![]() |
Abdul Majham |
![]() |
Abdul Majham |
Mwaka wa 2014
nilifanya Mahojiano na Mchezaj wa zamani wa timeu ya Taifa ya Zanzibar na timu
ya Vikokotoni Abdulmajham.
Yafwatayo ni mahijiano baina yangu Hamza
Z. Rijal na Abdumajham. Leo tarehe 4 October 2017 Abdulmajham katangulia kwenye
haki, Mola amlaze pema Peponi, Ameen
Wengi wanamjua
kwa jina lake la mkato: Majham. Kuna wanaomwita ‘Pele wa Zanzibar.’ Angelikuwa amezaliwa Ulaya,
Marekani au hata Amerika ya Kusini hii leo angeliku-wa anaenziwa. Hakujaaliwa bahati ya akina Bobby Charlton, Geoff Hurst, Johan
Cruyff, Platini, Pele, Blokhin, Hadji, Latto, Tostao, Gerson, Romario.
Angelijaaliwa bahati hiyo basi angelikuwa fahari ya nchi yake kwani zama zake
Majham alikuwa amebobea katika michezo miwili soka na hockey (mpira wa magongo).
Viwanja vya soka
vikimjua, viwanja vya hockey vikimtambua. Siku hizi ukimtafuta Majham hutompata
kwenye viwanja vya soka wala vya hockey. Kwanza vya hockey haviko tena Zanzibar
kwani hockey haichezwi tena nchini mwetu. Mchezo huo ulipigwa marufuku baada ya
Mapinduzi ukionekana kuwa ni spoti ya kibwanyenye. Siku hizi ukimtaka Majham
itakubidi wende Mchangani. Zikate kona mbili tatu hadi nyumbani kwake. Ukibahatika
utamkuta amekaa barazani. Saa zote anakuwa mpweke hapo barazani kwake akitafuta
rubaa la washabiki wa spoti wa kuweza kuzungumza naye. Ingawa ni mpweke hataki
kujinasibisha na chochote kile hii leo.
Majham jina kamili Abdul Majham Omar —
amekuwa mfano wa lulu iliyotupwa. Pamoja na uzee, ana umri wa miaka
79, Majham siku hizi ni dhaifu, ganzi ya miguu inamsumbua na haoni
sawasawa.
Mwandishi aligundua kitu kimoja chaki pekee Majham alichokuwanacho kinapotokea kitu katika
mazungumzo kinachomkuna husema, ‘awii.’
Mwandishi: Jee unakumbuka mwaka uliozaliwa?
Majham: Miye sikumbuki lakini labda uwaulize wale niliocheza nao watu kama
kina Sayyid Ali Soud, lakini ninachoweza kukisema kuwa ninafahamu fika kuyajuwa
yaliokuwa yanaendelea kwenye Vita Vikuu vya Pili wakati huo ni mtoto wa
makamo naenda chuoni kusoma Qur’an.
Mwandishi: Itakuwa labda una umriwa miaka 9 hivi wakati huo
wa VitaVikuu vya Pili vya dunia?
Majham: Zaidi, labda miaka 11 au 12.
Mwandishi: Nikifanya mahesabu unafikia umri wa miaka 79.
Majham: Nakubaliana na wewe.
Mwandishi: Nielezee maisha yako kwa mukhtasar?
Majham: Mi.mi ni mzaliwa wa mtaa wa Malindi na ndipo nilipokulia. Nalianza
masomo yangu ya Qur’an chuo cha Maalim Jeledi, Nilisoma hapo mpaka
nikahitimu na huku nikiendelea na masomo ya msingi katika skuli ya
Gulioni. Naikumbuka
Gulioni na nina masikitiko kuwa jengo la skuli hiyo halipo. Nawakumbuka baadhi ya
walimu wetu ambao walikuwa sio walimu wenye kusomesha lakini walikuwa ni wazazi
wetu. Unaposomeshwa na Maalim Burhan au Maalim Buda au Maalim
Badi unajikuta kuwa upo na sehemu ya wazazi wako. Sijabahatika kusoma na
kufika mbali, nalimaliza masomo hapo Gulioni skuli nilipofika chumba cha
5.
Mwandishi: Baada ya masomo yamsingi ulikuwa unafanya nini?
Majham: Zamani sio leo, kila mtu alikuwa ni mzee.
Nilitafutiwa kazi na wazee na kupata kazi sehemu ya Umeme pale Public Works
Department (PWD) na nilifanya kazi hapo kwenye miaka ya 1950 hadi kufikia Mapinduzi.
Halafu nikawa nafanya kazi katika Shirika la Umeme nanimefanya kazi hapo hadi
kufikia kustaafu.
Mwandishi: Baada ya kuzungumzia maisha yako kwa
jumla hebu tugeukia michezo. Kitu gani kilikuvutia kucheza soka, hockey (mpira wa magongo)na kriketi (cricket)?
Majham: Nimeanza kucheza soka nikiwa na umri wa
miaka sita na nilikuwa hodari wa kupiga chenga tangu umri huo. Ninapocheza
na watoto wenzangu kila mtu huvutiwa namna ninavyochukua mpira na kuwapiga
chenga wenzangu. Nilipokujakuona filamu ya Garincha pale Ofisi ya Filamu ya kina
Mohammed Kassim, hapo ndipo ikawa nikichocheo kikubwa kwangu kuwa
nakokota mpira na kuhesabu wachezaji, ingawa Mwalimu wetu ‘Mr. Mazal’, huyu ni Ahmed
Iddi Mjasiri. alikuwa hapendi kumuona mtu anakaa na mpira kwa muda mrefu.
Mwandishi: Majham wewe ni mzaliwa wa Malindi,
verejee ukachezeaVikokotoni?
Vikokotoni Sports Football Team 1959:
1. Mzee Mwinyi Mpiringo 2. Mussa Bakari 3. Coach Mzee Ahmed Iddi Mjasiri 4. Abdulmajham 5. Salum Mkweche 6. Nylon 7. Hijja Saleh 8. Magram 9. 10 Salum Hamdan 11. Maulidi Machprala 12. Bape 13. Wajih Sheikh 14. ??
1. Mzee Mwinyi Mpiringo 2. Mussa Bakari 3. Coach Mzee Ahmed Iddi Mjasiri 4. Abdulmajham 5. Salum Mkweche 6. Nylon 7. Hijja Saleh 8. Magram 9. 10 Salum Hamdan 11. Maulidi Machprala 12. Bape 13. Wajih Sheikh 14. ??
Majham: Ukweli miye sipendi mambo ya kifahari wala
kujiweka mbelembele. Miye mambo yangu ni kutopenda mambo ya kifakhfakh.
Kwasababu hizo ndio nikenda Vikokotoni, ingawa nilicheza muda mfupi katika
timu inayoitwa Hadhrami. Haya mambo ya Hadhrami yawache kwani yana hikaya
refu.
Mwandishi: Kwa nini isiwe Kikwajuni, Mwembeladu,
Miembeni?
Majham: Miembeni au Kikwajuni zama hizo kulikuwa
ni sawa kwa leo kama upo maeneo ya Mwanakwerekwe. Doooh, ingekuwa taabu kwangu.
Mwandishi: Taabu ya nini?
Majham: Uwwih, alaaa, kacheka sana bila ya kutaka kuendeleza.
Mwandishi: Ulianza kuchezea Gossage mwaka gani?
Majham: Nakumbuka nilianza kucheza Gossage 1952 nakupa na hiyo picha uone. Nilikuwa na kina Mzee Mwinyi (Mpiringo) Mzee Ahmed Islam, Seif Rashid,
Maulidi Mohamed (Machaprala) na wengineo. Tulicheza Nairobi tulikuwa
washindi wa pili. Tuliwafunga Waganda na Tanganyika, tulilala kwa Kenya na
ukweli Kenya ikitupa tabu sana, kwani wakitumia nguvu za hali ya juu na sisi
tulikuwa na wachezaji wachache ambao wakitumia nguvu. Sisi mchezo wetuni
dama, mfano wa Brazili. Unaweka karata kwenye bao, unaanza nyuma unafika kati,
unachezewa kidogo unapelekwa wingi, unawekwa kati, haooo, tunarudi, huo ndio
mtindo wetu. Kenya wao pasi tatu wako golini. Kutoka hapo niliendelea
kuchaguliwa kwenye timu ya Gossage mpaka mwaka wa 1968 ndio nikamalizia kucheza
timu ya taifa. Nimecheza na kina Kassim bin Mussa, Sururu, Khalid Kessi,
Boti mkubwa wa Malindi, nikaja nikacheza na vijana kina Boti mdogo, Abdimout
Ajmi, Saad, Hijja Saleh, Seif Rashid, Seif Nassor (Mshumaa). Kisha
nilikuwa na fowad nikistaladha kucheza nao, huku Ahmada Mwanga, huku Mossi
Kassim, Mkweche kushoto, Ahmada Mwangana,
mfalme wa hewani Mohammed Kassim, uwwih, alaaa. Hapo nakwambia kigoma
tukikipiga, waulize Warusi waliokuja na kuzifunga timu zote za Afrika Mashariki
na kuja hapa tukenda suluhu nao. Warusi hawajaweza kuamini, siku hiyo mpate
Ahmada Mwanga na Mkweche watakuelezea kigoma tulivyokipiga, ilikuwa kila mtu anazungumza
juu ya game hii.
Mwandishi: Mchezo gani unaoukumbuka na hutousahau?
Timu ya Gossage ya Zanzibar 1966 Majham watano kutoka kushoto waliosimama baada ya Bobeya
Majham: Gossage Zanzibar mwaka wa 1966, timu yetu ilikuwa 1. Bobea. 2.
Sleiman Amour 3. Tindo 4. Ahmed Himidi London 5. Majham 6. Kitwana Rajab 7.
Mossi Kassim, 8.Mohammed Kassim. 9. Peter 10. Ahmada Mwanga 11.
Maalim Seif Nassor (Mshumaa). Tulifungwa na Kenya, tukalala kwa Tanganyika na
tukenda suluhu na Uganda. Natamani kungekuwa na
filamu yake ungeona namna tunavyocheza. Yule kocha wa Tanganyika aliwahi kusema
lau ningeipata timu hii ya Zanzibarn ingekuwa juu.
Mwandishi: Tuzungumzie
hockey (mpira wa magongo) na kriketi(cricket).
Majham: Kriketi
sijacheza. Nilijaribu nikaona mchezo haunifai, kwani unachukua muda mrefu,
lakini mpira wa magongo nilicheza baadaya kushauriwa kuwa nitasaidia hockey ambayo ilianza kupotea baada ya Mapinduzi. Nikasema kuwa nipo tayari lakini
naogopa kucheza mbele, nikapendekezwa nicheze golikipa na nikakubali. Ukipa
wangu ulikuwa nachanganya na utaalamu wa soka nikawa natoa pasi nacheza
kijanja, nikapata sifa nikawa nachaguliwa timu ya taifa miye, kijana Islam Ahmed Islam
nimechea mpira na babake, halafu huyu Daktari Mohamed
Jidawi tukicheza pamoja timu ya Taifa ya Tanzania. Umetaja kriketi, nikipenda
kuwaangalia vijana wawili wazalendo wakichezea Comorian, Zaghalouli na Ahmed
Himidi. Wakikutana hao, basi utaona raha. Zaghalouli anapiga mipau, mipira
kaokote jumba la Makumbusho, lakini Ahmed Himidi kutwa yupo kiwanjani anazuia tu,
akiwapa taabu kwelikweli warushaji mipira. Mbona leo umeazimia kutaka kuniliza?
Leo wapi… nchi hii watu wakicheza futuboli, hockey, kriketi, tenis hata gofu.
Michezo yote imekufa isipokuwa soka. Kuna wachezaji kama Ahmed Himidi London
akicheza michezo yote hio, sio kucheza tu, lakini akichaguliwa katika timu
ya taifa kwa kwa kila mchezo.
Mwandishi: Unanyongeza?
Majham: Nyongeza
ninayo. Kwanza mbona hujaniuliza kuwa timu ya kwanza kucheza kombe la klabu la
Afrika ilikuwa ni Cosmopolitan chini ya Mwalimu Mansour Magram. Tulicheza na timu ya Somalia
tulikwenda suluhu 1-1 pale kiwanja cha Ilala Dar-es-Salaam na
tukashindwa kwenda Somalia kwa mbinu za FAT kutotaka twende. Silisahau
hili. Tupo klabu tunasubiri safari na mabegi yetu tunaambiwa hamna
safari. Tulikuweko pale kina Abdimout, Msuba, Msomali, Emil Kondo, Marandu, Abuu, Kitwana Douglas,
Masiku, Rajabu, Iddi Balozi, Makanda. Tulikuwa tuelekee Somalia zikafanywa hila na haya
yanakwenda na kujirejea. Jengine, kama unavyoniona nipo mgonjwa. Nashukuru
nimepata kuonana na Rais Ali Mohamed Shein nikaambiwa nitapatiwa matibabu nje
ya nchi, lakini hadi leo hakuna lilofanyika na hali yangu ya kiafya
inakwenda chini. Aidha namshukuru Waziri Mohammed Aboud na ile kamati ya mtoto wa muuza magazeti Farouk Karim na
wewe mwandishi naambiwa umo,
kufanyisha mchango wakuweza kunisaidia nashukuru sana, sana.
Wachezaji wa Timu ya Cosmopolitan ambo ndio walikua mabingwa wakwanza kuwakilisha Tanzania katika mashi dano ya klabu bingwa Africa. Waliosimama kutoka kushoto. Couch- Mansoor Magram, Abdallah Mgambo, Mbaraka Peter, Hamidu, Msuba, Hamisi Dibya, Abdu kiziwi, Walio chuchumaa kutoka kushoto. Mohamed Msomali, Emil Kondo (Capt.) Mohamed Mfaume, Abdul Mutti, Sharif Mansab, Harubu Iddi. Majham hayumo wala Mhammed Kassim hayumo, kutoka Zanzibar ni Kipa tu Abdi Mout Ajmi. Majham alisajiliwa kwa Africa Cup tu pamoja na Mohammed Kassim, kisha Mohammed Kassim alipokuja kujiunga na East African Airways akawa ndio anachezea Cosmopolitan. Majham Taifa Star alichezea Taifa Star ilipokwenda China, Madagascar na Mauritius. Amedumu katika team ya Hockey zaidi kwenye team ya Taifa. Wachezaji wa Timu ya Cosmopolitan ambo ndio walikua mabingwa wakwanza kuwakilisha Tanzania katika mashi dano ya klabu bingwa Africa. Waliosimama kutoka kushoto. Couch- Mansoor Magram, Abdallah Mgambo, Mbaraka Peter, Hamidu, Msuba, Hamisi Dibya, Abdu kiziwi, Walio chuchumaa kutoka kushoto. Mohamed Msomali, Emil Kondo (Capt.) Mohamed Mfaume, Abdul Mutti, Sharif Mansab, Harubu Iddi,
Wito wangu Serikali ijuwe sisi tulilitumikia taifa basi tuangaliwe kama
wenzetu huko Ulaya na kwengineko. Tumetupwa useme kanda la usufi, puuu.
Hapo
ndipo yalipomalizikia mahojiano yetu ikiwa siku ya mwezi wa Ramadhani.
![]() |
Abdulmajhal na Mohamed Kasim |
![]() |
Majham |
No comments:
Post a Comment