Na Ahmed Rajab
SIKU hasa siikumbuki.  Lakini mwezi na mwaka naukumbuka.   Na siku zenyewe kwa jumla ninazikumbuka. Zilikuwa siku za Morogoro Jazz Band na Mbaraka Mwinshehe.  Simba Wanyika hawakuwa wakinguruma, walikuwa bado hawakuzaliwa.
Hilo siku mahsusi nisiyoikumbuka ni siku Rais Julius Nyerere wa Tanzania alipowaita mawaziri wake akawaeleza jambo ambalo hadi leo, miaka 49 baadaye, bado linazusha utata katika kumtathmini Nyerere aliyekuwa akijinata kuwa alijitolea kupigana bara la Afrika liungane kisiasa na kiuchumi.
Sina hakika kama siku hiyo ilikuwa Aprili 13, 1968 au siku moja au hata mbili kabla ya hapo. Jengine nisilo na hakika nalo ni iwapo Nyerere alipowaita mawaziri wake aliwaita kwa mkutano wa kawaida, au wa dharura, wa Baraza la Mawaziri.
Miezi michache baadaye, waziri mmoja wa Nyerere alinihadithia, ingawa kwa ufupi, yaliyojiri katika kikao hicho cha Baraza la Mawaziri.
Waziri huyo, aliyekuwa Abdulrahman Babu, alinieleza jinsi Nyerere alivyoingia chumba cha mkutano akiwa na ajenda moja tu.  Alikwishaamua kuitambua jamhuri mpya iliyoundwa Mei 30, 1967 baada ya majimbo ya kusini-mashariki mwa Nigeria kujitenga na Shirikisho la Nigeria na kujibatiza jina la “Biafra”.  Nyerere aliwataka mawaziri wake wamuunge mkono.
Kwa vile Nyerere alikuwa Nyerere hakukosa ufasaha wa kuyatetea aliyokuwa akiyaamini.  Alionekana kama aliwateka mawaziri wake kwa hoja zake kwa sababu walikaa kimya na wakimwitikia kwa vichwa.
Babu alimpinga.  Hoja kubwa aliyoitoa ni kwamba hatua ya kuitambua Biafra ilikwenda kinyume na moja ya kanuni za kimsingi za Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) za kutambua mipaka ya nchi wanachama iliyorithiwa kutoka kwa wakoloni na kutounga mkono hatua ya kuigawa nchi yoyote ya Kiafrika.
Nyerere, kwa upande wake, alisisitiza kwamba Tanzania haiwezi kukaa kimya wakati serikali kuu ya Nigeria ikiwaonea watu wa kabila la Igbo waliokuwa wengi katika Biafra.  Kabla ya kuundwa Biafra palifanyika mapinduzi mara mbili huko Nigeria na mara zote hizo Waigbo waliokuwa wakiishi kaskazini mwa Nigeria waliuawa kikatili.
Mabishano yaliendelea kwa muda, Babu akishikilia uzi wake uleule wa kuzipinga hizo hoja za Nyerere. Mwishoni mwa mabishano ya kiungwana baina yake na Nyerere, Babu alihitimisha maneno yake kwa kusema kwamba “tukiitambua Biafra tutajitosa”.  Nyerere, naye akajibu: “Natujitose”.
Hivyo ndivyo ulivyokatwa ule uliosemekana kuwa “uamuzi wa Tanzania” wa kuitambua Biafra.  Hivyo ndivyo Nyerere alivyozicheza siasa.
Kuna dola zilizokuwa zikiisaidia sana Biafra, kwa hali na mali, lakini si kwa kuitambua rasmi.  Dola zenyewe zilikuwa Afrika ya Kusini (siku hizo ikitawaliwa na makaburu), Israel, Rhodesia (iliyokuwa ikitawaliwa na walowezi wachache wa Kizungu), Ufaransa, Uhispania na Vatikani.
Wakati huo hapakuwako na hata nchi moja ya Kiafrika iliyothubutu kuitambua Biafra.  Ni baada ya Tanzania kuitambua Biafra Aprili 13, 1968 ndipo nchi nyingine za Kiafrika zilipoiiga.
Nchi zenyewe zilikuwa nne: Gabon iliyoitambua Biafra Mei 5, 1968; Côte d’Ivoire (Mei 14, 1968) na Zambia (Mei 20, 1968).  Halafu Machi 23, 1969, Haiti, iliyo katika Bahari ya Caribbean, nayo pia iliitambua Biafra.
Haijulikani kwa nini hasa Haiti ilikata uamuzi huo. Nchi hiyo wakati huo ikiongozwa na dikteta Dk. François “Papa Doc” Duvalier ambaye imani yake ya kidini ilikuwa ni mchanganyiko wa ukatoliki, itikadi za kiasilia za Kiafrika na mambo ya kichawi.
Zambia ilikuwa inaongozwa na Dk. Kenneth Kaunda, ambaye ni muumini wa kanisa la Kiprotestanti la kipresibiteri.  Lakini Kaunda alikuwa rafiki mkubwa wa Nyerere.  Kiongozi wa Cote d’Ivoire alikuwa Félix Houphouët-Boigny. Alipozaliwa wazee wake walikuwa wakiamini dini ya kiasili ya Kiafrika.  Alipoingia skuli ya sekondari 1915 ndipo Houphouët-Boigny mwenyewe alipotanasari na kuwa Mkatoliki. Akiamini kwamba ukatoliki ni dini ya kisasa na ni kizingiti cha kuzuia Uislamu usienee Afrika.
Gabon ikiongozwa na Mkatoliki Albert-Bernard Bongo kabla hajawa Omar Bongo alipokwenda Libya na kusilimishwa  na Kanali Mu‘amar Qadhafi 1973.  Tanzania, iliyokuwa ya mwanzo barani Afrika kuitambua Biafra, ikiongozwa na Nyerere, Mkatoliki aliyekuwa na mahusiano makubwa na Vatikani, Makao ya Papa, mkuu wa Wakatoliki wa Roma duniani.
Ni wazi Nyerere alipoingia chumbani kwa mkutano na mawaziri wake alikuwa na lake moyoni. Alikuwa amekwishazipiga hisabu zake na siri yake aliibania mwenyewe. Labda mtu pekee aliyekuwa akijua nini aliazimia kufanya siku hiyo alikuwa Bi Joan Wicken, Mwingereza aliyekuwa msaidizi wake muhtasi.
Mama huyo wakati mwingi alikuwa ubavuni mwa Nyerere na alikuwa wa mwanzo pia kuijua mipango yake ya siri alipoamua 1967 kutaifisha benki, kampuni za bima, nyumba za watu binafsi na hata vinu vya kusagia unga.
Alipokuwa akibishana na Babu, mbele ya mawaziri wake wengine, Nyerere alisema kwamba uamuzi wake ulikuwa mgumu na alikiri kuwa ulikwenda kinyume na msimamo wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika.
Hata hivyo, Nyerere aliazimia kufanya alichoazimia kufanya. Aliazimia kuufanya uamuzi wake binafsi wa kuitambua Biafra uwe uamuzi rasmi wa nchi yake.  Hiyo ilikuwa mara yake ya pili kukata maamuzi binafsi yaliyokuwa nyeti na yaliyoushangaza ulimwengu kwa sababu hayakuwahusisha wananchi wenzake.
Mara yake ya kwanza ilikuwa mwanzoni mwa 1964 alipoamua kwa niaba ya Watanganyika kuwa nchi yao iungane na Zanzibar, Muungano ambao ulitangazwa rasmi Aprili 26, mwaka huo.
Hatua zote hizo mbili zilikuwa hatua zilizokinzana katika bahari za maji makubwa za siasa za kimataifa.  Ya mwanzo ilikuwa ya kuunganisha nchi mbili zilizokuwa huru.  Moja ya nchi hizo ilikuwa ni kubwa mithili ya jipapa na nyingine ilikuwa ndogo mithili ya kijidagaa.
Hatua ya pili ilikuwa ya kuimegua nchi ya Kiafrika yenye wakazi wengi kushinda nchi yoyote nyingine barani humo. Ilikuwa kama  kumfanya mtoto mwenye utajiri mkubwa wa mafuta na elimu, amsusie na ajitenge na “Mama Nigeria”.
Ilikuwa hatua iliyowakanganya watu wengi ndani na nje ya Afrika.  Ilimuonesha Nyerere kuwa mtu mwenye sura mbili.  Kuna waliomkebehi kuwa hakuwa na msimamo au hakueleweka.
Hatua ya Nyerere ya kuifanya nchi yake, Tanganyika, iungane na Zanzibar  ni hatua yenye kuangaliwa kwa namna mbili. Kuna wanaoiona kuwa ni mfano wa msimamo wa Nyerere wa kuleta umoja wa nchi za Kiafrika.  Kuna wanaoiona kuwa ni mfano wa nchi moja ya Kiafrika kuimeza nyingine.
Miongoni mwao wapo pia wasemao kwamba hatua ya Nyerere kuifanya Zanzibar imezwe na Tanganyika au iwe chini ya mbawa za Tanganyika iliongozwa na azma ileile iliyomfanya miaka mitatu baadaye aitambue Biafra.
Wanasema kuwa mara zote hizo mbili alikuwa akiongozwa na udini.  Hawa ndio wale wanaohoji kuwa Nyerere ndiye aliyeanzisha ule uitwao “Mfumo Kristo” nchini Tanzania.
Hoja zao zinaonekana katika maandishi ya wasomi wa Kiislamu, wakiwemo wanahistoria Mohamed Said, Khatib Rajab al Zinjibari, Profesa Ibrahim Noor Sharif na hata katika uanaharakati na siasa za aliyewahi kuwa waziri wa Nyerere, Marehemu Kighoma Malima.
Na wanaongeza kuhoji kwamba si sahihi kusema ya kuwa hatua hizo mbili zilimfanya Nyerere aonekana kuwa ni mtu asiye na msimamo.  Wanasisitiza kwamba alikuwa na msimamo madhubuti, ila msimamo wenyewe ulikuwa wa kidini.  Kwa maneno ya mitaani wakisema kwamba Nyerere akiicheza ngoma iliyokuwa ikipigwa Vatikani, Roma.
Vatikani ndiyo iliyokuwa mfadhili na mlezi mkuu wa Biafra. Na kuhusu Zanzibar lengo la Vatikani lilikuwa kuzuia dini na utamaduni wa Kiislamu usitapakae katika eneo zima la Afrika ya Mashariki na ya Kati.
Nyerere akisifika kwa kuwa Mkatoliki mwema.  Majimbo ya kusini-mashariki mwa Nigeria yaliyobatizwa jina “Biafra” baada ya kujitenga yalikuwa na wakazi wake wengi waliokuwa Wakatoliki.   Sehemu iliyobaki ndani ya Shirikisho la Nigeria ilikuwa na wakazi wengi waliokuwa Waislamu, hususan kaskazini mwa nchi hiyo .
Kwa upande wake, Zanzibar ya wakati huo, siyo hii ya leo, ilikuwa na wakazi waliokuwa Waislamu wasiopungua asilimia 99.9. Kadhalika, ikionekana kama kitivo cha ilmu ya Kiislamu na utamaduni wake.
Katika kadhia zote hizo mbili, za Zanzibar na Biafra, pamoja na kuicheza ngoma ya Vatikani Nyerere pia alikuwa kama mtu aliyekuwa akicheza dama.  Na mara zote hizo mbili aliibuka mshindi, ingawa ushindi wake wa Biafra haukudumu kwa muda mrefu. Ule wa Zanzibar, uliodumu hadi leo, ungeliendelea kumsakama kooni lau angekuwa hai.
Badala yake Muungano  sasa unawasakama warithi wake na wafuasi wake. Miongoni mwao ni wale wenye kumfuata ama kwa dhati kwa kuzijua dhamira zake halisi na wale wenye kumfuata kwa kuwa wamo tu kundini. Hawa ni wa akina wale “sukuma twende’.
Uamuzi alioukata Nyerere 1968 wa kuitambua Biafra ulikuwa uamuzi mgumu ulioumpa ushindi uliokuwa pia mgumu.  Ni ushindi ambao ukiuangalia kwa mapana na marefu ulikuwa sawa na kushindwa.  Ni aina ya ushindi ambao Waingereza wanauelezea vizuri kuwa ni “Pyrrhic victory”.  Hasara ilikuwa kubwa kuliko natija.
Diplomasia ya Nyerere ilishindwa nguvu.  Ushindi wa Biafra wa kutambuliwa na nchi chache ulikuwa ushindi uliopita kama upepo kwa sababu Januari 15, 1970 majeshi ya waasi wa Biafra yalisalim amri na Biafra ikarejea katika Shirikisho la Nigeria. Uasi huo, ulioungwa mkono na Nyerere, ulisababisha maafa makubwa.  Roho zisizopungua milioni moja zilipotea katika mapigano baina ya waasi wa Biafra na majeshi ya serikali ya Nigeria.
Viungo vya mwili zaidi ya idadi hiyo vilikatikakatika na kuvunjikavunjika.  Maelfu kwa maelfu walionusurika kifo katika mapigano hayo walijikuta ama hawana mikono au miguu.
Nigeria haikumsamehe Nyerere kwa dhati kwa kuiunga mkono Biafra, hata baada ya kwenda Nigeria miaka kadhaa baadaye na kutaka radhi akikiri kwamba alikosea.  Mwaka 1975 Nyerere alipoyaamrisha majeshi ya Tanzania yavuke mpaka na kuingia Uganda kumuangusha dikteta Idi Amin, Nigeria ilikuwa safu ya mbele kuulaani uvamizi huo.  Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa nchi moja mwanachama wa OAU kuivamia nyingine kijeshi.
Aprili 28, 1968, siku chache baada ya kuitambua Biafra, Nyerere aliandika makala kwenye gazeti la London liitwalo The Observer.  Makala hayo yalikuwa chini ya kichwa maneno “Kwa Nini Tuliitambua Biafra”.  Humo alieleza kwa urefu sababu zilizomfanya avunje mwiko wa OAU na aitambua Biafra. Kadhalika aliandika maneno muhimu kuhusu Muungano wa Tanzania yanayofaa yazingatiwe kwa makini na viongozi wa sasa wa Tanzania.
Aliandika kwamba akiwa Rais wa Tanzania ni jukumu lake kuilinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Lakini aliongeza kwamba ikiwa wengi wa watu wa Zanzibar, bila ya kuchochewa na walio nje, na kwa sababu yao wenyewe, wataamua kwamba Muungano unawadhuru basi hatotetea kwamba wapigwe mabomu ili wasalim amri na kuukubali. “Kufanya hivyo hakutokuwa kuulinda Muungano.”