Wednesday 5 July 2017

KUTOKA RAIA MWEMA: ALI MWINYI TAMBWE NI NANI HASA? MAKALA YA EZEKIEL KAMWAGA

Chini katikati waliokaa ni Sheikh Kassim Juma 
Nyuma kushoto ni Sheikh Hassan bin Amir, Al Habib Sheikh Omar bin Sumeit na Abbas Sykes
Nyuma katikakati ya Al Habib Sheikh Omar bin Sumeit ni Ali Mwinyi Tambwe

Raia Mwema limemwandika Ali Mwinyi Tambwe katika moja ya makala zake katika toleo la Julai 5 - Julai 11, 2017. Binafsi nimemfahamu Ali mwinyi Tambwe toka utoto wangu. Nilikutana na Ali Mwinyi Tambwe katika Nyaraka za Sykes wakati wa utafiti wa kitabu cha Abdul Sykes na hivi ndivyo nilivyomwandika Ali Mwinyi mzalendo aliyefanya mengi lakini yeye mwenyewe hakupenda kuyaeleza:

1954
''Kumbukumbu zinaonyesha kwamba Idd Faiz Mafongo alihudhuria mkutano wa uzinduzi wa TANU katika Ukumbi wa Arnautoglu. Haifahamiki kwa hakika hasa ni lini Idd Faiz alijiunga na TANU kwa sababu kadi yake ya kwanza ya uanachama ilipotea na akapewa kadi nyingine iliyokuwa na namba 915 iliyotolewa tarehe 28 Agosti, 1954. Lakini kwa kukisia tu kutokana na kadi ambayo Idd Faiz mwenyewe aliitoa kwa kaka yake Idd Tosiri ambayo ilikuwa kadi namba 25 na yenye saini yake kama afisa aliyetoa kadi hiyo, inaweza kuchukuliwa kwa uhakika kuwa Idd Faiz alikuwa miongoni mwa wale watu wa mwanzo kabisa kuingia TANU na huenda akawa miongoni mwa wanachama ishirini wa mwanzo. Ukichukua katika fikra ukweli kwamba Ali Mwinyi Tambwe aliyekuwa katibu wa Al Jamiatul Islamiyya aliingizwa TANU na Mtemvu katikati ya mwezi Agosti, 1955, huenda Ally Mwinyi kama katibu wa Al Jamiatul Islamiyya na Idd Faiz akiwa mweka hazina, wote wawili waliingia TANU wakati mmoja.''

Kushuto: Idd Faiz Mafongo, Sheikh Mohamed Ramia, Julius Nyerere, Saadan Abdu Kandoro na Haruna Taratibu, Dodoma. Idd Faiz Mafongo alikuwa Mweka Hazina wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika na pi Mweka Hazina wa TANU chama kilikpoasisiwa 1954. Yeye ndiye aliyeaminiwa kukusanya fedha za safari ya kwanza ya Julius Nyerere UNO, New York 1955


''Ilikuwa wakati Nyerere yuko Musoma ndipo John Hatch kutoka Chama cha Labour cha Uingereza alipokuja Tanganyika kama mgeni wa TANU. Chama kilifanya mkutano mkubwa sana Mnazi Mmoja na Hatch akawahutubia wananchi. Inakisiwa takriban wanachama wa TANU na mashabiki wake jumla yao kiasi watu elfu ishirini walijitokeza kwenye mkutano huo. Ali Mwinyi Tambwe alikuwa mkalimani wa Hatch. Denis Phombeah pamoja na katibu mkuu wa TANU, Oscar Kambona vilevile walihutubia halaiki ile. Hatch akiwa anaunga mkono ukombozi wa watu weusi aligundua kuwa TANU haikuwa na tawi la akina mama. Katika dhifa ya chai iliyoandaliwa na TANU kwa heshima yake, Hatch alilieleza tatizo hili kwa Schneider Plantan na John Rupia. Hatch alimwambia Schneider kwamba ili kuwa na chama chenye nguvu TANU isiwaache akina mama nyuma. Hatch alimwambia Schneider kwamba huko Uingereza Chama cha Labour kilikuwa kimejikita kwa wanawake kama moja ya nguzo yake kuu.''



1955
''Mkutano mkuu wa mwaka wa TANU ulifanyika katika ukumbi wa Hindu Mandal mjini Dar es Salaam. Siku kabla ya mkutano TANU ilimwalika Gavana Edward Twining kwenye tafrija katika Ukumbi wa Arnatouglo lakini alikataa kistaarabu na akamtuma Chief Secretary, Bruce Hutt, kumwakilisha. Baada ya mkutano, wakati wajumbe wengine wanaondoka kurudi kwenye majimbo yao, Mpunga na Mnjawale walibakia nyuma kukutana na uongozi wa makao makuu wa Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe, Said Chamwenyewe, Oscar Kambona na wengineo. Mpunga na Mnjawale waliwafahamisha viongozi wa makao makuu kuhusu hali mbaya ya siasa Jimbo la Kusini. Mbali na kampeni za kuipinga TANU za Mponda, katika ziara yake Lindi Gavana Twining aliwatahadharisha Waafriika wa Tanganyika wasijihusishe na ‘’wafanya fujo wanaotaka kuzusha vurugu.’’ Twining alikuwa akitoa onyo hili akiikusudia TANU ambayo ilikuwa imeanzishwa mwaka uliopita. Hotuba hii ya Gavana iliwatisha wananchi kujiunga na TANU. Mpunga na Mnjawale walisisitiza kuwa kuja kwa Nyerere mjini Lindi kulitakiwa haraka sana kukabiliana na vyote viwili, kwanza ile hotuba ya gavana na pili zile kampeni za kupinga TANU zilizokuwa zikiendeshwa na Liwali Yustino Mponda.'' 

Mkutano wa kwanza wa TANU Hindu Mandal Hall, Dar es Salaam 24 Oktoba 1955

''Wakati huo Abeid Amani Karume aliyehudhuria ule mkutano alimwalika Nyerere afanye ziara Zanzibar. Kitu cha kustaajabbisha ni kuwa, Nyerere alionekana kuiafiki zaidi ziara ya Zanzibar kuliko ile safari ya kwenda kusini kuiimarisha TANU. Mpunga alimsisitizia Nyerere umuhimu wa yeye kwenda Lindi ambako kunaweza kuwa ndiyo chanzo cha TANU kupata ufanisi Newala, Songea, Tunduru na Masasi ambako kulikuwa na upinzani mkubwa dhidi ya TANU. Kanisa lilikuwa likiwazuia Wakristo kujiunga na TANU. Sheikh Suleiman Takadir, Said Chamwenye, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe wote waliunga mkono ule ujumbe wa Lindi juu ya suala hili. Baada ya kufikia makubaliano, Mpunga na Mnjawale walipewa barua ya kuthibitisha safari ya Nyerere.  Ziara ya Nyerere ilikuwa ianze muda mfupi kutokea hapo kwa kuwa ilikuwa ndiyo siku za mwisho za kiangazi. Barabara sehemu ya kusini ya Tanganyika zilikuwa hazipitiki wakati wa masika, zikiitenga kabisa kusini toka sehemu zilizobaki za nchi. Ali Mwinyi Tambwe na Rajab Diwani walifuatana na Nyerere kwenda Jimbo la Kusini kuondoa wasiwasi na woga uliozushwa na Gavana Twining na kibaraka Yustino Mponda.''

Abeid Amani Karume

''Julius Nyerere, Ali Mwinyi Tambwe na Rajabu Diwani waliwasili Mikindani kutoka Lindi siku ya Jumamosi. Kabla ya kuwasili ujumbe huo, kazi kubwa kuliko zote waliyokuwanayo uongozi wa TANU Mikindani ilikuwa kutafuta mahali pa kumlaza Nyerere. Walimwendea Ahmed Adam, Mnubi mmoja tajiri na mtu wa makamo, aliyemiliki nyumba moja ya fahari. Nyumba hii ilikuwa ya ghorofa moja na ilijengwa kwa mawe na chokaa. Ahmed Adam aliombwa awe mwenyeji wa Nyerere na ujumbe wake. Nyumba hii tayari lilikuwa na kisa chake. Ilijengwa na hayati kaka yake Ahmed Adam baada ya Vita Kuu ya Kwanza. Kaka yake alikuwa askari wa Kinubi aliyekuwa katika jeshi la Wajerumani. Huenda alichukuliwa Misri mwishoni mwa  mwa karne ya kumi na tisa na Wajerumani kuja Tanganyika kama mamluki katika jeshi la Wajerumani wakati wa vita vya Maji Maji. Baada ya vita alilipwa kiinua mgongo na serikali ya Ujerumani na kwa kutumia fedha hizo alijenga nyumba hiyo. Katika Vita Kuu ya Kwanza yeye alipigana katika jeshi la Wajerumani dhidi ya Waingereza. Baada ya vita Wajerumani wakiwa wameshindwa vita,  Waingereza waliitikadi nyumba hiyo kama mali ya adui wa himaya ya Kiingereza na kwa hiyo ilibidi itaifishwe. Hii ilikuwa ndiyo nyumba pekee iliyokuwa nzuri yenye kumilikiwa na Mwafrika na kwa ajili hii haikuweza kukosa kuhusudika.''

...imeandikwa kwa msaada wa mada iliyowasilishwa na Aisha Daisy Sykes katika semina ya historia Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam mwaka wa 1968. Daisy aliandika mada hii kwa msaada wa baba yake Abdulwahid Sykes, kutokana na mswada ulioandikwa na Kleist Sykes. Angalia A.D. Sykes ‘’The Life of  Kleist Sykes,’’ University  of  Dar es Salaam Ref. No. JAN/HIST/143/15). Habari nyingine kuhusu Al Jamiatul Islamiyya zinatokana na mswada ulioandikwa na Tewa Said Tewa, ''A Probe Into the History of Islam in Tanganyika,'' (haujachapishwa). Habari nyingine zinatokana na maelezo ya Ali Mwinyi Tambwe aliyekuwa katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika katika miaka ya mwanzo ya 1940. Historia ya Nyerere na siasa za Jimbo la Kusini (Lindi) 1955 maelezo kutoka kwa Ali Mwinyi TambweYusuf Chembera na Salum Mpunga. Taarifa nyingine kutoka kwa Nyaraka za Sykes.

No comments: