IDDI S. KIKONG’ONA NINAYEMFAHAMU
NA SADIKI S. GOGO
Nilikutana nae kwa mara ya kwanza mwaka 1992 siku ambayo tarehe siikumbuki lakini ilikuwa ni katika
kipindi cha dini. Nilikuwa mgeni shuleni hapo nikiripoti kwa mara ya kwanza nikiwa mwanafunzi wa
kidato cha pili Morogoro Secondary School nikitokea shule ya Sekondari Ifakara maarufu kama Machipi.
Wakati tukisubiri mwalimu wa dini aingie, aliingia kijana maji ya kunde mfupi, mwembamba, mwenye
tabasamu la kuonesha mapenzi makubwa kwa watu anaokutana nao. Baada ya muda niligundua kuwa kijana huyu alikuwa anasoma kidato cha tatu na ndiye aliyekuwa mwalimu wa somo la EDK (Elimu ya
Dini ya Kiislamu) shuleni pale maarufu wakati huo kama Maarifa ya Uislamu. Alijitambulisha mara baada
ya kuona kuwa kuna sura mpya darasani. Nikamfahamu kwa mara ya kwanza Iddi Suleiman Kikong’ona
(The man of Decision).
Mada ya siku hiyo ilikuwa uchambuzi juu ya dini ipi ni stahiki kwa mwanadamu kuifuata. Namna
alivyowasilisha mada ile ilinivutia kiasi cha kuonesha umakini na hamasa kubwa ya kutaka kujua zaidi.
Alitoa mifano na hoja zilizomtesheleza kila mmoja kwa umakini, umahiri na kujiamini sana. Toka siku
hiyo nikatamani sana niwe kama yeye.
Sikujua niataanzaje. Hata hivyo kumbe alikuwa pia kwenye kazi
ya kutafuta vijana makini na kuwaunganisha kwenye Darasa Duara la vijana lililokuwa likiendelea mjini
Morogoro yakijumuisha madarasa ya watu wazima, vijana na wanafunzi. Baada ya kipindi aliniita na
kuniuliza nilikotoka na historia yangu kwa ujumla. Kwa bahati nzuri nami niliona kama nimeokota dodo
kwenye muarubaini. Kwani wakati huo nami ndio kwanza nilikuwa katika shauku kubwa ya kusoma
kuhusu Uislamu. Kiko akanishauri kujiunga na Elimu ya Kiislamu Kwa Njia ya Posta iliyokuwa ikitolewa na
IPC.
Nilikuwa mwepesi kumaliza juzuu moja hata nyingine hali iliyomshawishi kujenga ukaribu nami na
kunikaribisha nyumbani kwao Mtoni Street. Kwa miaka mingi baadae tuliishi kwao tukisoma pamoja na
vijana wengine huku tukiwa na program mbalimbali za usomaji wa Qur an, hadithi na vitabu vingine.
Nyumbani kwao kulikuwa ni kambi ya masomo mbalimbali kwa vijana wengi wenye maadili na
mwelekeo wa kidini.
Kutokana na juhudi na hamasa niliyokuwa nayo, Bro Kiko haraka akanishauri kuanza kufundisha kidato
cha kwanza. Pamoja na kuwa nilikuwa na shaka Bro Kiko alinitia moyo sana na kwa vile alikuwa mwalimu mzuri, mshauri na mtu anayependa kutekeleza falsafa ya kujifunza kwa kutenda.
Nilimudu na
kunikutanisha na watu ambao kimsingi walikuwa ni ''Role Models,'' kwa kweli. Udugu wa Kiislamu
waliokuwa nao wakati huo ulinitia hamasa na kuona kweli Uislamu ni dini ya haki na ni stahiki kufuatwa
na wanadamu. Mafundisho niliyokuwa nikiyapata kupitia EKP niliyaona waziwazi kwenye maisha ya
hawa brothers mtaani.
Ukaribu na urafiki wetu na Brother Kiko uliongezeka na kuwa udugu baada ya kushiriki Tamasha la Pili la
Ujenzi wa Shule ya Kiislamu Kirinjiko mwaka 1994, tukiwa vijana wadogo kuliko wote waliowawakilisha
wanaharakati wa Morogoro kwenye tamasha hili kubwa ambapo binafsi kwa mara ya kwanza nilipata
nafasi ya kukutana na Prof Hamza Njozi wakati huo akiwa ni Dokta. Brother Ilunga Kapungu na Jabiri
Koosa, Mwalimu Mushi, Sheikh Mohamed Kassim, Imamu Suleiman (Allah amrehemu), Mzee Salilu na
wengine wengi, orodha ni ndefu. Namshukuru Brother Kiko kwa kunitetea kuwepo kwenye msafara
mimi na yeye kwa vile wakubwa walikuwa na wasiwasi nami kuwa ni mgeni sana katika harakati. Kwa
umakini mkubwa Brother Kiko aliwasilisha ripoti ya Harakati za Kiislamu Mkoani Morogoro akieleza
shughuli zinazofanyika kuwazindua Waislamu mashuleni, makazini, mitaani madarasa duara maalum ya
kazi n.k mjini Morogoro.
Kila mmoja hakuamini kama kijana mwenye umbo dogo na mwonekano dhaifu
angeweza kutoa ripoti ile iliyosheheni mambo yanayogusa kila nyanja ikiwa ni pamoja na ushiriki wa
Waislamu kisiasa na kiuchumi.
Mwaka 1995 ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi Bro Kiko alikuwa anataraji kufanya Mtihani wa Taifa lakini
alionesha ujasiri mkubwa katika ushiriki wake kama mtu mzima akituunganisha vijana wa Kiislamu
kushiriki siasa na mambo ya kijamii. Baada ya mitihani alifaulu kwenda Pugu Sekondari katika mchepuo
wa sayansi PCB. Wakati huo pia Ubungo Islamic kwa mara ya kwanza ndio ilikuwa inatoa kidato cha nne
na iliazimiwa kuanzisha kidato cha tano. Kutokana na Mapenzi yake kwa dini yake na harakati kwa
ujumla aliamua kuacha kwenda Pugu na badala yake kwenda Ubungo Islamic wakiwa ni wanafunzi wa
mwanzo wa kidato cha tano. Kwa vile shule ndiyo ilikuwa inaanza hakukua na michepuo ya sayansi, hivyo
alilazimika kusoma EGM badala ya PCB. Katika kipindi chote Bro Kiko alikuwa ni Kiongozi (Amir) wa
wanafunzi darasani kwao kutokana na uwezo wa uongozi na kujitambua. Kila mmoja aliyekutana naye
alihisi kitu cha ziada alichokuwa nacho Bro Kiko. Kama si subra, uvumilivu, ukweli, uadilifu na mapenzi
kwa kila mmoja basi itakuwa ni mtazamo wake wa kutopenda kufuata vitu kibubusa bila ya kuwa na
hoja.
Baada ya kumaliza kidato cha tano alibaki Ubungo Islamic kwa ajili ya kusoma Diploma ya Ualimu katika
masomo ya Jiografia na Hesabu. Alimaliza na kufaulu vizuri. Alikuwa mwalimu na mpenzi mkubwa wa
Hesabu. Wakati Kirinjiko inaanza Brother Kiko aliungana na wenzake wengine kama akina Mnyero Janja,
Saidi Ally, Swahiba wake Musa Saidi Musa na wengine kwenda kuanzisha shule kidato cha kwanza
Kirinjiko. Walifanya kazi hiyo kwa moyo mmoja na mapenzi makubwa. Katika Kirinjiko ya leo kuna
mchango wake mkubwa (Allah SW amkubalie ibada yake hii), Amiin.
Marehemu aliwahi pia kuwa Mratibu wa IPC na EKP na baadae kushiriki shughuli za kuboresha vitabu vya maarifa ya
Uislamu kama mtaalamu wa Typesetting na Graphics, utaalamu ambao alianza kujifunza taratibu
mwenyewe na baadae kupata utaalamu zaidi toka kwa mtu aliyekuwa akimuheshimu sana Brother Kati
ka Batembo. Brother Kiko alikuwa miongoni mwa waandishi wakubwa wa makala gazeti la Annur.
Mfasiri wa makala alizokuwa akipewa na mwalimu wake Mhariri wa Annur wakati huo Brother Omar
Msangi. Brother Kiko alikuwa ni mtunzi mzuri wa mashairi. Mashairi yake ni ya kipekee sana (unique)
mafupi, yenye misamiati mingi na yenye ujumbe murua.
Baada ya kufanya kazi IPC miaka kadhaa alibadilisha upepo na kujiunga na Taasisi ya Munadhwamat Al
Daawa al Islamiya taasisi ambayo alidumu nayo mpaka mwisho wa uhai wake kwa miaka isiyopungua
tisa. Hapa alifanya kazi mbalimbali za kuhariri, na kufanya typsetting na graphics za vitabu mbalimbali
kama vile tafsiri ya Ibn Kathiir, Al Luulu wal Marjaan, Ar Rahiiq al Makhtoum, Njia za Kujikinga na Zinaa,
Mwongozo wa Daawah nk. Si chini ya vitabu 30 alishiriki kuvifanyia kazi moja ama nyingine. Kazi yake ya
mwisho ilikuwa ni Kitabu cha Malezi katika Uislamu ambacho kimetolewa na IIIT ya USA. Historia ya Bro Kiko haiwezi kukamilika bila kutaja mchango wa Bro Kifea aliyekuwa mwalimu wake wa
kwanza wa dini baada ya ile aliyoipata madrasa kwa Sheikh Dadi, Allah sw amlipe kila la kheri kwani
alimpa mwelekeo mzuri wa dini na kumfanya awe kijana makini. Jambo hili silisemi mimi bali mwenyewe
siku zote enzi ya uhai wake na hata muda mchache kabla ya kurejea kwa Mola wake aliniomba nimtafute Brother Kifea atoe shukran zake kwa kumfanya kuwa kijana makini. Sheikh Mohammed Qassim, Brother
Omar Msangi, Prof Hamza Njozi ni walimu wake aliowapenda sana na kuwakumbuka muda wote.
Mambo ya Kujifunza katika maisha ya Bro Kiko:
- MAMBO YA BINAFSI Imani: Mwenyezi Mungu ni mjuzi zaidi lakini imani ya bro Kiko juu ya uwepo wa Allah sw ni ya hali ya juu. Msimamo wake siku zote ulikuwa ni kuwa yeye atakufa katika saa na dakika aliyopanga Allah sw na si vinginevyo. Hili ni jambo la kuwa na yakini nalo.
- Tabia yake: Kiko alikuwa Mkweli kwa kiasi kikubwa, muadilifu na mpenda amani na utulivu muda wote wa maisha yake. Moja ya mambo aliyopenda kunihusia ni kujihusisha kusuluhisha migogoro kwa kurejea kauli Bro Kiko alikuwa anapenda sana kujifunza mambo mapya kila siku ndio maana alikuwa akitembea na kitabu na kompyuta muda wote wa maisha yake. Hili ni jema.
- Alikuwa na mapenzi makubwa na Qur an. Kiasi ambacho muda mwingi wa mazungumzo yake alirejea Qur' an hata katika jambo dogo kiasi gani ambalo usingedhani kama waweza pata ushahidi au ufafanuzi wake kwa kutumia Quran. Nilivyomfahamu hakuwa na kawaida ya kusoma Qur an wakati wa Ramadhani au katika miezi na masiku maalum tu. Bali Alisoma Quran wakati wote wa maisha yake. Jambo hili lilimfanya awe mtu tofauti sana. Hili si la kuliacha litupite
- Alikuwa na mapenzi makubwa na Watoto. Akifika nyumbani kwako hata ikiwa ni mara ya kwanza muda mchache kama kuna watoto atakuwa rafiki yao mpaka utashangaa. Waliosafiri na Kiko kwenda sehemu mbalimbali watathibitisha hili kila mahali alipokwenda hata mikoani alikuwa na marafiki watoto, akiwapiga picha, kuwasomea Qur an na kuwawekea katuni nzuri toka kwenye kompyuta yake. Hili ni zuri ndugu zangu tulichukue Benki yake ilikuwa ni watu.
- Alikuwa na mapenzi makubwa ya kusaidia watu kutoka moyoni kwake. Ukipata bahati ya kuongozana na Kiko akiwa na pesa utashangaa kila anayekutana naye mwenye uhitaji alimsaidia bila kuhoji au kuwa na shaka. Falsafa yake ilikuwa ikiwa utatoa unaweka akiba mbele ya Allah (SW) na mara kwa mara alinieleza kuwa kutoa ni jambo kubwa kiasi ambacho hata waliokufa wakipewa muda mchache kurudi duniani jambo rahisi na muhimu kwao litakuwa kutoa swadaka kama inavyosema Qur an. Alitoa kwa siri na kwa dhahiri na pia alishawishi watu wengine kufanya jambo hili. Tuombe dua maalum ikiwa bado tuna uzito wa kulichukuwa hili.
- Aliwajibika sana kwa Madeni yake: Brother Kiko alikuwa akiogopa kuondoka akiacha madeni kwa kiwango cha hali ya juu sana. Kabla ya kufanya chochote mara apatapo mshahara wake anachofanya kwanza ni kuhakikisha hana deni. Hali hii ilimpa faida nyingi kwanza watu walimheshimu sana mtaani kwake, kazini na hata madukani kwa wauza vyakula. Alipenda kutowakwaza waliomuamini. Siku chache kabla ya kufariki kwake alitumiwa pesa toka MUM kama sehemu ya malipo ya kazi alizokuwa akizifanya kwa taasisi hiyo. Pesa hizo alizitumia kulipa madeni madogo madogo aliyokuwa akidaiwa. Lakini alibaki na deni moja la sh. 600,000 ambalo alikuwa akidaiwa na mmoja wa ndugu zetu katika imani. Jambo hili lilimshughulisha sana kiasi ambacho kila nilipokwenda kumjulia hali cha kwanza aliniuliza nini cha kufanya ili ndugu yetu huyu avumilie na kulipwa baadae. Akanituma niende kuongea nae. Nilimtafuta mahali ambapo anapatikana mara kwa mara na kuongea nae Alhamdulillah. Nikajifunza kitu toka kwa ndugu yetu huyu “Wema wako wengi”. Kwanza alitoa kauli ya kumsamehe Sheikh Kiko deni lote. Nilivyokuwa namjua Bro Kiko jambo hili lingemsononesha zaidi. Nikamwomba alipunguze na kumwomba amwongezee muda wa kulipa akakubali, nami nilimfikishia taarifa hiyo Bro Kiko. Kwa kweli kwa siku hiyo pamoja na uchovu wa kuumwa alitoka nje akiwa mchangamfu na mwenye nguvu. Ndugu yetu huyu Allah atamlipa. Amesamehe deni hili mara tu aliposikia Kiko karejea kwa Mola wake. Tunamuomba Allah (s.w) atufanye wenye kujali madeni yetu na pia tuwe wenye kusameheana madeni pindi unapoona kwa dhati nduguyo kakwama pamoja na kuwa na niya thabiti na mwelekeo wa kulipa deni lake. Kusamehe madeni Kusamehe madeni ilikuwa ni miongoni mwa tabia yake hasa pale alipoona nduguye ana niya ya kulipa ila ametingwa.
- MAMBO YA KIJAMII Kufanya kazi kwa Timu Tanzia hii inaonesha Kiko alijali sana kufanya kazi kwa timu, kuandaa watu kwa kuongea na vijana na pia umuhimu wa kudumisha udugu wa Kiislamu ili kuvutia wale tunaowataka wawe Waislamu umuhimu wa Madarasa Duara, muhimu wa kuwa na ''circles,'' za fikra na kuwafuata vijana mashuleni, kuna akina Iddi wengi tunawakosa kwa kutokwenda kuongea nao. Sote tujikumbushe jukumu hili muhimu. Ukitoa hupotezi Kiko hakutangulia mbele ya haki kwa kuwa alikosa matibabu mazuri, pesa za kununulia dawa na hata chakula kizuri. Hivi vyote vilipatikana katika namna ya ajabu, majirani Waislamu kwa Wakristo, wote walikuwa na shauku ya kuokoa maisha yake. Hii ni kwa kuwa alikuwa mtoaji na aliwekeza kwenye jamii. Alisaidia watu na kuishi na watu vizuri. Japo hakuacha cha maana sana katika vitu, Kiko ameacha hazina kubwa watu aliowasaidia kwa namna moja ama nyingine. Alirejea kwa mola wake kwa kuwa muda wake wa kuishi hapa duniani ulikuwa umekwisha. Bro Kiko kama wanadamu wengine si mkamilifu kwa kila jambo. Hayo tunamwachia Allah (SW) Nasi wajibu wetu ni kumwombea maghfira na msamaha kwa pale alipokosea. Namuomba Allah (s.w) atusamehe makosa yetu sote na atujaalie tuwe ni miongoni mwa waja wema. Tukumbuke ya msingi kwa ajili ya akhera yetu.
No comments:
Post a Comment