Shajara ya Mwana Mzizima:
''BWANA MKUBWA'' JOHN RUPIA
Na Alhaj Abdallah
Tambaza
Kushoto John Rupia, Julius Nyerere na Zuberi Mtemvu, nyuma yao ni Bantu Groups walinzi wa viongozi wa TANU na wahamasishaji, 1955 |
Raia Mwema 22-23 Januari 2018 |
KATIKA
ukurasa huu wa Shajara ya Mwana Mzizima, Jumatatu iliyopita, tuliandika kuhusu
madhila na manyanyaso waliofanyiwa watu weusi katika taifa hili wakati wa
utawala wa kishenzi wa Wakoloni wa Kingereza pamoja na vibaraka wao wa Kihindi
waliowaleta hapa kuwasaidia kazi.
Tulieleza
kwa kirefu namna sisi, wana wa nchi hii, tulivyobaguliwa katika nyanja
mbalimbali kuanzia makazi, ajira, elimu na tiba mpaka ikawa inakera sana
kuvumilia hali ile. Hali zetu zilikuwa zinatisha—dhalili kupita maelezo.
Sijui
kama watu wa kileo ambao hawakuyashuhudia haya wanaweza kuamini, lakini wakoloni – tena wote Mngereza na
Mjerumani— hawakututawala kwa wema na upole, pamoja na kwamba ilikuwa ni sisi
tuliochangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya nchi zao kwa jasho na nguvu zetu.
Kwa
kutumia ile dhana ya ‘Mercantilism’, ambayo maana yake ni kwamba kwenye makoloni
ya Kiingereza, watu walime kwa nguvu sana na kusafirisha malighafi kwa ‘bwana
mkubwa’ ambaye atatengenezea bidhaa kwenye viwanda vyake na kuuza kwenye nchi
nyingine na yeye kufutika faida yote—wizi mtupu.
Hakuna
faida kurudi kwenye koloni au nchi husika kuja kusaidia maendeleo, bali fedha
zote zilibaki kwenye himaya ya mtawala. Hapa zililetwa fedha kiduchu sana kwa
ajili ya uendeshaji ofisi na kununulia sare za kazi (uniforms), karatasi, penseli,
kalamu na vidawati vya wino maofisini mwao.
Elimu
ile ya kibaguzi na finyu, ilitolewa katika mazingira magumu sana. Hawakuta
kusomesha mtu mazungu yale bali walitaka wasaidizi tu kidogo. Mwandishi huyu,
alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Mnazi Mmoja kuanzia mwaka 1958
mpaka 1961 alipohamia shule ya kati ya Kitchwele Boys Middle School mjini DSM,
mwaka 1962.
Shuleni
tulivishwa magwanda ya khaki ngumu kuanzia kaptura na mashati; yote ni khaki tu
bila kujali mji wa DSM una joto sana. Walimu, ingawa wengi walikuwa ni waafrika
wenzetu, lakini walifuata maadili na maelekezo ya ‘mabwana wakubwa’ ya
kuendesha taasisi zake kibaguzibaguzi.
Pale
shuleni Mnazi Mmoja, hatukuruhusiwa kwenda shule tukiwa tumevaa viatu vyovyote
hata kandambili! Sheria za shule hazikuruhusu. Ni nini hiyo kama si
udhalilishaji, wakati walimu wao wakiwa wamepiga tai, wei kichwani (ni ule
mstari unaogawa nywele kichwani mafungu mawili), wakipendeza kama mabwana zao Wazungu.
Kutovaa
viatu pale maana yake ni kwamba, hata chooni tulikuwa tukiingia na kupishana
hivyo hivyo watoto wote; na miguu yetu ikawa inakumba na kukanyaga vimajimaji vya chooni na haja ndogo kutwa
nzima— Subhanallah!
Katika
shule hizo, vichocho, visonono na magonjwa mengine ya kuambukiza yalikuwa ni
kama kila mtu anaugua wakati wowote. Sasa unapopata ugonjwa huo hapo ni
sindano! Sindano! Sindano tu kila siku— kali sana zenye kuleta kichefuchefu,
kutapisha na kutia homa. Kila nikikumbuka hapa nasikia uchungu sana, kwani ni
mara nyingi sana nimekumbana na kadhia hizo pale shuleni.
Kwenye
ajira vilevile, nimeshuhudia watu wazima wakienda maofisini bila viatu. Juu
wameweka magwanda yao na soksi ndefu mpaka magotini—viatu usivae ukafanana na
mkubwa Mzungu!
Kwenye
mchezo wa mpira waliotuletea; wenyewe ukicheza nao wao wanavaa viatu vyenye
njumu za kuchoma; wewe pekupeku huku wakikuumiza na misumari kwenye viatu vyao.
Kwenye Ligi ya DSM ya Soka, Wazungu walikuwa na timu yao kutoka Gymkhana na
Wahindi (Magoa) nao walikuwa na timu ikiwa Goans Institute (ikitamkwa na
wenyeji Goanisi)— hata maana yake walikuwa hawajui masikini. Timu hizo zote
zilikuwa zikicheza na viatu wanapokutana na Yanga, Sunderland (sasa Simba),
pamoja na timu za makuli wa bandarini za Dockyard na Cargo and Handling. Hawa
wote wakicheza wamefunga mabandeji miguuni.
Katika
timu ya Dar Combine kulikuwa na wachezaji watatu wa ‘daraja za juu’. Sentahafu
wa timu ambaye pia ndio kepteni alicheza na viatu; Goalkeaper alikuwa mzungu
mmoja mnene ‘tipwatipwa’ akiitwa Mavrodis yeye naye alikuwa na viatu na
mwingine Tony Fernandes kutoka Goanisi yeye naye alicheza na viatu.
Waliobaki
wote wa wakati huo, pamoja na kwamba walikuwa wanacheza timu moja ya Dar
Kombaini walicheza bila viatu na ikaoneka sawa tu! Waafrika weusi; viatu vya
nini. Timu ile naikumbuka vizuri sana nikiwa nasoma pale Kitchwele Middle
School. Walikuwamo akina Ayoub Mohammed, Ishaka Mzee, Billy Bandawe, Wilcokson,
Yahya Mbiki, Lukongo, Chaurembo, Yussuf Mwamba na Waziri.
Mambo
hayo na mengineyo mengi tukipata muda tutayaelezea, ndiyo yaliyowasukuma kwa
uchungu mkubwa wazee wetu wale wakajiunga pamoja kimyakimya, wakaanda mipango
madhubuti kwa hali na mali ili wao— na sisi tujao— tuondokane na mateso yale.
Mmoja
katika wazee waliojitolea pakubwa ni hayati
Mzee John Rupia. Huyu ‘Bwana Mkubwa’ wetu, wakati wa ukoloni hakuwa lofa
hata kidogo. Alimiliki majumba hapa mjini, mashamba makubwa kule Mbagala na
Kigamboni, malori ya kusomba mawe, kokoto na mchanga pamoja na machimbo ya mawe
kule Kunduchi kukiitwa Maweni.
Mzee
Rupia alijihusisha na biashara nyingine nyingi sana. ‘Bwana Mkubwa’ yule hakuwa
na shida ya fedha ndogo wala kubwa. Kwa kiasi fulani aliishi kama wale jamaa
wengine wa madaraja ya pili (Wahindi) na la tatu (Waarabu).
Mzee
John Rupia asili yake ni Msukuma wa
maeneo ya Mwanza, lakini aliishi hapa Mzizima kwetu kwa miaka mingi toka
utotoni kwake hivi; na hivyo kuwa sehemu ya historia ya mji huu. Alikuwa mmoja
wa Waswahili wa mwanzo kabisa kujenga mjengo wa ghorofa katika makutano ya
Barabara ya Kitchwele (sasa Uhuru) inapokutana na Msimbazi. Kwa wakati ule
halikuwa jengo la kuchezea. Lipo pale mpaka leo likisomeka kama Rupia Building.
likiwa limesheni maduka ya biashara na ‘flats’ za kukaa watu juu ghorofani.
Mwenyewe,
kabla ya uhuru akikaa Mtaa wa Ndanda pale Misheni Kota akila, akinywa, akilala
na kushuhudia maovu yote ya Wazungu Waingereza akiwa na nduguze watu weusi.
Baadaye alikuja kuishi maeneo ya Upanga karibu na Makao Makuu ya Jeshi na Ofisi
za Takukuru. Sasa nini basi ‘Bwana Mkubwa’ yule alichofanya kusaidia harakati?
Japo si
kwa wingi unaostahili, lakini habari zake hivi karibuni zinatajwa, zinaandikwa,
zinazungumzwa na kutathiminiwa na wanaharakati mbalimbali wa historia
iliyofichwa ya ukombozi wa taifa hili na washiriki wake waliofanya makubwa na
mazito. Kitabu mashuhuri cha Mwanahistoria maarufu nchini, Sheikh Mohammed
Said, ‘’The Life and Times of Abdulwahid Sykes, The Untold Story of the Muslim
Struggle against Colonialism in Tanganyika,’’ kinachosambazwa na Ibn Hazm Media
Centre, kimemtaja Mzee John Rupia kwa mapana na marefu. Msomaji kisome ujionee
mwenyewe. Tusiandikie mate na wino upo.
Alikuwamo
katika kuasisi na kuanzisha AA, TAA, TANU ambapo alishiriki vizuri katika
baraza maarufu la wazee wa TANU wakati huo akiwa pamoja na kina Mzee
Mwinyikambi, Tambaza, Mshume, Chamwenyewe, Haidar Mwinyimvua na Rajab Diwani.
Kubwa ni kwamba walipotoka TAA na kuanzisha TANU, ‘Bwana Mkubwa’ Rupia
alitwishwa mzigo wa kuwa Makamu Mwenyekiti wake chini ya uongozi wa Julius
Nyerere, akiwa na kadi namba 7.
Tofauti
na makamu wengine wa vyama kwa sasa wenye kulipwa mishahara na pensheni;
kulipiwa nyumba na mashangingi ya kutembelea; kulipwa mamilioni ya posho za
vikao; kulipwa mamilioni wanapotembelea mikoani kwa shughuli za chama; kuwa na
wasaidizi na makatibu kibao wa kumfanyia yeye kazi zake. Rupia hakuwa hivyo
kwenye ‘chama chake’ kichanga cha TANU.
Anatajwa
kuwa ndiye aliyekuwa mfadhili namba moja kwa kukiendesha na kukikuza chama cha
TANU. Mishahara na posho akijitolea mfukoni; alimlipia sehemu kubwa Mwalimu
Nyerere katika safari yake mashuhuri ya Umoja wa Mataifa kwenda kuelezea dunia
kwamba Watanganyika walikuwa tayari kujitawala. Alimnunulia suti za kuvaa
safarini na kumpa pesa za kujikimu Mwalimu akiwa kule Marekani. (Angalia:
Gazeti la Jamhuri www. Jamhurimedia.co.tz: Alikuwa nani katika maisha ya
Mwalimu Julius Nyerere).
Mzee
John Rupia ni baba mzazi wa Balozi Paul Rupia aliyepata kuwa Balozi Marekani,
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika
uongozi wa Alhaji Mwinyi na Ben Mkapa. Balozi Rupia ni Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Benki ya Watu wa Dar es Salaam.
Watoto
wengine wa Mzee John Rupia ni Alban Rupia (sasa marehemu) na mfanyabiashara
maarufu jijini Stephen ‘Mpuya’ Rupia ambaye kwa kiasi fulani ndiye mwendeshaji
wa shughuli za kibiashara za marehemu babake. Msomaji ukitaka kumfahamu vizuri ‘Bwana
Mkubwa’ wetu huyu John Rupia, mwenye historia ya kutukuka katika taifa letu,
basi mwangalie mwanawe Stephen Rupia. Mwana Mzizima huyu amepita mlemle mwa
babake kwa upendo, bashasha, huruma, maingiliano miongoni mwa jamii na mambo
kama hayo.
Nilimjua
Mpuya kwenye miaka ya 70, sote tukiwa vijana wadogo tukifanya kazi katika Idara
ya Usalama wa Anga (sasa TCAA) kwenye
‘marehemu’ Jumuiya ya Afrika Mashariki ya zamani, yeye akiwa Radar
Engineer aliyehitimu Urusi; na mimi nikiwa Aeronautical Telecommunications
Officer. Mpaka hii leo tumeendelea kuwa masahiba wakubwa wa kufa na kuzikana.
Sasa
basi, wakati huu tukiwa tunamtazama na kumtathimini ‘Bwana Mkubwa’ huyu
aliyejitolea kwake na kwetu, ili tuwe tulivyo leo, tuangalie namna ya kuutambua
mchango wake kwa kutoa jina lake kwenye moja ya barabara kubwa za hapa kwao
DSM.
Mbona
Yusuf Makamba kapata heshima kwa kuwa Mkuu wa Mkoa tu bila kuacha haiba yeyote
ile. Mbona Pius Msekwa kapata heshima ya kupewa Msekwa Hall kwa kuwa Makamu
Mwenyekiti wa CCM na Spika wa Bunge tu? Tusiache wapite hivi hivi; tutakosa
utu!
Simu: 0715
808 864; atambaza@yahoo.com.
No comments:
Post a Comment