Thursday, 22 February 2018

MOHAMED H MAGORA MWANDISHI WA RIWAYA CHIPUKIZI


Kushoto Mwandishi wa Riwaya Mohamed H. Magora na Mohamed Said

Mohamed Magora ni mwanangu nimemuona akiwa mtoto akitambaa wakati nikienda kwao kwa baba yake kwa kazi za uandishi. Nikikaa katika varanda ya kwao na baba yake, Mohamed  mtoto mchanga akitambaa kwenye busati siku hizo kitoto kidogo kabisa. Sikutegemea kuwa iko siku Mohamed na mimi tutakutana uso kwa uso tena katika taaluma niipendayo ambayo na yeye pia kaipenda nayo ni uandishi. Lakini Mohamed kanishinda kwa kuwa mwenzangu, somo yangu yeye ni mtunzi wa riwaya zenye kusisimua sana tena zilizojaa mapenzi kitu kilicho aziz katika umri wa ujana kama huo wake.

''Baba nataka ukisome kitabu changu, baba kasema nikuletee.'' Mohamed huyo ananiambia baada ya kufika kwangu na baada ya mamkuzi.

Nimepigwa na butwaa kwani hata miaka miwili haijapita bwana mdogo huyu alikuwa kanipa kitabu chake cha kwanza, ''Masha Johari ya Kale,'' mara karejea tena kwangu na kitabu kingine. Ikanipitikia kuwa Mohamed si mwandishi wa kawaida na sioni kingine mbele yake ila In Shaa Allah mafanikio makubwa kwake katika uandishi.

Mohamed ni kijana hodari na fikra zake kazielekeza vizuri katika jamii anayoishi. Kalamu yake imelenga kwanza kwa vijana wenzake kueleza hali zao halisi katika ulimwengu huu wa usasa na kisha akageuza shingo upande wa pili kuwangalia wazazi wa vijana hawa jinsi wanavyohangaika katika kuwaelewa na kuwaelekeza watoto wao na pia kuelewa mazingira yanayowakabili. Kwa hakika ukimsoma Mohamed unapata picha ya mgongano wa nyakati, tabia, mwelekeo na mategemeo ya pande zote mbili ya watoto hawa wa kizazi kipya na wazee wao waliogubikwa na historia ya kale huku wakivutwa na mambo ya dunia hii ya leo. Mohamed anawasihi wazee wajaribu kuangalia mwelekeo wa dunia ya leo na changamoto zake.

Mwandishi Mohamed mwenyewe ana Kiswahili kizuri cha kuvutia unapomsikia akizungumza na halikadhalika ujuzi huu unaakisiwa katika kalamu yake. Mohamed katika kitabu hicho hapo juu anasema katika moja ya kurasa, ''...ajabu ya mbalamwezi kuanikia muhogo...'' Usemi  huu umenigusa pasipo kiasi kwani juu ya uzee wangu na umri wangu katika uandishi sijapatapo kusikia maneno haya na mimi  si mtu wa kucheza ngoma na mzigo kichwani katika dunia hii ya uandishi. Mzigo nimeutua uko chini. Naandika nikiwa sina hofu ya kuubwaga mzigo wangu.

Nashawishika kuuweka hapa utangulizi wa kitabu hiki, ''Chuo Kikuu ''Shaurimoyo,'' ili sote tufaidi kama mwenyewe mwandishi alivyoandika:

''Chuo Kikuu Shaurimoyo,’’ ni kitabu kinachosawiri uhalisia wa maisha ya wanafunzi wa Chuo Kikuu.

Ngazi ya elimu ya chuo kikuu huhesabiwa kuwa na dhima ya kufanya maandao ya maisha ya wanafunzi. Wanachuo hujifunza taaluma mahsusi walizochagua kwa hiari zao ili wazitumikie katika kuendesha maisha yao. Hujifunza maisha ya uhuru na kujitegemea, hujifunza namna ya kutangamana na wanajamii, hukuza ndoto zao za maisha na hivyo kuwa na kiu ya kujistawisha. Mambo yote hayo ni muhimu sana katika kujenga msingi wa kuta za ustawi kama yataendewa kwa nidhamu, uvumilivu, juhudi na maarifa.

Njia ya kuelekea katika kilele cha fanaka haipo tambarare wanachuo hukumbana na changamoto mbalimbali za kijamii zinazosogeza karibu hatari ya kudamirika kwa mustakabali wao. Changamoto za kimaadili hupelekea wanachuo kuathiriana na kujikuta wapo katika shimo la maangamivu kwa kuzama katika matendo yanayopambanulika kuwa ni haramu kama ulevi, kamari, na mambo mengine yanayokwamisha mafanikio.

Kitabu hiki ni cha kusomwa na wakubwa na wadogo kwani wote kwa namna moja au nyingine wameguswa sana humo ndani na naamini katika wasomaji wako ambao watakuja kusema, ‘’Ala, kumbe mambo ndivyo yalivyo?’




No comments: