SHAJARA YA MWANA MZIZIMA:
MZEE HAIDAR MWINYIMVUA
(1905 - 1987)
ALIUZA NYUMBA KUIKOMBOA TANGANYIKA
Alhaji Abdallah Tambaza
Raia Mwema Februari 26 - 27, 2018 |
AWALI ya yote napenda kuwashukuru
wale wote ambao wametokea kuipenda safu hii ya Shajara ya Mwana Mzizima,
hususan wale ambao wamekuwa wakinipigia simu za pongezi mara kwa mara au kutuma
ujumbe wa sms.
Jumatatu ya leo, Shajara inamwangazia
mmoja wa wanaharakati za kupigania Uhuru aliyekuwa mstari wa mbele kabisa,
lakini jina lake limesahaulika kabisa baada ya nchi na watu wake kukombolewa
kwenye mikono michafu ya ukoloni wa Kiingereza. Jina lake ni Sheikh Haidar
Mwinyimvua.
Ni bahati mbaya sana, watu wetu wa
leo hawayafahamu vizuri madhila na mateso ya utawala wa Kiingereza, wakidhani
kwamba walikuwa wema na wazuri kama vile zilivyo nzuri timu zao za mpira za
Liverpool, Manchester, Arsenal na Chelsea ambazo watu huzishabikia
kiwendawazimu kabisa, huku wakisema; sisi Arsenal, sisi Manchester, sisi
Liverpool.
Walitugawa vipande vipande hapa ili
iwe rahisi kwao kututesa watakavyo. Ingawa wenyeji hapa kwetu Mzizima hatukuwa
na ubaguzi kwa ndugu zetu waliotoka mikoani, Wangereza walileta mpango wa kila
kabila kuwa na kiongozi wao atakayekuwa akipokea amri kutoka bomani na kuzifikisha kwa wengine.
Wamanyema walikuwa na mkuu wao;
Wanyamwezi walikuwa na mkuu wao; Waluguru walikuwa na mkuu wao; Wangindo
walikuwa na mkuu wao; Wamwera walikuwa na mkuu wao na hata wenyeji Wazaramo na
Wamashomvi nao walikuwa na wakuu wao pia. Hapo nyuma, Watanganyika, pamoja na
makabila yetu haya kuwa nayo, lakini tulikuwa wamoja tukicheka na kutaniana
kwenye utani wa asili wa kikabila, pamoja na ule wa Sunderland na Yanga.
Wakristo na Waislamu tuliishi tu
kidugu bila tabu tukila na kuzungumza pamoja na kila mtu akifuata dini yake; na
inapotokea Mkristo anataka kuchinja kuku, basi humwendea jirani yake Mwislamu
amchinjie ili isije kuwa taabu kwa watoto kula pamoja. Kwenye misiba, harusi na
sherehe mbalimbali tulijumuika pamoja kama jamii moja tu.
Mtawala Mwingireza, ambaye ni mkuu wa
Kanisa lake la Kianglikana duniani, alisema hapana; akaagiza maeneo ya Misheni
Kota ndiyo wakae Wakristo huko. Wakristo wengi wa Kianglikana hapa jijini
waliishi huko na barabara zikapewa majina ya wanakotoka kama Ndanda, Magila,
Muheza na Masasi.
Misikiti ya Waislamu nayo pia
ikatengwa kwa misingi ya kikabila. Upo Msikiti wa Manyema, Warufiji, Wayao,
Wazaramo, Wamakonde, Wangazija, Ibadhi n.k. Tokea zamani watu hawakupenda hali
hii ya kubaguana kwenye ibada, hivyo walikuwa wakienda kusali popote pale wakati
na muda wa sala unapomkuta. Ilikuwa haishangazi kumwona Imam Mmakonde, akienda
Msikiti wa Manyema, akawatania na kuingia kwenye mihrabu kuswalisha. Hakuna
sala ya Kimakonde peke yao wala Kimanyema peke yao, lakini ndio ujinga wa
kutawaliwa huo jambo likaenda hivyo.
Pale karibu na soko la Kariakoo kuna
Msikiti wa Mtoro. Mtoro ni jina la muasisi wa msikiti huo huko nyuma. Kamwe
hapaitwi Msikiti wa Kwa Mtoro, kama ndugu zetu wa Kirangi wanavyodhani ni
Msikiti wa kutoka kwao ‘Kwa Mtoro’ kule Kondoa; na hivyo kujinasibisha nao visivyo
kabisa kama nao ni Msikiti wa Warangi.
Mzee Haidar Mwinyimvua alitokea
maeneo ya Winde, Bagamoyo na aliishi
eneo la Kisutu hapa Dar es Salaam. Nyumba yake ilikuwapo pale Kisutu Mivinjeni,
mita chache tu kutoka kwenye uzio wa makaburi ya Kisutu, kwenye Barabara
iliyojulikana kama Wadigo Street. Wadigo Street namba 5, ndiyo nyumba
alimokulia mwandishi huyu iliyomilikiwa na baba yake mkubwa hayati Mzee
Abdallah Saleh Diwan Tambaza, aliyekuwa Jumbe wa Kisutu. Wadigo Str. Namba 7
ilikuwa mali ya Jumbe Abdallah pia.
Mzee Haidar Mwinyimvua alijiunga na
TANU mapema kabisa akiwa mwenyekiti wake eneo la Kisutu, lakini tawi lilikuwa
mtaa wa Mvita, Kariakoo. Mvita Branch ndiyo lililokuwa tawi lenye nguvu kabisa
jijini na nchi nzima kwa wakati huo. Uzinduzi wa tawi la Mvita umeweka historia
mpaka leo, kwani walihudhuria watu wengi mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi
akiwamo na Bwana PC pia. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wakati huo, Sheikh
Suleiman Takadir kutokana na kumpenda Nyerere kupindukia, ndipo kwa mara ya
kwanza alipomfananisha Nyerere kama ni ‘nabii wa watu weusi’ kutoka kwa Mola
wao— Inna Lillah Wainna Ilayhi Rajuun!
Kutokana na ushupavu na mapenzi yake
kwenye mapambano, Mzee Haidar haraka haraka, akaingizwa kwenye Baraza lenye
nguvu la Wazee wa TANU na pia Halmashauri Kuu ya TANU pale Makao Makuu. Huko
aliungana na viongozi wengine waandamizi wakati huo kama vile John Rupia,
Julius Nyerere, Zuberi Mtemvu, Jumbe Tambaza, Suleiman Takadir, Oscar Kambona,
Bhoke Munanka na wengineo wakawa wanashughulikia ukombozi wa nchi yetu kwa
karibu kabisa wakitoa nguvu na mali zao.
Kuwemo ndani ya Baraza la Wazee au
Halmashauri Kuu ya TANU siku zile, kamwe haikuwa nafasi ya wewe kwenda
kujitengenezea posho za vikao au safari za nje upate pesa za kujikimu—hapana.
Ni nafasi adhimu ya kuonyesha ni kwa kiasi gani wewe utaweza kuitumikia nchi
yako kuliko kungojea nchi ikutumikie wewe (Rejea maneno mashuhuri ya aliyepata
kuwa Rais wa Marekani John Kennedy ‘...ask not what your country can do for
you; but what you can do for your country)—tafsiri ya maneno hayo ni kwamba;
usiulize nini nchi yako itakufanyia, bali wewe useme kwanza nini utaifanyia
nchi yako.
Mzee Mwinyimvua, aliifanyia nchi yake
mengi sana wakati ule wa ukombozi. Alizunguka na kina Nyerere, Titi na wengineo
nchi nzima hii kuelezea mustakabali wa kudai uhuru. Wao wenyewe wakijigharimia
kula, kunywa, kulala na usafiri wa kwenda na kurudi. Alhamdullilah, nchi yetu
si ndogo kwa mapana na marefu, sasa pimia mwenyewe watu wale walijinyima kiasi
gani kwa ajili yetu.
Mzee Haidar Mwinyimvua alikuwamo
kwenye ujumbe wa kutoka Jimbo la Mashariki na Makao Makuu ya TANU wakati huo,
kwenye mkutano ule mashuhuri wa ‘Kura Tatu’ kule Tabora; mkutano ambao nusura
ukisambaratishe chama kwa kutoelewana kuhusu kushiriki au kususia Uchaguzi Mkuu
wa mwaka wa 1958. Kazi waliofanya kina Mzee Mwinyimvua na wenzake kwa kufikia
kile kilichoitwa ‘Uamuzi wa Busara’, kule mkutanoni ndicho kilichotufikisha
hapa leo tuko ‘huru huria’.
Moja ya masharti magumu ya uchaguzi
ule ni kwamba ili mtu aingie kwenye Baraza la Kutunga Sheria, ilibidi lazima
awe na kiwango fulani cha elimu, ambayo wengi wa viongozi waandamizi wa chama
cha Tanu wakati ule hawakuwa nayo. Kina Mzee Haidar na wenzake wakaondoa mawazo
ya kuwa wajumbe katika Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO)—Legislative Council of
Tanganyika—sawa na Bunge kwa sasa. Waliwapisha wasomi ambao hawakuwamo mwanzoni
kwenye mapambano. (Angalia kitabu Mohammed Said, Maisha na Nyakati za
Abdulwahid Sykes,uk. 266/274).
Kitendo cha kuwaingiza mapandikizi
mapya katika harakati, tena wengi wao wakiwa ni wa kutoka upande wa pili wa
dini nyengine, ambao mwanzoni hawakushabikia mapambano yale kwa kuhofia
kupoteza ajira zao serikali, kilimsononesha sana Sheikh Suleiman Takadir,
ambaye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU lenye nguvu zote.
Mzee Haidar Mwinyimvua, ambaye
alikuwa rafiki mkubwa wa Sheikh Takadir anaelezea tukio la kihistoria lilotokea
mwaka 1958 Makao Makuu ya Chama:
“Ilikuwa katika ofisi ya zamani ya
TANU tukisubiri kufanya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Ghafla tu Sheikh
Takadir alisimama wima akishikilia fimbo yake ya kutembelea akimuelekea Nyerere
huku akisema “Huyu mtu katu hatakuja kutujali sisi bali atawajali ndugu zake.
Usipoziba ufa utajenga ukuta”. …sisi sote katika chumba tulipigwa na butwaa na
maneneo yale …nilimwona Nyerere akilia na akatugeukia sisi na kutuuliza, ‘ je,
Sheikh Suleiman amesema maneno yale kwa niaba yenu?’. Tulijibu kwa pamoja kuwa
hatukuwa na habari na shauri lile; na mkutano ulivunjika hapo hapo.” (Angalia
Mohamed Said, uk. 274).
Katika kukisaidia chama na harakati
zake pale zilipokwama, habari zinasema kwamba Mzee Haidar Mwinyimvua, baba wa
watoto kadhaa mashuhuri hapa nchini, akiwamo Imam Mkuu wa Msikiti wa Mwinyikheri
Akida, Kisutu, Dar es Salaam, Sheikh Ahmed Haidar, aliuza moja ya nyumba zake
na kupeleka pesa zote katika mapambano dhidi ya mkoloni! Mungu wangu; ni
uzalendo wa hali ya juu huo.
Wanao wana njaa; wake zako wana njaa;
mama mzazi ana njaa; nguo zenu matambaratambara; humiliki hata baiskeli mbovu
ya kutembelea; unauza nyumba unapeleka fedha kusaidia ukombozi wa taifa lako—
Mh! Mh! Mh! Taifa lenyewe kiziwi; taifa lenyewe bubu; taifa lenyewe kipofu, leo
halina ahsante wala shukrani ya kukumbuka mchango mkubwa kama ule.
Mzee wetu huyu, Mungu amrehemu huko
alipo, amghufirie madhambi yake na, naam, ampe pepo siku ya hesabu; aliamini
sana katika malezi na maadili mema miongoni mwa wanafamilia yake. Alijitahidi
katika hali hiyo duni ya Kiafrika siku hizo, kuhakikisha wanawe wamepata elimu
bora.
Sheikh Ahmed Haidar Mwinyimvua, ni
mtoto mkubwa wa Mzee Haidar; ana shahada
tatu za juu katika elimu ya dini ya Kiislamu kutoka Al Azhar Shariff kule
Cairo, Misri. Amekuwa mwalimu kule nchini Yemen, Chuo cha Kiislamu cha Markaz,
Chang’ombe na Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro.
Mwanawe mwengine, Twahir Haidar
(ameshatangulia mbele ya Haki), alibobea katika sheria akiwa na degree yake
kutoka Urusi, alikopelekwa na chama cha TANU. Kwa miaka mingi sana alifanya
kazi katika Ofisi ya Kabidhi Wasii (sasa Rita), kama mtaalamu wa masuala ya
sheria za vyama na NGOs.
Serikali ya Tanzania ilipotaka
kurejesha Mahakama ya Kadhi nchini, Twahir Haidar ndiye aliyepewa kazi ya
kutembelea nchi mbalimbali na kuangalia namna gani wanavyoendesha Mahakama hizo
nchini mwao, akilinganisha na zile za hapa wakati wa ukoloni.
Ripoti yake ndefu kuhusu suala hilo,
ndiyo aliyoitumia Waziri Bernard Membe, pale alipolihakikishia Bunge kwamba ni
bora Tanzania ikaridhia kuruhusu Mahakama ya Kadhi kwa Waislamu na kujiunga na
OIC. Katika uhai wake Twahir Haidar
ndiye aliyekuwa tegemeo kubwa la Waislamu pale walipokuwa wakikusudia kuanzisha
taasisi au kutengeneza katiba zao za misikiti kabla kupeleka RITA.
Mtoto mwengine wa Mzee Mwinyimvua, ni
Adam Haidar, aliyewahi kufanya kazi katika Ofisi za ‘Interline’ kwenye Shirika
la Ndege la Afrika Mashariki ya zamani EAAC na baadaye akafanya kazi pia kwenye
Shirika la Ndege la Tanzania – ATCL. Yuko pale anaishi maisha ya kustaafu
kwenye maeneo ya Biafra, Kinondoni, Dar es Salaam.
Watanzania tuamke na tutafute habari
za watu wa namna hii, ili nasi angalau leo tuseme ahsante kwa watoto wao basi!
Kwani watoto wale walikosa sehemu fulani ya malezi ambayo baba zao waliilekeza
kwenye taifa zima.
Kaburi la Sheikh Haidar Mwinyimvu Kisutu kaburi hili lipo jirani sana na walipozikwa Abdul na Ally Sykes na hawa wote walikuwa wazalendo waliopigania uhuru wa Tanganyika |
Simu: 0715808864
No comments:
Post a Comment