Monday 3 July 2017

WALIFIKAJE TAREHE 7 MWEZI WA SABA 1954 NA KUASISI TANU?


Waasisi wa TANU 1954


Kushoto wa pili aliyekaa ni Mashado Ramadhani Plantan
Kushoto waliosimama wa kwanza Mwalimu Mdachi Shariff

Kuna mtaa Dar es Salaam sisi tulimezaliwa tumeukuta ukiitwa Stanley Street. Baada ya kupatikana uhuru mtaa huu ukabadilishwa jina ukaitwa Aggrey Street kisha baadae wakati marehemu Kitwana Kondo alipokuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam ukabadilishwa tena jina ukaitwa Mtaa wa Max Mbwana. Mtaa huu umepewa majina ya watu maarufu watatu ambao wote wamekuwa na uhusiano wa kihistoria kuanzia Tanganyika hadi kufika Tanzania. Henry Morton Stanley ndiye aliyetumwa kuja Tanganyika kumtafuta David Livingstone na akamkuta Ujiji. Dr. Aggrey alikuwa Mwafrika kutoka Ghana. Umaarufu wake unatokana na kuwa yeye alikuja Tanganyika mwaka wa 1924 akiwa mmoja wa wajumbe wa kamisheni iliyokuja Tanganyika kuja kuchunguza elimu ya Waafrika. Wajumbe wengine wote waliobakia katika kamisheni hii walikuwa Wazungu. Kleist Sykes anaeleza katika mswada wa maisha yake alioandika kabala ya kifo chake mwaka wa 1949 kuwa alikuwa Dr.Aggrey ndiye aliyemtia hima aunde African Association. Dr. alimpa Kleist ushauri huu baada ya kutambua kuwa Waafrika wa Tanganyika hawakuwa na umoja wao, wakati Wazungu, Waasia na Waarabu wote tayari walikuwa na jumuia zao. Katika mswada wake ule Kleist anasema kuwa Waafrika waliwakiishwa na Father Gibbons kutoka Misheni ya Minaki ambae yeye anastaajabu kwa kuwa hakuwa na uhusiano wala muiingiliano wowote na Waafrika wa Tanganyika.


Father Gibbons ni huyo wa kwanza waliosimama kushoto

Kwa sifa hii ya Aggrey kuja Tanganyika akiwa Mwafrika msomi  Jiji la Dar es Salaam wakabadili jina la Stanley na kuliweka jina la Dr. Aggrey. Kitwana Kondo akiwa Meya wa Dar es Salaam akabadili tena jina la mtaa kutoka Aggrey ukaitwa Mtaa wa Max Mbwana. Mzee Max Mbwana alikuwa mmoja wa wazee maarufu wa Dar es Salaam waliounga mkono harakati za kuunda TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.  


Baraza la Wazee wa TANU 1950s


1.        Abdallah Shomari (Tandamti Street No. 3)
2.       Nassoro kalumbanya (simba str.)
3.        Said Chamwenyewe (Aggrey/Congo Street)
4.       Mtoro Ally (Muhonda Street.)
5.       John Rupia (Misheni Kota)
6.        Julius Nyerere( Pugu Sekondari)
7.       Said Chaurembo (Congo/Mkunguni Street.)
8.       Jumbe Tambaza( Upanga)
9.       Sheikh Suleiman Takadir (Mafia /Swahili)
10.    Dossa Aziz ( Mbaruku /Somali Kipande Street )
11.      Mshume Kiyate (Tandamti Street)
12.     Juma Sultan (Kitchwele karibu na kanisa dogo )
13.     Maalim Shubeti (Masasi/Likoma Street)
14.     Rajab Simba (Kiungani Street)
15.     Waziri Mtonga (Kilosa no. 18, Ilala)
16.     Mwinjuma Mwinyikambi (Mwananyamala)
17.     Maxi Mbwana ( Aggrey /Kongo  Street)
18.     Usia Omari (Sungwi ,Kisarawe) 
19.     Sheikh Issa Nasir (Bagamoyo) 
Kulia wa pili waliokaa Sheikh Suleilan Takadir Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU 1954 - 1958) 
(Swahili/Kariakoo Street)

Muhimu kufahamika ni kuwa Jiji la Dar es Salaam lilipotoa jina la mtaa wa huu kwa Dr. Aggrey hawakutoa kwa kuenzi ile fikra yake ya kuwataka Waafrika waunde African Association. La hasha, jina la mtaa lilitolewa kwa ile sifa yake ya yeye kuwa Mwafrika msomi aliyefika Tanganyika wakati ule wa ukoloni. Max Mbwana alipewa mtaa kwa mchango wake katika kuunga mkono TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika. 


Mayor Kitwana Selemani Kondo

Kushoto: Mwinjuma Mwinyikambi, Max Mbwana Julius Nyerere na Mshume Kiyate, 1962
Historia ya TANU inaanza hapa alipofika Dr. Aggrey Tanganyika na kumshauri Kleist na wenzake kuanzisha umoja wa Waafrika wa Tanganyika. Hata hivyo ilimchukua Kleist miaka mitano hadi 1929 kuasisi African Association akiwa katibu muasisi na rais muasisi akiwa Cecil Matola. Mkutano wa kuunda African Association ulifanyika nyumbani kwa Cecil Matola Mtaa wa Ndanda na Masasi. Nyumba hii baadae ikaja kununuliwa na John Rupia na ipo hadi leo. Waliokusanyika pale kuasisi African Association walikuwa Kleist Sykes, Cecil Matola, Mzee bin Sudi, Ibrahim Hamis, Zibe Kidasi, Ali Said Mpima, Suleiman Majisu, Raikes Kusi na Rawson Watts. Hili lilikuwa kundi la wazalendo tisa walioanza kufunga safari ngumu ya kuelekea New Street kuja kuunda TANU tarehe 7 Julai 1954. Bahati mbaya sana ni kuwa wazalendo hawa hawafahamiki katika historia ya Tanganyika na kwa hakika historia hii isingelijulikana kama Kleist asingeandika historia ya maisha yake. 
Kleist Sykes (1894 - 1949)

Kushoto: John Rupia, Julius Nyerere na Zuberi Mtemvu
Waliosimama nyuma ni Bantu Group kikundi cha walinzi wa viongozi wa TANU na wahamasishaji na nyuma yao wa kwanza mwenye shati jeupe ni Ali Msham mzalendo wa kwanza kufungua tawi la TANU Magomeni Mapipa 1955


Mswada wake huu ulichukua miaka 24 hadi 1973 kufikia kuchapwa na kama si juhudi za John Iliffe mswada ungebaki kama ulivyoandikwa na mwishowe kutoweka kama zilivyotoweka nyaraka nyingi katika historia ya Waafrika wa Tanganyika. Mswada huu ulichapwa katika kitabu alichohariri Iliffe, ‘’Modern Tanzanians,’’ Kilichopigwa chapa na Tanzania Publishing House. Nyaraka hizi za Sykes zimesaidia sana katika kuhifadhi si historia hii ya African Association bali hata historia ya TANU. Abdul Sykes alimpa mswada huu pamoja na nyaraka nyingine binti yake Daisy, wakati ule mwanafunzi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na kupitia nyaraka hizi mwalimu wake wa historia, John Ilife aliweza kujua mengi ambayo yalimsaidia katika kuiandika kwa uhakika historia ya African Association. Nyaraka hizi ndizo nyaraka pekee zilizoweza kuhifadhiwa kutoka kwa waasisi wa African Association waliokuwapo kati ya mwaka wa 1929 hadi 1954 ilipokuja kuasisiwa TANU.



Erika Fiah 


Mswada wake huu ulichukua miaka 24 hadi 1973 kufikia kuchapwa na kama si juhudi za John Iliffe mswada ungebaki kama ulivyoandikwa na mwishowe kutoweka kama zilivyotoweka nyaraka nyingi katika historia ya Waafrika wa Tanganyika. Mswada huu ulichapwa katika kitabu alichohariri Iliffe, ‘’Modern Tanzanians,’’ Kilichopigwa chapa na Tanzania Publishing House. Nyaraka hizi za Sykes zimesaidia sana katika kuhifadhi si historia hii ya African Association bali hata historia ya TANU. Abdul Sykes alimpa mswada huu pamoja na nyaraka nyingine binti yake Daisy, wakati ule mwanafunzi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na kupitia nyaraka hizi mwalimu wake wa historia, John Ilife aliweza kujua mengi ambayo yalimsaidia katika kuiandika kwa uhakika historia ya African Association. Nyaraka hizi ndizo nyaraka pekee zilizoweza kuhifadhiwa kutoka kwa waasisi wa African Association waliokuwapo kati ya mwaka wa 1929 hadi 1954 ilipokuja kuasisiwa TANU.

African Association kabla ya Vita Kuu ya Pili (1914 – 1938) ilipitia misukukosuko mingi ya uongozi. Viongozi wenyewe kwa wenyewe walikuwa wanagombana kwa kupishana mitazamo na migongano ya haiba. Maarufu katika migongano hii ni ugomvi wa mwaka wa 1933 kati ya Kleist na Erika Fiah ikapelekea Kleist kususa chama kabisa hadi alipoandikiwa barua na Mzee bin Sudi aliyoainza kwa ‘’Bismillah RahamanRahim, ‘’ akimuomba Kleist arejee kwenye chama. Mzee bin Sudi wakati ule alikuwa ndiyo rais wa African Asociation.  Erika Fiah alikuwa Mganda aliyeingia Tanganyika na majeshi ya Uingereza katika Vita Vya Kwanza. Huyu Fiah alikuwa na fahamu nzuri sana na inaaminika ni katika ‘’ma-leftist,’’ wa mwanzo, watu walioingiza siasa za kikomunisti Tanganyika. Erika Fiah alikuwa na gazeti lake mwenyewe, ‘’Kwetu,’’ na yeye binafsi akiwa mhariri.

Gazeti hili lilikuwa mfupa wa kooni kwa serikali ya Kiingereza. Fiah alikuwa bingwa wa vijembe na wakati mwingine hata kwa Waafrika wenzake na aliyepata kipigo hiki sana alikuwa Kleist. Yawezekana kwa ajili ya biashara alizokuwanazo Kleist na kutokana na msimamo mkali wa Fiah kama mtu wa mrengo wa kushoto, Fiah alihisi Kleist hakufaa kuongoza African Association kwa ule ‘’ubepari wake.’’ Vijembe vya Fiah katika gezeti lake vikawa havipungui ndani ya kurasa za Kwetu. Fiah katika hamasa zake alipata kujaribu hata kuwaunganisha wakulima na wafanyakazi wa Tanganyika dhidi ya Waingereza. Juu ya hali hii ya siasa mjini Dar es Salaam lakini mahafali hawa wawili wote kwa macho ya wenyewe wenyeji wenye mji wao wa Dar es Salaam kama Wazaramo, Wamashomvi, Wandengereko na Warufiji hawa walikuwa, ‘’watu wa kuja,’’ wakiwaona hodari wa kujitiatia katika mambo kutaka wao siku zote wawe viongozi. Ukiangalia utaona jinsi ukoloni ulivyokuwa na uhodari wa kuwagawa watu ili watawaliwe kirahisi.

 Thomas Saudtz Plantan

Ndani ya uongozi wa African Association kulikuwa na watoto wa askari wa Kizulu waliokuja na Herman Von Wissman kutoka Mozambique na Sudan mwishoni mwa miaka ya 1800. Hawa walikuwa akina Kleist Sykes, watoto wa Plantan kama Thomas, Schneider na Mashado;  na  Hassan Machakaomo. Kulikuwa na Wanubi kama Ibrahim Hamisi na Wamanyema kama Mzee bin Sudi. Fiah hulka yake hii ya kuwashambulia wenzake ili furtu ada pale alipomshambulia Martin Kayamba alipokufa katika taazia aliyoaindika na kumweleza Kayamba kama kibaraka wa Waingereza ambae wananchi wa Tanganyika hawakunufaika no lolote kutola kwake si kwa elimu yake wala madaraka makubwa aliyopewa na Waingereza. Fiah alikuwa kiboko.

Hawa watoto wa Kizulu na Kinubi walisomeshwa katika shule za Kijerumani na wakawa wanasema Kijerumani kama maji. Hii iliwanyanyua na wakawa katika ule ukoloni wao wana nafasi nzuri katika jamii ya kuweza kuwa na kazi za maana ukilinganisha na mathalan, Wamashomvi waliokuwa maarufu kwa biashara ya soko ,(kiasi kuwepo kwa msemo kuwa, ‘’Mmashomvi mmoja hawezi kufunga soko,’’)na Wandengereko. Hapa tayari tabaka lilikuwa lishajengeka. Palikuwa na magomvi mengi baina ya hawa watu, ‘’wakuja,’’ na ‘’wenye mji,’’ kufikia hadi kugombana katika Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ambao ulikuwa umoja wa Waislam wa Tanganyika chama ambacho Kleist alikiasisi mwaka wa 1933 akiwa katibu muasisi na Mzee bin Sudi akiwa rais. Hali hii ya sintofahamu iliwafurahisha mno Waingereza kwani vita vya panzi furaha kwa kunguru. Sasa ikiwa siasa zilikuwa hivi  vipi watu hawa watajiunga kuunda cha kimoja cha siasa chenye nguvu kupambana na ukoloni? Waswahili wana msemo, ‘’Mungu si Athumani.’’ Waingereza watajikwaa na huku kujikwaa kwao ndiko kutawaleta Waafrika wa nchi nzima kuwa kitu kimoja. In Shaa Allah tutafika huko baadae.



Kulia: Abdul Sykes na mdogo wake Ally wakiwa Burma
Vita Kuu ya Dunia

Lakini huu ushawishi wa Wazulu na Wamanyema katika African Association haukumalizika haraka hata kidogo ingawa kufikia baada ya Vita Kuu ya Pili wakati sasa wasomi wa Makerere walipoanza kujiingiza katika siasa katika TAA misuguano hii ya ‘’uzawa,’’ pole pole na kwa taratibu ikaanza kupotea kwani upepo mpya ulikuwa unavuma Afrika. Waafrika walianza kuwaza kudai nchi yao na vijana wa Makerere walitegemewa kwingi kama wangeliongoza vita hivi. Lakini Makao Makuu ya TAA New Street palikuwa bado na uongozi wa wazee wa enzi ya Wajerumani na uongozi huu ulikuwa umechoka. Rais alikuwa Mwalimu Thomas Plantan na Katibu wake alikuwa Clement Mtamila. Uongozi huu haukupigwa vita na watu kutoka mbali la hasha. Schneider Abdillah Plantan mdogo wake Mwalimu Thomas Plantan alisimama kidete kuona kuwa TAA inashikwa na vijana. Uongozi huu uliangushwa na Dr. Vedasto Kyaruzi akachaguliwa katika Ukumbi wa Arnautoglo rais wa TAA na Abdul Sykes Katibu. Kaondoka Mzulu, Mwalimu Thomas Plantan katika uongozi ambae alikuwa ni baba yake Abdul katika ukoo akaingia Abdul mtoto wa Kleist ambae yeye ni Mwalimu Thomas Plantan ni ndugu yake na kuna wakati kwa kuwa Kleist alilelewa na Affande Plantan toka mtoto machanga baada ya baba yake kufa njiani wakati wakitoka katika kupigana na Chief Mkwawa Kalenga, Kleist akijulikana kama Kleist Plantan. Kigingi cha kuweka msingi wa kuunda TANU ulisimikwa kipindi hiki mwaka wa 1950 kwa fikra aliyokujanayo Abdul kutoka Burma akiwa askari wa King’s African Rifles (KAR).

Earle Seaton na Mwalimu Julius Nyerere


Mwaka huu wa 1950 utaingia katika historia kuwa ndiyo mwaka ambao viongozi wa TAA waliikabili serikali ya kikoloni na mapendekezo ya kutaka wakabidhiwe nchi yao kama sheria za nchi zilizokuwa chini ya Udhamini wa Umoja wa Mataifa zinavyoelekeza. Tanganyika ilikuwa Mandate Territory chini ya uangalizi wa Uingereza na wakati wakiwa tayari kujitawala Waingereza sharia iliwalazima kuipa Tanganyika uhuru wake. Hiki ni kisa kirefu kukieleza lakini muhimu ni kueleza kuwa uongozi wa Dr. Kyaruzi na Abdul Sykes uliunda ndani ya TAA Political Subcommittee ambayo ilipeleka kwa Gavana Edward Francis Twining mapendekezo ya katiba yaliyoshauri Tanganyika ipewe uhuru wake baada ya miaka 13 huku kukiwa na uchaguzi wa kura moja mtu mmoja katika kuchagua wajumbe wa LEGCO. 


Hamza Kibwana Mwapachu


Wajumbe wa Kamati Ndogo ya Siasa katika TAA walikuwa Mufti wa Tanganyika Sheikh Hassan bin Amir, Abdul Sykes, Hamza Kibwana Mwapachu, Sheikh Said Chaurembo, Dr. Vedasto Kyaruzi, Stephen Mhando na John Rupia. Katika kamati hii alikuwapo mjumbe mmoja ambae hakuwa akitokeza lakini yeye ndiye alikuwa mshauri mkuu katika mambo yote ya sheria na katiba kuhusiana na Nchi Chini ya Udhamini wa Umoja wa Mataifa. Mtu huyu jina lake lilikuwa Earle Seaton.


Kushoto Mwandishi akiwa na Dome Okochi Ruiru, Nairobi 1972

Mwaka wa 1952 Wazungu Meru waliwadhulumu Wameru ardhi yao na Wameru walikataa kudhulumiwa. Kaimu Rais na Katibu wa TAA Abdul Sykes alimuomba Earle Seaton atoe msaada kwa Meru Citizens’ Union chama kilichokuwa kinaongozwa na Japhet Kirilo kupinga dhula ile na Seaton akiongozana na Japhet Kirilo walifikisha malalamiko yao UNO na Kirilo alizungumza mbele ya Kamati ya Udhamini, Seaton akiwa mkalimani wake. Wameru hawakupewa haki yao na hapa ndipo walipojikwaa Waingereza. Abdul Sykes aliunda kamati iliyomjumuisha mdogo wake Abbas Sykes, Saadan Abdu Kandoro na Japhet Kirilo iliyotembea nchi nzima kueleza dhulma ile na madhila mengine ya ukoloni. Suala la ardhi ya Wameru liliwasha moto nchi nzima. Fikra ya kuunda chama cha siasa aliyokuwanayo Abdul Sykes, Ally Sykes, Hamza Mwapachu na wazalendo wengine pale Makao Makuu ya TAA New Street ikawa sasa imepata mahali pa kushika. Yako mengi katika historia hii ya kuundwa kwa TANU lakini si rahisi kueleza yote hapa. Inatosha kueleza kuwa Nyerere alipofika nyumbani kwa Abdul Sykes mwaka wa 1952 akiwa na barua ya utambulisho kutoka kwa Hamza Mwapachu hali ya siasa Tanganyika ilikuwa kama moto wa makumbi ukiwaka chini kwa chini.

Mwaka wa 1953 ulifanyika Uchaguzi wa kuwania urais wa TAA. Julius Nyerere alikuwa anagombea nafasi ile dhidi ya Abdul Sykes aliyekuwa kaimu rais baada ya Kyaruzi kuhamishwa Dar es Salaaam ili kupunguza nguvu ya TAA. Uchaguzi huu ulikuwa tarehe 17 April kwenye Ukumbi wa Arnautoglo. Nyerere alishinda kwa kura chache sana. Hiki ni kisa cha kusisimua sana lakini hapa nafasi haitoshi kukieleza. Ila inatosha kusema kuwa safari ya kuelekea Saba Saba 1954 kuunda TANU ilikuwa imewiva. Mwaka ule wa 1953 viongozi wa TAA walikuwa hawa wafuatao: J. K. Nyerere, Rais, Abdulwahid Sykes, Makamu wa Rais; J. P. Kasella Bantu, Katibu Mkuu; Alexander M. Tobias na Waziri Dossa Aziz, Katibu wa pamoja wa muhtasari; Wajumbe wa kamati: Dr Michael Lugazia, Hamisi Diwani, Tewa Said Tewa, Denis Phombeah, Z. James, Dome Okochi, C. Ongalo na Patrick Aoko.


Mwaka wa 1954 tarehe 7 Julai, 1954, TAA ilikutana Makao Makuu New Street kujadili katiba mpya ya chama kipya cha siasa - TANU. Jimbo la Mashariki ambalo liliwakilishwa na, ndugu wawili Abulwahid na Ally Sykes, Dossa Aziz, Tewa Said Tewa, Patrick Kunambi, Kasella Bantu, John Rupia, Julius Nyerere na C. O. Milinga; Jimbo la Kaskazini liliwakilishwa na na Joseph Kimalando na Japhet Kirilo; Jimbo la Ziwa liliwakilishwa na Abubakar Kilanga, L. M. Makaranga. Katika wanachama 17 waasisi, 9 kati yao walitoka Makao Makuu, 5 walitoka Jimbo la Ziwa, 1 alitoka Jimbo la Magharibi na 2 Jimbo la Kaskazini. Huu ukawa ndiyo mwisho wa safari iliyoanza mwaka wa 1924 na Dr. Aggrey alipomshauri Kleist Sykes kuunda Umoja wa Waafrika wa Tanganyika ambao Kleist aliuunda African Association mwaka wa 1929 akishirikiana na wenzake wengi wao wakiwa marafiki zake.

Waasisi wa TANU 7 Julai, 1954


Kulia Daisy Abdulwahid Sykes na Mwandishi Daisy akiwa ameshika kitabu cha maisha ya baba yake
Abdulwahid Sykes (1924 - 1968) alichoandika Mwandishi

















No comments: