Masheikhe wetu: Sayyid Omar Abdalla (Mwinyi
Baraka)
Sehemu ya (3)
Makala
haya nitamalizia juu ya kusoma kwake, kufanya kazi kwake na misukosuko ya hapa
na yapale aliokumbana nayo. Tunaona katika nyakati mbalimbali wasomi wa
Kiislamu hupata misukosuko ya kila aina hasa kwa kufanyiwa fitna na wengi wao
humalizikia kuwekwa korokoroni na kuonekana kama ndio shahada ya kuwa
mlinganiaji wa dini ya Kiislamu. Wengi wao huwekwa korokoroni na Waislamu
wenzao. Kuna maandiko yanaonyesha kuwa Sayyid Omar Abdalla kafungwa mara mbili
kwa misimamo yake, lakini unapopitia kumbukumbu mbalimbali na kufanya mahojiano
na mtu ambaye alibahatika kuwa naye Zanzibar, Uiengereza na kufungwa pamoja
naye anathibitisha kuwa kafungwa mara mmoja tu.
Katika makala iliopita nilijaribu
kuonyesha kusoma kwake na tumeona kuwa Sayyid Omar Abdalla kwanza alikwenda
kusoma Chuo cha SOAS na kupata shahada ya Diploma ambayo ndio aliokuja nayo na
kuwa sasa kishakuwa msomi anayotakiwa kuwa anaongoza Chuo cha Kiislamu “Muslim
Academy” ingawa mwenyewe alikuwa akiona kuwepo na pengo na kuwa hajaaelimika
atakavyo.
Bada ya kurudi masomoni na kuwa
anashirikiana na watawala katika kuweza kukiendeleza Chuo cha Muslim Academy,
Sayyid Omar alihudhuria mikutano mingi na hata ikajiri afike Nigeria kwenda
kuweza kuangalia namna wao wanavyoendesha masomo ya Kiislamu katika nchi ambayo
Kiengereza kinatawala na kipo juu.
Unapopitia nyaraka mbalimbali saa
nyengine unahangaishwa kufahamu mtawala Muiengereza katika utawala wake namna
ambavyo alivokuwa anaziangalia dini kuu mbili na kuhakikisha kuwa hazipishani
na wakati huo huo anakuja na upendeleo kwa upande mmoja halafu upendeleo huo
unakuja unafichwa na kuonyeshwa juhudi za kuwaweka waumini wa dini kuu mbili
Afrika ukiwa Uislamu na Ukiristo kuwa upo sawa.
Muiengereza alikuwa amejaribu katika
nchi ya India, Sudan na Nigeria kuweka mtaala wa elimu ya dini ya Kiislamu
ambao unafahamika na utaweza kutumika unavyostahiki, aidha alifanya katika nchi
hizo kuwa na Makadhi pamoja na Mahakama zake ambazo Waislamu hawatakuwa na
shida na ili kuweza kuyatolea ithibati hayo, utayaona katika kumbukumbu za
kuanzishwa kwa Muslim School mkolini alijaribu kukaa na viongozi mbalimbali wa
dini na wasomi wa kuiweka Ofisi ya Kadhi na Mahkama yake, na akahakikisha kuwa
wale wasomi wanaofahamika na wenye ujuzi ndio wakupewa nafasi ya kuongoza
kuanzia Kadhi na watendaji wake.
India na Sudan walifanya vizuri sana
katika kujipanga kwa mitala ya dini ya Kiislamu, utaona hadi leo Sudan wana taratibu nzuri ya
kuwanisha baina ya uongozi wa dunia na akhera.
Sayyid Omar bin Abdalla alipata fursa
yakwenda Nigeria na alivutiwa kuona mpangilio wa mitala ya Madrasa namna
ilivyopangiliwa namna walimu walivyofunzwa namna ya kumsomesha mtoto kujua
kusoma Qur’an na Sheria na hapo hapo kufunzwa msingi wa mwanzo wa lugha ya
kiarabu, kujua vitu mbalimbali vinaitwaje kwa Kiarabu hasa vile
vilivyomzunguka, haya yalimvutia sana Sayyid Omar Abdalla na safari yake hio ya
Nigeria ilikuwa akipenda kuielezea katika mihadhara yake na kuanza kuandaa
mipango ya utekelezaji kwa Zanzibar na Afrika ya Mashariki kwa jumla.
Sayyid Omar aliporudi Ulaya akawa
anasoemsha dini katika Skuli ya Teacher Training na akaja kuwa mwalimu Mkuu wa
Skuli ya Muslim Academy kwa hakika alikuwa anaposemesha dini mara zote akipenda
kuingiza na taaluma yake alioipata Chuo cha Makerere College ikiwa elimu ya
viumbe (Biology).
Ilipofika mwanzo wa miaka ya 60 Sayyid
Omar Abdalla alifanikiwa kupata Scholarship nyengine kwenda Uiengereza. Wakati
huo akiwa Muiengereza akijua makoloni yanamtoka lakini alianza kujisafisha na
kuweka nidhamu ambayo kila mwaka akijaribu kuhakikisha wanafunzi wangapi
wanakwenda nje kusoma masomo ya juu na Zanzibar kwa wakati wake ikiwa na idadi
ya watu 300,000 ukichukua na asilimia na uwastani wake ilikuwa na wanafunzi
wasiopungua 400 wakiwa wapo nchi za kigeni wanasoma, wengi wao walikuwepo Misri
kwa program ya Gamal Abdulnasir na wengine wakiwepo Uiengereza, Iraq, Marekani,
India na kwengineko.
Sayyid Omar Abdalla alijiunga na Chuo
Kikuu cha Oriel College, Oxford na safari hii akafanya shahada ya Masters
ambayo somo lake lilikuwa juu ya Falsafa na hapa ndipo mkanganyiko nitajaribu
kuweka sawa na haya ninayosema nasema kwa kupitia Faili lake na mazungumzo
nna murid wake Sheikh Ahmed ambaye kawa
naye hapa Zanzibar kama katika wanaohudhuria mihadahara yake na kuwa naye
kwenye rubaa za kheri na wakawa pamoja Uiengereza na wakafungwa jela pamoja.
Katika Chuo cha Oxford Sayyid Omar
Abdalla alisoma somo la Falsafa (Philosophy) alipokuwa anajifunza somo hili
alionyesha maajabu mengi namna alivyokuwa akiweza kuona wana Falsafa
watangulizi wa Kiyunani kina Aristotle na wengineo walivyokuja kuwa athiri
wasomi wa Kiislamu kama Ibn Sinna (Avicenna) na kuweza kuwafahamu wana falsafa
wa Kiislamu ambao wengine hata roho walikua wakielezea katika kitu chengine
ambacho kitabaki na kuondoka na kurejea kwa njia nyengine.
Sayyid Omar alivutiwa na Mwanafalsafa
Ibn Bajja na Imam Ghazali na unaposoma Risala yake ya mwisho Chuwomi Oxford
(Thesis) alioipa jina “Some Felicity in Medieval, Islamic Philosophy” ndio
utapofahamu kwanini alishikana na Ibn Bajja akawa tafauti na Ibn Rushd, hawa
kina Ibn Rushd na Ibn Sinna waliuweka pembeni Uungu na wakenda katika nadharia
ambayo mwanadamu ameiasisi.
Sayyid Omar alivutiwa zaidi na Imam
Ghazali ambaye akiweza yeye kumfahamu zaidi, Imam Ghazali alianza kuzama na
nadharia za kina Aristotle, kisha akazama kuona Uungu na umoja yaani sii umoja
huu lakini upweke wa Allah kuwa hakuna mwengine wa kuabudiwa ila ni yeye tu
katika mamlaka yake na uongozi wake.
Leo katika elimu ya Ikolojia (Ecology)
kunazungumzwa juu ya mwindaji na
mwindwaji na haya Imam Ghazali katika kitabu chake cha Ihya Ulumu
Deen anagusia na utafahamu utapomsikia Sayyid Omar Abdalla alivomfahamu
Imam Ghazali, naye kuwa na uelewa wa somo la ilimu ya viumbe.
Imam Ghazali akifahamisha namna ya
ndege Allah alivyomjaalia kuwa kila saa awe anakula kisha anakitoa chakula kama
kinyesi, anakula tena na kurudia kula, Imam Ghazali anaeleza kuwa kuumbwa kwa
ndege kuwa na umbo dogo w ni kwasababu awe yupo natunaendelea kuwaona kwa
dahar, lakini kuweza kubakia kwake ndege kuepukana na maadui awe kila akila
akikaa awe hashibi bada ya muda mdogo anataka kula tena na hio inamfanya kuwa
kwa udogo wake angekuwa anakula na kushiba basi maadui wake kina nyoka na
wengine wangewamaliza kirahisi, hapa ndipo kunakazi kufahamu na inataka
malinganisho ya ilimu ya dunia na akhera.
Katika somo la Ikolojia haya
maingiliaano wanayaita “Predator prey relation) na Sayyid Omar Abdalla
nilimsikia anamuelezea Imam Ghazali kwa wigo wa Ikolojia na namna wanyama
wanavyopotea kutoonekana tena (Extinct) ni namna Allah alivyopanga vipi viumbe
viweze kupambana na wengine na kujihami na kuendelea kukuwepo, Falsafa ya Imam
Ghazali ilimvaa vya kutosha na Sayyid Omar Abdalla alifika hadi hawezi kutoa
mhadhara bada ya kutoa aya chache na kuja na hadithi za Mtume Muhammad (SAW)
asimgusie Imam Ghazali. Bahati
nzuri hii risala yake ya Oxford imechapishwa na vyema ukaipata ukaisoma.
Sayyid Omar Abdalla alirejea Zanzibar
mwaka wa 1963 bada ya kumaliza masomo yake hapo Oxford na alifika kuwa na kasi
kubwa ya kutoa mihadhara na akipata nafasi iwe kwenye hitima, majlisi, radio au
popote pale akichukua nafasi hio kuweza kutoa mawaidha mazito ambayo ni zaidi
yalikuwa ulinganisho wa dini ya Kiislamu na Kikiristo.
Yalipotokea Mapinduzi ya 1964 alikuwa
ni mwalimu bado hakuyapa kisogo aliendelea kufanya kazi na kwenda sambamba na
mabadiliko yaliotokea, ithibati ya hio ni hio picha ya ujenzi wa uwanja wa
Amani, akiwa yumo katika ujenzi wa taifa na huku ana shoka anachanja mnazi.
Sayyid Omar Abdalla na Maalim
Zubeir Rijal katika ujenzi wa taifa
Matokeo machache juu ya Sheikhe huyu:
Sayyid Omar Abdalla ilikuwa kila siku ya Ijumaa akipenda kuwa na rubaa na
wenzake ya kumuomba Mungu katika zile taratibu ambazo Mola anasema “Niombeni
nikujibuni” yeye na wenzake waliweka
taratibu ya kuleta maombi au tuite Nyiradi siku za Alkhamisi na Ijumaa, katika
mwaka wa 1968 alikamatwa na wenzake kama 25 kwa kuambiwa wanapanga njama ya
kupindua Serikali, akawekwa korokoroni kwa mwezi mmoja badaye ilikuja kuelekweka kuwa ilikuwa ni fitna tu, tena
hapo Mzee Abeid Amani Karume akaamua kuwachia, afya yake iliathirika sana kwani
akisumbuliwa na kisukari na akawa hapati dawa ya kupiga shindano ya Insulin.
Sayyid Omar bada ya kutolewa jela alikuwa akiishi na khofu akaona asije
akafungwa tena akaamua kuhama Zanzibar huku
tayari kapatiwa nafasi ya kurudi Uiengereza lakini aliona vyema kwenda
kusihi katika visiwa vya Comoro ambavyo ana nasaba navyo.
Safari mmoja akiwa anasafiri kutokea
Kenya anaelekea Ulaya, amesimama kwenye foleni, binti wa Kikenya alio katika
kupima mizizigo na kutoa namba ya viti kwenye ndege kumuona mzee na majuba na
kashika bakora akamshika kumwambia “eeh muzee nenda kwenye foleni ile ya kwenu
Mombasa, ndege itakukimbia.” Sayyid Omar alikaa kimya lakini jeuri ya kitoto
ikazidi kwa kumtaka mmoja ya wafanyakazi kumtoa kwenye Foleni, Sayyid Omar
akatoa Pasi ya kusafiria ikiwa na hadhi ya kidiplomasia na mrundo wa tiketi,
mpaka akaiona tiketi yake anayokwenda Ulaya, aliyotumwa akamjibu yupo pahali
sawa, binti akasema haiwezi kuwa, akawa anajipanga sasa kwenda kumtoanyeye
mwenyewe kilichomudhi hakifahamiki, lakawa anamuhudumia msafiri wa Kifaransa
ambaye hajui Kiengereza, ikawa vuta ni kuvute na wakati unakwenda Sayyid Omar
akamsogelea yule bibi wa Kifaransa na kumuamikia kwa Kifaransa na kutaka kujua
nini shida yake, akawa Sayyid Omar sasa anatafsiri kutoka Kifaransa anapeleka
kwa Kiengereza kwa mratibu wa Tiketi, binti wa Kikenya hakuamini,
alivyoyasuluhisha binti akataka kujua wapi aliposoma kujua Kiengereza na
Kifaransa, Sayyid Omar Abdalla akamwambia “You better asked Kibaki, he knows me
better, we were together at Makerere College” Binti wa Kikenya alitahayari bali aliogopa asije kushtakiwan
kwa wakubwa wake na Sayyid Omar alipomuona anatetemeka huku hana raha akamwabia
“Jitahidi kuwaona watu wote ni sawa.”
Alifika Chuo Kikuu cha DaresSalaam
akatoa uwaidh juu ya umuhimu wa kujiendeleza kiroho kwa kuwa na dini, wakati wa
masuala kijana akaona aaah, huyu mzee ndio watu wa kizamani Wakoloni
waliwafundisha lugha ndio katuhutubia kwa Kiengereza, akamvaa akamwambia unajua
nini Karl Marx kasema? “Religion is the opium of the mass” kwa maana ya kuwa
“Dini ni kasumba kwa umma.” Sayyid Omar Abdalla kwa mshangao wa wengi aliusoma
ukurasa mzima wa Das Capital juu ya maneno hayo na kusema ukurasa gani
upo wenye manerno hayo ambayo aliyasoma
kwa ghibu, na akamtaka kijana huyo amsome Maurice Bucaile katika kitabu
“What is the Origin of man na The Qur’an, The Science and the Bible.” Kijana
badala ya kutaka kumshushua Sheikhe alijikuta kajishusha hadhi na kujuta
aliyotaka kuyafanya.
Sayyid Omar Abdalla akipenda kuurejea
na kurejea msemo wa mwana sayansi wa Fizikia maarufu kwa jina la Albert
Einstein usemayo “Science without religion is lame, religion without science
is blind.” Somo la
sayansi pasi kujuwa dini ni sawa na kilema na sayansi pasi kujuwa dini ni
mithili ya kipofu.” Sheikhe huyu alikuwa na elimu zote mbili hizo na akiweza
kufahamisha na kutowa ujumbe kwa watu wa rika zote wakiwa wasomi na wale
wasiokuwa wasomi.
Yapo mengi ambayo ningeweza kumzungumza
Sheikhe huyu, nategemea haya machache yanatosha, fatwana na mie wiki ijayo
umjua Sheikh Abubakar Bakathir. Tumuombe Allah nasi tufwate nyayo za Sayyid
Omar Abdalla (Mwinyi Baraka), Ameen.
No comments:
Post a Comment