Monday 24 July 2017

PROF. LIPUMBA JANA NA LEO


PROF. LIPUMBA ALIPOUNGURUMA TANGAMANO TANGA UCHAGUZI MKUU 1995

Discussion in 'Jukwaa la Historia' started by Mohamed Said5 minutes ago.



  1. Mohamed Said

    Mohamed SaidVerified User 

    #1
    5 minutes ago
    Joined: Nov 2, 2008
    Messages: 10,053
     
    Likes Received: 4,509
     
    Trophy Points: 280








    [​IMG]

    Prof. Lipumba akizungumza katika mkutano wa kampeni ya urais Same Uchaguzi Mkuu 1995


    Picha hiyo hapo juu ni Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, msomi wa Chuo Kikuu Cha Stanford Marekani, akihutubia mkutano Same wa kampeni ya urais Uchaguzi Mkuu 1995. Lipumba alikuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CUF. Prof. Lipumba alikuwa akitokea Moshi alifanya mkutano mwingine siku hiyo hiyo Muheza lakini mkutano uliovunja rekodi ulifanyika Tangamano Tanga siku ya pili yake. Wenyeji walituambia kuwa katika historia ya mji wao hawajapata kuona umma mkubwa kama ule. Baada ya mkutano ule Prof. Lipumba na waliokuwa katika msafara wake walifanyiwa dhifa kubwa nyumbani kwa marehemu Mama Ummy binti Anzuwani, Ngamiani.


    Kundi kubwa la wananchi waliizunguka nyumba ile ya Bi. Mkubwa huyu wakiimba nyimbo za kuwahamasisha watu waunge mkono CUF. Hali ilikuwa ngumu kwa CCM ikabidi Mwalimu Nyerere aje Tanga kusaidia. Ilibidi Mwalimu Nyerere aende Tanga kwa sababu katika hotuba yake katika viwanja vya Tangamano, Prof. Lipumba alizungumza na nyoyo za watu wa Tanga. Hali ya uchumi wa Tanga ilikuwa mbaya, viwanda vyote vilivyokuwa mjini hapo vilikuwa vimekufa, mkonge ambao ndiyo lilikuwa zao kuu ulikuwa umekufa na mengi ya mashamba yalikuwa katika hali duni sana. Prof. Lipumba akiwa mchumi bingwa aliwapitisha katika njia kuwaonyesha ilivyokuwa Tanga katika miaka ya nyuma. Prof. Lipumba aliwauliza Tanga, taarab ya Shakila iliyokuwa ikivuma wapi imekwenda, akawauliza tena zile timu kali za mpira za Tanga za Coastal Union na African Sports na wachezaji mashuhuri ambao yeye akiwasikia akiwa mtoto Tabora, kama Abdallah Luo, Hemed Seif, Mbwana Abushir, John Limo, Saleh na Omari Zimbwe ule moto umefia wapi. Watu walikuwa kwa hakika wameguswa nafsi zao na walikuwa wakishangilia kila nukta aliyoigusa Prof. Lipumba kuhusu hali ya Tanga. Ikawa lazima Mwalimu Nyerere afike Tanga kuokoa jahazi lililokuwa linazama.


    [​IMG]

    Nyumbani kwa marehemu Mama Ummy Bint Anzuani kushoto ni Juma Duni, Prof. Lipumba na wenyeji wake.



    Katika mkutano wa Mwalimu Nyerere Tangamano alisema maneno mengi ambayo kwa hali ya sasa kuhusu, ‘’uchochezi,’’ ni vigumu kwangu kuyaandika na kufanyia uchambuzi. Kwa mukhatasari Mwalimu Nyerere alionya kuhusu ''kuchanganya dini na siasa,'' na ''umwajikaji wa damu.'' Leo nikiangalia nyuma tulikotoka miaka 20 iliyopita na khasa baada ya CUF kupata mafanikio makubwa Tanga katika uchaguzi wa 2015 picha ile ya 1995 inanijia kwa majonzi makubwa. Hali ya Tanga ilikuwa inashabihiana na hali ya Tanga 1955 wakati wazalendo akina Hamisi Kheri, Mohamed Kajembe, Sheikh Rashid Sembe, Mwalimu Kihere, Mzee Makoko kwa kuwataja wachache walipokuwa wanajikusanya kujiondoa katika dhulma ya utawala wa Waingereza...

    Kushoto: Prof. Ibrahim Lipumba, Shekue, Mama Ummy Anzuani na Ummy

    Baada ya dhifa ile wakati wa kuondoka Mama Ummy alitukabidhi keki iliyotengenezwa na binti yake Ummy mwenyewe makhsusi kwa ajili ya Prof. na tuliibeba hadi White Rose Hotel tulipofikia. Usiku ule ule Mariam Shamte wa BBC, London alifika hotelini kufanya mahojiano na Prof. Lipumba na Juma Duni mgombea mwenza na asubuhi Prof. Lipumba alisikika akinguruma BBC Idhaa ya Kiswahili. Hakika Prof. mtu ambae mwezi mmoja tu uliopita hakuna mtu aliyekuwa akimfahamu sasa akawa midomoni mwa wananchi wengi.


    [​IMG]

    Mariam Shamte wa BBC akimhoji Prof. Lipumba


    Asubuhi tuliikata keki ya Mama Ummy na kuila wakati wa kifungua kinywa. Furaha ilikuwa kubwa mno wala haisemeki...msingi mzuri wa siku za baadae ulikuwa umewekwa na baada ya miaka 20 CUF iliiangusha CCM Tanga...


    Msiba mkubwa ni kuwa nguzo za CUF zilizojengwa kwa kipindi cha miongo miwili kwa jasho na vumbi na katika hali ngumu sana inaelekea kuna nyundo kubwa na nzito ikizipiga ili kuzivunja jengo lipate kuanguka.


    Historia hujirudia In Shaa Alah ikitokea nafasi nitakileta hapa kisa cha namna TANU ilivyoingia Tanga kwa kishindo kama hiki cha Prof. Lipumba siku Mwalimu Nyerere na Bi. Titi Mohamed walipokwaa jukwaa katika viwanja vya Tangamano kuwaita wananchi katika TANU wajikomboe na utumwa wa Waingereza.


    Wakoloni hawakukaa kimya kupitia United Tanganyika Party (UTP) walitengezeza nyundo nzito kuivunja TANU...

No comments: