Wednesday 11 October 2017

HISTORIA YA AGA KHAN NA WAISLAM WA TANZANIA



KIONGOZI WA WAISMAILIA AGA KHAN KATIKA TANGANYIKA YA KIKOLONI


Aga Khan na Rais Magufuli Ikulu 11 Oktoba 2017


Sheikh Matimbwa,

Tumekushukuru kwa kutuwekea, ''clip,'' adhim ya Aga Khan alipokuja Tanganyika mwaka 1956.

Nimeingia maktaba ili nai nichangie kitu katika mambo ambayo Waismailia, yaani Aga Khan walifanya katika kusaidia Waislam wa Tanganyika.

Katika miaka ya 1930s Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika walikuwa wanajenga shule ambayo sote tunaijua lakini hela zilikuwa tatizo jengo likawa limechukua muda mrefu kukamilika.

Sababu ya kujenga shule hii ni kuwa wazee wetu na wao walitaka wawe na mahali pa kuwasomesha watoto wao kuepuka vijana wao kubatizwa katika shule ambazo serikali ya kikoloni iliziweka mikononi kwa kanisa.

Kleist akiwa kiongozi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika alitambua mapema sana kuwa tatizo kubwa lililokuwa likiwakabili Waislam ilikuwa ni kukosa elimu ambayo serikali ya kikoloni iliwaachia wamishionari waisimamie.

Si kama Waislam hawakuwa wanatambua faida ya elimu kwa watoto wao. Wazazi wengi walichelea kuwapeleka  watoto wao shule kwa sababu wamishionari walichukua fursa hiyo kuwabatiza. Kuliko kwa watoto wao kutolewa katika Uislam na kuwa murtad, wazazi wengi waliamua kuisamehe elimu yenyewe kabisa.

Kleist aliona kuwa ufunguo wa tatizo hilo kwa Waislam ilikuwa ni kuanzisha shule zao wenyewe ambazo zitasomesha Qur’an pamoja na masomo mengine.

Wakati ule, na hata hivi sasa, Qur’an ilikuwa ikisomeshwa kwa mtindo wa asili ambapo mwanafunzi anakaa chini sakafuni mbele ya maalim akiwa na ubao wake na juzuu.

Katika madras kuchapa viboko, kwa jina maarufu mkambaa, ndiyo ulikuwa mtindo wa kusomeshea. Kleist hakuona sababu kwa nini Qur’an nayo isisomeshwe kama elimu nyingine, wanafunzi wakiwa madarasani wakikaa katika madawati.

Alilitoa wazo hili kwa rafiki zake akashauri madras ipanuliwe ili masomo mengine yasomeshwe pamoja na Uislam.

Ushauri huu ulijadiliwa kati ya Kleist, Ali Kiro, Maalim Popa Saleh na Shariff Salim. Wakitambua kazi kubwa iliyokuwa ikiwakabili, waliamua waanze hiyo shule kwa kidogo kidogo kwa awamu. Nyumba itakayokuwa shule ya muda ilitafutwa na wanafunzi wakaanza kusoma.

Kati ya walimu wa mwanzo wa shule hiyo walikuwa Mzee Ali Comorian na Sheikh Abdallah Idd Chaurembo ambao walikuwa kati ya wasomi wa Kiislam waliokuwa wakiheshimika.

Wazazi wa Kiislam waliombwa wachange fedha ili jengo la kudumu lijengwe.

Al Jamiatul Islamiyya ikawa inapita nyumba hadi nyumba ikusanya michango kutoka kwa Waislam.

Bahati nzuri mwaka wa 1936 Aga Khan alitembelea Tanganyika na akafahamishwa kuhusu ujenzi wa shule ile.

Katika hafla ile mtoto aliysoma risala kwa Aga Khan alikuwa Abdul Sykes akiwa na umri wa miaka 12.

Marehemu Kanyama Chiume amenihadithia kuwa wakati huu alipofika Aga Khan Tanganyika yeye alikuwa anasoma Shule ya Kitchwele na alikuwa katika bendi ya shule iliyompokea yeye akipiga, ‘’triangle,’’ na alinieleza kuwa picha yake yeye akipiga, ‘’triangle,’’ ilitokea katika gazeti.

Aga Khan alitoa fedha na shule ikajengwa New Street si mbali sana na ilipokuwa ofisi ya African Association.
Al Jamiatul Islamiyya Muslim School iliyojengwa kwa msaada wa Aga Khan
Kleist akawa katika kamati ya ujenzi akikagua kazi hadi ujenzi ulipokamilika. Hii ni moja kati ya shule za mwanzo kujengwa na Waislam wa Tanganyika. Jengo la Al Jamiatul Islamiyya lipo limesimama hadi leo kama ushahidi na kumbukumbu za juhudi za Waislam katika kujiletea maendeleo yao.

Serikali katika kuthamini mchango wa Kleist katika kupeleka mbele elimu kwa ajili ya watoto wa Kiislam ikamchagua kuwa katika Provincial Education Committee of Tanganyika Education. Mwanae Abdulwahid na yeye vilevile akaja kuwa katika Aga Khan Education Committee.

Halikadhalika walimu wawili wa Al Jamiatul Islamiyya walipewa nafasi muhimu katika siasa na uongozi wa nchi. na Sheikh Juma Mwindadi alifanywa mjumbe katika Baraza la Mji wa Dar es Salaam.

Mwaka 1956 Aga Khan alipotembelea Tanganyika Waismailia walimnunulia Mercedes Benz 280S yenye usajili DSQ 666 na hii ndiyo alikuwa akitembeanayo mjini Dar es Salaam.

Mwaka wa 1959 Waismailia waliamua kuiuza gari hii lakini hawakutaka inunuliwe na Muismailia ila inunuliwe na mtu yoyote mwenye hadhi katika jamii ya Watanganyika nje yao.

Gari hii aliuziwa Abdul Sykes na alikaanayo hadi alipofariki 1968.

Kisa Cha Aga Khan na Viongozi wa BAKWATA

Rais Mstaafu Sheikh Ali Hassan Mwinyi akiwa na viongozi wa Ismailia


Mwaka wa 1968 ulizuka mgogoro katika EAMWS ikidaiwa kuwa Waislam wa Tanganyika waikuwa hawataki kuongozwa nan a EAMWS ambae kiongozi wake alikuwa Aga Khan. Hapo chini ndiyo niliyoandika katika kitabu cha Abdul Sykes.

1968
''Juma lile lile Aga Khan ambae ndiye aliyekuwa akishambuliwa na kundi la Adam Nasibu, baada ya kutambua kuwa EAMWS isingeweza kamwe kuokolewa, akiwa Paris, Ufaransa alijiuzulu nafasi yake kama patron wa EAMWS.''


Aga Khan with Nyerere on his right and Kawawa on his left

1980s
Ungelitegemea viongozi wa BAKWATA wawe wamejifunza baada ya miaka hiyo yote ya udhalili wa Waislam lakini haikuwa hivyo.


Hata watu wazima hupigiana hadithi...

Leo nimeona picha nyingi za Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi katika Michuzi Blog zikimuonyesha rais mstaafu akiwa na viongozi wa Aga Khan katika maonyesho ya jumuia hiyo.

Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi na viongozi wa Jamii ya Ismailia

Aga Khan si mgeni Tanzania na waliomuingiza nchini ni Waislam katika miaka ya 1930 kwa ajili ya kutoa misaada kwa Waislam. Katika miaka ya 1930 baba yake huyu Aga Khan wa sasa Shah Karim Al Hussein, Sir Sultan Mohamed Shah alitembelea Tanganyika na katika mradi mmoja wapo aliofika kuuangalia ulikuwa ujenzi wa shule ya Al Jamiatul Islamiyya School, Mtaa wa Agrrey na New Street uliokuwa ukijengwa na Waislam chini ya Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika jumuia ya Waislam iliyoanzishwa mwaka 1933 viongozi wake wakiwa Kleist Sykes, Ali Jumbe Kiro, Mzee bin Sudi na wazee wengine wa mjini. Katika hafla ile mwanafunzi aliyesoma risala mbele ya Aga Khan alikuwa mtoto wa Kleist, Abdulwahid. (Miaka mingi baadae Abdulwahid Sykes sasa kijana na mwanasiasa akajachaguliwa kuwa mjumbe katika Bodi ya Elimu ya Aga Khan). 

Aga Khan alivutiwa sana na juhudi zile walizoonyesha Waislam  za kutaka kujiendeleza katika elimu na akatoa fedha zilizowezesha kumaliza ujenzi wa shule yote kwa ukamilifu wake. Aga Khan akatoa changamoto kwa Waislam wa Afrika Mashariki kuwa Muislam akichanga shilingi moja kwa ajili ya maendeleo ya umma yeye ataoa shilingi moja vilevile juu yake. Huu ulikuwa sasa wakati wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS). Kitendo hiki cha Aga Khan kilikuwa msaada mkubwa kwa Waislam kwani wakati wa ukoloni ni Ukristo pake yake ndiyo ulikuwa na fursa ya kupata misaada kutoka nje. Ushirikiano huu wa Aga Khan na Waislam wa Tanganyika uliendelea vizuri sana. Aga Khan kupitia EAMWS alijenga shule nyingi hadi kufikia sasa kutaka kujenga Chuo Kikuu cha Kiislam chini ya usimamizi wa Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Tewa Said Tewa na Aziz Khaki aliyekuwa mwakilishi wa Aga Khan Tanzania. Hii ilikuwa mwaka 1968 baada ya Tanganyika kuwa huru. Aga Khan na EAMWS kutaka kujenga chuo kikuu hapo ndiyo matatizo yakaanza baina ya Nyerere na uongozi wa EAMWS. Kisa hiki ni maarufu hapana haja ya kukirejea kuwa kipo hapa katika mtandao chini ya anuani ''BAKWATA.'' EAMWS ikavunjwa kwa amri ya Julius Nyerere na Sheikh Hassan bin Amir akafukuzwa Tanzania Bara.

Sasa tuingie kwenye hadithi yenyewe.


Aga Khan


Miaka mingi ikapita na mwishowe Nyerere akatoka madarakani na serikali ikashikwa na Ali Hassan Mwinyi. Kwa takriban miaka 20 Aga Khan hakupata kutia mguu Tanzania. Katika utawala wa Mwinyi Aga Khan akaja Tanzania. Katika mazungumzo na Rais Mwinyi, Mwinyi akaomba msaada wa Aga Khan katika nyanja tatu - Elimu, Kilimo na Afya. Aga Khan akamueleza Rais Mwinyi kuwa Aga Khan walikuwapo Tanzania miaka ya nyuma wakisaidia katika elimu. Hili suala la elimu likamgusa sana Aga Khan kiasi cha yeye alipomaliza mazungumzo na Mwinyi akamwamrisha Katibu wa Elimu wa Aga Khan Tanzania, Riyaz Gulamani awakaribishe viongozi wa Waislam wa iliyokuwa EAMWS pamoja na viongozi wa BAKWATA katika chakula cha jioni ili wajadili maendeleo ya Waislam. Katika viongozi wa EAMWS walioalikwa katika hafla ile alikuwa Tewa Said Tewa. BAKWATA walioalikwa walikuwa Sheikh Mkuu wa BAKWATA Hemed bin Jumaa, Adam Nasibu aliyekuwa katibu wa BAKWATA, Mustafa Songambele mzee wa CCM na mwanakamati katika BAKWATA na Waislam wengineo. Baada ya chakula Aga Khan akawaeleza nia yake ya kuwaita na akawataka watoe wanachotaka wafanyiwe na Aga Khan katika elimu.


Hapa ndipo ''drama,'' ilipoanza.

Akasimama kiongozi mmoja wa BAKWATA na mzee wa CCM, Mustafa Songambele, akamwambia Aga Khan, ''Serikali ya Tanzania inawatosheleza Waislam katika elimu na hawahitaji msaada kutoka kokote.''

Mustafa Songambele
Naomba nisimame hapa.

Mkasa huu kwa mara ya kwanza alinihadithia Riyaz Gulamani. Sikuamini kama inaweza kuwa kweli.

Kisa hiki nikaja kuhadithiwa tena na Tewa Said Tewa kama vile alivyonihadithia Riyaz Gulamani. Hapo ndipo nikaamini kuwa kisa kile hakika kilitokea na Mzee Tewa akanipa na jina la huyo aliyesema maneno yale.

Tuendelee.

Aga Khan kwa upole kabisa akajibu kuwa jana yake alikuwa na Rais na yeye kaomba msaada wa elimu. Hapo sasa ndipo likazuka zogo baina ya viongozi wa BAKWATA na Waislam wengine mbele ya mgeni Aga Khan.

Kufupisha mkasa.

Kabla hajaondoka kufuatia yale aliyosikia na aliyoshuhudia, Aga Khan akamwambia Riyaz, ''Inaelekea hawa ndugu zetu bado hawajawa tayari lakini ushauri wangu ni kuwa uache mlango wetu wazi. Siku yoyote watakapokuwa tayari basi tutatoa msaada.''


Mwisho wa hadithi yangu.
   
Mkapa na Aga Khan Kutoka Mwaka wa 1968
Hadi Mwaka wa 2014

Kuna msemo wa Kizungu unaosema, '' If you have patience you will see the end of everything.'' Maana yake kwa Kiswahili ni kuwa endapo utakuwa na subra utaona hatma ya kila kitu. Leo asubuhi  kituo kimoja cha TV kimemuonyesha Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa akiwa katika hafla ya Aga Khan akimsifia Aga Khan kwa kusaidia maendeleo ya Tanzania. Picha za TV zilimuonyesha Mkapa akiwa na viongozi wa juu wa Aga Khan. 

Mwaka wa 1968 huyu huyu Aga Khan alibidi ajiondoe Tanzania kwa idhara kubwa. Wakati ule Aga Khan alikuwa Patron wa East Africa Muslim Welfare Society (EAMWS). Kilichomfanya Aga Khan ajitoe Tanzania ni kuwa alikuwa anawasaidia Waislam na kulikuwa na mchakato wa kuwajengea Waislam wa Tanzania Chuo Kikuu yeye akiwa mmoja wa washirika. 


Nyerere ndiye aliyekuwa rais na alikuwa na udhibiti wa kila kitu katika nchi. Nyerere na Kanisa Katoliki walikuwa na hofu kubwa na Waislam na ni kutokana na hofu hii ndipo njama zikatengenezwa kumpiga vita Aga Khan ili EAMWS ivunjike na Chuo Kikuu kisijengwe. Propaganda dhidi ya Aga Khan na uongozi wa EAMWS zikaanza na mmoja wa waliokuwa wakiendesha vita hii alikuwa Benjamin Mkapa. Wakati ule Mkapa alikuwa Mhariri wa magazeti mawili ya TANU - ''Uhuru'' na ''Nationalist.'' 


Katika radio Mkurugenzi wa Radio Tanzania alikuwa Martin Kiama. Ikulu yuko Nyerere mwenyewe. Huu ulikuwa Utatu Mtakatifu. Mashambulizi dhidi ya Aga Khan yalipangwa vyema. Benjamini Mkapa akitumia gazeti la ''Nationalist'' ataandika habari yoyote dhidi ya EAMWS na viongozi wake.  Martin Kiama akitumia Radio Tanzania atatumia habari ile kama habari muhimu katika radio na habari hiyo itatangazwa kutwa nzima huku ofisi ya rais ikiwa kimya kwa fitna ile. 


Mwaka ule wa 1968 Mkapa hakuwa na ndoto kuwa ipo siku atajakuwa rais wa Tanzania. Ni wazi vilevile kuwa haikumpitikia hata kidogo kuwa huyu Aga Khan waliyekuwa wakimpiga vita atajarudi Tanzania kutoa misaada ila safari hii hatorudi kuwasaidia Waislam. Hakika ukiwa na subra utaona mwisho wa kila jambo. Aga Khan adui wa jana leo amekuwa rafiki kipenzi wa kusifiwa na kushukuriwa hadi akajua kashukuriwa.


No comments: