Kitwana Selemani Kondo katika ujana |
BURIANI MZEE KITWANA KONDO
Ramadhani K Dau
Siku
ya Jumatano tarehe 24 Mei 2017 ni siku ambayo itakumbukwa na Watanzania wengi
na haswa Waislamu kwa kuondokewa na mzee wetu Alhaj Kitwana Selemani Kondo
maarufu “KK” au mzee wa mjini. Siku 4 kabla ya kifo chake, mwanawe wa kiume
Bwana Adnan-Msakuzi alinitumia ujumbe kwenye WhatsApp akiniarifu kuwa Mzee KK
amelazwa Hindu Mandal na hali ya afya yake inazidi kuzorota. Siku ya pili yake
nilimtumia ujumbe Adnan-Msakuzi kutaka kujua hali ya Mzee inaendeleaje. Majibu
ya Adnan yaliniashiria kuwa mzee wetu amekaribia kufika mwisho wa safari yake
hapa duniani. Aliniambia kuwa kwa sababu ya ukaribu wangu na Mzee KK hanabudi
aniarifu ukweli ulivyo. Aliniarifu kuwa hali ya mzee ni mbaya sana na kwamba
kinachosubiriwa na Rehma Zake Mwenyezi Mungu. Kwa kweli ujumbe ule ulinihuzunisha
sana na sikuweza kuhimili uchungu ule peke yangu. Nikamwarifu Profesa Hamza
Mustafa Njozi, Makamu Mkuu wa Chuo cha Waislamu Morogoro na Bwana Faraji
Abdallah Tamim, mwalimu wa chuoni hapo.
Ilipofika
siku ya Jumatano tarehe 24 Mei nikapata taarifa kupitia moja ya kundi sogozi
(chat group) kuwa Mzee KK amefariki dunia. Pamoja ya kuwa hali hiyo ilikuwa
tayari inatawala fikra zangu tokea siku niliyopata ujumbe kutoka kwa Adan lakini
kifo hakizoeleki. Taarifa hiyo ilinikuta nikiwa najiandaa kwenda uwanja wa
ndege wa Kuala Lumpur kumsindikiza shemeji yangu. Wakati huo kwa saa za
Malaysia ilikuwa kiasi cha saa 4 usiku. Nilipwelewa sana kwa sababu ya uhalisia
kuwa sitowahi kumzika mzee wangu Mzee KK. Haikuchukua dakika 10 baada ya
taarifa hizo, Adnan kanipigia simu ambayo hatukuweza kuzungumza hata neno moja
kutokana na vilio vyetu. Kila mmoja alikuwa analilia kwake. Ghafla akakata simu
na kunitumia ujumbe mfupi uliosema “KK is dead. Allah is Great”. Mara tu baada
ya kupata taarifa hiyo nilichanganyikiwa na kuona uchungu sana baada ya kuona
kuwa sitoweza kumzika Mzee KK ambaye aliwahi kunitamkia mbele ya mkewe Bi
Hanifa kuwa ikitokea atafariki kabla mimi basi angependa asaliwe Masjid Mtoro,
azikwe makaburi ya Tambaza na mimi niwe mmoja kati ya watu watakaoingia
kaburini.
Katika
maishani mwangu, hii ni mara ya tano kuandika taazia yaani “obituary”. Buriani
zilizotangulia ni za aliyekuwa mwalimu wangu Chuo Kikuu DSM na rafiki yangu wa
karibu Profesa Ken Edwards mwenye asili ya Jamaika, aliyekuwa Afisa wa Uhusiano
wa NSSF Alfred Ngotezi, rafiki yangu tokea utotoni Abubakar Mohamed Saleh
Tambaza maarufu “Babu Chela” na Saidi Masimango aliyekuwa Mkurugenzi wa
Teknohama NSSF. Kila niandikapo taazia
huwa nafanya hivyo nikiwa na moyo mzito na huzuni sana. Kila niandikapo huwa naomba
kuwa hiyo iwe ndio ya mwisho kwani kuandika taazia ni jambo zito sana haswa
ikiwa inamuhusu mtu wa karibu yako kama nilivyo mimi kwa Mzee KK na hao
waliotangulia kabla yake.
Kwa
huzuni niliyokuwa nayo niliamua kutoandika taazia hii kwa sababu nisingeweza
kufikia mwisho kwa kilio. Lakini mara tu baada ya habari za msiba kuenea
nikaanza kupata salaam toka kwa watu mbali mbali akiwemo Prof Hamza Njozi,
mdogo wangu Abdul Dau na Adnan-Msakuzi. Ujumbe kutoka kwa Adnan ndio ulizidisha
majonzi yangu lakini pia ulinipa nguvu ya kuandika kwani kama alivyosema Adnan
na nakuu “Dr please write a eulogy for KK. You knew him well, no one can
talk of him better than you”. Baada ya kutafakari nikaona kama sikuandika
ntakuwa sikumtendea haki Mzee Kondo. Kwa kuwa nimekosa fursa ya kumtimizia
wosia wake kuwa niwe miongoni mwa watu watakaoingia kaburini kumzika, nimeona
nisikose vyote. Kwa kuzingatia kanuni ya
fiqh kuwa kama jambo haliwezi kufanyika lote basi lisiachwe lote. Waswahili
nao wana msemo wao “lisobudi hutendwa”. Hivyo basi nimeamua kuandika taazia hii
kwa huzuni na unyonge mkubwa.
Mzee
Kitwana Selemani Kondo alizaliwa Mtoni Kijichi, Dar es Salaam tarehe 1 Agosti
1930. Pale Mtoni Kijichi ukoo wake ni ulijulikana kwa jina la Mahembe. Wazazi
wake wote wawili ni Wazaramo. Kiumeni kwake ni Mtoni Kijichi na kikeni kwake kijiji
cha Gumba, Kisarawe. Alipata elimu ya msingi Mchikichini kisha akaenda Tabora
Boys na baadae Chuo Kikuu cha Howard kilichopo Washington DC, Marekani. Pia
Mzee Kondo alichukua masomo ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa
darasa moja na marehemu Sheikh Mohamed Ali Al-Buhry.
Kwa
upande wa kazi, Mzee Kondo alikuwa Polisi kwa muda mrefu hadi kufikia ngazi ya
Inspekta na baadae akawa Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje, marehemu Oscar
Kambona. Wakati wa uhai wake Mzee KK ameongoza Taasisi kadhaa za Umma zikiwemo Shirika
la Magari la Taifa yaani State Motors Corporation (Mkurugenzi Mkuu),
Mwenyekiti wa Bodi za TANESCO, Mamlaka ya Bandari na Bodi ya Korosho. Wakati wa
uhai wake, Mzee Kondo alijaaliwa kupata watoto 8. Kati ya hao wanaume 3 na
wanawake 5.
Nimemfahamu
Mzee tokea nikiwa mdogo kwa sababu ya kuzaliwa na kulelewa Mwembetogwa, jijini
Dar es Salaam. Wakati wa utoto wangu sikuwa na ukaribu sana na Mzee Kondo kwa
sababu ya tofauti ya umri. Ukaribu wangu kwake ulianza mwaka 1995 wakati
alipoteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya
Bandari Tanzania (THA) ambapo mimi nilikuwa Mkurugenzi wa Masoko kwa miaka
tisa. Nakumbuka siku moja mara tu baada ya kumaliza kikao cha Bodi niliamua
kumsindikiza mpaka kwenye maegesho ya gari. Baada ya kufika kwenye gari yake,
nikaona nichukue fursa hiyo nijitambulishe zaidi kwake kwani mpaka wakati huo
alikuwa ananifahamu kama Mkurugenzi wa Masoko. Nikajitambulisha kuwa mimi
nimezaliwa na nina asili ya Dar es Salaam.
Mara
tu baada ya kumwambia hivyo haraka kabisa akaniuliza baba yangu nani. Ili
kumtosheleza kiu chake sikutaka kumtambulisha baba yangu. Badala yake, na kwa
makusudi kabisa nikamwambia mimi ni mtoto wa “John” Iddi. Mara tu
nilivyojitambulisha akasema “wewe mwanangu, “John” Iddi alikuwa mkwe wangu”.
Nilifanya makusudi kumtaja “John” Iddi ambaye ni baba yangu mkubwa. Jina lake
halisi ni Thabit Iddi Dau. Jina la “John” aliitwa na mama yake baada ya kumzaa
akiwa ana umri mkubwa sana. Baada ya kujifungua akasema mtoto huyu nimempata
“Jioni” kwa maana ya kuwa amemzaa hali ya kuwa yeye ana umri mkubwa sana na
alikwisha kata tamaa ya kupata mtoto. Pamoja
ya kuwa jina lake halisi lilikuwa Thabit lakini tokea utotoni alijulikana kwa
jina la “Jioni” ingawa kwa urahisi wa matamshi badala ya kusema “Jioni” likavuma
jina la “John”. Marehemu Bwana Thabiti alijulikana sana kwa jina hilo la utani hadi
kufa kwake.
Nimesema
niliamua kujitambulisha kupitia baba yangu mkubwa kwa makusudi kwa sababu Mzee
Kondo aliwahi kumuoa Bibi Kijakazi wa Mgoto ambaye alikuwa anafanyakazi
Halmashauri ya Jiji (City Council). Kwa bahati mbaya hawakuwahi kupata mtoto.
Katika ndoa yake nyingine, Bibi Kijakazi alijaaliwa mtoto wa kike ambaye jina
lake ni Kurwa. Sasa huyu Bibi Kurwa ndiyo aliyekuwa mke wa kwanza wa marehemu Mzee
“John” Iddi. Katika uhai wao walijaaliwa kupata watoto wawili. Iddi “John” na
Mwatatu Thabit. Iddi alifariki mwaka 2001. Mwatatu yu hai ameolewa na Mohamed
Mfaume maarufu “Difu” ambaye alikuwa golikipa wa Yanga, Cosmo na Timu ya Taifa.
Mpaka sasa Mwatatu anaishi Kariakoo mtaa wa Swahili kwenye nyumba ya urithi wa
mama yake.
Kinasaba,
Mzee Kondo alikuwa anamwita Mzee “John” Iddi mkwe kwa sababu yeye (Mzee KK)
alimuoa Bibi Kijakazi ambaye alikuwa mkwe wa Mzee “John” Iddi. Kwa upande
mwingine, marehemu Mzee “John” Iddi (Thabit Iddi Dau) na marehemu baba yangu
mzazi (Kitwana Ramadhani Dau) ni mtu na kaka yake. Wazungu wanasema ni first
cousins, sisi Waswahili tunasema wamezaliwa nyumba kubwa na ndogo (kwa
maana ya baba mkubwa na baba mdogo) au kwa lugha nyingine tunawaita watoto wa
Simba kwa Simba. Kwa hiyo kinasaba, uhusiano wangu na Mzee Kondo ni kwa kupitia
baba yangu mkubwa marehemu Mzee “John” Iddi Dau.
Tokea
siku ile ambayo nilijitambulisha kwa Mzee Kondo, tukajenga ukaribu sana na
alikuwa ananipenda sana. Ilikuwa haipiti wiki bila kwenda nyumbani kwake Hill
Road Oyster Bay na baadae mtaa wa Mtitu Upanga kwenda kumwamkia na “kupata
habari za mjini”. Ni kutokana na mazoea
hayo ndipo Mzee KK akapata jina lingine la utani la “mzee wa mjini”. Na ni
kweli, wakati wa uhai wake, kila utakapoenda nyumbani kwa Mzee KK hukosi kupata
“habari za mjini” ingawa wakati mwingine zinakuwa ni habari au fikra zake yeye
lakini ili kuzipa uzito atakwambia kuna habari mjini kuwa …(hapo anaeleza hiyo
habari ilivyo). Moja katika hizo habari za mjini zilininufaisha sana na kuninusuru
na janga kubwa sana ambalo lingenikuta. Leo hapa si mahala pake kuzungumzia
habari hiyo. In Shaa Allah kuna siku ntaitafutia nafasi kuizungumza. Naendelea kumshukuru sana kwa hilo na mengine
mengi ambayo amenifanyia mimi na watu wengine wengi.
Mzee
KK atakumbukwa na kuliliwa na wengi kwani alikuwa mwepesi sana kusaidia watu
wenye shida. Marehemu alikuwa mcheshi na mwenye kupenda maskhara sana.
Alichanganyika na watu wa kila rika. Alikuwa mtu wa msaada sana kwa watu wa
aina zote, wake kwa waume. Nyumbani kwake kulikuwa hawapungui wageni wa kila
aina kuanzia wanasiasa, wana michezo, viongozi wa dini nk. Mmoja kati ya watu
wengi waliosaidiwa na Mzee Kondo ni marehemu Profesa Idrisa Ali Mtulia. Wakati
wa uhai wake, Profesa Mtulia alinisimulia namna ambavyo marehemu Mzee Kondo
alivyomsaidia kwenda kusoma Uingereza. IIikuwa mwaka 1978 wakati Profesa Mtulia
alipochaguliwa kwenda kusoma Clinical Fellowship kwa miaka miwili kwenye
hospitali ya Hammersmith ambayo ni sehemu ya Chuo cha Imperial London,
Uingereza. Gharama zote za masomo zilikuwa zilipwe na Serikali. Kwa bahati
mbaya siku chache kabla ya safari, jina la Profesa Mtulia halikuwemo kwenye
orodha. Profesa akawa hana la kufanya. Akaamua kwenda kuomba msaada kwa Mzee Kitwana
Kondo. Mzee Kondo akamhakikishia kuwa ataenda kusoma mwaka ule ule na wala
asiwe na hofu. Mzee Kondo akazungumza na Karimjee na baada ya siku 4 tu Profesa
Mtulia akapata udhamini kamili (full scholarship), ambao ulijumuisha tiketi ya
ndege na fedha zote za matumizi akiwa Chuoni. Udhamini huo ulitolewa na mama
yake mzazi Karimjee. Kutokana na masomo hayo, Profesa Mtulia akatunukiwa kuwa Member
of Royal College of Physicians (MRCP) na baada ya kudhihirisha umahiri wake
akatunukiwa kuwa Fellow of Royal College of Physicians (FRCP). Profesa
Mtulia alikuwa ni mmoja kati ya watu wengi waliosaidiwa na Mzee KK. Baada ya kurudi masomoni na baadaye kutunukiwa
FRCP, Watanzania waliokuwa na hadhi hiyo walikuwa wachache sana; nadhani
hawakufika 5. Mmoja kati ya hao alikuwa marehemu Dr. Aaron Chiduo; wengine
nadhani ni Profesa William Makene na Profesa Shaba.
Kwa
upande wa siasa Mzee Kondo ametoa mchango mkubwa sana kwa muda wote wa uhai
wake nje na ndani ya Serikali, Bunge, TANU na CCM. Mzee KK alikuwa mzalendo
ambaye aliitakia sana mema nchi yetu. Kwa wale wazee wa Dar es Salaam waliobaki
watakumbuka sana mchango alioutoa tokea wakati wa Ukoloni na haswa baada ya
Uhuru. Yapo mengi ya kihistoria aliyoyafanya kwa kuinusuru nchi yetu na kufika
hapa ilipofika leo. Mambo mengine hapa
si mahala pake.
Moja
kati ya sifa zake nyingi ni ujasiri. Mzee KK hakuwa mwoga na alikuwa na ujasiri
wa kusimamia jambo ambalo anaamini ni sahihi na lina manufaa kwa nchi yetu.
Mifano iko mingi. Kwa leo itoshe tu kuwa alisimamia suala la upatikanaji wa
Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro kwa kujenga hoja kwa Rais wa wakati huo Mhe
Benjamin William Mkapa mpaka Mhe Rais akashawishika kuwa ni jambo jema
kuanzishwa kwa chuo hicho kwenye majengo ya kilichokuwa Chuo cha Mafunzo cha
TANESCO. Kama kuna mtu mmoja ambaye ametoa mchango wa kipekee uliopelekea
upatikanaji wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) mtu huyo ni Mzee
Kitwana Selemani Kondo. Kwa kuenzi jitihada zake hizo, na kwa kuzingatia Mzee
Kondo ni Mwenyekiti mwanzilishi wa Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF), Taasisi
ambayo ndiyo Mmiliki wa MUM, nashauri uongozi wa Chuo ubadili jina la kampasi
ya Morogoro iitwe Muslim University of Morogoro, Kitwana Kondo Campus. Natoa rai hiyo kwa kujua kuwa Chuo kina
mpango wa kujenga kampasi nyingine Lindi (Kitunda), Kilwa (Mpara), Morogoro
(Sangasanga) na Dar es Salaam (Kigamboni). Kwa siku za usoni, Chuo kitakapoanza
kutoa Shahada za Uzamivu (PhD), nashauri Mzee Kitwana Kondo atunukiwe PhD (Honoris
Causa) posthumously.
Kwa
kawaida, Shahada ya Uzamivu ya Heshima, yaani PhD (Honoris Causa), ndiyo
shahada ya juu zaidi katika Chuo Kikuu chochote. Shahada hii hutolewa kwa watu
ambao wanaoheshimika sana na ambao wametoa mchango mkubwa katika jamii kwenye
nyanja mbalimbali. Mchango wa Mzee Kondo katika nchi yetu hauna mithali. Aidha
Mzee KK alikuwa mwepesi sana wa kuelewa vitu (sharp) na mtu wa mikakati sana.
Hakuna alilofanya bila kufikiria nini kinachoweza kutokea usoni na ni namna
gani anaweza kuikabili hiyo hali. Nimeyashuhudia hayo wakati akiongoza vikao
vya Bodi ya Mamlaka ya Bandari na ushiriki wake katika vikao vya maandalizi ya
kuazishwa kwa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro. Kwa wote ambao wamewahi
kufanyakazi na Mzee Kondo, watakubaliana nami kuwa staha yake, weledi wake, busara
zake na mchango wa katika taifa letu anastahili kutunukiwa Shahada ya Uzamivu
ya Heshima, yaani PhD (Honoris Causa).
Wakati
alipokuwa Meya wa Jiji, Mzee Kondo alithamini sana mchango wa watu mbalimbali
walioshiriki katika harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika. Ili kuweka
kumbukumbu kwa vizazi vijao, Mzee Kondo aliwashawishi madiwani wenziwe
kupitisha azimio la kubadili majina ya baadhi ya mitaa ya Dar es Salaam ili
ipewe majina ya wazee wetu wa Dar es Salaam walioshiriki kwenye harakati hizo.
Utaratibu uliotumika ni kuupa jina la mtaa kwa kila Mzee ambaye alieishi katika
mtaa huo. Mifano ya mitaa iliyobadilishwa majina ni mtaa wa Kipata (Kleist
Sykes), mtaa wa Tandamti (Mshume Kiyate), mtaa wa Aggrey (Makisi Mbwana), mtaa
wa Somali (Omari Londo), mtaa wa Ndanda (John Rupia) na mtaa wa Mwananyamala
(MwinyiJuma MwinyiKambi). Jambo la kusikitisha ni kuwa hadi leo baadhi ya mitaa
hiyo haijawekwa vibao vya majina mapya. Ili kuendeleza dhamira nzuri ya
kuwaenzi wazee wetu waliotoa mchango mkubwa katika nchi yetu naishauri Manispaa
ya Ilala ibadili jina la mtaa wa Mtitu ambapo alikuwa anaishi marehemu Mzee
Kondo na kuitwa mtaa wa Kitwana Kondo.
Sambamba
na ujasiri, Mzee KK alikuwa anaipenda sana dini yake na alikuwa mtetezi mkubwa
wa Waislamu. Ilikuwa kila ukienda nyumbani kwake ukimtajia Aya kwenye Quran
basi haraka huchukua kitabu chake kidogo (note book) na kuiandika ili
akaifanyie kazi kwa vitendo au hata kwa kuzungumza kwa wengine. Miongoni mwa
Aya ambazo Mzee KK alikuwa akizipenda sana ni Aya ya 10 na ya 11 kwenye Sura ya
61 (As-Saff), pia Aya ya 31 kwenye Sura ya 76 (Al-Insan au kwa jina lingine
Dahr). Kwa kumuenzi Mzee KK sitotoa tafsiri ya Aya hizo kwa makusudi ili
msomaji upate ushawishi wa kwenda kuzisoma mwenyewe ili nawe upate fadhila za
kuisoma Quran. Katika kuonesha mapenzi aliyonayo kwa dini yake, siku zote Mzee
Kondo alikuwa mstari wa mbele kuchangia maendeleo ya Waislamu. Moja katika
jitihada zake nyingi ni kupatikana kwa kiwanja ambacho kimejengwa Masjid Maamur,
Upanga.
Mzee
Kondo alijivunia sana Uswahili na Uzaramo wake. Watoto wake wengi aliwapa
majina ya Kizaramo kama vile Mtogole, Azimala, Msakuzi nk. Pamoja na nyadhifa
mbalimbali alizokuwa nazo Serikalini, kamwe Mzee Kondo hakusahau marafiki zake
ambao wengi wao walikuwa ni watu wa kipato cha chini sana. Baadhi yao ni
marehemu Mzee Kibiriti, marehemu Mzee Sindano, marehemu Omar AbdulRahman
maarufu “Ugundo”, Mzee Gulu, Captain Maliki, marehemu Ramadhani Mangilile, marehemu
Ali Abbasi, na marehemu Mapepe. Wengine ni marehemu Hamisi George, marehemu Abbas
Mzee, marehemu Saleh Mtumwa, marehemu Maalim Mbegu wote wa Egyptian Musical
Club. Hao na wengine wengi wanaofanana na hao ndiyo waliokuwa wazungumzaji wa
Mzee KK. Ilikuwa haipiti mwezi bila ya Mzee Kondo kwenda Kariakoo (na haswa
klabu ya PAN) kwenda kupiga soga na watu wa mjini wenziwe.
Ukaribu
wake na watu wa kawaida umefanya mpaka baadhi ya watu wafikirie kuwa Mzee Kondo
hakusoma shule. Nakumbuka mwaka 1996 wakati Mzee Kondo akiwa Mwenyekiti wa
Bandari nilikwenda Shirika la Bima ya Taifa (NIC) kufuatilia madai ya gari
yangu MUSSO TZH 3336 ambayo ilipata ajali. Nilifika NIC na kuonana na Afisa mhusika
wa madai. Katika mazungumzo yetu akabaini kuwa mimi ni Mkurugenzi wa Masoko wa
THA. Alinipa pole sana kwa sababu kwa maneno yake mwenyewe, THA tumepata
Mwenyekiti ambaye hajui kusoma. Alishangaa Mzee Kondo anawezaje kusoma
makabrasha na kuongoza vikao vya Bodi ikiwa hata kuzungumza Kiingereza hawezi.
Nikamjibu kuwa Mzee Kondo ni msomi kwani mwaka 1963 alihitimu shahada kwenye “Strategic
Studies” kwenye Chuo Kikuu cha Howard Washington DC, Marekani. Aidha Mzee
KK amepata mafunzo kwenye nchi kadhaa zikiwemo Ujerumani na Yugoslavia. Yule
afisa hakuamini na tukawa na malumbano makali sana. Msingi wa hoja yake ni kuwa
mzee KK anaandikwa vibaya sana kwenye gazeti (pamoja ya kuwa kwa sasa gazeti
hilo limekufa lakini jina nalihifadhi) na picha inayojitokeza ni kuwa mzee huyu
hakusoma kabisa.
Nimesema
hapo awali kuwa Mzee Kondo alikuwa anajichanganya sana na watu wa aina na rika
zote. Nina hakika si wengi wanaofahamu kuwa wakati wa uhai wake Mzee Kondo aliwahi
kuwa Katibu wa klabu ya Yanga, Dar es Salaam miaka ya 1950s. Pia mwaka 1962
alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga. Wakati huo Mwenyekiti alikuwa Mzee Mohamed
Sultan Mabosti, Katibu Mkuu ni Mzee Jabiri Katundu (alichukua nafasi hiyo
kutoka kwa Mzee Juma Vijiga) na Makamu wake Mzee Juma Shamte. Wote hao
wameshatangulia isipokuwa Mzee Jabiri Katundu ambaye anaishi kwenye nyumba yake
ile ile iliyopo Ilala mtaa wa Tabora. Tunamwomba Mwenyezi Mungu Ampe Mzee
Jabiri umri mrefu na wenye tija ili tuendelee kuvuna busara zake sio tu katika
masuala ya mpira bali maisha kwa ujumla.
Kati ya mambo mengi sana ambayo nimejifunza kutoka kwa Mzee KK ni kuwa unapoitwa na mkubwa wako wa kazi iwe ofisini au nyumbani jiandae kwa kujua saa ya kuitwa na sio saa ya kuondoka. Katika hili alinisimulia kisa kimoja wakati akiwa Meya wa Dar es Salaam. Kuna Jumapili moja Mwalimu Nyerere aliwaita viongozi wa Mkoa (akiwemo Mzee KK) nyumbani kwake Msasani saa 4 asubuhi. Ujumbe huo uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa wakati huo. Walipofika Msasani wakakuta Mwalimu ameenda kanisani. Baada ya misa Mwalimu akaenda ofisini Ikulu. Ujumbe ulisubiri Msasani kwa muda mrefu. Ilipofika saa 7 mchana Mkuu wa Mkoa akatoa rai kuwa waondoke na kama kutakuwa na taarifa yoyote watafahamishana. Mzee KK alirudi nyumbani kwake Hill Road Oyster Bay. Haikuchukua muda kapigiwa simu kuwa Mwalimu anamwita Msasani. Alipofika Msasani Mwalimu akataka kujua sababu zilizomfanya Mzee Kondo asiende nyumbani kwake saa 4 asubuhi kama alivyoagiza. Mzee Kondo akajitetea kuwa alikwenda saa 4 kama alivyoagiza na walisubiri hadi saa 7 ndipo kiongozi wa msafara wao Mkuu wa Mkoa akawaruhusu waondoke. Mwalimu akamwambia Mzee Kondo kuwa yeye aliwapa muda wa kufika Msasani saa 4 asubuhi lakini hakuwaambia muda wa kuondoka. Baada ya maneno hayo Mwalimu akamwambia kuwa ameshatengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa na kwamba yeye Mzee Kondo ana bahati kwani yeye ni diwani wa kuchaguliwa kwa hiyo hana namna ya kumfukuza kazi.
Mzee
Kondo ameondoka na mambo mengi kifuani mwake. Alikuwa hazina kubwa sana kwa
taifa. Mimi binafsi nimejaribu mara kadhaa kumwomba aandike historia yake lakini
alikataa kabisa. Pamoja ya kuwa Mzee Kondo alinisikiliza na kukubali ushauri
wangu kwenye mambo mengi, lakini hili la kuandika historia yake alikataa
kabisa. Mara zote ninapokuwa namkumbusha kuhusu suala hili jibu lake lilikuwa “Bwana
Dau, mie mzee, nataka nife huku nimenyooka”. Kwa bahati mbaya sana udhaifu huu
wa kutoandika historia zao wanao viongozi wetu wengi. Wamebeba hazina kubwa na
wakiondoka wanaondoka nazo bila kutuachia urithi huo adimu. Sisi wazee
watarajiwa tusirudie makosa ya wazee wetu. Tujenge utamaduni wa kuandika ili watakaokuja
baada ya sisi wanufaike na uzoefu wetu.
Yapo
mengi sana ya kuandika kuhusu Mzee KK lakini nafasi hapa haitoshi. Kwa kumalizia,
kwa wale wasiofahamu, Mzee KK alikuwa mpenda sana mashairi. Miongoni mwa
mashairi yake aliyokuwa akiyapenda ni shairi la Muyaka bin Ghassany wa Mombasa.
Alipoanza kuumwa kiasi miaka 3 iliyopita ilikuwa kila nikienda kumjulia hali
huwa namsomea shairi la Muyaka. Pamoja na kutokuwa na fahamu lakini nikianza tu
kumsomea shairi la Muyaka hufungua macho na kunitazama kisha akatokwa na
machozi na baadae kufunga macho. Kwa kumuenzi Mzee Kitwana Kondo, nimeamua
kulinukuu shairi ambalo wakati wa uhai wake, alikuwa analisoma ghibu.
Akutendeae Mema, Kushukuru
ni lazima
Jaza ya mema ni mema, Maovu
kutoyatia
Mbona umeghafilika? Kwa
jambo lisilo shaka?
Shetani umemshika, Na
kumuacha Nabia?
Unajifanya Mtesi, Kwa
Mola wako Mkwasi
Unavitupa viasi, Sina
la kukwambia
Silaha zote ni Zake, Wala
na riziki Zake
Unakunywa maji Yake, Mbona
umekosa haya?
Vita vyako fahamu, Havimdhuru
Karimu
Ila wewe Bahaimu, Jijue
Utaumia
Itunze yako fikara, Uwafikiri
mabora
Wenye ngome na minara, Na
panga za kuchinjia
Yatafakari mauti, Yeyote
hayamuachi
Wala hayana wakati, Ghafla
hukujilia
Yu wapi Firauni, Yu
wapi Karuni
Na Shadadi maluuni, Wote
wameangamia
Zao zilipokwisha, Ziraili
kawafisha
Wameyawacha makasha, Na
mambo haya na haya
Waimefika akhera, Madhalili
mafukara
Uwapi wao bora, Wote
umewakimbia
Kaburi zimewakaza, Hapana
la kupumbaza
Kote kumefunga kiza, Adhabu
kuwashukia
Adhabu hiyo ni kuu, Tena
motoni kuwa juu
Majuto ni mjukuu, Tahadhari
na dunia
Wapita na Siratini, Kuwangukia
motoni
Kuteketea maini, Maisha
kuteketea
Na yote ninayoyasema, Yatakufika
lazima
Safari mbele na nyuma, Wengine
hutangulia
Kitwana Kondo alipokuwa Meya wa Dar es Salaam |
Naam
ni kweli kabisa safari ni mbele na nyuma wengine hutangulia. Mzee KK
ametangulia. Kwa kuondokewa na Mzee Kitwana Selemani Kondo, Dar es Salaam
imepwaya sana. Jiji limegubikwa na simanzi na ukiwa na hasa ukizingatia kuwa
tokea mwaka huu uanze Dar es Salaa imeondokewa na Kamanda Dr. Mohamed Awadh
(Chiko), Mzee Iddi Sungura, Mzee Issa Ausi (“Smart Boy”) na hivi karibuni Ali
“Bob” wa Cosmopolitan. Maskini Dar es Salaam, imeondokewa na kubaki mkiwa.
Mwenyezi
Mungu Amlipe mema na azipe uzito amali za Mzee Kitwana Kondo ziwe na mizani ya
juu kuliko mapungufu yoyote ya kibinaadamu ambayo alikuwa nayo. In-ShaAllah
Mwenyezi Mungu Amruzuku Pepo na In-ShaAllah Atukutanishe Peponi Firdaus, Ameen.
No comments:
Post a Comment