Tanga ya
zamani zile, ya jagina Shaabani
Aliyesifika
kule, na kote Uswahilini
Mbona kama
izamile, haipo kwenye ramani
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga yake
Jinamizi, Sheikih Ali Zakuwani
Ilo ikikaza
uzi, kwa mambo yenye thamani
Imegota zake
mbizi, nani wa kuiauni?
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga ya
Mwalimu Pera, Pera bin Ridhiwani
Zama zake
iling'ara, na kushika usukani
Doro leo
yadorora, haitajwi midomoni
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga ya
Sheikh Mdanzi, wa Hanasa muhisani
Iloenea
mapenzi, na baraka tani tani
Ya sasa ni
kama bunzi, makaziye jalalani
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga ya
Mwinyihatibu, Mohamedi nambawani
Aloandika
vitabu, vizuri vyenye maani
Mbali
imejitanibu, haipo hatuioni
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga ya
Sheikh Ghulamu, Mwabondo mtu makini
Aloifunza
kaumu, ushairi pamwe dini
Umekwisha
umuhimu, Tanga sasa Tanga duni
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga ya
Sheikh Hemedi, Buhry wa Mnyanjani
Ilolea
auladi, kwa kumcha Rahmani
Imeenda
hairudi, imakeni hii shani
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga ya
Sheikh Salimu, Kibao niambieni
Iko wapi
waadhamu, nikaishufu kwa mboni
Nikajifunze
nudhumu, nikiwamo Tanga ndani
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga ya
Sheikh Saidi, Nuru aso mshindani
Ilopendwa ja
waridi, au vile asumini
Hae! Imezama
sudi, bahati si mara thani
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga yake
Sheikh Ali, Hemedi mwanachuoni
Iliyotajika
mbali, Ulaya na Arabuni
Leo imelala
chali, waruka watu na nyuni
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga yake
Mohamedi, Ali Buhry mwendani
Aliyekuwa
stadi, na fasaha wa uneni
Ilo sasa si
ya jadi, ya jadi i wapi kwani?
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga ya
Sheikh Kigamba, gwiji la Chongoleani
Iliyotoa
miamba, waloongoza safuni
Kwa umbuji
walitamba, kilugha hata kifani
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga ya
Sheikh Kihere, Kihere wa Vibambani
Ilotamba si
kwa sare, ingiapo shindanoni
Hadi wakaona
gere, kina fulani fulani
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga yake
Abdalla, wa Baruwa Baruwani
Iliyokosa
kulala, kwa kukirimu wageni
Watu
wakanywa na kula, kindugu na kijirani
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga ya
Mwalimu Mbega, yeye kwake ujombani
Wa kuiga
wakaiga, kwa mazuri kusheheni
Tangu yahame
mafiga, hakuna chungu jikoni
Iko wapi
Tanga ile?
Tanga ya bin
Matunga, Abdi alo rubani
Ilojaliwa
malenga, mwambao huu wa Pwani
I wapi nende
ienga, nikumbukie zamani
Iko wapi Tanga
ile?
I wapi ile i
wapi, Tanga ile nijuzeni
Imebadilika
vipi, toka juu kuwa chini
Na warithiwe
wa kupi, walipo nionesheni
Iko wapi
Tanga ile?
Hassan R Hassan
Hassan R Hassan
No comments:
Post a Comment