Tuesday 31 October 2017

HABIB OMAR BIN AHMAD BIN ABUBAKAR BIN SUMEYT 1886 - 1976

HABIB OMAR BIN AHMAD BIN ABUBAKAR BIN SUMEYT
1303 – 1396
1886 - 1976

Jina lake

Habib Omar bin Ahmad bin Abubakar bin Sumeyt Aal-Baalawy, nasabu yake inapita kwa Sayyid Alwy bin Muhammad (Sahibul Mirbat) ami yake Imam Muhammad (Faqihul Muqadam) bin Ali bin Muhammad (Sahibul Mirbat). Ukoo huu wa Aal Baalawy ni wajukuu wa Mtume Muhammad (Rehma na amani ziwe juu yake) kupitia kwa Sayyidna Husein bin Ali bin Abi Talib. 

Wazee wake

Babu yake Habib Abubakar ndie mzee wake wa mwanzo alietokea
Hadhramout na kufikia Ngazija na akafariki huko Ngazija mwaka 1290Hiria na baba yake Habib Ahmad ndie aliyehamia Zanzibar na akafariki Zanzibar mwaka 1343 Hijria na kuzikwa mbele ya Msikiti wa Ijumaa wa Malindi.

Kuzaliwa na kulelewa kwake

            Habib Omar alizaliwa siku ya Alkhamisi mwishoni mwa Dhulhijja mwaka 1303 AH sawa na Septemba 1886AD katika mji wa Itsandaa uliopo Ngazija (Comoro). Alilelewa malezi mazuri na mama yake aliyekuwa mchamungu Bibi Fatma bint Maalim Shanziy ambaye alipomzaa baba yake Habib Ahmad bin Sumeyt alikuwa Istanbul (Uturuki) wakati huo.
            Habib Omar alipofika umri wa miaka sita alilelewa na baba yake Habib Ahmad visiwani Zanzibar, hapo akapata malezi mazuri chini ya uangalizi wa baba yake ambaye alikuwa Mwanachuoni mkubwa wa Afrika Mashariki na Ulimwengu mzima.


Kusoma kwake

Habib Omar alipofika umri wa miaka minane alipelekwa na baba yake Hadhramout kwa ajili ya kusoma kwa Wanavyuoni wachamungu waliojaa katika miji mbalimbali ya Hadhramout.
            Alimuweka katika mji wa Shibam nyumbani kwa Mwanachuoni mkubwa Habib Tahir bin Abdalla bin Sumeyt, ambaye ni ami yake Habib Ahmad bin Sumeyt na akawa chini ya malezi yake na uangalizi wa mwanawe Habib Abdallah bin Tahir bin Sumeyt.
            Habib Omar baada ya kushiba elimu ya Shibam akapewa idhini ya kwenda kuchota elimu zaidi kwa Wanavyuoni waliokuwepo katika miji ya Hadhramout iliyokuwa maarufu kwa Elimu na Wachamungu. Alienda kusoma katika miji ya Hawta, Seyun, Tareem na kwengineko na akasoma fani tofauti na kwa kiasi kikubwa mpaka kuwapita wenzake wa rika moja.
            Habib Omar alisoma Hadhramout mpaka ujajani mwake akiwa anakwenda na kurudi Zanzibar kila baada ya muda. Alipomaliza masomo yake alirudi Zanzibar na akaongeza elimu nyingi kwa baba yake Habib Ahmad bin Sumeyt na Sheikh Abdallah Bakathir mpaka akafikia upeo mkubwa kwa fani tofauti.
            Habib Omar alibobea katika fani nyingi zikiwemo Tafsiri ya Qur-an, Hadithi, Fiqhi, Usulul Fiqhi, fani za Lugha,Tasawwuf na nyenginezo.
             

Mashekhe zake

            Habib Omar alipata fursa ya kusoma kwa Mashekhe wengi sana, kila aendapo huchota kutoka kwa Wanavyuoni wa eneo hilo, Mashekhe wake wengi walitokea Zanzibar na Hadhramout.

Baadhi ya Mashekhe zake wa Zanzibar

1.     Habib Ahmad bin Abubakar bin Sumeyt (baba yake mzazi).
2.     Sheikh Abdalla bin Muhammad Bakathir.
3.     Sheikh Said bin Muhammad bin Abdalla bin Dahman.
 Baadhi ya Mashekhe zake wa Hadhramout.
1.          Habib Aidarous bin Omar Alhabshy.
2.          Habib Ali bin Muhammad Alhabshy.
3.          Habib Abdalla bin Hasan bin Saleh Albahr.
4.          Habib Ahmad bin Hasan Al-Attas.
5.          Habib Omar bin Muhammad Alhaddad.
6.          Habib Tahir bin Abdalla bin Sumeyt.
7.          Habib Abdalla bin Tahir bin Sumeyt.
8.          Habib Ubeydillah bin Muhsin Assaggaf.
9.          Habib Ahmad bin AbdulRahman ASsaggaf.
10.    Habib Abdalla bin Ali bin Shihab.
11.    Habib Hasan bin Muhammad Balfaqiih.
12.    Habib AbdulRahman bin Muhammad AlMash-hur.
13.    Habib Abdalla bin Omar Asshatiry.
14.    Habib Salim bin Hafiidh Al Shekh Abubakar bin Salim.
15.    Habib Mustafa bin Ahmad AlMihdhaar.

Baadhi ya Mashekhe wake wa Hijaaz (Makka na Madina)

1.     Sheikh Omar bin Abubakar BaaJuneyd.
2.     Sheikh Omar Hamdan AlMahrusy.
3.     Habib Husein bin Muhammad Alhabshy.
Hao ni baadhi ya Mashekhe zake ambao wengine alisoma kwa kupiga goti na wengine kwa kupewa Ijaza na kutabaruku nao.  

Madhehebu yake

 Habib Omar bin Sumeyt alikuwa Sunni katika Akida, akifuata
Madhehebu ya Kishaafii katika Fiqhi na alikuwa na Tariqa ya wazee wake Al-Baalawy katika Tasawuf. Pia alipata ijaza za Tariqa tofauti na kuhudhuria baadhi ya hadhara zao mfano wa Tariqa ya Shadhiliya na Qadiriya.

Kusomesha kwake 

 Habib Omar baada ya kumaliza kusoma kwa Mashekhe zake wa Zanzibar alionelea vyema arejee Ngazija alikozaliwa akaanze kuwanufaisha watu kwa kuwasomesha na kuwaongoza katika kheri. Akarudi Ngazija na kusomesha wanafunzi wengi sana na watu wa Ngazija walimpenda na kumheshimu sana, pia alisomesha sana Zanzibar alipohamia mnamo mwaka 1355 Hijria baada ya kuteuliwa awe Kadhi na na Mfalme wa Zanzibar Sayyid Khalifa bin Harub.
Alikuwa na darasa baada ya Sala ya Laasiri katika msikiti wa Ijumaa wa Malindi, alikuwa akisomesha kitabu cha Fiqhi “Fat-hul Muiin” na vyenginevyo, wakihudhuria watu wengi wa kila tabaka na kila rika wakiwemo Mashekhe, watu wa kheri, vijana, wazee, wafanya biashara, na wengineo.
Aidha alikuwa na darasa nyumbani kwake kwa nyakati tofauti khasa baada ya kujiuzulu Ukadhi, ikawa wanafunzi wanafurika kujichotea kila aina za elimu.

Wanafunzi wake

Habib Omar alikuwa na wanafunzi wengi katika maeneo mbalimbali na wengi wao walikuwa ni Wanavyuoni wakubwa katika zama zao. 
Miongoni mwa wanafunzi wake wakubwa wa Afrika Mashariki (Zanzibar na Kenya) ni:
1.          Sheikh Suleiman bin Muhammad Al-Alawy.
2.          Habib Ahmad bin Husein bin Sheikh Abibakar bin Salim.
3.          Sheikh Ilyas bin Ali bin Ilyas Assinesry.
4.          Sheikh Salim bin Abdalla bin Wad-aan.
5.          Sayyid Ali bin Jaafar Al-Waht Saggaf.
6.          Sheikh Burhan Muhammad Mkele.
7.          Sayyid Abal-Hasan bin Ahmad Jamali-Leyl.
8.          Habib Ahmad Mashhur bin Taha AlHaddad (wa Kenya).
9.          Sheikh Ali bin Muhammad Baaqashmar.
10.    Sheikh Abdalla Saleh Farsy.
11.    Sayyid Muhammad bin Alwy Jamali-Leyl.
12.    Sayyid Alwy bin AbdulWahhab Jamali-Leyl.
13.    Sayyid Omar bin Abdalla Aal Sheikh (Mwenye Baraka).
14.    Sheikh Abdalla bin Ahmad Baafadhil.
15.    Sayyid Ali bin Ahmad Badawy Jamali-Leyl (wa Lamu).
16.    Sayyid Abdurahman Khitamy (wa Lamu).
17.    Sayyid Abubakar (Shibli) bin Omar Qullatein.
18.    Sayyid Said bin Abdalla Albiidh (wa Mambrui).
19.    Ustadh Muhammad bin Sharif Said Albiidh (wa Mambrui).
20.    Sayyid Muhammad bin Alwy Bunamay.
21.    Sayyid Mustafa bin Alwy  Bunamay.
22.    Sayyid Muhammad bin Adnan Aydid (wa Dar es Salaam).
23.    Sayyid AbdulQadir bin AbdulRahman Al-Juneyd (wa Dar es Salaam).             Na wengi wengine tusiowataja waliokuwa wametawanyika katika kila pembe ya dunia.

Wahudumu wake

Habib Omar alikuwa bwana mkubwa katika elimu na uchamungu, baadhi ya wanafunzi wake walijitolea kumtumikia katika hali zake za kila siku hata anapokuwa safarini.
Miongoni mwa waliowahi kumhudumia:
1.        Sheikh Said Al-Khusty, alianza kumhudumia tokea Ngazija, Madagaska na hadi alipohamia Unguja na akafariki Unguja.
2.        Sayyid Muhammad Alwy Bunamay, alipata bahati kubwa ya kuwa khadimu wa Habib Omar hadi kumuoa mjukuu wa Habib Omar kwa upande wa binti yake.
3.        Sayyid Mustafa Alwy Bunamay, ambae alisogezwa na kaka yake Sayyid Muhammad.
4.        Watoto wa nyumbani, walikuwepo watoto nyumbani kwa Habib
Omar nao walipata bahati ya kumhudumia, miongoni mwao ni Ali Amour
Bubahy, Rashid M. Seif, Sayyid Mahsen, Shee Hamadi, Sayyid
Muhammad Ahmed Al-Hindwani, Sheikh Abdallah Said Azzan na Said Ali Aboud.

Kazi alizozifanya

Habib Omar bin Sumeyt baada ya kusoma Hadhramout alirejea
Ngazija mji aliozaliwa. Alisomesha watu wengi huko Ngazija, Madagaska, Zanzibar na kwengineko, alifanya biashara mbalimbali ikiwemo ya kuuza mafuta mazuri (uturi).
Alisilimisha watu wengi Madagaska kupitia Daawa yake, alijenga misikiti, alichimbisha visima na kujenga mahodhi khasa Ngazija ambapo walikuwa wakitegemea zaidi maji ya mvua kwa kunywa na kupikia, visima alivyovichimba vimewanufaisha watu wengi na vyengine vinatowa maji hadi sasa vikiwa na khabari nyingi za maajabu.
Habib Omar alikuwa Kadhi wa Zanzibar, alihukumu kwa uadilifu mkubwa, vile vile alikuwa ni marejeo katika Fatwa kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki hadi nchini Afrika ya Kusini.
 

Kuchaguliwa kwake kuwa Kadhi

Ilipofika mwaka 1355 Hijria (1936 AD) aliyekuwa Mfalme wa Zanzibar Sayyid Khalifa alimteuwa Habib Omar bin Sumeyt kuwa Kadhi wa Pemba na ndio ikawa sababu ya kuhamia Zanzibar kutoka Ngazija, kisha akamchaguwa kuwa Kadhi wa Unguja mnamo mwaka 1357 Hijria.             Ilipofika mwaka 1362 Hijria (1942 AD) Sayyid Khalifa alimchaguwa Habib Omar kuwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar wadhifa ambao alidumu nao hadi alipojiuzulu katika mwaka 1379 Hijria (1959 AD).

Habib Omar ni mzalendo katika Ukadhi wa Unguja kwani baba yake na babu yake wote walikuwa Makadhi wa Unguja.

Mambo muhimu aliyoyafanya akiwa Kadhi Mkuu Zanzibar

Habib Omar alikubali wadhifa wa Ukadhi pamoja na uzito wa wadhifa huo kutokana na haja ya Waislamu kuwa na Kadhi katika kila nchi na kwa Zanzibar yeye ndie aliyekuwa anaestahiki zaidi kuwa Kadhi.
Alikuwa muadilifu wa hali ya juu, kesi zake nyingi huzimalizia kwa suluhu bila ya kutowa hukumu, na alikuwa hawakubalii mawakili kila walisemalo bali alihukumu kulingana na Elimu aliyonayo.
Katika mambo makubwa aliyoyafanya Zanzibar ni kushauri kuwekwa mfumo mzuri wa kusimamia Mali za Wakfu. Mali nyingi za Wakfu zilikuwa hazitekelezwi manufaa yake yaliyokusudiwa, na Wakfu nyengine zilikuwa chini ya Serikali zikitumika kinyume na makusudio ya waweka Wakfu na Misikiti mingi ilikosa Mali za kuisimamia.
Akashauri kuwekwe utaratibu mzuri wa kuinufaisha Misikiti iliyokosa Mali za Wakfu ili Misikiti yote ipate kutumikiwa kama Wakfu mmoja. 

Tabia zake

Habib Omar bin Sumeyt alisifika na sifa nyingi zilizokuwa njema, alikuwa mkarimu sana, mwenye huruma, mvumilivu, msamahevu kwa wale waliomkosea, aliwapenda wanafunzi na akiwasaidia, hapendi dhuhuri, hasemi sana, alikuwa amejipangizia nidhamu maalumu katika maisha yake kwa kila jambo, alikuwa maridadi, na alisifika na sifa nyingi nyenginezo.

Hadhi yake na heshima aliyokuwa nayo

Habib Omar alikuwa Mwanachuoni Mchamungu wa kupigiwa mfano katika zama zake, kila aliyemuona hakuwacha kumsifu kwa sifa ya UchaMungu. Alipendwa na Wanavyuoni waliomsomesha na kumtanguliza katika Majlis tofauti. Wanafunzi wake walikuwa wakimuheshimu upeo wa kumheshimu, viongozi wa Kidunia walimtukuza na kumfanya katika washauri wa mambo yao hadi kutumika picha yake katika noti ya elfu kumi (10,000) ya visiwa vya Komoro.
             

Safari zake muhimu

Habib Omar alisafiri kwenda Hadhramout, Hijaz, Misri, Ngazija, Madagaska, Kenya, Somalia, Mauritius, Tanganyika na nchi nyenginezo.         Alikwenda Hadhramout (mbali na safari yake ya kusoma) mara kwa mara mji wa wazee wake na Mashekhe zake kwa ajili ya kuwaunga na kutabaruku nao kama ilivyokuwa ada ya WachaMungu ya kutembeleana.  Habib Omar ameziandika baadhi ya safari zake za Hadhramout na Hijaz, ameziandika kwa ukamilifu kila sehemu alizozuru na Mabwana aliokutana nao, Ijaza walizopeana pamoja na kuelezea matukio muhimu. Safari moja ameiita “Annafhatu-Shadhiyya” alipokwenda Hadhramout tu, pia ameiandika safari ya Hijazi na Hadhramout na kuiita “Talbiyatu- Sawt”, tungo hizo mbili zimechapishwa katika kitabu kimoja na sasa kipo mikononi mwa watu wa kheri. 
Pia imeandikwa safari yake nyengine ya Hadhramout na mwanafunzi wake Sheikh Muhammad Jubran ambayo imeitwa “Arrihlatu-
Sumaytiyyah fil-Araadhil Hadhramiyyah” nayo imechapwa karibuni kama alivyokusanya na kuiandika safari ya Habib Omar ya Misri ambayo bado haikuchapishwa.

Vitabu alivyotunga

Habib Omar alitunga baadhi ya vitabu ambavyo vimesheheni elimu pamoja na kushughulika na kazi ya Ukadhi ambayo ilimnyima muda wa kutosha wa kufaraghika na uandishi. 
Miongoni mwa vitabu vyake:
1.     “Hadiyyatul-Ikhwan” sherehe ya Aqidatul-Iman.
2.     “Annafahatul-Shadhiyyah”, Safari yake ya Hadhramout.
3.     “Talbiyatu Sawt”, safari yake ya Hijaaz na Hadhramout.
4.     Tarekhe ya baba yake Habib Ahmad bin Sumeyt na Shekhe wake
Sheikh Abdallah Bakathir, vyote vimechapwa pamoja na kitabu cha Habib Ahmad bin Sumeyt kiitwacho “Al-Ibtihaj fiy bayanil Istilahil Minhaj” 5. “Shadhiyul Azhaar”, ziara ya Habib Salim bin Hafiidh Unguja.
6. Diwani ya mashairi, bado haijachapishwa.
Mkusanyiko wa maneno yake ya hikma “Majmuu Kalam”.
“Majmuu kalaam” ni moja ya aina ya Utunzi maarufu kwa Wanavyuoni wa Tasawwuf khassa Aal-Baalawy.
Ni mkusanyiko wa matukio mbalimbali na maneno ya hikma aliyoyatowa mhusika katika hali mbalimbali. Mkusanyiko huo huandikwa na wale waliomlazimu na kuishi nae na huwa kwa utungo mzuri wenye kumvutia msomaji kiasi ya kujihisi yupo katika matukio.
Habib Omar ametungiwa “Majmuu Kalaam” yake na watu tofauti ambayo yameandikwa kwa khatti za mkono na nyakati tofauti kila mmoja na sehemu alipokutana nae.
Miongoni mwa walioandika “Majmuu Kalaam” yake ni wafuatao:
1.               Sheikh Ubeid bin Said Damis Bajubeir, alipokuwa akiishi Zanzibar.
2.               Sayyid Hadi bin Ahmad Alhaddar, alipokuwa anaishi Unguja na Pemba. 3. Sheikh Fadhil bin Muhammad bin Awadh Bafadhil alipomzuru Habib Omar Zanzibar.
4. Sheikh Omar bin Hassan bin Muhammad Arfan Barajaa, wakati Habib Omar alipokuwa Kenya, Aden, Shihr na Zanzibar.
Zote hizo zipo mbalimbali, kisha zikakusanywa katika tungo moja na Sayyid Abdul-Qadir bin Abdul-Rahman Al-Juneyd.

Zanzibar katika zama za Habib Omar bin Sumeyt

Zanzibar ilikuwa ni kitovu cha elimu ya dini ya Kiislamu katika miaka iliyopita na ilinawiri sana wakati wa Habib Omar bin Sumeyt. Wanavyuoni wengi waliokuwa baada yake walisoma kwake, watu wa kawaida walifurahishwa na mwenendo wake na wakimpa heshima kubwa. Habib Omar alikuwa na bustani yake huko Sharif Msa nje ya mji wa Zanzibar aliyoiita “Aniisah” kama Shekhe wake Habib Ali Habshy alivyokuwa nayo bustani kwa jina hilo huko Seyun Hadhramout. Kila siku ya Jumapili walimiminika Sharif Msa Wanavyuoni wa Zanzibar pamoja na wanafunzi wao pamoja na wapenzi wake kwenda kumsalimia Habib Omar na kusoma baadhi ya vitabu pamoja na kutabaruku nae, nae akiwakirimu wale waliokuwa wakimzuru.
Zanzibar katika wakati wa Habib Omar ilitembelewa na Wanavyuoni wachaMungu wakubwa sana wa Hadhramout wa zama hizo na wote walizuru Zanzibar kutokana na kuwepo kwake, ziara hizo zilikatika mara tu baada ya Habib Omar kuhamia Shihri.
Miongoni mwa Wanavyuoni waliozuru Zanzibar zama za Habib Omar ni:
1.     Habib Abdalla bin Tahir bin Sumeyt (aliyekuwa mlezi wake Shibam).
2.     Habib Salim bin Hafiidh Ibni Sheikh Abibakar bin Salim.
3.     Habib AbdulRahman bin Ubaydillah Saggaf.
4.     Habib Muhammad bin Salim bin Hafiidh.
5.     Habib AbdulQadir bin Muhammad bin Ali Alhabshy.
6.     Sheikh Fadhl bin Muhammad bin Awadh Bafadhl.
7.     Habib Ali bin Hassan Al-Attas.
8.     Habib Abubakar bin Tahir Al-Haddad.

Maneno yake ya Hekima

Habib Omar alikuwa na maneno mingi ya Hekima kwa tungo za mashairi na za kawaida. Wameyapokea wanafunzi wake maneno hayo na mengi yamo katika “Majmuu Kalam” zilizokusanywa.
Miongoni mwa maneno yake ya Hekima:
    Unapotaka raha ya kweli ya Akhera basi wacha raha za kidunia.
    Baalawy hawapendi dhuhuri tofauti na watu wengine, wanaona hilo sio ukamilifu wa mtu isipokuwa kwa yule aliyepewa idhini.
    Kulingania kwa ajili ya Allah hakuhitaji elimu kubwa wala ufasaha bali kunahitaji upole na tabia njema, na anapokumbusha mkumbushaji (anapotowa mawaidha) akamuona yule anaemnasihi ni bora kuliko yeye basi maneno huwa yanatoka moyoni na huathiri, ama akijiona yeye bora kuliko anaowanasihi basi maneno hutoka katika nafsi na yanakosa kuathiri wasikilizaji.

Kuhama kwake Zanzibar

  Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar  mwaka 1964 Habib Omar alipendelea kuishi Shihr  moja ya miji maarufu ya Hadhramout na akahamia mwaka 1385 Hijria (1965 AD), akaishi huko kwa kipindi akinufaisha watu kwa elimu yake.
Habib Omar aliombwa na Maraisi wawili wa visiwa vya Komoro ahamie Ngazija alikozaliwa na walipo jamaa zake wengi nae akaamua kuhamia visiwa vya Komoro na ndipo alipomalizia uhai wake wa duniani.

Kufariki kwake

Habib Omar alifia katika visiwa vya Ngazija katika mji aliozaliwa Itsandaa usiku wa kuamkia Jumanne tarehe 9 Safar mwaka 1396 Hijria sawa na tarehe 10/2/1976 akiwa na miaka tisiini na tatu takiriban.
Ilikuwa ni siku ya huzuni kubwa kwa Waislamu wote wa Ngazija na Afrika ya Mashariki.
Maziko yake yalihudhuriwa na umma wa watu kutoka kila pembe ya  Afrika Mashariki na akasaliwa na kuzikwa na watu wa kheri akiwemo Sayyid  AbdulQadir bin AbdulRahman Al-Juneyd ambae alishiriki kushuka kaburini.

Familia yake

  Habib Omar hakuwa na watoto wa kiume, kizazi chake kimeendelea kupitia kwa Sayyid Muhammad Bunamay aliyemuoa mjukuu wake kwa upande wa bint yake. Habib Omar alikuwa na ndugu wa kiume anaeitwa Habib Abubakar aliyefariki Unguja, pia alikuwa na ndugu wa kike.

Hizi ni miongoni mwa khabari za Bwana huyu mtukufu, na amesifiwa na kutajwa kwa kheri na Wanavyuoni wengi wa kila pembe ya Dunia, tumeyakusanya haya kwa ufupi kuepuka kumchosha msomaji.
Rejea:
1.   Kitabu “Baadhi ya Wanavyuoni wa Mashariki ya Afrika” cha Sheikh Abdallah Saleh Farsi.
2.   Kitabu cha maisha ya Habib Omar “Nubdhah min hayatil Imam Al-
Allamah Habib Omar bin Sumeyt” cha Sayyid AbdulQadir AlJuneyd.
3.   Kitabu “Uqudul-Jaaizah” cha Sayyid AbdulQadir AlJuneyd
4.   Kurasa alizoandika Sayyid Abubakar (Shibli) Qullatein kuhusu Habib Omar.
5.   Majmuu kalaam za Habib Omar alizozikusanya Sayyid AbdulQadir Al-Juneyd kutoka kwa watunzi wanne.









Aliyesimama Nyuma ya Masheikh ni Abbas Sykes na Waliokaa Kulia ni 
Sheikh Omar bin Sumeit na Kushoto ni Sheikh Ahmed bin Hussein
Wakati hii miaka ya mwanzoni 1960 Abbas Sykes Alikuwa Regional Commissioner
wa Jimbo la Mashariki

Maahad Juneyd Islamiy
                                     Kitengo cha Bahthi na Utafiti
                      +255 777 878 047 – Zanzibar  

No comments: