Monday 2 October 2017

SHEIKH ABDULRAZAK MUSSA SIMAI MAARUFU KWA JINA LA ''KWACHA,'' ANAKUMBUKA NA KUKUMBUSHWA

Utangulizi

Sheikh Abdulrazak Mussa Simai (Kwacha)

Mwandishi wa makala haya ya Sheikh Kwacha (jina nimelihifadhi) mie humuusudu sana na huwa sipiti wala sithubutu kufanya hivyo ninapoona makala zake. Kalamu yake kaitia barafu, maneno baridi lakini yanatia ganzi. Msome hapo chini anavyomweleza Maalim Sheikh Abdulrazak Musa Simai, mwanasiasa wa Hizbu, bingwa wa tajwid lakini ikafika wakati akiwa jukwaani akiambiwa asome Qur’an anasema, ‘’Haya hii Qur’an nasoma, ‘’Alif, Be, Te, The…Wasalaam.’’ Walioijua ilm yake wakabaki wameinamisha vichwa huku wakivitingisha. Msikilize Sheikh Kwacha wa leo hapo chini na msome mwandishi baridi anavyomweleza katika wakati wake.


Kwacha ana tarekhe ya namna yake ambayo inamuweka mtu kuona namna mtu anavyokuwa anabadilika kutokana na zama na kushindwa baadhi yao kutanabahi kuwa wakati sio wauuendekeza ila akhera ndio ya mtu kuiweka usoni.

Jina la Kwacha kamili ni Abdulrazak Mussa Simai mzaliwa wa Paje, amebahatika kwa zama za katika miaka 50 na mwanzo ya 60 kuweza kusoma elimu ya dini na dunia.

Kwacha alikuwa katika wenye kupenda kusikilizwa anaposimama kwenye jukwaa na kuzifasili siaza za Hizbul Watan-ZNP.

Akipanda jukwaani atatoa mwito, ‘’Kwaacha.’’ Hujibiwa, ‘’Kweupe,’’ yaani kumeshakuchaa!
Wasikilizani humjibu Kweupee yaani sasa walikuwa wanataka uhuru.

Vigogo vya ZNP wakati huo ni Abdulrahman Mohammed Babu na Ali Muhsin Barwany ukitaka kuyajua hayo mbali ya kuhadithiwa jitupe kwenye Ofisi ya Nyaraka (Archives) kisha nenda moja kwa moja kwenye sehemu ya magazeti yaliopita uombe, ‘’Mwongozi,’’ ya 1950 kisha mtafute Babu halafu Ali Muhsin, Babu msome, ‘’Fikra za Mwanadamu,’’ na Sheikh Ali Muhsin msome, ‘’Barua kutoka Cairo,’’ hapo kama mwaka wa 1958 utapowasoma ukawaona namna afkar zao zilivyokuwa na hoja nzito walizonazo unaona hata hawa wanasiasa wetu wa leo na kuwa na mitandao hawakaribii hata shubiri.

Kila kitu huandikwa, wazee wetu wakipenda kusema ‘’aaah, Maktoub,’’ yameandikwa hayo.
Nini kilichotokea?

Kilichotokea ni pale shetani alipoingia Babu kuja na hoja Kwacha aje Mjini kugombania kiti kwa ZNP na Sheikh Ali Muhsin aende Ng’ambo hapo ndipo sawtafaham kubwa ambayo ilikuwa na sababu nyuma ya pazia, na nyenginezo kama kina Ali Sultan kuwekewa makartasi na mengineo.

Umma Party ikabidi iundwe, katika kipindi hiki ilihitajika nasaha watu kuja pamoja badala ya kufarikiana kwani hapo ndipo paliporaruka Zanzibar hadi leo kuwa hapashoneki.

Chama cha ZNP kilikuwa ni tishio kubwa kwa wakoloni na Afrika, kilikuwa ni Chama cha Kizalendo ambacho kikiunga mkono harakati za Mau Mau Kenya, FNL Algeria na kuwa wapo mstari wa mebele katika masuala mazima ya Pan Africanism, wakati huku ASP washapewa Land Rover kutoka Jeresulem na wao wapo na Siasa ya Gozi Zuia.

ZNP ilikuwa ndio yenye kutaka kuleta uhuru na kuunganisha Waafrika na suala zima la Pan Africanism, fitna na Muingereza akayasuka yake kuuparaganya umoja wa kikweli wa Wazanzibari ambao kina Mzee Vuai Kitoweo, Maalim Mandowa, Shaalabi wahadimu wa asili walipompa Uongozi Ali Muhsin hao waliitakia Zanzibar iwe ya umoja na iwe ya watu wote ingawa kila mmoja anayake ya kuyaelezea.

Kwacha akawa Umma Party sasa, Mapinduzi yakaja akapata mpaka U-Regeional Commisioner, akawa alivyokuwa kama walivyokuwa wengine bada ya Mapinduzi na vishindo vya Kimapinduzi.

Paa! 72 imefika Karume kauliwa Tarehe 7 April, 1972 Macomrade wakaanza kukamatwa mmoja bada ya mwengine na Kwacha akawemo kama wakati huo wenyewe ASP wakisema, ‘’Aliomo yumo asiokuwemo hayumo.’’


Abeid Amani Karume

Yeye akakuwemo akafungwa na akaja kutolewa akiwa mnyonge kabisa, akaamua kurejea Paje na kusomesha Qur’an na Darsa kwa misingi aliopita kwa wazee wake.

Kwacha akaonekana siasa kamwe hatoitaka tena, lakini dunia sio mgando bali ni mtiririko, (It is not static but is dynamic) akaja mwanawe wa kike akifaya kazi Manispaa (Zanzibar Municipal Council) akiwa mshika fedha pakatokea matatizo kazini kwake yakawa bimdogo huyo hana njia ya kutoka, hapo Kwacha akategwa kuwa yaeshe kwa mwanawe aje kwenye Chama tawala na apande kwenye majukwaa arushe cheche na fashfashi na fataki akama alivyokuwa akizivurumisha wakati wa Hizbu, naam akaitikia wito, heeehe ukajiuliza huyu Kwacha aliotulia na kurudi kwa Mungu au aliokuja tena kuwa Firauni?

Kwani maneno yake yakawa ya Kifirauni, baadhi ya watu wakamhama msikitini kwa kuona kichakuwa burtangi amekwenda arijojo.

Nasita hapa, kisha nitarudia kuyaeleza ninayoyajua, nilioyasikia na niliyoyasoma.

Nionavyo sivyo uonavyo na haina maana sote tuone sawa sawa, ila wazee huja wakasema hizo nilizozimwaga ni  tarahambi, mimi naona kama mzee Al Marhum Amani Thani alivyosema kwenye kitabu chake, ‘’Ukweli ni Huu,’’ aliposema, ''Mie naandika kama nisemavyo, hizo kanuni za uandishi sinazo.''

Naibwaga nanga hapa bada ya safari iliokuwa shwari bila ya mawimbi ya aina yoyote ile.

No comments: