Thursday 27 July 2017

KUTOKA FB: MGOGORO WA CUF UMESHABIHIANA NA MGOGORO WA EAMWS WA 1968

Ndugu zangu hapajatokea mgogoro mkubwa kama mgogoro wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) wa mwaka wa 1968.

Mgogoro huu umeacha athari kubwa sana katika maendeleo ya Waislam wa Tanganyika. Huu ndiyo mgogoro ambao uliokuja kuleta Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA).

Wakati mgogoro huu unazuka EAMWS ilikuwa katika mipango ya kujenga Chuo Kikuu Cha Kiislam, Chang’ombe Dar es Salaam na kila kitu kilikuwa kimekamilika. 

Mgogoro huu uliwaondoa katika uongozi viongozi wote waliokuwa na ridhaa ya Waislam kuanzia Mufti Sheikh Hassan bin Amir hadi Tewa Said Tewa na ukaja uongozi mpya ambao hakuna Muislam alijua umetokea wapi.

Hili liliwezekana vipi? 

Watafiti wawili tu ndiyo waliotafiti na kuandika historia hii - Dr. Mayanja Kataroge Kiwanuka na mtu mmoja anaitwa Mohamed Said. 

Yaliyoelezwa na watafiti hawa yanatofautiana sana. 

Utafiti wa Dr. Kiwanuka uko katika tasnifu yake: ‘’The Politics of Islam in Bukoba District,’’ (1973), utafiti wa Mohamed Said ni ‘’Islam and Politics in Tanzania,’’ Al Haq International, Karachi (1989). 

Kwa nini kuna matokeo yanayokinzana katika utafiti wa somo moja na kwa nini nimeeleza haya? 

Dr. Kiwanuka alikuwa na bwana anaemtumikia kwa hiyo utafiti wake ulikuwa lazima useme kile anachokitaka bwana na alikuja kuwa kiongozi mkubwa wa CCM Makao Makuu, Dodoma.

Nimesoma hapa naona wengi wa wachangiaji wanazungumza kuwa katika huu mgogoro wa CUF kuna nguvu kutoka nje inayosaidia upande mmoja. 

Hali ilikuwa kama hii mwaka wa 1968 katika mgogoro wa EAMWS.


Vyombo vyote vya dola vilikuwa vikitumikia upande mmoja wa wa kile kilichoitwa mgogoro wa Waislam. 

Kwa ushahidi wa mazingira kulikuwa na mkono kutoka nje ukisaidia upande mmoja na matokeo ya mgogoro ule kila Muislam anaujua. 

Mgogoro wa EAMWS na huu wa CUF unafanana sana.
Viongozi wa EAMWS walitimuliwa kama leo viongozi wa CUF wanavyotimuliwa. 

Swali la kujiuliza ni kuwa iliwezekanaje viongozi wenye hadhi zao katika jamii ya Waislam kama Mufri Sheikh Hassan bin Amir kufukuzwa katika uongozi wa Waislam na mtu kama Adam Nasibu? 

Leo inawezekanaje viongozi wa CUF na wao wakafukuzwa, viongozi ambao wamechaguliwa na wananchi na badala yao wakaletwa watu ambao haijulikani hata walikotokea?

Hii inawezekanaje na nani ananufaika katika mgogoro huu? 
Je haya yana maslahi na taifa letu? 

Kuvunjwa kwa EAMWS kulikuwa katika maslahi ya taifa letu? 
Jambo hili linataka utulivu wa fikra kulielewa.

No comments: