Tuesday, 6 February 2018

KUTOKA GAZETI LA UHURU: ALLY KLEIST SYKES MPIGANIA UHURU ALIYEMPOKEA MWALIMU NYERERE DAR ES SALAAM

Uhuru, Jumanne Februari 6, 2018
ALLY KLEIST SYKES
Mpigania uhuru aliyempokea Nyerere Dar es Salaam
L Alimkabidhi kadi namba moja ya TANU
L Mwandishi wa karatasi zilizowakera Wakoloni
NA MUSSA YUSUPH
UHURU wa Tanganyika haukuwa kazi rahisi kupatikana kama ambavyo wengi wanadhania.
Ili kuwa ni shughuli pevu iliyohitaji kujitoa kwa hali na mali ili kuhakikisha Waafrika kutoka Tanganyika ambalo lilikuwa koloni la Uingereza, wanajitawala.
Jitihada hizo zilifanywa na wapigania uhuru mbalimbali waliounganishwa kupitia chama cha Tanganyika National Unioni (TANU), kilichoundwa na na watu waliojawa na shauku la kujitoa kwenye makucha ya kikoloni.
Ally Kleist Sykes mzaliwa wa Mtaa wa Gerezani, Kariakoo Dar es Salaam, ni miongoni mwa waasisi waliopigania uhuru wa Tanganyika ambaye ana mengi ya kukumbukwa.
Mzee huyo aliyezaliwa Oktoba 10 mwaka 1926 kisha kufariki Dunia Mei 19 mwaka 2013 alikuwa mzalendo aliyeanza harakati za kisiasa kwenye miaka ya 1950.
Ally Sykes ndiye aliyemwandikia na kumkabidhi Hayati Mwalimu Julius Nyerere kadi ya TANU namba moja.
Pia alikuwa miongoni mwa waasisi wa TANU, kati ya wazee watu saba waliokuwa katika kamati ya TAA iliyounda TANU.
Alikuwa miongoni mwa wafadhili wakuu wa TANU, huku akiwa tegemeo la chama hicho katika kutekeleza mikakati hatari dhidi ya utawala wa Uingereza.
Katika siasa za sasa Mzee Ally Sykes anaweza akaelezewa kama "Mzee wa fitna" kwani alikuwa majukumu ya kuwagombanisha wananchi dhidi ya serikali ya kikoloni.
Majukumu hayo aliyatelekeza kwa kuchapa karatasi ambayo Waingereza waliyaita ya kuchochea ghasia kwani majasusi wa serikali ya kikoloni walimfahamu kwa uhodari wa kutengeneza mambo.
Waingereza walipata wakati mgumu kumkabili kwani licha ya uhodari wa kisiasa aliokuwa nao, Ally Sykes pia alikuwa na medali ya mlenga shabaha mahiri, aliyopata kwenye Vita Kuu vya Pili ya Dunia.
Kwenye vita hiyo Ally Sykes alikuwa kwenye bataliani ya sita (Battalion 6 Burma Infantry) King's African Rifles (KAR) 
Hakika Ally Sykes alikuwa mzalendo, mweledi wa mambo na miongoni mwa waasisi muhimu wa TANU ambaye sahihi yake ndio iko katika kadi ya TANU ya Mwalimu Nyerere.
Umaarufu wake ni kama aliurithi kutoka kwa Baba yake Mzee Kleist Sykes aliyekuwa watu mashuhuri  Dar es Salaam katika miaka ya 1900 hadi alipofariki mwaka 1949.
Baba yake alikuwa maarufu kwa kuwa alilelewa na Affande Plantan aliyekuwa askari kiongozi katika jeshi la Wajerumani lilokuja Tanganyika na Herman Von Wissman.
Kleist alikuwa ndiye katibu muasisi wa African Association mwaka 1929 chama kilichokuja baadae kujibadili na kuwa TANU ambacho Ally Sykes akiwa mmoja wa waasisi.
Pia baba yake aliasisi Al Jamiatul Islamiyya Fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika) na kupitia jumuia hiyo akajenga shule ya kwanza ya Kiiislam Dar es Salaam, ambayo ilisomesha Qur’an pamoja na elimu ya kimagharibi.
Jumuiya hiyo ilichangia vijana wengi wa kiislamu kuingia kwenye siasa za TAA na TANU katika harakati za kudai uhuru.
AKUTANA NA NYERERE
Ally Sykes na kaka yake Abdulwahid Sykes ndio watu wa mwanzo kumpokea Mwalimu Nyerere alipokuja Dar es Salaam mwaka 1952.
Nyerere alifika nyumbani kwa akina Sykes na ilijenga urafiki ambao ulipitiliza na kuwa udugu mkubwa wa mapenzi ya dhati si baina yao tu bali hata kwa wake na mama zao.
Mama yake Nyerere, Bi. Mugaya mara kwa mara alipenda kumtembelea nyumbani Bi Mruguru biti Mussa ambaye ndiye mama wa Sykes.
Pia Mama Maria Nyerere alikuwa mwenye urafiki wa karibu na Bi. Zainab ambaye ni mke wa Ally Sykes aliyekuwa akiishi Mtaa wa Kipata.
Wakati huo harakati za kuanzisha TANU zilikuwa zimepamba moto huku fitna za Waingereza kuwatokomeza viongozi shupavu wa TAA kama Hamza Mwapachu, Dk. Vedast Kyaruzi, Dk. Wilbard Mwanjisi, zilikivunja nguvu chama hicho.
Ndio maana TANU ilipokuja kuasisiwa mwaka 1954 Ally Sykes kadi yake ya TANU ikawa namba mbili, Nyerere namba moja, Abdulwahid Sykes kadi yake namba tatu, Dossa Aziz kadi namba nne na John Rupia kadi yake ilikuwa namba saba.
Kipindi hicho Ally Sykes alikuwa Katibu wa Tanganyika African Government Servants Association (TAGSA) na vilevile alikuwa mwakilishi wa chama hicho katika Kamati ya Uajiri ya Serikali (Government Establishment Committee).
Thomas Marealle ndiye alikuwa rais wa TAGSA na Rashid Kawawa alikuwa mwanakamati.
Wanasiasa hao walijipa jina la ‘’Wednesday Tea Club’’ wakikutana kila siku ya Jumatano kunywa chai pamoja na kupanga mikakati ya kuwang’oa Waingereza katika ardhi ya Tanganyika.
Kupitia Ally, Abdulwahid na Dossa Aziz, Nyerere aliweza kujuana na wenyeji wa Dar es Salaam maarufu baadhi yao ni Sheikh Hassan bin Amir, Mshume Kiyate, Jumbe Tambaza, Sheikh Suleiman Takadir, Clement Mtamila, Titi Mohamed na Tatu biti Mzee.
NYARAKA ZA HISTORIA YAKE
Baadhi ya nyaraka za historia alizozitunza nyumbani pake na kumpatia Mohamed Said, mpaka Ally Sykes, anafariki dunia zinadaiwa bado zilikuwa kwenye mikono ya Mohamed Said.
Ally Sykes aliwahi kumlalamikia kuwa nyaraka hizo ni mali ya taifa na lazima azikabidhi serikalini kwa kuhifadhiwa na kuwekwa kama urithi wa kizazi kijacho.
Inadaiwa kuwa nyaraka za Ally Sykes zinakwenda zimeelezea historia tangu babu yake Sykes Mbuwane alipoingia Tanganyika kutoka meli ya kivitia ya Wajerumani iliyotia nanga Pangani akitokea Msumbiji.
Nyaraka hizo zinadaiwa kuwa na barua za wanasiasa wa mwanzo katika Tanganyika mbali historia ya baba yake.
Inasemekama zimeelezea habari kuhusu wazalendo na machifu, wanasiasa wenye asili ya Kiasia na Waingereza wenyewe waliokuwa watawala.
Ally Sykes ameelezea harakati za Dk Joseph Mutahangarwa, Chifu Abdieli Shangali wa Machame, Paramount Chief Thomas Marealle wa Marangu, Chifu Adam Sapi Mkwawa wa Wahehe, Chifu Harun Msabila Lugusha na Dk. Wilbard Mwanjisi.
Wengine ni Abdulkarim Karimjee, Dk. Vedas Kyaruzi, Liwali Juma Mwindadi, H.K. Viran, Stephen Mhando, Dossa Aziz, Ivor Bayldon, Yustino Mponda, Ivor Bayldon, Rashid Mfaume Kawawa, Bhoke Munanka, Rashid Kheri Baghdelleh na  Robert Makange.
Wanasiasa wengine aliowaelezea ni Saadani Abdu Kandoro, Malkia Elizabeth, Chief Secretary Bruce Hutt, Gavana Edward Twining, Gavana Ronald Cameron, Mwalimu Thomas Plantan na ndugu zake Schneider Abdillah Plantan na Ramadhani Plantan.
Pia wapo wakina Mwalimu Mdachi Shariff, Mwalimu Nicodemus Ubwe, Kassela Bantu, John Rupia, Hamza Kibwana Mwapachu, Othman Chande, Leonard Bakuname, Stephen Mhando, Oscar Kambona, Peter Colmore, Albert Rothschild, Ali Mwinyi Tambwe, Alexander Thobias, Japhet Kirilo, Joseph Kimalando, Ian Smith, Roy Welensky, Jim Bailey na Kenneth Kaunda.
Ally Sykes kwenye nyaraka hizo zinadaiwa amewaelezea wakina, Meida Springer, John Hatch, Gretton Bailey, Brig. Scupham, Dome Okochi Budohi, Annur Kassum, Nesmo Eliufoo, Yusuf Olotu, Joseph Kimalando na Mwalimu Julius Nyerere kwa nyadhifa walizokuja kuzishika kwenye Tanganyika huru.
xxxx

No comments: