Mchango wa Baadhi ya Machifu Wazalendo katika
Harakati za
Kudai Uhuru wa Tanganyika
Mwami Theresa Ntare (1922 - 1999) |
''Chachu,
Hii makala sikuandika mimi mwandishi hataki jina lake litokee lakini siku hiyo ya mazungumzo tulikuwa pamoja ilikuwa November 1992.''
Tuliyohadithiwa
na Wazee wetu Paramount Chief Dantes Ngua na mkewe Mwami, Theresa Ntare
Ilikuwa mnamo
mwezi wa Novemba 1992, mida ya adhuhuri katika mizuguko ya kuwatembelea wakongwe
walioshiriki katika harakati za ukombozi wa Tanganyika kutoka ukoloni wa
Waingerza.
Safari yetu
ilitufikisha nyumbani kwa Alhaj Chief Abdallah Saidi Fundikira eneo la
Magomeni Mikumi, Dar es Salaam. Tulipata bahati kubwa kwa kuwa tulimkuta Chief
Fundikira akiwa na rafiki zake Chief Dantes Ngua na Mhe. Joseph Kasella Bantu
pamoja na watu wengine wawili, wakiwa katika mazungumzo ya kawaida. Baada ya
kuwasalimia, tulikaribishwa tukaketi.
Chief Abdallah Said Fundikira |
Mohamed Said
hakupoteza muda. Aliwachokoza na maswali yahusuyo mambo muhimu wanayoyakumbuka
sana katika enzi za harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika. Wote
walitabasamu huku kila mmoja wao akimuangalia Chief Fundikira kana kwamba
wakitaka Mzee Fundikira aanze yeye. Mzee Fundikira akasema kuwa yapo mengi ya
kuzungumzwa ila muda ule haukuwa wa kutosha kwa sababu alikuwa ameshauriwa asikae
muda mwingi pasipo kupumzika. Masharti hayo alipewa na daktari baada ya kutoka
katika mtikisiko wa homa. Na hapo tukatambua kuwa wale wazee walienda kumjulia
hali baada ya kupata taarifa ya kuumwa kwake. Hata hivyo,
Mzee Fundikira akanyanyuka huku akisema; “Mohammed, ngoja nikuletee zawadi…”
Alipanda ghorofani na kurudi na kitabu kidogo cha kurasa 55 kiitwacho, Ukombozi wa Tanganyika kilichoandikwa na Simon Ngh’waya; na kuchapwa na Chief Printer, CCM Printing Press, Dodoma, 1991. Mzee Fundikira akasema, “huyu mwandishi aliniletea mimi hiki kitabu. Nimekipitia na ninaona kitakufaa.” Mzee akaongeza kusema, “Ni vyema watu waandike watakavyoweza kuandika juu ya yale yaliyotokea wakati wa enzi za kudai uhuru.”
Sahhihi ya Chief Abdallah Said Fundikira na ya Mwandishi Simon Ngh'waya |
Baada ya hapo
yakafuatia mazungumzo machache tena, ya kuagana tu. Mzee Dantes Ngua
akatuambia, “karibuni nyumbani, siyo mbali ni hapo jirani huku akituelekeza na
kumalizia njooni, mtanikuta.” Mzee Kasella Bantu yeye alituaga akisema yeye
atakuwa tayari kwa mazungumzo siku yoyote tutakayopanga na kwamba tukipita kwa
Mzee Fundikira itakuwa rahisi kujua alipo na namna ya kuwasiliana nae.
Kasella Bantu |
Hivyo wazee wale walipoondoka nasi hatukuwa na haja ya kumchosha Mzee Fundikira ingawa hakuonyesha dalili ya kutaka tuondoke kwa haraka. Tukamuaga na kuelekea kwa Chief Dantes Ngua.
Wakati tukiwa
kwa Chief Fundikira, Mohamed Said alimfahamisha Mzee Ngua kwamba alikuwa
akiwafahamu baadhi ya vijana wake ambao baadhi yao wakati ule wakiongoza kampuni
ya kuingiza magari kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Hiyo ilituongezea ukaribu
kwa Mzee Ngua.
Mazungumzo
yetu kwa Mzee Ngua hayakuchukuwa muda kuanza. Mzee alianza kwa kutufahamisha
kuwa yeye kimila ni Paramount Chief wa Ufipa ambako makabila ya Wafipa wakati
huo yalienea kutoka maeneo ya Rukwa hadi kaskazini mwa Zambia ambako wakijulikana
pia kama Wawemba. Hivyo yeye alikuwa ni Chief Mkuu (Paramount Chief) wa machifu
wadogo, wajumbe na wazee wa koo mbalimbali, wakiongoza katika maeneo yao. Alitujulisha
pia kuwa na Mkewe Bibi Theresa Ntare alikuwa Mwami, yaani Chief Mkuu wa kabila
la Waha wote waliokuwepo maeneo ya Kigoma hadi katika maeneo ya Burundi. Makao
yake makuu kiutawala yalikua Kasulu.
Jinsi Dantes Ngua na Julius
Nyerere Walivyokutana kwa Mara ya Kwanza
Chief Dantes
Ngua alituhadithia jinsi walivyokutana na Mwlalimu Julius Nyerere kwa mara ya
kwanza.
Chief Dantes
alisema:
Wakati huo nilikuwa
Mwanafunzi Tabora School mwaka wa pili. Ilikuwa kipindi cha kupokea wanafunzi
wapya. Wakati huo pale palikuwa na utaratibu wa kuwathamini watoto wa machifu. Waliorodheshwa
na kupewa Head Prefect kiranja wao.
Pale shuleni pia wanafunzi walikuwa wakipewa vyakula vya kurutubisha afya;
karanga na maziwa. Watoto wa Machfu pia walikuwa wakipata ration (mgao) huo; ila kwao ulikuwa mkubwa kiasi. Hivyo mimi
nilikuwa Head Prefect wa wanafunzi ambao ni watoto wa Machifu.
Siku moja
wakati wanafunzi wapya wakipokewa pale shule, niliitwa ofisi ya Head Master.
Nilipofika nikawakuta wanafunzi wapya wawili. Head Master akaniambia, ‘Hawa ni
wanafunzi. Ni watoto wa Machifu.’ Kisha akanitajia majina yao. Mmoja alikuwa ni
Julius Nyerere na mwengine Wilbert Chagula.
Chief Dantes
alituambia kuwa yapo matukio mengine muhimu ya kipindi cha mapambano ya kudai
uhuru na katika muelekeo wa kupatikana uhuru. Matukio yaliyojaa visa vya
wakoloni na vituko vya Nyerere. Mama Theresa alikuwepo pale sebuleni katika
yale mazungumzu, bahati mbaya hakuwa akijisikia vizuri. Lakini alikuwa na
shauku ya kuzungumza mengi kuhusu jinsi alivyoshiriki mapambano yale ya kudai
uhuru wa Tanganyika.
Aliyotuhadithia Mwami Theresa
Ntare Jinsi Alivyoipa Nguvu TANU Buha
Mzee Dantes
alitushauri tumsikilize Mama Theresa kisha tumpe nafasi akapumzike. “Mama yenu
msimuone hivyo, ana mengi sana,” alisema Chief Ngua, na kuongeza, “Tena yeye
uhuru ulipopatikana alipewa uwaziri.” Kwa maneno hayo ya sentensi ya mwisho ya
Mzee Dantes Ngua, Mwami Theresa akaitikia; “Ah, nikikumbuka yale niliyokumbana
nayo katika mapambano ya kudai uhuru wetu na kitendo nilichofanyiwa na kuondolewa
uwaziri, ah, basi tu.”
Mwami Theresa
hakutaka kuzungumzia kilichomtoa katika uwaziri. Aliamua kutuhadithia kisa cha
mpambano wake na maafisa Wazungu wa serikali ya kikoloni kwa ajili ya
kuipa nguvu TANU ili nchi hii iwe huru:
Serikali ya
kikoloni haikutaka sisi machifu tuwe katika siasa hasa kuisaidia TANU. Hata hivyo
tukiwa wananchi na viongozi wa wanchi wanaotaabika chini ya utawala wa
kikoloni, tuliiamua kushiriki siasa kwa siri na kuipa nguvu TANU ili
tujitawale. Kuna wakati taarifa zilinifikia kwamba ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulikuwa unakuja kusikiliza
maoni ya kudai uhuru. Utaratibu wa kikoloni ni kuwa chama japo ni cha kitaifa,
kilitakiwa kipate pia usajili katika kila jimbo. Hivyo TANU ikidai kuwa
inawakilisha wananchi wote, watawala wa mikoa walikuwa wakijiandaa kukisuta kuwa
si kweli na kuonesha sehemu ambako hakikuwa na wanachama. Moja ya sehemu hizo
wakoloni waligundua ni katika himaya ya utawala wangu wa Buha. Waligundua TANU
haipo kwa Waha. Taarifa za siri zikanifika kwa wakoloni wataiambia tume hiyo ya
UNO juu ya hilo. Nikaamua kuchukua hatua kwa siri na kwa haraka.
Nilitoa pesa
zangu binafsi na kuagiza haraka kadi za TANU elfu tatu. Zikaletwa kwenye
vikapu. Nikaweka mkakati wa siri na watu wangu jinsi ya kuzigawa kadi hizo kwa
haraka kwa wananchi wa maeneo ya Buha. Majira ya saa tatu za usiku lilipigwa baragumu
la wito wa dharura watu waje kwa Mwami. Wito ulifikishwa kwa haraka kila eneo. Wananchi
wakamiminika. Eneo la makazi yangu lilikuwa na uwanja mkubwa sana. Niliwapanga
watu wangu katika lango la kuingilia wakiwa na vikapo vilivyokuwa na kadi za
TANU na karatasi zake za risiti.
Kila mtu
alipoingia alipewa kadi na risiti isiyoandikwa. Kisha akaambiwa aifikiche kadi
na hiyo risiti pasipo kuichana. Na asiongee chochote hadi afike lango la nyuma
ambalo ni la kutokea. Hapo palikuwepo watu wamejipanga katika meza. Walipofika
hapo walimpa huyo aliyekuwepo katika meza hiyo kadi na risiti kisha kumtajia
majina yake, anakoishi nk. Yule karani
aliiiandika ile kadi na risiti kwa tarehe za miezi ya nyuma, meza nyingine
ilipiga muhuri. Mwisho mwenye kadi aliambiwa kuwamba ameisha kuwa mwanachama wa
TANU wa muda mrefu. Akiulizwa atoe kadi na aitetee TANU pasipo kumtaja Mwami
wala kilichotokea usiku ule; kwake hicho ni kiapo cha utiifu kwa Mwami.
Aliruhusiwa na kusisitizwa kuitunza hiyo kadi na risiti yake.
Mwami Theresa
alitufahamisha kuwa zoezi lile lilikamilika mnamo saa tisa za usiku. Meza
zikaondolewa na wafanyakazi wakatawanyika na kwenda kulala. Mzee Ngua akasema,
“Sisi machifu tulikuwa na utiifu mkubwa toka kwa wananchi. Hata hili tatizo la
Ukimwi, kama ingelikuwa enzi zile, tungetoa tamko la muongozo wa kuacha zinaa,
Ukimwi ungeishatokomezwa.”
Mwami
akaendelea kutuhadithia:
Ilipofika
alfajiri karibu ya saa kumi na mbili za asubuhi, nikaambiwa kuna msafara wa
magari ya polisi unaelekea kwenye makazi yangu. Niliyategemea hayo, maana
vibaraka wapelelezi walikuwepo enzi hizo. Hata hivyo, kwa tukio lile walikuwa
wameshachelewa. Mimi siku ile sikuwa nimelala wala kupata usingizi. Nilikuwa
katika nguo zangu za kawaida. Nilipoletewa taarifa ile, nikaingia chumbani na
kuwaambia walinzi wangu kuwa wakifika, kwanza kuweni imara kuhusu siri ya
kilichotokea usiku.
Pili
waambieni kuwa Mwami hajamka. Ngoja tukamwamshe. Kisha mje kunigongea. Na
kwamba nitakapotoka na kufokeana nao, nyiye onesheni utiifu kwangu na
kuwakasirikia wao; wala msioneshe kuwahofu. Mkakati huo ukaeleweka.
Mwami Theresa
akatueleza kuwa wakaingia maofisa wa polisi akiwemo mmoja Mzungu na DC
(District Commissioner) Mzungu pia. Wakauliza kama Mwami yupo. Wakaambiwa
amelala, na kwamba wanaenda kumuamsha. Walinzi wa Mwami wakaenda kugonga
mlango wake. Baada ya muda akaitikia na kuuliza kwa sauti ya juu, “Kuna nini
mnanigongea usiku huu?” wakamjibu, “Kuna Bwana DC na mkubwa wa polisi.” Mwami
akajibu kwa sauti kali, “Wanataka nini wakati hakujakucha ngoja nije.”
Akatuambia
kuwa alijiandaa kwa kuvaa “night dress” akatimua nywele zake kisha
akajiviringisha shuka na blanketi akatoka akiwa ameshikilia na alipofika
sebuleni na kuwaona hakuwa salimia wala kusubiri salam zao. Alianza kwa
kuwafokea kwa lugha ya Kiingereza:
“How dare you
wake me up at this time of the hour? Can you do this to the Queen of the UK? Don’t
you know I am the the Queen of Buha? Is it because I’m an African that’s why
you are doing this to me? I will file my complaints and report you to the Governor
for this.”
Mwami
akatuhadithia kuwa wale maofisa wa kikoloni walichanganyikiwa na kuanza
kujitetea kuwa walipata taarifa kwamba alikuwa akigawa kadi za TANU usiku.
Akawajibu, “Je, mmkuja na ‘’Search Warrant?” Kisha akaongeza kwa kuwaambia,
“Nyiye askari wanaume watupu pamoja na DC mmekuja kunipekua mimi mwanamke?
Nitamlalamikia Gavana.''
Hawakuwa na ‘’Search Warrant.’’ Mwami akawageukia walinzi wake na kuwataka wawaambie wale DC na
mapolisi wake watoke mara moja au wapige baragumu kuashiria Mwami amevamiwa ili
waje wamhami. Yule DC na watu wake waliomba radhi haraka na kuondoka.
Baada ya
kutuhadithia kisa hicho Mwami Theresa Ntare alituambia bora turudi pale siku ya
Jumamosi iliyofuata kwa mazungumzo na mahojiano zaidi. “Jumamosi mtapata mengi.
Maana kuna waandishi Wamarekani watakuja kunihoji kuhusu harakati za wanawake
kuhusu kupigania uhuru wa Tanganyika.”
Bahati mbaya hatukuweza kupata fursa ya kwenda siku hiyo. Mwami akasafiri. Na hatukuonana nae tena.
Bahati mbaya hatukuweza kupata fursa ya kwenda siku hiyo. Mwami akasafiri. Na hatukuonana nae tena.
No comments:
Post a Comment