Sunday 29 October 2017

SHEIKH ALI BIN HEMED AL-BUHRY KINDAKINDAKI WA "UMWAMWANDE"


[​IMG]

Sheikh Ali bin Hemed bin Abdallah bin Said bin Abdallah bin Mas’uud bin Khelef bin Ali bin Said bin Nassor bin Suleiman Al-Buhriy Al-Hinai amezaliwa katika Kijiji cha Saadani, Tanga tarehe 29 August 1889 (sawa na Muharram 1307).

Sheikh Ali bin Hemed alilelewa na wazazi wake hapo Saadani na baadae wazazi wake wakahamia Kijiji cha Darigube (Wanga) kilichopo katika vijiji vya Maere na Kiwavu, Umwamwande, Tanga.

SILSILA YAKE

Sheikh Hemed bin Abdallah bin Said bin Abdallah bin Mas’uud bin Khelef bin Ali bin Said bin Nassor bin Suleiman Al-Buhriy Al-Hinaiy - Maarufu Mwalimu "KIBAO" ndiye baba wa Sheikh Ali Bin Hemed.

Shughuli kubwa ya Baba yake ilikuwa Utabibu na Uandishi. Baadhi ya tenzi maarufu alizotunga Baba yake Sheikh Ali bin Hemed ni kama "Utenzi wa Abdirrahmani na Sufiyani", "Utenzi wa Kadhi Kassim bin Jaafar", "Utenzi wa Seyyidna Huseni bin Ali" na "Utenzi wa VITA VYA WADACHI KUTAMALAKI MRIMA".

Pia aliandika vitabu vingi kama kitabu cha sharia za NIKAH na vinginevyo. Tenzi hizi nyingi zilichukuliwa na J.W.T Allen na kuzitafsiri kwa Kiingereza ambaye alipewa na Sheikh Muhammad bin Hemed, mwanawe Sheikh Hemed bin Abdallah. 

Tenzi hizi za familia ya Sheikh Hemed bin Abadallah sasa zimewekwa kwenye Maktaba za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mahali kwengineko kwenye tovuti tofauti tofauti za vyuo na za tafiti za Kiswahili.

Mama yake Sheikh Ali Bin Hemed Al-Buhry ni Bibie Maasimbu binti Mwinyimkuu bin Mwinyiamiri.

MASOMO YAKE

Alianza masomo ya Qur'ani hapo kijijini Saadani akisomeshwa na Mwalimu Kadhi Mwinchande. Masomo ya awali ya ilimu ya dini alianza akusomeshwa na baba yake Mzee Hemed bin Abdallah. Pia alihudhuria masomo ya shule, Tanga School, na kusitisha masomo ya shule akiwa darasa la pili ili aendelee na masomo ya dini.

Aliendelea na masomo yake ya dini kwa Sheikh Faqih (kutoka Magunyani na kuishi Mafere, Muheza - Tanga). Alisomeshwa na Sheikh huyu Rubu'ul Ibadah.

Alisoma ilimu ya Faraidh (Mirathi) kwa Sheikh Khamis bin Salim Riyamy wa Tanga. Sheikh Khamis alikuwa Kadhi wa Tanga.

Vilevile alisoma tena ilimu ya Faraidh na ilimu ya Nahau kwa Sheikh Umar bin Stambuli bin Abubakar As-Saady wa Tanga. Sheikh Umar alikuwa Kadhi wa Tanga.

Kisha akaenda Unguja kuzidi kuongeza ilimu yake. Akasoma hapo Unguja kwa Kadhi Sayid bin Abubakar bin Sumeyt. Vile vile akasoma kwa Sheikh Abdallah bin Muhammad Bakathir.

Akazidi kuongeza ilimu yake ya Faraidh kwa kusomeshwa na Sheikh Salim bin Said bin Seif Ash-Sheheyby ambae alikuwa ndiye mjuzi wa ilimu ya Urithi zama hizo kuliko mwanachuoni yeyote mwengine wa pande hizi.

Vile vile hapo Unguja alisoma ilimu ya Balagha na Mantiq kwa Sheikh Abubakar bin Abdallah Bakathir (Huyu ni mtoto wa Sheikh Sheikh Abdallah Bakathir).

Lakini mwanachuoni, kama tajiri, hakinai kwa alichopata, hutaka kila siku kuongeza. Kwa hiyo alikwenda Mombasa kwa Sheikh Al-Amin bin Ali Mazrui akachukuwa aliyoyachukuwa. Ilimu ya Miqaat aliisomea huko.

KIFO CHAKE.

Ilikuwa Jumaapili tarehe 4 August 1957 siku ambayo aliendesha shughuli zake za kusomesha darsa zake kama kawaida mchana kutwa bila ya dalili zozote za dhahiri kwamba lipo tatizo la afya yake na kwamba mchana ule ndio ungekuwa mchana wake wa mwisho wa uhai wake duniani.

Ilipofika usiku majira ya saa nne hivi aliingia ndani kulala. Na huo siku hiyo ukawa mwisho wa umri wake duniani. Alifariki.

Alizikwa mchana wa Jumatatu tarehe 5 August 1957 katika kijiji kile kile alipozaliwa, yaani Saadani.

No comments: