![]() |
Sheikh Ramadhani Abbas |
Sheikh Ramadhan ibn Abbass ibn
Muhammed Ahmed Said Al Shirazy Rahimahullah (Mzee Baba), alizaliwa mwaka 1913,
Magogoni, Kigamboni, Dar es Salaam. Alisoma Bagamoyo na Unguja mpaka Misri.
Alisoma kwa Sheikh Omar Ally Hassan Al Mazrui, Sheikh Gombe aliezikwa makaburi
ya Magomeni Dar es Salaam.
Akiwa Sheikh tayari mwalimu bado
alikuwa hatosheki na ilmu, akapata pia kwa swaahib zake masheikh zake, maulamaa
wenzake kama wakina Sheikh Amer Taju, Sheikh Hassan Bin Amir, Sheikh Mtumwa wa
Nyuki, Sheikh Sulayman Alawi Rahimahullah.
Alianza kusomesha 1931 New Street (Mtaa wa Lumumba).
Alikuwa akipenda watu nao wakimpenda kila rika, hakuwa tu mwalimu bali ni mlezi
pia wa wanafunzi zake , jirani zake alikuwa mkarimu, mnyenyekevu, mcheshi mtu
wa matani hajui kuchukia. Wanafunzi wake ni wengi, miongoni mwao Ni mwalimu
wangu Sheikh Uwesu bin Mzee Kibosha (Mudir Madrasatil Khairiyyah), Sheikh
Zubeir ibn Yahya Imamu Mkuu wa Msikiti wa Mtoro, Sheikh Hamid Jongo Imamu wa
Msikiti wa Manyema, Sheikh Pongwa na wengine wengi.
Rafiki yake mkubwa Sheikh Qassim bin
Juma Imam Msikiti wa Mtoro, Rahimahullah. Akiwapenda sana masharifu alikuwa
kipenzi chake mkubwa na swaahib yake Shariff Hussein Badawy pamoja na Sayyid
Ali Badawy Rahimahullah , na ndo mtu wa kwanza kwa Tanzania kupokea Maulidi ya
Habshy (Suntum Durur) kutoka kwa Sayyid Ali Badawy na mpaka ile tareikh ya
Maulid Riyadhwa, Lamu ndo ile ile tareikh ya huku kwetu Madrasatul Abbasiyyah, Alkhamisi
ya mwisho wa Mfungo Sita.
Nanukuu kutoka kwa masheikh na
masharifu zangu waliopokea hii, "Kwamba ukiyakosa maulidi ya Riyadhwa na
ukajaaliwa kuyapata haya ya Abbasiyyah, au ukikosa Abbasiyyah ukapata ya Riyadhwa
basi ni sawa (na hilo alilisema mwenyewe Sayyid Ali Badawy Rahimahullah.
Maulid Abbasiyya |
Sheikh Ramadhan ibn Abbas alifariki tarehe
31 Januari 1983 sawa na Mfungo Saba tarehe 16 saa tano usiku Hospitali ya Aga Khan.
Rabbi awarahamu wanazuoni wetu wote
waliotutangulia mbele ya Haqq.
Allahumma Aamiin.
Sheikh Abbas Ramadhani Abbas Mudir wa Madras Abbassiya |
No comments:
Post a Comment