Muhammad
Ali bingwa wa masumbwi aliandika kitabu cha maisha yake, ‘’The Greatest My Own
Story,’’ ambamo ndani yake ameeleza pigano lake na George Foreman kwa kirefu
sana. Huyu George Foreman alipigananae mwaka wa 1974 na katika maisha yake yote
katika masumbwi hapakutokea mpiganaji dhidi yake ambae watu waliona kuwa safari
hii Ali atapigwa ila huyu Foreman.
Sababu
kubwa ya watu na washabiki wa Ali kuona kuwa safari hii Ali hatovuka kiunzi ni
kuwa Foreman alimpiga mpinzani mkubwa wa Ali, Joe Frazier katika raundi ya tatu
na Frazier akiangushwa chini mara tatu katika raundi moja. Kila aliyepigana na
Foreman alikuwa hakatizi raundi ya tatu anakuwa yuko chini hoi. Wengi wakadhani
kuwa na Alii ataishia chini kama waliomtangulia kupigana na Foreman.
Katika
hiki kitabu chake Ali aliweka sura akaipa jina, ‘’Bossman Comes,’’ katika sura
hii ndimo alimoeleza pigano lake na Foreman kwa kirefu sana. Bossman ni jina la
mpiganaji masumbwi wa uzito wa juu, pandikizi la jitu na alikuwa ndiyo,
‘’sparring partner, yaani mfanya mazoezi ya kupigana. Huyu Bosman ndiye Foreman
akifanyanae mazoezi.
Ali
katika mkakati wake wa mazoezi alitaka kujua kila kitu na mbinu zote za Foreman
aliyekuwa na sifa za kuwamaliza wapinzani wake chini ya raundi ya tatu. Kwa
ajili hii basi alimuajiri Bossman kama, ‘’sparring partner,’’ wake ili amfunze
mbinu na kumpa siri za mpinzani wake Foreman ulingoni.
Ali
alikuwa anafanya mazoezi ya raundi 30 kila siku akijitayarisha kwa pambano
hilo.
Lakini
Bossman alimuambia Ali bila kumficha kitu kuwa hatoweza kumpiga Foreman na
akamueleza sababu zake kwa nini Ali atapigwa. Alimwambia Ali kuwa Foreman ana
ngumi nzito na nguvu nyingi atakuwa anamsukuma nyuma kama karatasi. Ali
alimuuliza Foreman, ‘’Niambie, Foreman anaweza kujitolea kufa ili ashinde abaki
na taji?’’
Wakati
ule Foreman ndiye alikuwa anashikilia taji la dunia la uzito wa juu.
Hapa Ali
alitaka kujua ujasiri wa Foreman. Bossman alitingisha kichwa kuonyesha shaka.
Katika pigano lile ilipofika raundi ya tatu Ali alikuwa bado yuko wima na akimrushia
Foreman makonde ya uhakika.
Ali
anasema alijua Foreman atachoka haraka na atampiga kwa sababu ngumi zake nyingi
zilikuwa hazimpati zikiishia hewani na katika mchezo wa ngumi Ali anasema, hiyo
ni dalili mbaya kwani mpiganaji anajichosha mwenyewe akimwacha mpinzani na
nguvu zake.
Katika
pigano lile Foreman alipigwa kwa, ‘’knockout.’’
Wataalamu
wa masumbwi wanasema kilichomfanya Foreman apigwe ni kitu kimoja tu nacho ni
kutegemea ushindi wa haraka wa raundi tatu. Foreman hakuwa amejitayarisha kwa
safari ndefu ya jasho na damu. Ali alikuwa akifanya mazoezi ya raundi 30 ilhali
masumbwi ni raundi 15.
Nimekileta
kisa hiki cha Ali na Foreman kutaka kuwafikirisha wasomaji wangu. Nilikuwa
nasoma hapa FB jinsi baadhi ya watu wanaomuunga mkono Prof. Lipumba walivyokuwa
wamefurahishwa na kufukuzwa kwa wabunge 8 wa CUF na Spika wa Bunge kwa kasi ya
ajabu kuwafuta ubunge na Tume ya Uchaguzi kupokea majina ya wabunge wapya
walioteuliwa.
Lakini
kilichonishangaza zaidi ni pale nilipoona katika TV jinsi baadhi ya hao
"wabunge," walioteuliwa walivyokuwa wakijibu maswali na kufurahi na
kuona kuwa tayari wameshakuwa washindi na weshaapishwa na kuwa wabunge. Nikawa
najiuliza, ‘’Inakuwaje watu wetu wakawa na uwezo mdogo wa kutafakari mambo
kiasi hiki kufikia kushindwa kuona kuwa hivi ni vita vikubwa na sasa vilikuwa
vinaingia katika kipindi muhimu na kigumu kitakachoacha katika sakafu damu
nyingi sana, inawezekanaje?’’
Ndipo
kiliponijia hiki kisa cha Muhammad Ali na mipango yake ya kupigana pambano la
muda mrefu na kwa mkakati huu akaibuka mshindi.
Mgogoro
wa CUF sasa uko katika kipindi muhimu sana na Tanzania inaandika historia mpya.
Wabunge 8 waliofukuzwa na Prof. Lipumba wamekwenda mahakamani na kwa mara ya
kwanza Spika, Msajili wa Vyama Vya Siasa, Mkurugezi wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi na hao ‘’Wabunge,’’ waliochaguliwa na Prof. Lipumba watasimama
mahakamani kujibu mashtaka kama washitakiwa. Haya si waliyotegemea hasa kwa
hawa ‘’Wabunge,’’ watarajiwa, hawa hawakutegemea kabisa kushtakiwa.
Hivi sasa
sakata hili linaingia katika safari ndefu ya nenda rudi, panda shuka ya
mahakama. CUF wana uzoefu wa kutembea safari ndefu zenye shida, mihangaiko na
damu na hii ndiyo silaha yao kubwa iliyowawezesha kuwapo hadi leo na kubaki
wakiwa na nguvu kubwa juu ya shida zote walizopitia.
Kuanzia
juzi naona hali imebadilika kwa upande waliokuwa wakifurahi kwa kupata
‘’Wabunge,’’ wapya. Ukweli wa hali halisi taratibu unazama na kueleweka uzito
wake kuwa hii si safari ya raundi tatu alizotegemea Foreman bali hii sasa ni
safari ya raundi 30 alizokuwa anazisubiri Ali na akawa amejitayarisha kwa
safari ya mwendo mrefu. Ali alimuuliza Bossman ikiwa Foreman yuko tayari kufa
kupata ushindi. Je, hawa wanaopelekwa makahamani bila ya khiyari zao wako
tayari kubeba zigo hili zito ambalo hawakujitayarisha wala kutegemea?
Kwa kuhitimisha ningependa ieleweke kuwa pambano hili la Ali na Foreman la
mwaka wa 1974 juu ya umaarufu wake si, ‘’Pambano la Karne,’’ kamwe. Pambano la
Karne ni lile Ali alipopigana na Joe Frazier mwaka wa 1971 na Ali akashindwa
kwa, ‘’points.’’
Ukifika
Madison Square Garden, New York ambako ndipo walipopigana Ali na Frazier
katika, ‘Pambano la Karne,’’ nje liko bango kubwa sana la wanamasumbwi hawa.
Naingia maktaba kutafuta picha ya bango
hili nikiiipata nitaiweka hapa jamvini.
LikeShow more reactions
No comments:
Post a Comment