DARASA LA PAPO KWA PAPO NA MZEE KISSINGER
Mzee Kissinger |
Nimefika kwenye walima wa harusi ya bint wa ndugu
zangu akina Tambaza aliyenipokea Sheikh Ali Sindo. Uwanja umejaa lakini badala
ya kunitafutia mahali pa kukaa ananipeleka kwa Mzee Kissinger nikamuamkie ndipo
anionyeshe mahali pa kukaa. Kissinger kaka pembeni kidogo katika kiti si
jamvini akiwa pamoja Mwinyikhamis na Muharram Kobe. Baada ya kutoa salaam tu Mzee
Kissinger ananiambia, ‘’Mohamed kuna mambo katika mkasa wa Sharif Mwinyibaba
hukuandika katika kitabu cha marehemu Abdul…’’
Kulia Mwinyikhamisi, Mzee Kissinger na Muharram Kobe |
Hapo hapo nikapiga Bismillah na kushukuru,
Alhamdulillah… kimoyomoyo. Nilitambua kuwa nimekuja na mguu mzuri kwanza
nitakula biriani na vilevile nitasomeshwa.
Baada ya kumaliza kula karamu haraka nimemkimbila Mzee
Kissinger nipige goti kalamu na karatasi mkononi nisomeshwe. Lakini siku hizi
kalamu na karatasi hazina kazi tena. Simu zetu za mkononi zinamaliza kila kitu.
Zinachukua picha na sauti kwa wakati mmoja.
Mzee Kissinger baada ya miaka 16 kupita toka ilipotoka
tafasiri ya Kiswahili cha kitabu cha Abdul Sykes ndiyo kwanza kakisoma sasa na
ananieleza kuwa amekuwa akikisoma usiku hadi amekimaliza. Lakini kuna kipande
katika historia ya Sharif Badawy na kaka yake Sharif Hussein sikueleza chote
kwa ukamilifu wake.
Shariff Hussein Badawy |
Inawezekana kuwa Shariff Hussein Badawy na nduguye
Mwinyibaba wakawa ndiyo Waafrika wa kwanza Tanganyika kupigwa PI yaani
Prohibited Immigrants – Wahamiaji Wasiotakiwa.
Nini kisa cha ndugu hawa wawili kufukuzwa Tanganyika
mwaka wa 1963, miaka miwili tu baada ya Tanganyika kupata uhuru wake?
Katika Maulid ya Mfungo Sita mwaka wa 1963 Mwinyibaba
alipanda jukwaani kujibu hotuba ya sheikh mmoja maarufu na kiongozi wa juu
katika TANU ambae katika hotuba yake vijana waliona kama vile alijikomba sana
kwa serikali.
Majibu kutoka kwa kijana mdogo Mwinyibaba yalikuwa
makali sana kama ilivyo ada ya vijana. Damu zao zinachemka na hawachagui maneno
lile linalokuja ndipo hilo litatoka kinywani.
Mzee Kissinger alikuwapo katika maulid yale pale Mnazi
Mmoja usiku ule na yeye pia kama alivyokuwa Mwinyimababa, pia alikuwa kijana.
Katikati ya
khutba ya Mwinyibaba iliyokuwa inaunguruma katika vipasa sauti vilivyoenea pale
uwanjani ilisikika sauti ikitokea sehemu ya nyuma karibu ya Hospitali ya Mnazi
Mmoja ikipiga ukelele, ‘’Unachanganya dini na siasa.’’
Shariff Mwinyibaba akiwa Maulidini Lamu 2007 |
Sauti hii ilikuwa sauti maarufu hakuna katika mji wa
Dar es Salaam mtu ambae alikuwa haijui sauti hii.
Wakwanza kushoto mbele ni Iddi Tosiri, watatu ni Julius Nyerere akifuatiwa na Kaluta Amri Abeid,
Mstari wa mwisho wapili kulia ni Rashid Sisso. Picha hii ilipigwa miaka ya mwishoni 1950 New Street
mbele ya ofisi ya TAPA (Tanganyika African Parents Association)
Hii ilikuwa sauti ya Rashid Sisso. Mpigania uhuru,
mmoja wa vijana wa mwanzo kuingia TANU na kufanya kazi kubwa ya kuhamasisha wananchi
kujiunga na TANU na kubwa zaidi Rashid Sisso alikuwa rafiki wa Mwalimu Nyerere.
Katika watu waliokwenda uwanja wa ndege kumsindiza
Mwalimu Nyerere katika safari yake ya kwanza UNO, Rashid Sisso alikuwa mmojawapo
pamoja na Idd Faiz Mafungo, Bi. Tatu bint Mzee, Bi. Titi Mohamed, John Rupia,
Zuberi Mtemvu, Robert Makange, kuwataja wachache.
Kulia wa kwanza Bi. Tattu bint Mzee wa nne Julius Nyerere na wa tano Bi. Titi Mohamed safari ya kwanza ya Nyerere UNO 1955 |
Katika mikutano ya TANU Rashid Sisso akisimama nyuma
ya Mwalimu Nyerere wakati akihutubia. Mwalimu Nyerere akampachika jina akawa
anamwita, ‘’Afisa.’’ Hakuna ajuaye kwa nini alimpa jina hilo.
Sauti ya Rashid Sisso ili ilikuwa sauti ya onyo kali
na Rashid Sisso hakuwa mtu wa kupuuzwa. Mwinyibaba alipuuza zauti ile na
aliendelea na khutba yake kali hadi alipomaliza.
Kuchanganya dini na siasa ulikuwa mwiko mkubwa katika TANU na mwaka wa 1958 Sheikh Suleiman Takadir Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU alifukuzwa chama kwa kosa hilo na alitengwa na jamii.
Kuchanganya dini na siasa ulikuwa mwiko mkubwa katika TANU na mwaka wa 1958 Sheikh Suleiman Takadir Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU alifukuzwa chama kwa kosa hilo na alitengwa na jamii.
Watu walijua kuwa Mwinyibaba tayari alikuwa matatani. Baada
ya Maulid kumalizika walimwendea wakamwambia asisubiri hadi asubuhi akimbie aende
kwao usiku ule ule kwani asubuhi taarifa itafika katika vyombo vya usalama na
hakuna shaka yoyote askari watamfuata kumkamata.
Mwinyibaba hakupuuza ushauri ule.
Usiku ule ule majira ya saa sita usiku Mwinyibaba
akapanda lori la mizigo lililokuwa linakwenda Tanga na hata kabla jua
halijapanda siku ya pili Mwinyibaba alikuwa keshavuka mpaka wa Horohoro
anaelekea kwao Mombasa.
Asubuhi siku ya pili mapema Mzee Kissinger anapita
Msikiti wa Badawy Kisutu anaelekea kazini kwake African Printers, anawaona
maofisa wa Uhamiaji Wazungu wawili wanaingia na viatu ndani ya msikiti wa
Badawy kuwatafuta Sharif Hussein na nduguye Mwinyibaba kuwapa notisi za PI kuwa
wanafukuzwa Tanganyika hawatakiwi kuwapo nchini.
Mzee Kissinger akasimama pembeni na watu wengine
wakistaajabu kuwaona maofisa Wazungu wakiwa katika sare zao za kazi wakiingia
msikitini bila ya kuvua viatu.
Notisi ile aliipokea Sharif Hussein peke yake.
Ilikuwa siku ya Ijumaa na alikwenda Msikiti wa Kitumbini
kusali sala ya Ijumaa na baada ya sala alisimama na kuwaaga Waislam.
Hali ilikuwa ya simanzi sana kwani Sharif Hussein
alikuwa na madras maarufu hapo msikitini akisomesha vijana na watoto na sifa
kubwa ya madras ile ilikuwa usomaji wa tajwid, nyuradi na kasda za kupendeza
katika maulid.
Kundi kubwa la Waislam lilimsikindikiza hadi kutoka
Msikiti wa Kitumbini Masjid Badawy na baada ya hapo Sharif Hussein akaondoka
kurudi kwao Kenya.
Kulia Mwandishi, Shariff Mwinyibaba na Sheikh Abubakar Badawy, Lamu 2007 |
Haya ndiyo aliyonieleza mwalimu wangu Mzee Kissinger
ambayo alinambia yalistahili niyaeleze katika kitabu cha Abdul Sykes.
Kushoto Mwandishi, Shariff Hussein Badawy, Abdallah Othman, Abdallah Tambaza na Abdallah Kageta, Dar es Salaam |
No comments:
Post a Comment