Wednesday, 14 February 2018

DEDAN KIMATHI KATIKA HISTORIA YA TANU NA UHURU WA TANGANYIKA

Dedan Kimathi
''Minong’ono ilikuwa ikisikika kutoka kanda ya ziwa kuwa kiongozi wa wapiganaji wa Mau Mau, Dedan Kimathi alikuwa anaonekana mjini Mwanza. Wakati ule pale Mwanza kulikuwa na Wakikuyu wengi wakifanya biashara sokoni. Ilivumishwa kuwa Dedan Kimathi alikuwa akiwasiliana na Wakikuyu wenzake na wao walikuwa wakimkusanyia fremu za baiskeli za zamani ili zitumike kutengenezea magobole ili zitumiwe misituni dhidi ya majeshi ya Waingereza. 

Mapigano yalipoonza kati ya Mau Mau na Waingereza kulikuwa na Wakikuyu kama elfu kumi na sita wakiishi na kufanya kazi kaskazini ya Tanganyika. Kama tahadhari, Wakikuyu wachache walioonekana kuunga mkono Mau Mau, walikamatwa na kupelekwa Kenya ambako waliwekwa kizuizini katika kambi mbali mbali. Wakati Budohi na Wakenya wengine walipopita Korogwe wakati wakirudishwa Kenya kupitia Taveta, Ally Sykes, ambaye alikuwa amehamishiwa Korogwe, alikwenda hadi stesheni ya reli kuwaaga. Watuhumiwa hawa wa Mau Mau walikuwa wametiwa katika mabehewa ya kubebea ng'ombe huku wamefungwa minyororo. Dome Budohi na wazalendo wengine waliwekwa kizuizini kwa miaka saba. 

Dome Okochi Budohi TANU kadi no. 6

Kulikuwepo na wazalendo kutoka nchi jirani ya Kenya kama vile Dome Okochi Budohi na Patrick Aoko ambao walikuwa wanajua vyema siasa za walowezi za kupora ardhi za  wananchi. Kutoka kwa wazalendo kama hawa, Abdulwahid alipata usikivu wa mawazo yake ya kuigeuza TAA kuwa chama cha siasa chenye nguvu. Lakini mara tu baada ya kuundwa kwa TANU wazalendo hawa wa Kenya wakakamatwa na serikali. Kwa miezi sita walihojiwa na kuwekwa rumande Central Police Station huku wamefungwa minyororo. Budohi na Aoko walikuwa wakifuatwa na makachero (Special Branch) toka mwaka wa 1952 baada ya hali ya hatari kutangazwa Kenya. Inasemekana Dome Budohi aliponzwa na barua iliyotoka Kenya ambayo ilikamatwa na makachero. Barua hii ilikuwa inamuhusisha Budohi na Mau Mau. Inasemekana Budohi alisalitiwa na Mkenya mwenzake aliyeitwa Martin ambaye alikuwa pamoja naye katika Blackbirds. Martin alikuwa akipuliza tarumbeta.

Askari waliokuwa wakiwalinda kule rumande walitoa habari kwa TANU kuwa kulikuwa na mpango wa kuwapa sumu wafungwa wale, Budohi na mwenzake Aoko. Baadaye wafungwa hawa walihamishiwa Handeni ambako kulikuwa na kambi ya kuwafunga watuhumiwa wa Mau Mau. Kawawa alikuwa amehamishiwa hapo kutoka Dar es Salaam. Baadhi ya wafungwa walikuwa wananachama wa TAA na baada ya kuundwa TANU wakawa wanachama wa TANU. Kawawa alikuwa akifahamiana na wengi kati ya wafungwa wale. Budohi na Aoko waliwahi kuwa  viongozi wa TAA. Kawawa aliwaangalia wafungwa hawa kwa moyo wa huruma akijaribu kupunguza shida zao pale kambini kila alipopata mwanya wa kufanya hivyo.''


***


''Mara tu baada ya kuundwa kwa chama cha TANU Wakenya walikamatwa na kurudishwa Kenya ambako waliwekwa kizuizini Manyani na katika kisiwa cha Lamu. Wazalendo wa Kenya waliokuwa katika harakati nchini Tanganyika hawakuwa na uhusiano na TANU baada ya uhuru na wala chama hakikufanya juhudi kuwasiliana nao. Dome Budohi alijaribu mara nyingi kuomba kukutana na Nyerere alipozuru Nairobi lakini ilishindikana. Budohi hafahamu kama maafisa wa serikali ya Tanzania walimzuia wao tu au walifanya hivyo kwa amri ya Nyerere. Hadi anafariki Dome Budohi hakuwahi kuonana na Nyerere ambae wakati wa enzi za TAA na TANU walikuwa wakifahamiana vizuri.''
(Kutoka kitabu cha Abdul Sykes)


No comments: