Tuesday 2 January 2018

SHEIKH PROF. JUMA MIKIDADI MTUPA NA RASHID MTAGALUKA


Prof. Juma Mikidadi


SHEIKH PROFESA JUMA MIKIDADI MTUPA: Kutoka kuchunga mbuzi hadi udaktari wa falsafa ya Sheria na sharia
NA RASHID MTAGALUKA
Kama unadhani ipo siku utashushiwa mafanikio kutoka mbinguni mithili ya vyakula vya Manna na Sal-wa ambavyo Allah aliwashushia Wana wa Israeli enzi za Nabii Musa (amani ya Allah imshukie), utakuwa umekosea!
Hilo ni somo kubwa tunalojifunza tunaposoma maisha ya Sheikh Profesa Dkt Juma Mikidadi Omar Mtupa, aliyewahi kuwa mchunga mbuzi na kuwa msomi wa kutegemewa mwenye Shahada ya Uzamivu (PhD) katika fani ya Sheria na Sharia kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh nchini Uingereza.
SHEIKH PROFESA JUMA MIKIDADI NI NANI?
Yeye ni katika wasomi wachache wa Falsafa ya Sheria na Sharia (Legal Philosophy & Islamic Law) hapa nchini na ukanda mzima wa Afrika ya Mashariki aliyezaliwa Deta, kijiji cha Mbwela, wilaya ya Rufiji (sasa Kibiti) mkoani Pwani Julai 7, 1949 akiwa ni mtoto wa nne kati ya watoto 14 wa marehemu baba yake.
Katika mahojiano naye nyumbani kwake Mkundi, Manispaa ya Morogoro hivi karibuni, Prof Mikidadi alinambia, akiwa na umri mdogo, kabla hata hajaanza shule, alilazimika kufanya kazi ya uchungaji mifugo kwa sababu watoto wawili wakubwa wa Mzee Mtupa walikuwa wanawake na mwingine, kaka yake, alikuwa masomoni.
“Nilichelewa kuanza masomo yangu ya sekula kutokana na kibarua cha uchungaji mbuzi na kondoo wa marehemu mzee, ila kaka yangu aliyekuwa akisoma Dar es Salaam aliacha akarudi nyumbani ili mimi nami nianze kusoma, akaniokoa na kazi ya uchungaji mbuzi,” alisema huku akiangua kicheko.

SAFARI YAKE YA KIMASOMO
Sheikh Prof. Mikidadi alianza masomo mwaka 1957 katika Shule ya Msingi Mbwela hadi darasa la nne alipopelekwa Shule ya Kati (Middle School) ya Manerumango, Kisarawe mkoani Pwani. Akiwa darasa la sita, alihama kutoka Shule ya Kati Manerumango, Kisarawe na kuhamia Shule ya Kati Utete ambako alimaliza darasa la nane mwaka 1964 na kufaulu mitihani yake yote.
Mwaka 1965 Sheikh Prof. Mikidadi alijiunga na Shule ya Indian Sekondari (sasa Azania) kwa ajili ya darasa la tisa. Hata hivyo, ada ya shilingi 900 kwa mwaka ilikuwa kubwa mno kwa hali ya maisha ya mzee wake ambaye hakuwa muajiriwa wa serikali. Hivyo, akiwa kidato cha pili aliomba uhamisho kwenda Shule ya Sekondari Mpwapwa, Dodoma ambako alimaliza kidato cha nne mwaka 1968 na kurudi Mbwela kuendelea na masomo ya dini.
“Elimu yangu ya dini ya awali niliipata kwa baba yangu mzazi ambaye alifungua madrasa kubwa mara baada ya kurudi Zanzibar alikokwenda kusoma kwa Sheikh Hassan bin Amir Al Shirazy miaka hiyo kabla hatujazaliwa.Hivyo wakati nikisubiri matokeo ya kidato cha nne, nikawa naendelea kusoma na kufundisha wenzangu Qur’an, Hadithi, Fiq’h na kadhalika” alisimulia Sheikh Prof Mikidadi.
Kwa bahati, Sheikh Mikidadi alichaguliwa kwenda kusomea ualimu katika Chuo cha Chang’ombe jijini Dar es Salaam ambako alijifunza mbinu nzuri za kufundisha pamoja na kufundishwa Sayansi mpya (New Science) kwa shule za msingi. “Mpango ule wa sayansi mpya ungeendelea, nchi isingekuwa na uhaba wa wataalamu wa sayansi shule za msingi hadi vyuo vikuu, sijui hata serikali waliuuaje mpango mzuri wa elimu kama ule,” alisema kwa mshangao.
Alipomaliza chuo na kuhudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, Profesa Mikidadi aliajiriwa na Wizara ya Elimu kwenda kufundisha katika Shule ya Msingi Ndundunyikanza, Rufiji mkoani Pwani, kisha alihamishwa Kihongoroni, Mbwela karibu na kwao ambako alipangwa kuwa Mwalimu Mkuu Msaidizi na baadaye kupandishwa daraja kuwa Mwalimu Mkuu.
Miongoni mwa wanafunzi wake akiwa Kihongoroni ni pamoja na Abdul Jabir Marombwa, Mbunge wa Kibiti aliyemrithi baada ya Prof Mikidadi kuachia jimbo hilo mwaka 2005.
Baada ya miaka miwili, Kihongoroni, Sheikh Prof. Mikidadi aliomba uhamisho kwenda kufundisha Dar es Salaam akilenga kujifunza zaidi elimu ya dini ya Kiislamu, jambo ambalo alifanikiwa na alipangiwa Shule ya Msingi Darajani. Kuishi Dar es Salaam ikawa ni fursa nyingine ya kusoma zaidi Misingi ya Qur’an, Fiqh, Hadithi na lugha ya Kiarabu, mmoja wa walimu wake akiwa ni Katibu Mkuu wa kwanza wa Bakwata, Marehemu Sheikh Muhammad Ali Al-Buhriy.
Aidha, Sheikh Prof Mikidadi pia alisoma kwa wanafunzi waliokuwa wakisoma Markaz ya Chang’ombe ambayo ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Azhar Sharif cha nchini Misri, na alimtaja Sheikh Jabir Katura kuwa ni miongoni mwa wanafunzi waliomsaidia sana kupata vitabu.
Kutokana na watu kufuatilia juhudi zake, mwaka 1971/72 Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) chini ya Sheikh Mkuu, Mufti Hemed Bin Jumaa Bin Hemed, lilimuomba kutoka Serikalini ili akafundishe katika Shule ya Sekondari ya Kinondoni Muslim.
“Kutokana na uchapaji kazi wangu, nilipandishwa na kuwa Makamu Mkuu wa Shule kabla sijapata ufadhili wa kwenda Saudi Arabia mnamo mwaka 1972 kusoma masomo ya dini katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Madina,” alisema.
Profesa alianza kusoma lugha ya Kiarabu kwa miezi sita, na alipofaulu vizuri alipelekwa moja kwa moja katika kitivo cha Sheria.
Kwa mujibu wa Profesa, alisoma masomo mengi yakiwemo Qur’an, Hadithi, Lugha ya Kiarabu na alimtaja msomi maarufu nchini humo ambaye alipata kuwa Mufti wa Saudia, Sheikh Abdulaziz bin Abdallah bin Baz kama mwalimu aliyechangia mafanikio yake makubwa ya kielimu.
“Ingawa alikuwa kipofu, alihifadhi Hadithi nyingi kama siyo zote alizokuwa akitufundisha pale Chuo Kikuu kiasi kwamba, sisi wazima tulikuwa tukikosea kuzisoma, yeye alikuwa akisahihisha,” alisifu.
Alipomaliza Shahada yake ya kwanza mwaka 1979 alirejea nyumbani Tanzania na kuripoti Wizara ya Elimu. Hata hivyo, Bakwata waliendelea kumng’ang’ania arudi kwao aongoze Idara ya Elimu iliyohitaji msomi kama yeye. “Nilirudi Bakwata na kupangiwa nafasi ya Katibu wa Idara ya Elimu Makao Makuu hadi mwaka 1982 nilipopata tena ufadhili kutoka kwa taasisi ya Mfalme Faisal (King Faisal Foundation) kwenda Riyadh kusoma Shahada yangu ya pili,” alisimulia.
Alipofaulu mtihani wake wa usaili mjini Riyadh aliambiwa aende Kampasi ya Madina akaanze kusoma kozi mpya ya Falsafa ya Sheria (Legal Philosophy) ambayo kwa maelezo yake haikuwa na wanafunzi wengi.
“Kwa kuwa nilichelewa kozi hii kwa miezi mitatu nyuma, nilijitahidi kujisomea hadi mwalimu wetu mmoja alipogundua mimi naelewa vizuri lugha ya Kiingereza, aliniteua kuwa mkutubi katika maktaba ya Chuo, jambo lililonisaidia kusoma zaidi kila kitabu kilichokuwemo kwenye maktaba ile,” alisema huku akicheka akifananisha hali ile na Fisi aliyepewa ulinzi wa ngozi za mbuzi!
Mwaka 1985, Sheikh Prof Mikidadi alihitimu shahada yake ya pili. Ufaulu wake mzuri ulimpelekea mmoja wa walimu wake kumshawishi akatafute Chuo nchini Uingereza kwa ajili ya PhD ya Falsafa ya Sheria.
“Ili uweze kukubalika kusoma ngazi hiyo ya elimu, ilikuwa lazima ufaulu mtihani wao wenye maswali 200 kwa dakika 30 tu, nilijitahidi na hatimaye nilifaulu na hivyo mwaka 1987 nilianza masomo yangu katika fani ya Falsafa ya Sheria ya Kimagharibi na Sharia za Kiislamu (Legal Philosophy & Islamic Law) katika Chuo Kikuu cha Edinburgh nchini Uingereza,” alibainisha.
Mwaka 1989, Prof. Mikidadi alimaliza masomo yake na kurejea nchini. Alikwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutafuta ajira lakini alikosa kwa kuwa wakati huo chuo hicho hakikuwa na Kitivo cha Falsafa ya Sheria na Sharia.
Mwaka 1991 alifanikiwa kupata kazi ya kufundisha katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya ambacho kilikuwa na kitivo hicho mpaka mwaka 1994 alipoomba likizo.

NAMNA ALIVYOINGIA KWENYE SIASA
Mwaka 1994 akiwa Chuo Kikuu cha Nairobi, aliitwa na wazee wa Kibiti ili akagombee ubunge wa jimbo hilo jipya ambalo awali lilikuwa ni sehemu ya jimbo la Rufiji.
Alisema haikuwa rahisi kuwakatalia wazee hao walioonesha imani naye. Katika kinyang’anyiro cha uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, Prof Mikidadi alishinda ubunge na aliliongoza jimbo hilo hadi mwaka 2005 alipoamua kwa hiyari yake kuachana na kazi hiyo na kurejea darasani kufundisha.
Akiwa Mbunge wa kwanza wa jimbo la Kibiti linalozungukwa na visiwa 16 Sheikh Prof Mikidadi alifanikiwa katika mambo mengi ikiwemo kuimarisha elimu, afya na miundombinu, ingawa alikiri katika baadhi ya maeneo hakukamilisha mahitaji na matarajio yake mwenyewe na wananchi wake.

KWA NINI ALIACHA UBUNGE
Nilitaka kujua sababu iliyomfanya Sheikh Prof Mikidadi aache kuwania tena ubunge wakati wanasiasa wengine ‘wanakomaa’ zaidi ya miaka 20.
“Kulikuwa na sababu tatu za msingi. Kwanza Afya yangu haikuruhusu kuendelea na kazi ya ubunge, ukizingatia ni kazi ya kuwazungukia wananchi kila mara. Pili ilikuwa tayari vijana wa kushika nafasi hiyo wapo, na mimi sikuona haja ya kung’ang’ania. Na tatu, nilipata taarifa ya kuyumba kwa Kitivo cha Falsafa kule Chuo Kikuu cha Nairobi, kwa hiyo nilikusudia nirudi kuendelea na kazi yangu niliyoisomea,” alibainisha.
Hata hivyo, wakati akijiandaa kwenda Nairobi, aliombwa na watu anaowaheshimu aache kwenda kujenga nyumba ya wenzake wakati yake inaporomoka, akimaanisha alitakiwa akafundishe kwenye Chuo Kikuu kipya cha Waislamu cha Morogoro (MUM).
Alikubaliana na fikra hiyo na kuanzia mwaka 2006 Sheikh Prof Mikidadi alianza kazi MUM kama Mhadhiri wa muda mfupi katika Idara ya Sheria na Sharia, na ilipofika mwaka 2007 aliajiriwa na kukabidhiwa Kitivo cha Sheria na Sharia kama Mkuu wake, kazi aliyoitumikia mpaka mwaka 2013 alipoomba na kupewa likizo kutokana na kutetereka kwa afya yake.

ALIVYOUPATA UPROFESA
Sheikh Prof Mikidadi alisema uprofesa katika mchakato wa elimu unaweza kuwa mzunguko mrefu sana au unaweza kuwa mfupi sana, inategemea na jitihada za muhusika katika kufanya tafiti mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Aidha, alisema mbali ya tafiti, uandishi wa vitabu na machapisho mbalimbali yanayoweza kutumika kama rejea kwenye taasisi za elimu na nyinginezo, kunaweza kukamfanya msomi afikie daraja la uprofesa.
“Kwa upande wangu imenichukua miaka zaidi ya 10 kukamilisha tafiti na uandishi wa vitabu katika fani yangu ya Falsafa ya Sheria na Sharia ambayo hapa nchini sina hakika tuko wangapi, lakini idadi yetu ni ndogo sana,” alisema.

ANAZUNGUMZIAJE MITAALA YA DINI TANZANIA
“Kwa kweli mitaala ya dini hapa kwetu haijakaa vizuri, hivyo ni vema wadau wote wa elimu ya dini ya Kiislamu wakajadiliana kwa maslahi mapana ya kizazi hiki na kijacho,” alishauri Sheikh Prof Mikidadi.
Prof Mikidadi pia alitoa wito kwa wasomi wa dini ya Kiislamu wakutane na kupeana majukumu ya kufanya utafiti katika fani yao ili kupata majibu yatakayoisaidia jamii ya Waislamu kuendelea kuwa Umma mmoja. Sheikh Prof Dkt Juma Mikidadi Omar Mtupa ameoa na ana watoto 12.



Kulia: Dr, Ramadhani Dau, Rostam Aziz, Adam Malima, Sheikh Talib,
Prof. Juma Mikidadi na Mohamed Said Eid El Fitr, Masjid Maamur
21 February 1996

No comments: