TAAZIA
KOMREDI KINGUNGE
NGOMBALE MWIRU
(1932 – 2018)
Sasa ni miaka mingi
imepita lakini nakumbuka kama vile ilikuwa jana. Nimemfahamu Balozi Juma
Mwapachu mwaka wa 1967 nyumbani kwa ‘’class mate,’’ wangu Edward Makwaia, mtoto
wa Chief Kidaha Makwaia wa Siha. Siku hiyo Edward tukizoea kumwita Ted
alitualika marafiki zake nyumbani kwao Upanga yalipokuwa Makao Makuu ya Red
Cross kwenye tafrija ya kuzaliwa kwake. Siku hiyo ndipo nilipojuana na Juma
Mwapachu na nikawa nimepata kaka na akanisaidia mengi sana katika ulimwengu wa
kusoma na kutafuta elimu. Mwaka ule Kaka Juma kama wengi wadogo zake
tulivyozoea kumwita alikuwa yuko nyumbani baada ya kufukuzwa Chuo Kikuu Cha Dar
es Salaam kwa wanafunzi kugoma kwenda National Service. Kuanzia siku ile hadi
sasa karibu nusu karne kila ninapokutana na Kaka Juma mazungumzo yetu
yatajikita katika masuala ya kusoma na siasa hasa historia ya siasa katika
Tanganyika chini ya ukoloni wa Waingereza.
Siku moja Juma Mwapachu akaniambia
kuwa baba yake katika maktaba yake Tanga alikuwa na nakala ya kitabu cha
Karl Max, ‘’Das Kapital,’’ toleo la mwaka wa 1924 na maktaba hii imehifadhiwa
na mama yao kama alivyoiacha mwenyewe marehemu Hamza Mwapachu. Kitabu hiki kwa mara
ya kwanza kimechapwa mwaka wa 1867. Nikamuuliza, ‘’Kwani Mzee alikuwa Mkomunisti?’’
‘’Baba alikuwa, ‘’Leftist,’’ jibu lilikuja. Lazima nikiri kuwa Juma Mwapachu
katika miaka ile ya utoto wangu alikuwa ananitia darasani. Mwanafunzi wa
sekondari unamweleza kuhusu Karl Marx na ‘’Das Kapital,’’ kisha unamweleza
‘’concept,’’ za ‘’left’’ na ‘’right...’’ Haya yalikuwa nje ya dunia niliyokuwa
naifahamu. Mwaka wa 1967 ndiyo ulikuwa mwaka wa Azimio la Arusha na moja katika
masomo tuliyokuwa tunafundishwa ilikuwa somo la siasa na kwa hakika walimu
walijitahidi kutueleza ubaya wa ‘’Mabepari,’’ na ‘’Wanyonyaji.’’ Hapa ndipo
nilipotaka tupafikie ili tumpate Komaredi Ngombale Mwiru. Sikupata kujua kuwa
Azimio la Arusha liliandikwa na Ngombale Mwiru hadi baada ya kusoma taazia ya
Mh. Zito Kabwe. Miaka yote toka niko shule nikijua ile ni kalamu ya Mwalimu
Nyerere. Ngombale Mwiru si tu aliandika Azimio la Arusha bali aliandika na
Mwongozo wa TANU wa 1971 na Muongozo wa CCM wa 1981. Nyaraka hizi tunaambiwa
ndizo zilikuwa dira ya kuongoza Tanzania wakati wa utawala wa Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kila kitu kina chanzo chake.
Tuangalie ni wakati gani siasa za mrengo wa wa kushoto zilibisha hodi kwanza
katika African Association miaka ya 1930 na kisha katika chama cha TANU
kilipoasisiwa 1954. Kabla ya Vita Kuu ya Pili na baadae ukipitia gazeti la
Zuhra chini ya mhariri wake Mashado Plantan utakuta makala nyingi za kuisifia
Urusi ambayo ndiyo dola iliyokuwa hasimu mkubwa wa Waingereza na Wamarekani na
washirika wao. Katika miaka ya 1950 Gamal Abdul Nasser alipoanzisha Radio Free
Africa, Cairo ili isaidie ukombozi wa makoloni ya Afrika, radio hii ilipata
wasikilizaji wengi Tanganyika khasa kwa kuwa mtangazaji katika idhaa ile
alikuwa Ahmed Rashad Ali kijana maarufu kutoka Zanzibar na mchezaji mpira wa
sifa, kiasi ikawa watu wakisema tumsikilize Ahmed Rashad badala ya kusema
tusikilize Sauti ya Cairo. Sauti ya Cairo ilipiga propagamda kubwa dhidi ya
wakoloni ambao Rashad aliwapa jina la ‘’Majibwa Meupe,’’ yaani, ‘’Mbwa Weupe.’’
Katika siku za mwanzo za vita baridi kufuatia kumalizika kwa
Vita Kuu ya Pili kulikuwapo katika Tanganyika mwamko mpya wa kuipenda Urusi
kama taifa linalotetea wanyonge. Mashado Plantan ndiye aliyekuwa akiongoza
kampeni ya kuwafahamisha Watanganyika siasa na misimamo ya Urusi kuhusu
makoloni kupitia gazeti lake ‘’Zuhra.’’ Mashado katika tahariri na makala zake
aliitukuza Urusi bila kifani. Mashado alikuwa msikilizaji maarufu wa matangazo
ya Ahmed Rashad kutoka Cairo akiushambulia, ‘’Ubeberu na Vibaraka wake.’’
Ilikuwa kutoka kituo hiki cha redio ndipo Mashado alipata baadhi ya tahariri na
makala zake. Lakini ukweli ni kuwa
Tanganyika kabla ya Vita Kuu ya Pili (1938 – 1945) tayari ilishakuwa na
viongozi waliokuwa na siasa za mrengo wa kushoto kama Erika Fiah mhariri wa
gazeti la ‘’Kwetu.’’ Fiah hakuishia katika kuandika fikra hizi katika gazeti
lake bali alijaribu hata kuwakusanya wakulima na wafanyakazi dhidi ya serikali
ya Waingereza bila ya mafanikio.
Katika uongozi wa TAA kulikuwa na Steven Mhando ambaye
Waingereza wakimchukulia kuwa ni Mkomunisti. Steven Mhando yeye alikuwa kalitua
jicho lake akiwa kama mwalimu Government School Kitchwele, kwa wanafuzni wake
akijaribu kuwafunza kuhusu ubaya wa wakoloni. Steven Mhando akiwaita
Waingereza, ‘’wezi wa fadhila,’’ akitoa mfano wa Susi na Chuma, Waafrika wawili
waliobeba mwili wa David Livingstone kutoka Northern Rhodesia kijiji cha Ilala
alikokufa 1873 hadi kwao
Uingereza. Mhando akiwaambia wanafunzi wake kuwa juu ya wao kufanyiwa hisani
hii kubwa na Susi na Chuma wanapowataja katika vitabu vyao vya historia watu
hawa wanatajwa kama, ‘’watumishi,’’ wa Livingstone badala ya kuwapa heshima
kuwa wale walikuwa rafiki zake. Mwalimu Steven Mhando akawa anaendelea kwa
kuwauliza wanafunzi wake ni mfanyakazi gani atabeba maiti kichwani akitembea
kwa miguu kwenye mvua na jua kutoka kijiji Northern Rhodesia kuileta hadi
Bagamoyo?
Maneno haya yaliwafikia wenyewe Waingereza na
hayakuwafurahisha. Mwandishi wa taazia hii ameona picha kubwa ya James Susi na Abdullah
Chuma katika Makumbusho ya David Livingstone, Blantyre Glasgow Scotland, wakiwa
na jeneza la Livingstone kwenye meli wakati wa safari kupeleka maiti ya
Livingstone Uingereza. Ukiangalia
nyuma utaona kuwa hisia za siasa za siasa za mrengo wa kushoto zilianza
kujipenyeza kuanzia miaka ya 1930 zikianza na akina Erika Fiah kufikia miaka ya
mwanzoni 1930 na mwaka wa 1950 zilipokelewa na akina Mwalimu Steven Mhando.
Lakini hizi zilikuwa ni hisia tu katika nyoyo za baadhi ya wazalendo wa nyakati
zile. Kwa upande wao Waingereza walikuwa na hofu kubwa kwa kuenea kwa fikra
hizi za Kikomunisti na serikali ikishirikiana na wamishionari waliokuwa ndiyo
wamehodhi elimu kwa ajili ya kuwa na shule nyingi Tanganyika, walijitahidi sana
kuwakinga wanafunzi ambao kwao ndiyo kilikuwa kizazi cha kesho na fikra hizi za
Marx wakijitahidi na wao kueneza propaganda kueleza ‘’uovu,’’ wa Ukomunisti
hasa katika kupinga kuwepo kwa Mungu.
Waafrika waliokuwa na msimamo mkali kama huo hawakuvumiliwa
hata kidogo. Father Van Ostroom akiandika
katika Kiongozi Gazeti Katoliki, mwaka
wa 1950, alipatapo kutoa onyo kwa kusema, ‘’Upumbavu wa mwanadamu
unathibitisha kuwa hauna kikomo. Urusi na utawala wake wa kikomunisti bila tone
lolote la shaka ni adui wa mwanadamu asiyeweza kusuluhishwa naye.’’ Huu ndio ulikuwa msimamo wa Kanisa na
serikali kuhusu Ukomunisti. Katika hali kama hii vipi Ngombale Mwiru aliyekuwa
mfuasi wa Kanisa Katoliki angeweza kusalimika katika mfumo huu kwani yeye
alianza kuonyesha fikra za kupinga dini na kuwepo kwa Mungu mapema sana akiwa
mwanafunzi wa darasa la sita.
Tuangalie hali ilikuwa
katika TAA. Taarifa ya TAA kwa wanachama wake mwaka wa 1951, katibu ta TAA
Abdulwahid Sykes anawaonya wanachama juu ya hatari za Ukomunisti. Abdu Sykes akitahadharisha
kuhusu madhara ya Ukomunisti katika siasa za Tanganyika. Wakati huo baadhi ya
viongozi wa TAA walikuwa tayari wakifahamika kwa misimamo mikali. Miongoni mwao
alikuwa Steven Mhando na Hamza Mwapachu na baadae Zuberi Mtemvu akaingia katika
orodha ile. Wakati huo Mwapachu alikuwa akiandika katika ‘’The Sentinel,’’
jarida la Fabian Society lililokuwa likichapishwa London. Siku Juma Mwapachu alipokuwa akanieleza uhusiano wa
baba yake na Fabian Society, aliponambia kuwa Fabians wao walikuwa, ‘’Left of
the left, ‘’ katika siasa za Uingereza. Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza
kuwasikia hawa Fabians. Sasa TANU ilipokuja kuundwa na viongozi kama hawa, vipi
kijana mdogo mwenye fikra kali kama Ngombale Mwiru aliweza vipi kuenea vizuri
na uongozi huu? Halikadhalika vipi Komredi Ngombale aliweza kuelewanana Mwalimu
Nyerere, mtu aliyekuwa na mapenzi makubwa na Ukristo na kanisa lake katika
Tanganyika huru?
Ngombale Mwiru anaeleza kuwa alikuwa
Ally Sykes ndiye aliyemuingiza TANU mwaka wa 1954 walipokuwa pamoja katika
uongozi wa Tanganyika African Government Servant Association (TAGSA), Ally
Sykes akiwa katibu. Ally Sykes ndiye aliyempa Ngombale Mwiru kadi za TANU
atafute wanachama. Bila shaka Ngombale Mwiru katika uongozi wa TAGSA alikuwa
kajikuta katikati ya ‘’petty bourgeoisie,’’ akina Sykes; ’’aristocrats,’’ na ‘’landed
aristocracy; ’’Chief Thomas Marealle, ‘’the intelligentsia’’ Hamza Mwapachu,
Dr. Wilbard Mwanjsi na Dr. Michael Lugazia hawa baadhi yao wakiwa pia mstari wa
mbele katika TANU. Lakini ndani ya TANU
kulikuwa na Baraza la Wazee wa TANU chini ya Mwenyekiti wake Sheikh Suleiman
Takadiri lililokuwa na wajumbe Waislam watupu wenye ushawishi mkubwa katika siasa
za nyakati zile. Vipi Komrade Ngombale aliweza akaogolea na mchanganyiko huu? Hanishangazi
kuwa wakati kwangu mimi nimekuta mengi katika utafiti ushahidi wa uhusiano mzuri
kati ya viongozi wa TANU na Fabian Society, lakini sijapatapo kuona popote kama
Komrade Ngombale Mwiru aliwahi kuwa na uhusiano na chama hiki.
Ingawa Ngombale Mwiru alikuwa mdogo kwa
umri lakini kwa ule msimamo wake wa kuchukua msimamo toka mwanzo yeye tayari
alikuwa keshavuka ‘’Rubicon,’’ siku nyingi tena kwa mbali sana na hakubadilika
hadi kufa kwake. Ndani ya TANU Ally Sykes alikuwa na
mawasilaino na Menahem Bargil, Katibu Mkuu wa International Union of Socialist
Youth iliyokuwa Vienna akijaribu kutafuta nafasi za masomo kwa vijana
wanaharakati halikadhalika akiwasiliana na Asia Socialist Conference
Anti-Colonial Bureau ambayo ikifahamika kwa siasa za mrengo wa kushoto. Hata
hivyo ushawishi wa siasa hizi za mrengo wa kushoto hazikuwa na athari kubwa katika
siasa za Tanganyika. Hadi sasa wanahistoria hawajaweza kueleza ni kwa kiasi
gani uhusiano huu ulikuja kuweka misingi ya siasa ya Ujamaa pale Mwalimu
Nyerere alipoamua kubadilisha mwelekeo wa Tanzania kupitia Azimio la Arusha
ambalo alama za vidole za Ngombale Mwiru katika waraka ule zinaonekana kote. Ningependa
kuhitimisha taazia hii kwa mambo machache ya hisani, yaani wema ninayoyafahamu
ambayo Komarade Kingunge Ngombale Mwiru amewafanyia Waislam ingawa wengine
hawajui wa kuwa mkono wake haukuonekana.
Katika matatizo makubwa yalioukumba
utawala wa Rais Benjamin Mkapa ni kushambuliwa kwa Msikti wa Mwembechai na
vyombo vya usalama mwaka wa 1998 na yaliofuatia baada ya shambulizi lile.
Kilichofuata ni kukamatwa kwa masheikh
na kuwekwa rumande na kufungwa kwa Msikiti wa Mwembechai. Yaliyotokea
Mwembechai yalikuwa hayajapatapo kutokea toka uhuru mwaka wa 1961. Haikupatapo
hata siku moja Waislam kuingia barabarani kupambana na askari chini ya nembo ya
Uislam. Rais Mwinyi na yeye utawala wake ulikumbwa na kuvunjwa kwa mabucha ya nguruwe. Jambo hili Rais Mwinyi alipata kwa faragha kueleza kuwa lilimhuzunisha
kupita kiasi. Lakini baya zaidi kadhia hizi zote zilivyokuwa zinashughulikiwa
ilijengeka dhana kuwa taasisi ya urais yenyewe ilikuwa haina usemi wala haiwezi
kufanya lolote kuzuia vurugu zile na watendaji wa serikali wengi wao wakiwa
Wakristo walikuwa wanafanya maamuzi dhidi ya Waislam wapendavyo. Nguvu kubwa
pasi na sababu ilikuwa inatumika dhidi ya Waislam kwa ujumla na hii ilizusha
taharuki kubwa sana.
Chuki Athumani |
Kulikuwa na kisa cha mtoto mdogo wa
shule ya msingi Chuki Athumani mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Al Haramain yeye siku ya mapambano ya askari na Waislam pale
Mwembechai alikuwa anatoka shule na akapigwa risasi na askari. Chuki kama
ilivyokuwa kwa wote waliojeruhiwa katika ghasia zile walipelekwa hospitali ya
Muhimbili na wakafungwa pingu katika vitanda vyao na hawakupatiwa matibabu. Picha
ya mtoto Chuki katika kurasa za mbele za gazeti la An Nuur akiwa amelazwa na
pingu hospitali akiwa kapooza mwili mzima lilikata maini ya akina mama wengi.
Taarifa na tahariri za gazeti la An Nuur zilifikirisha wengi. Suali kubwa
likiwa, nchi yetu imefikaje hapa na nani kaifikisha hapo? Ngombale
Mwiru alipata taarifa hizi kuwa majeruhi wa Mwembechai wako hospitali lakini
hawapati huduma stahiki na wako chini ya ulinzi wa askari wa magereza na
wamefungwa pingu vitandani hali ni wagonjwa. Komredi Ngombale Mwiru alikwenda
hospitali na alimtembelea mtoto Chuki Athumani na kumkuta kweli kapooza na ana
pingu mikononi. Siku ya pili mtoto Chuki alifunguliwa pingu pamoja na wenzake
wote.
Tukio lingine ni jinsi Komredi
Ngombale Mwiru alivyozuia serikali isilifungie gazeti la An Nuur kutokana na makala
iliyoandika iliyokuwa imemshambulia kiongozi wa juu wa serikali. Mhariri wa An
Nuur alipewa taarifa afike Maelezo kupokea barua ya kufungiwa gazeti kwa miezi
mitatu. Mhariri na mpashaji wangu habari walikwenda hadi Dodoma kumfuata
Ngombale Mwiru wakati huo Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa. Ilikuwa
Jumapili lakini yeye alikuwa kazini. Ngombale Mwiru akamfanyia dhihaka mpashaji
wangu aliyefuatana na Mhariri wa An Nuur akamwambia, ‘’Leo Jumapili lakini mimi
sifungwi na dini hivyo niko kazini.’’ Mpashaji wangu kwa namna yake ni ‘’free
thinker,’’ kama Ngombale Mwiru na hawakuwa wakijuana kwa muda mrefu lakini siku
walipopata kujuana huko nyuma na kuzungumza, mapenzi yalijengeka baina yao kila
mmoja akiusudu kichwa cha mwenzke. Kuanzia siku ile wakawa wanaitana, ‘’Komredi.’’
Ngombale Mwiru alimsikiliza komredi mwenzake wa kuchovya. Mapashaji wangu
tayari alikuwa keshamsoma Ngombale Mwiru katika mazungumzo yao siku za nyuma
wakiwa Dar es Salaam na alijua amweleze nini wapate kuelewana. ‘’Komradi
Waislam walipokuwa hawana gazeti walikuwa wanamwaga makaratisi misikitini
kueleza hisia zao na kama ujuavyo makaratasi ya ‘’protest,’’ tena kutoka jamii
kubwa kama hii yetu athari yake ni kubwa. Serikali ikilifungia gazeti letu
patakuwa na ombwe na vijana watarudi msituni na kuanza kumwaga makaratasi
kuisema serikali na hili halitakuwa na maslahi si kwenu serikali wala kwetu
sisi Waislam.’’ Mpashaji wangu akanambia. Ngombale Mwiru akamjibu kwa kumwambia
kuwa yeye siku nyingi alishatoka Habari hana sauti tena kule. Hawa makomredi
wawili wakaagana na safari ya kurudi Dar es Salaam ikaanza. Jumatatu asubuhi na
mapema Mhariri wa An Nuur akafika Maelezo kumuona mkurugenzi ili apokee barua
yake ya kufungia gazeti. Mkurugenzi wa Maelezo akamwambia hakuna kitu kama
hicho aondoke kwa amani akaendelee na shughuli zake za kujenga taifa. Haikuwa tabu
kwa Mhariri wa gazeti lile kujua kuwa Komredi Ngombale Mwiru kwa busara zake
alikuwa kanyanyua mkono wake kusaidia gazeti la Waislam lisifungwe. Komrade
Ngombale alikuwa msomaji wa An Nuur na akiwekewa nakala mbili kila Ijumaa
katika duka moja la Muhindi.
Ngombale Mwiru na Kitwana Kondo |
Mwisho na hili ndilo kubwa sana ni
msaada wa Komrade Ngombale Mwiru katika serikali kuwapatia Waislam majengo ya
TANESCO Morogoro wafungue Chuo Kikuu. Marehemu Kitwana Kondo alikuwa heshi
kumshukuru Komrade Ngombale Mwiru kila alipokuwa anakizungumza chuo hiki. Waswahili
wanasema, ‘’Damu nzito kuliko maji.’’ Kadri itakavyokuwa Komrade Ngombale Mwiru
ni Mswahili wa Kilwa Kipatimu na haiwezekani kuwa asiijue vizuri historia ya
Vita Vya Maji Maji na historia za wale waliotoa roho zao katika vita ile kupambana
na ukoloni wa Wajerumani. Ngombale Mwiru alikuwa anayajua matatizo ya msuguano
uliokuwapo katika nchi yetu katika masuala ya dini. Komrade Ngombale Mwiru alikuwapo
toka siku ya kwanza TANU inampandisja katika jukwaa Mwalimu Nyerere katika
viwanja vya Mnazi Mmoja kupaza sauti kudai uhuru wa Tanganyika. Komrade Ngombale
Mwiru kayaona yote toka siku ya kwanza umoja wa wananchi chini ya TANU ulivyokuwa
na nguvu na Mungu akamjalia umri mrefu wa pia na kuona taratibu umoja ukimeguka
kidogo kidogo na mabadiko yaliyokuja baada ya uhuru kupatikana. Kwake yeye
mkinzano dhidi wa dhulma ya aina yeyote katika jamii ndiyo yalikuwa maisha
yake. Akili yake haikuwa na tabu ya kuiona dhulma inapojitokeza. Ukweli huu ndiyo
uliomsukuma Komrade Ngombale Mwiru asimame pamoja na Waislam katika wakati wao
wa shida. Misaada hii aliyotoa kuwasaidia Waislam inasema mengi kumweleza Mzee
Ngombale Mwiru.
Nahitimisha taazia hii kwa kusema kuwa
Komredi Ngombale Mwiru amekufa katuachia muujiza mkubwa usio na kifani. Komredi
Ngombale Mwiru ambae Balozi Juma Mwapachu alimwita Susilov jina la ‘’ideologue,’’
wa Soviet Union Communist Party, Mpanga
Mikakati wa TANU na CCM kutangazwa kuwa akiwa katika siku zake za mwisho
duniani katika kitanda chake cha umauti amempokea Bwana Yesu Kristo na kurejeshwa
kundini hakika huu ni muujiza katika miujiza na ni mapinduzi katika mapinduzi
yatakayozungumzwa kwa miaka mingi sana baada ya kizazi hiki chetu chote
kutoweka. Hakuna mtu aliyetegemea kuwa Komredi Ngombale Mwiru atasindikizwa
safari yake ya mwisho akiwa Mkristo na akiimbiwa pambio.
No comments:
Post a Comment