Mayor wa Jiji la Dar es Salaam Kitwana Selemani Kondo |
ILIKUWA
siku ya Jumanne, Mei 24, mwaka huu, baada ya Magharibi kupita, nikiwa ndani ya
Pantoni ya MV Magogoni nikielekea nyumbani Tuangoma, simu yangu ya kiganjani
ikalia. Kutokana na kelele na muungurumo wa injini wa kivuko kile, sikupenda
hata kidogo kuijibu nikichelea kwamba nisingesikilizana na mtu wa upande wa
pili. Lakini kwa taabu niliipokea; “…mzee wetu Kitwana Kondo amefariki jioni ya
leo hospitalini Hindu Mandal maziko kesho, tupashane habari,” alisema ndugu
yangu Mwinyi Mussa kutoka upande wa pili.Nilijizoazoa kuelekea nyumbani nikiwa
nimehuzunika kupita kiasi, kwani vifo vya ukubwa huu vilikuwa vimeongozana hapa
kwetu Dar es Salaam katika mwezi mmoja.
Alianza
Mzee Issa Ausi kama wiki tatu tu zilizopita, akafuata mzee mwengine, Ali
Mbaraka ‘Bobo’ na sasa tena Mzee KK- Inna Lillahi Waina Ilayhi rajuun! Marehemu
mzee KK alizikwa katika makaburi ya Tambaza siku ya Jumatano, Mei 25 mwaka huu
baada ya sala ya alasiri. Miongoni mwa watu mashuhuri waliokuwapo mazikoni pale
ni ni Mzee Ali Hassan Mwinyi, ambaye ni rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya
Pili; Dk. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais Mstaafu; Edward Lowassa, mmoja
wa viongozi wa katika UKAWA na Waziri Mkuu Mstaafu; na Prof. lbrahim Lipumba wa
CUF. Wengine ni Mzee Ngombale Mwiru, Abdulrahman Kinana, Prof. Hamza Njozi,
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM) pamoja na masheikh mbalimbali wa
hapa jijini akiwemo Mufti Zubeir.
Taazia ndefu na timilivu, kumhusu mzee huyu,
ambaye wengine ni baba yetu, tayari imeshaandikwa na ndugu yangu kutoka Kuala
Limpur Malaysia, Balozi Ramadhani Kitwana Dau. Ndani ya taazia ile hakikubaki
kisichoelezwa hadi kufanya mtu mwingine naye achukue kalamu na kuandika—bila
shaka yeyote hiyo itakuwa ni fujo! Lakini hali halisi ni kwamba, kila watu
wanapotokeza kwa wingi kumuenzi marehemu mzee huyu ndivyo ambavyo tutakuwa
tumemuenzi na kumlipa fadhila alizotukirimu.
Jina
lake kamili ni Kitwana Selemani Kondo au KK kama alivyofahamika zaidi kwa
upendo kutoka kwa marafiki zake. Jina hili lilivuma sana nchini kwetu hata kwa
watu ambao hawakupata kumwona wala kukutana naye. Jina la KK limekuwa mithili
ya ngoma ya mbali ambayo huvuma kwa mdundo mzuri ikiwa haina uhalisia. Kwa
sababu hiyo basi, watu wengi hapa kwetu walimjengea taswira, kwa sababu ya
kutomjua vzuri, kwamba ni mtu pengine anayebwabwajabwabwaja maneno tu kama Mswahili
mwengine na kibahatibahati akawa Mbunge, Meya na Diwani.
Ndugu
msomaji, mimi najisikia fahari pamoja na majonzi niliyokuwa nayo ya kuondokewa
na mzee KK, kwa sababu mimi ni sehemu ya historia ya Dar es Salaam. Jina langu
ni Abdallah Mohammed Saleh Tambaza. Familia yetu iko karibu kabisa na historia
ya jiji la Dar es Salaam. Ikutoshe kwamba, ukisoma historia ya TANU na uhuru wa
Tanganyika, unamuona Jumbe Tambaza pale Upanga, Msikiti wa Tambaza, Makaburi ya
Tambaza, Shule ya Tambaza na Hospitali ya Muhimbili. Kwenye maeneo mengine ya
jiji hili, kama vile Magomeni, alikuwapo Diwani Mwinyimkuu Mshindo na Diwani
Ndugumbi Kitembe. Wote hao ni kina Tambaza. Mzee KK alizaliwa kijijini kwao
Mtoni Kijichi maeneo ya Mbagala. Huko nako ni sehemu ya Diwani Tambaza
Mwenyekuuchimba. Hivyo Mzee KK, pamoja na kwamba ni Mzaramo wa kutoka Mtoni
Kijichi, Mbagala, hakukosea kitu kuamua azikiwe katika makaburi ya Upanga kwa
Tambaza kwa sababu ana asili nako kinasaba—aliishi wakati wote na kusomea
jijini Dar es Salaam.
Kwa
mnasaba huu mambo matatu aliyapenda sana, moja ni utaifa usiotenganishwa kwa
maana ya Dar es Salaam na Tanzania ni kitu kimoja; aliipenda Dar es Salaam yake
kama alivyoipenda Tanzania kutoka Lindi hadi Mara; Tanga hadi Rukwa; Dsm hadi
Mwanza, Kigoma na Mbeya—kwa maana ya Tanzania nzima—akipendelea zaidi utani wa
makabila mbalimbali hasa kwa Wanyamwezi, Wasukuma na Wadigo.
Nimemjua
Almarhum Mzee KK katika sura kama tano hivi:
Kwanza,
Mzee Kitwana alisoma pale Shule ya Kitchwele Dsm wakati wa ukoloni pamoja na
baba yangu mkubwa Mzee Yahya Saleh Tambaza na nduguye (babangu mzazi) pamoja na
marafiki wengine wa baba zangu, wakiwamo akina Sykes, akina Aziz, Iddi Simba,
Said Kassim, Zuberi Mtemvu na Harold Mgone ambao pia alicheza nao mpira wa
chandimu utotoni na katika timu za Yanga na Sunderland (Simba). Kila mara nilipokuwa
nikimwona Mzee KK akiwa na baba zangu hao ilikuwa ni masikhara, vicheko na
mambo ya namna hiyo ikiwemo utani wa Simba na Yanga.
Babangu
mimi mzee Mohammed Saleh Tambaza, ni mwasisi wa Sunderland na Mzee KK yeye ni
mwasisi wa timu ya Yanga huko mwanzoni, akiwa na kina Mzee Mangara, Kondo
Kipwata, Saidia Msafiri, Mtaruke Mangara, Juma Shamte na Juma Vijiga na
wengineo wengi. Kila palipokuwa na shughuli ya aina yeyote nyumbani kwetu, iwe
harusi au misiba, daima nikimwona Mzee KK yuko jamvini akiupiga mpunga huku
akiwarushia rafiki zake, kwa upendo, maneno ya utani na ngonjera. Pili,
historia inasema kwamba miaka mingi nyuma wakati wa utawala wa Kiingereza hapa
kwetu, Mzee KK alikuwa afisa katika Jeshi
la Polisi mwenye cheo cha Inspekta. Pamoja na kwamba hawakuwapo Waafrika wengi
kwenye ngazi hiyo ya upolisi, lakini wale walioupata uinspekta hawakuwa watu wa
kawaida hivi.
Katika
miaka ya 1950s wakati wa harakati za kupigania uhuru wetu, habari zinasema KK
aliitumia nafasi hiyo ya upolisi kuwapa akina Nyerere na wenzake habari
nyetinyeti za serikali ambazo zilikuwa zikipangwa dhidi ya mapambano ya
uhuru. Mingi ya mikutano hiyo kati ya KK
na viongozi wa TANU wakati huo ilikuwa ikifanyika katika majumba ya watu
Kariakoo na wakati mwengine pale kwenye klabu ya Yanga mtaa wa Mafia na Sukuma,
huku Mwalimu Nyerere akiwa kajibadilisha kwa kujifunika baibui ili kupoteza
maboya asitambulikane.
Msomaji,
unaweza kuona namna gani marehemu KK alivyohatarisha maisha yake kwa ajili ya
taifa hili, maana kama wakoloni wangejua, si kama angepoteza kazi peke yake,
lakini pengine angeuawa! Basi potelea mbali na iwe hivyo, yeye aliendelea
kuifanya TANU kazi, tena na tena na tena mpaka leo kimeeleweka tuko huru.
Mzee
KK, kutokana na umaridadi na utanashati wa kipolisi, alikuwa akijua kuvaa
vizuri sana. Katika maisha yangu ya utoto nilikuwa nikimwona akirandaranda
kwenye mitaa ya kwetu Kariakoo kwa madaha sana na miondoko ya maringo ya
kiaskari huku akiwa amepangilia kama ni suti, suti kweli; kama suruali na shati
basi ni vya hatari tupu! Huku kiatu chake cha ‘bei mbaya’ kikiwa ng’areng’are
mguuni.
Hivyo
ndivyo ilivyokuwa kwa vijana wa zamani. Na hapa nawakumbuka wazee wengine wa
namna hiyo akiwamo Mzee Senga Mlela wa pale Mtaa wa Chura, Kariakoo; marehemu
Mzee Jagna Shaha na Maalim Abubakar Mzinga wa Mzinga & Sons Muslim School. Hawa
wote wakati wa enzi zao walikuwa wakivaa ‘pamba kali’ kutoka maduka ya B.
Choitram, Jan Mohammed, J.R. Steven’s, Teekay na Afi yote yakiwa pale Accacia
Avenue (sasa Samora).
Miaka
kadhaa baadaye, sasa nikiwa mwanafunzi wa sekondari pale katika Shule ya Mtakatifu
Joseph, pale Forodhani, nilishangazwa kila nikimwona kwenye mitaa yule mzee
ambaye namjua kama ‘rafiki yake babangu aliyekuwa Inspekta wa Polisi na baadaye
kwenda mpaka Scotland Yard, akiwa katika magari mazuri mazuri ya kifahari kule
mjini Dar es Salaam, wakati huo kukiitwa Uzunguni.
Kumbe
nilikuwa sikufahamu umuhimu wake. Yule mzee alikuwa ameshika wadhifa wa
Serikali ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Sikujua ana mchango mkubwa sana
katika kufanikisha Muungano na harakati za vyama vya ukombozi wa nchi za Kusini
mwa Afrika, yakiwemo mapinduzi ya Zanzibar—KK alikuwa rafiki mkubwa wa Karume
na Kassim Hanga. Ah! Pia, sikuwa nimejua KK yule ‘rafiki yake baba’, ndiye kwa
namna ya kipekee kabisa alifanikisha kuzibadili siku za Sikukuu ya Pasaka
wakati huo zikijulikana kama, ‘’Bank Holidays,’’ na kupatikana msimu wa ‘Sports,’
baina ya vilabu vya Dar es Salaam na Zanzibar kutembeleana.
KK,
alikuwa kiongozi mwandamizi wa Yanga aliyeasisi udugu baina ya klabu yake na
ile ya African Sports ya Karume kule Unguja. Simba wao walikuwa na uhusiano na
klabu ya Kikwajuni pia ya hukohuko Unguja. Udugu huu, ulioendelezwa miaka nenda,
miaka rudi; haukuishia mpirani tu bali baadaye ukahamia kwenye siasa na hivyo
kuja kuunganisha nchi na kuzaliwa nchi ya Tanzania baada ya Sultani kupinduliwa
kule Zanzibar. Habari zinasema, ilikuwa ni kutokana na urafiki mkubwa baina ya
KK na Karume wa Unguja na kwa ushawishi mzito wa KK, marehemu mzee Karume
akaizawadia klabu ya Yanga jengo la makao makuu yaliopo mitaa ya Jangwani na
Twiga jijini Dsm.
Habari
zinasema, ilikuwa ni KK pia aliyemuunganisha aliyekuwa mwenyekiti wa Klabu ya
Sunderland (sasa Simba) wakati huo na hayati Mzee Karume ambaye alikuja
kuwamalizia Simba sehemu ya jengo lao iliyokuwa haijakamilika. Mambo kama hayo
ndiyo yalikuwa yakifanyika katika vilabu vya Simba na Yanga kwa wakati wa
zamani. Ni kusaidiana, kuhurumiana, kutembeleana na kuzikana wakati wa misiba.
Watu waliopo sasa katika vilabu hivi kamwe hawawezi kuyafanya haya walioyafanya
watangulizi wao—ni chuki, hasama na uadui tu vilivyotamalaki.
Zaidi
ya mpira, marehemu mzee KK alipenda burudani za aina mbalimbali ikiwamo muziki
wa dansi na ule wa taarab asilia. Aliipenda bendi ya Dar es Salaam Jazz wakijulikana
kwa jina la, ‘’Majini wa Bahari,’’ ya wakati huo ikiongozwa na Mzee Mubba wa Gerezani;
Kilwa Jazz ya Ahmed Kipande; Ulanga Jazz na Western Jazz iliyoongozwa na Yanga
mwenziwe marehemu Daudi Makwaia. Nyengine ni ile ya Merry Black Birds
ikiongozwa na rafiki yake Ally Sykes waliokuwa wakitumbuiza kwa nyimbo na
mitindo ya kizungu ya Rumba, Chacha, Foxtrot na Bolero kila Jumamosi pale
ukumbi wa Arnautoglo. Kwa upande wa taarab asilia, mzee KK alikuwa mpenzi
mkubwa wa bendi ya Egyptian Musical Club ya Kariakoo. Bendi hii ilikuwa na
uhusiano wa karibu na klabu yake ya Yanga. Kwa mtu wa namna yake kwa wakati ule
ni lazima angevutiwa na taarab tu; maana muziki ule ulikuwa ni sehemu ya
utamaduni wa watu wa Dar es Salaam na pwani yake kutokana na maudhui, mashairi
na lugha ya Kiswahili. Vitu ambavyo almarhum Mzee Kitwana alivipenda sana.
Daima nikipenda kumsikiliza akizungumza Kiswahili chake fasaha kama ambavyo leo
watu wa Amerika walivyokuwa wakipenda kumsikiliza Obama akizungumza Kingereza.
Kiswahili
cha Mzee Kondo hukipati Unguja wala Tanga na hata Mombasa. Ni Kiswahili cha
Mrima kile na wenyewe ni watu wa Mrima. Kwa sasa ukipata bahati msikilize Mzee
Iddi Simba au Suleiman Hegga utaamini ninachokizungumza. Misaada na michango ya
marehemu mzee wetu huyu kwa jamii katu haiwezi kupimika kwa mizani ya kilo,
rula kwa marefu na mapana, wala si kwa lita kwa ujazo wa ndoo za maji. Ni
mkubwa sana. Jiji la Dar es Salaam lilipozidi kukua baada ya uhuru kupatikana,
KK alifanya bidii kwa kushirikiana na marehemu rafiki yake mpenzi Mzee Kibiriti
wakaanzisha kwa fedha za KK, klabu mpya ya taarab waliyoipa jina la New Extra
Musical Band. New Extra iliongozwa na magwiji wa taarab wakati huo kama Maalim
Abubakar Mzinga na mwanawe Hamis Mzinga; Bi. Pili na dadake Kibibi bint
Abdallah. Nakumbuka kama vile ni jana, uzinduzi wa bendi hii ulifanywa na
aliyekuwa rafiki mkubwa wa KK wakati huo, hayati Abdallah Kassim Hanga
aliyekuwa Waziri Nchi Ofisi ya Rais Masuala ya Muungano. Bendi hiyo
iliyojizolea umaarufu wakati huo, ilivuma sana kwa nyimbo zake za, ‘’Shambani Mazao
Bora Shambani,’’ na ule wa kuhamasisha kujiunga na TANU, ‘‘Kina mama TANU, kina
baba TANU, Afro yajenga nchi.’’ New Extra haipo tena. Imekufa kama zile
zilizoitangulia za Alwatan, Egyptian na Jamhuri.
Katika
kipindi alichofanya siasa Mzee Kitwana Seleman Kondo alikuwa Mbunge wa
mwanzomwanzo baada nchi hii kujitawala akipata nafasi, kwa nyakati tofauti
kuwakilisha sehemu mbalimbali za majimbo ya Dar es Salaam, ikiwamo Ilala,
Kigamboni, Temeke, Dar es Salaam Magharibi, kasoro Kinondoni na Magomeni. Kutokana
na uwakilishi wake uliotukuka uliomfanya awe anarudi bungeni kila mara, wabunge
wenzake wa Bunge la Tanzania chini ya Spika Chifu Adam Sapi Mkwawa, hawakusita,
kwenye miaka ya 70, kumpa ridhaa ya kuiwakilisha nchi nzima kwenye Bunge la
Afrika Mashariki (East African Legislative Assembly). Wawakilishi wengine wa
Tanzania aliokuwa nao siku zile kule EALA walikuwa ni akina Bhoke Munanka,
Joseph Nyerere, Edwin Mtei akiwa Katibu Mkuu East African Community, na
mawaziri wakiwa ni Alnoor Kassum, John Malecela, Salim Rashid kutoka Zanzibar
na Spika alikuwa Chief Sarwart wa Mbulu.
Bunge
lile lilikuwa motomoto sana likipendeza kweli kulifuatilia majadiliano yake. Sasa
katika kipindi hicho miaka ya 70, nilikuwa mfanyakazi pale Idara ya Usalama wa
Anga Afrika Mashariki (Directorate of Civil Aviation E.A) nikiwa Aeronautical
Communications Officer pale Nairobi. Pale habari za Bunge lile zilizomhusu Mzee
KK zilipoandikwa na magazeti ya Nation na Standard ya Kenya, haraka haraka
niliwageukia wenzangu ofisini kuwaonyesha kwamba yule mzee ni baba yangu kutoka
kwetu TZ. Nilijivunia sana.
Sura ya
mwisho ya Mzee Kitwana Kondo niliiona kwenye miaka ya 1990s wakati niliporejea
kutoka masomoni Marekani baada ya muda mrefu. Nilimkuta Alhaj Mzee Kondo
akihimiza elimu kwa Waislamu; utaifa na mshikamano wa watu wa Dar es Salaam
pamoja na nchi yote hii aliyoipenda na kuitumikia sana. Akiwa Meya wa jiji,
aliwakumbuka na kuwaenzi wapigania uhuru wenziwe wa Dar es Salaam kwa kuwapa
majina ya mitaa. Uliokuwa ukiitwa Somali Street, ulikwenda kwa Mzee Omari Londo; Aggrey Street aliupa jina la Max
Mbwana; Kipata Street aliuita Kliest Abdallah Sykes; Tandamti ukawa Mshume
Kiyate na Kongo ukawa Iddi Tulio. Alikuwa ni mzee KK aliyeurudishia jina tena
mtaa wa Bibi Titi Mohammed baada ya kufutwa alipokosana na Mwalimu Nyerere ukawa
Mtaa wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT). Kondo hakupenda hilo!
Moja ya
kazi kubwa ya kupigiwa mfano ya mzee huyu ni pale alipohangaika huku na huku
kuhakikisha kwamba Waislamu wanapunguza pengo la elimu miongoni mwao kwa
kuhakikisha wanapata majengo yaliyokuwa ya TANESCO Morogoro kuanzisha Chuo
Kikuu akiwa Mwenyekiti wa Bodi. Haikuwa kazi rahisi kwa maana viongozi wengi
waandamizi serikali wakati huo, akiwamo Waziri Mkuu Sumaye, walilipinga wazo
hilo kwa nguvu kubwa. Marehemu KK hakukata tama; alitumia turufu kubwa na
hatimaye majengo yale yakapatikana na leo Alhamdullilah chuo kinatoa wasomi si
haba. Kwa hili sina shaka yeyote inaweza kuwa ni sababu ya kuingia peponi kwa
mzee huyu. Mungu ameshaahidi hilo kwa wale wanaofanya mambo ya namna hii
duniani.
Mzee KK
aliugua kwa muda mrefu akiwa anapumzika zaidi nyumbani kwake. Miaka michache
nyuma kabla kifo chake, kama wadhamini wakuu wa Masjid Mwinyikheri Akida wa
Kisutu, Dar es Salaam, tulipokea taarifa mimi na ndugu yangu Mzee Mwinyikhamis
Mussa kwamba mzee Kitwana Kondo alikuwa anataka kutuona nyumbani kwake kwa
jambo la haraka sana. Ndiyo ikawa mara yangu ya mwisho kumwona akitembea na
kuzungumza kwa shida kwelikweli. Alitukaribisha na kusema hivi, “…nimepata
taarifa kwamba mmepokea barua kutoka kwa Mwenyekiti wa TAPA – Taifa, Abdallah
Bulembo ya kusema kwamba haraka sana mvunje msikiti katika muda wa wiki 3 kabla
hatua kali hazijachukuliwa kupisha ujenzi wa Makao Makuu ya Tapa na kwamba
nyinyi ni wavamizi wa kiwanja kile, Mzee aliendelea, sasa nyinyi mamwinyi
msisumbuke na hilo …kiwanja nilikitoa mimi na mimi ndiyo nitakayejibu upuuzi
huu. Nilipewa kibali na Nyerere kutoa eneo hilo kwa msikiti na hivyo wakati
bado nikiwa hai niachieni mimi nijibu hili, nyinyi mamwinyi pumzikeni tu …
nitawaletea nakala yenu…” alimaliza mzee kwa sauti ya chini kabisa.
Huyo
ndiyo Mzee KK alivyolishughulikia suala hilo pale Abdallah Bulembo, ulevi wa
cheo cha CCM ulivyomzidi akasahau kuwa msikiti ni nyumba ya Allah yeye anataka
auvunje ajenge ofisi yake ya TAPA—Inna Lillah Waina Ilayhi Rajuun. Sasa KK
hatunaye najua TAPA watatafuta namna ya kuja tena kutusumbua. Msikiti ule unaojulikana
kama Mwinyikheri Akida ndiyo wa kwanza kujengwa jijini zaidi ya miaka 150
imepita. Una umri mrefu kuliko hata nchi yenyewe ya Tanzania.
Kwa
kumalizia, ni kwamba hadi anafikwa na umauti, umaarufu wa mzee KK kwa masheikh,
viongozi wa Serikali ya Tanzania, na viongozi wa SMZ, wakazi wa jiji na hasa
viongozi wa Simba na Yanga, ulikuwa mkubwa sana kama ilivyoonyesha kwenye
maziko yake. Balozi wa Tanzania nchini Malaysia Alhaj Dk Ramadhani Dau, katika
taazia yake ndefu kwa mzee wake huyu alipendekeza kwa uongozi wa MUM utafute
jengo moja lipewe jina la KK ili kumuenzi marhum. Mimi niliwasikia waombolezaji
pale makaburini wakiteta kwamba ni vyema basi moja ya barabara za jiji
hili—hata ndogo—iitwe Kitwana Selemani Kondo.
Mwisho, tunamwomba Allah (sw) aipokee roho ya
Mzee Kitwana Kondo kwa wema na aipumzishe bila shaka katika pepo ya Firdaus. In
shaa Allah.
Amin.
Simu:
0715808864; 0628985862
atambaza@yahoo.com
No comments:
Post a Comment