini, la hasha. 

Alikuwa anajua nani amweke na nani. Nani hali biriani au pilau kwa hiyo amweke na nani kwa wali mweupe wale pamoja wakitie chakula barka. 

Alikuwa kama atakuweka basi atakuweka na mtu wako ili ufurahi. Hakika aliitia fani ya uandaaji kitu ambacho hakikuwapo kwa wengi.

Mashaallah Bobo alikuwa mtu wa watu, mtu wa kujishusha hata kwa wadogo zake. 

Mtamwita kumuomba akuongeezeeni chakula au kitoweo au hata kuleta maji ataleta huku anatabasamu. 

Itakuwa sijamweleza Ali Bobo vizuri katika kuwatumikia waja wa Allah ikiwa sitamtaja rafiki yake Sheikh Abdallah Awadh. 

Hawa wawili walinogesha shughuli yoyote ile ambayo watakuwapo kuwaandalia watu. 

Namkumbuka Ali Bobo na pick up yake ambayo ndiyo ulikuwa usafiri wake mkubwa enzi za mimi kumfahamu.

Kwa umri wake wote yeye alikuwa akifanya biashara ya duka la jumla pale Kitumbini karibu na Msikiti Mkubwa wa Ijumaa kama ulivyojulikana.

Baadae alikuwa na duka Kariakoo mtaa wa Swahili karibu na Soko la Kariakoo. 

Kisha aliingia katika shughuli za ujenzi wa majumba kisha akastaafu na akawa sasa anafanya biashara nyepesi ya ‘’catering,’’ na kwa kweli alifanikiwa khasa kwa ajili ya umaarufu na utu wake.

Kwa nini Sheikh Ali asiwe hivi ninavyomueleza ilahali yeye kalelewa na ami yake maarufu tukimwita Sheikh Kilemba ambae alikuwa mmoja wa maimamu wa Msikiti wa Kitumbini na mtu wa karibu sana na Sharif Abdulkadir Juneid?

Siku moja nikizungumza na Ali Bobo basi kwa maskhara nikamwabia,’’Kaka hebu niambie iweje kila shughuli wewe unakuwa mwandazi?’’ 

Akanijibu huku anacheka akasema, ‘’Mimi shughuli nyingine hualikwa kama wewe, lakini nikiwa nimekaa nikaona mambo hayaendi vyema basi nachelea shughuli ya ndugu yangu isiharibike basi hapo husimama kutengeneza mambo. 

ikawa nimefanya hivi mara mbili tatu basi ikawa sasa kila shughuli utaniona sikai tena husimama kuandalia hata kama sijaombwa kufanya hivyo.’’ 

Swali hili hili nilimuuliza rafiki yangu sasa marehemu Athmani Zakuwani wakati niko Tanga. Yeye kama alivyokuwa Ali Bobo kila shughuli pale Tanga akisimama kutuwekea chakula.

Akanijibu akanambia, ''Kuna msemo wa Kiarabu usemao, ''Awatumikiae watu ndiye bwana wao.’’

Allah amsamehe ndugu yetu Ali Mbarak madhambi yake na amweke mahali pema peponi, Firdaus awe jirani na waja wema wa Allah na Mtume, rehma na amani zimshukie.
Amin.

No comments: