Friday 8 December 2017

KUTOKA JF: MWANDISHI ALIPOKAMATWA UWANJA WA NDEGE WA JULIUS NYERERE 2007



Mtoto...
Unanituhumu kwa udini na nadhani tuhuma hii ni kwa sababu mimi nimeweza
kuthubutu kuuliza mengi ambayo wengine walishindwa.

Kubwa ambalo wengi limewachoma ni kule mimi kuandika kitabu cha Abdul
Sykes 
na kupitia kitabu kile nikaweza kueleza historia ya TANU na uhuru wa
Tanganyika.

Kwa mara ya kwanza historia ya kweli ya uhuru ikajulikana na majina yale
ambayo kwa miaka yalikuwa hayamo katika historia hii yakajitokeza.

Ikiwa wewe unaona huu ni udini basi hii ni bahati mbaya kwako.

Tuje kwenye mimi kukamatwa uwanja wa ndege kwa kushukiwa kuwa ni
muuza unga.

Tatizo halikuwa unga tatizo langu lilianza Chuo Kikuu Cha Ibadan, Nigeria mwaka
wa 2006.

Nilialikwa kwenye mkutano kuhusu ugaidi na nilitoka mada ambayo iliwakera
Marekani ambao walikuwa waandaaji wa mkutano ule wakishirikiana na Iran na
Chuo Kikuu Cha Ibadan.

Maneno yaliyowachoma ni mimi kueleza historia ya taifa lile katika mauaji mengi
duniani kwa njia za dhulma.

Nikaeleza pia Sheria ya Ugaidi iliyopitishwa Tanzania mwaka wa 2002 na kwa hakika
niliichambua na kueleza athari yake kwa Waislam wa Tanzania na nikatoa mifano ya
vipi Waislam ambao wanajishughulisha na maendeleo ya umma wa Kiislam kwa
miaka mingi walivyokamatwa na kuwekwa mahabusi baada ya kupitishwa sheria hiyo.

(In Shaa Allah nitaiweka hiyo paper mwisho ili uisome na uelewe kile nnilichosema).

Wakati naeleza haya Wamarekani ambao walikuwa na timu kubwa katika mkutano ule
walikuwa wanachukua, ''notes,'' na video.

Mmoja wa waliokuwapo katika mkutano ule alikuwa mwakilishi wa Ubalozi wa Tanzania
kutoka Lagos.

Nilirudi Dar es Salaam salama na nikasahau.

Mwaka unaofuatia yaani 2007 nilialikwa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran
kwenye Hawli ya Imam Khomeni.

Iran ilialika watu dunia nzima na mkutano ulikuwa mkubwa.

Tanzania walialikwa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na waandishi wa habari kutoka
''electronic'' na ''print media,'' yaani magazeti na televisheni.

Ilikuwa nilipofika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere ndipo nilipokamatwa kwa
kushukiwa kusafirisha mihadarati.

Nilifanyiwa mahojiano na vyombo vya usalama na nikafanyiwa upekuzi wa mizigo yangu
lakini hapakuwa na chochote.

Wakati mwingine maswali yao yalikuwa ya kuchekesha.

Waliniuliza kwa nini ninaingiza vitabu vya Khomeni Tanzania na mimi nikawa nawajibu
kwa kuwauliza kuwa kwani hairuhusiwi?

Waliniuliza imekuwaje nimefahamika na Iran kiasi cha mimi kualikwa huko.

Nami nikawapa orodha ya nchi ambazo nimealikwa na nimezungumza katika vyuo vyao
na nikawaeleza kuwa hata mimi sifahamu wananijua vipi ila huwa napata mialiko tu na
mimi sijaona haja ya kuwauliza wamenijuaje.

Waliniweka pale uwanja wa ndege hadi asubuhi na wakanieleza kuwa hawawezi kuniachia
hadi wapate maelekezo kutoka juu.

Asubuhi wakaniachia na wakanitaka radhi wakisema kuwa kumekuwa na makosa kwa upande
wao na wakajitolea kunipa usafiri kunipeleka nyumbani kwangu.

Niliwashukuru na nikawaambia kuwa nitachukua taxi.

Kitu kilichonifurahisha ni pale nilipoona wahojaji wangu wakinibebea mizigo yangu hadi nje
ya uwanja huku wakizungumza na mimi kwa adabu na bashasha na kuniambia kuwa ninapopita
hapo nikiwa nasafiri nisikose kuwapitia ofisini kwao kuwasalimu.

Ukweli ni kuwa ile yote ya mie kukamatwa haikuwa katika madawa ya kulevya bali ilitokana
na ile mada ambayo niliwasilisha Chuo Kikuu Cha Ibadan.

Wamarekani hawakupendezewa na yale niliyosema na kwa hivyo walileta taarifa hapa nyumbani
kuhusu mimi.

Haikuishia hapo.

Mimi bila kujua pasi yangu ikawekewa alama ambayo haionekani kwa macho ila inasomeka katika
''computer,'' za Uhamiaji.

Ikawa sasa kila ninaposafiri inajulikana nakwenda wapi na kwa shughuli ipi na nikiwa ''transit,''
napekuliwa kwa uangalifu zaidi.

Nafuatiliwa wapi nimefikia, ''transactions'' za ATM wakati napokea fedha kutoka nje ya nchi na pia
ninapokuwa safarini.

Huchukua zaidi ya siku moja kwa mimi kupokea fedha Western Union jambo ambalo
kwa kawaida ni kazi ya dakika chache.

Kadi yangu ya ATM ilikataa kutoa fedha New York kwa kweli ni hali si nzuri sana.

Nimepata kutolewa katika foleni ya kuingia katika ndege Schipol Airport Amterdam nikielekea
Marekani.

Usumbufu ni mwingi.
Nakuwekea hapo chini paper niliyowasilisha Chuo Kikuu Cha Ibadan ambato ilisababisha haya yote:
Mohamed Said: ISLAM, TERRORISM AND AFRICAN DEVELOPMENT

[​IMG]

Tehran, Iran nikiwa katika Ukumbi wa Mkutano

No comments: