Arthur Mambeta |
Marehemu
Athman Kilambo alikuwa mzungumzaji wangu sana na nilifahamiana na yeye mwaka wa
1972 nilipoanza kazi East African Cargo Handling Services (EACHS). Kilambo
alinisomesha mambo mengi sana katika mpira wa hapa nyumbani na Afrika ya
Mashariki. Katika moja ya kazi niliyopewa kufanya nilipoajiwa bandarini ilikuwa
kuitumikia Hydra Club.
Hii
ilikuwa club ya mpira kwa wachezaji wa mpira wa timu ya bandari na kwa ajili
hii nikafahamiana na wachezaji wengi sana wa mpira wa wakati ule kwa karibu
sana na kwa hakika hawa ndiyo walikuwa, ‘’the cream,’’ katika mpira wa
Tanzania. Katika wachezaji niliowafahamu ambae alikuwa hana tabasamu usoni
kwake alikuwa marehemu Mustafa Mabuge wa Cosmo. Lakini wakati mimi naanza kazi
Mustafa alikuwa amestaafu kucheza. Kinyume chake Arthur kila alipokuja ofisini
kwangu yeye alikuwa mtu wa kutabasamu na akipenda sana kuvaa vizuri. Katika wavaaji
wa sifa pale bandarini katika wachezaji mpira alikuwa Arthur Mambeta na
Abdulrahman Lukongo.
Nakumbuka
nilimshughulika Arthur Mambeta kumpatia mkopo wa pikipiki kupitia Hydra. Hii
club ya Hydra ilikuwa na fedha nyingi sana ‘’revolving fund,’’ ambayo wanachama
wake wakikopeshwa kufanyia mambo tofauti. Ingawa mimi nikipenda Sunderland
ambayo mwaka 1971 ikawa Simba nilikuwa na marafiki wengi sana Yanga. Sunday
Manara alikuwa mtoto mwenzangu nah ii ilitufanya tuwek karibu zaidi kuliko wale
‘’senior players.’’ Kilambo akifahamu kuwa nilikuwa ‘’hasimu,’’ wake lakini
hili halikuathiri uhusiano wetu hata chembe, zaidi ilizidisha sana mapenzi kati
yetu na yeye akipenda sana kunitisha vipi Yanga itakavyotuadhibu katika Nationa
League na wao kuchukua kikombe.
Kilambo
alikuwa na akili safi sana ya kujua mambo hasa ya mpira. Ninapoangalia picha za
zamani za Yanga na Simba toka enzi ya Sunderland kumbukumbu nyingi zinanijia.
Asubuhi leo na kwa kweli kutoka jana nimekuwa napokea picha za Arthur mtandaoni
na kumbukumbu nyingi zimenijia kwani katika picha hizo wengi wametangulia mbele
ya haki.
Nimemuona
Arthur Mambeta akicheza mpira viwanja vya Mnazi Mmoja katika club ndogo katika
miaka ya mwanzoni 1960 kama Kahe na Liverpool Arthur akicheza pamoja na vijana
wenzake wa wakati ule kama Hamisi Kisiwa, Hussein Shariff maarufu kwa jina la
Italo, mchezaji wa Ethiopia, Bruno, Abdallah Mzee aliyekuwa mzungumzji wangu
sana, Hamisi Dracula kijana mtanashati sana, Yusuf Salum Maleta, Shida Stua,
beki mstaarabu sana, Emmanuel Mbele kuwataja wachache. Hawa walikuwa kaka zangu
kwa umri na wakati ule bado walikuwa hawajanyanyukia kucheza Yanga wala
Sunderland. Miaka ikapita na hawa wakaja kuwa wenzangu tukikaa pamja na
kuzungumza na wakati ule sasa walikuwa wanacheza katika club hizi kubwa na timu
ya taifa.
Nathubutu
kusema kuwa katika hawa wachezaji ambao nimewataja hapa Arthur Mambeta alikuwa
ndiyo bingwa wao katika kila idara kuanzia, ‘’dribbling,’’ ‘’ball control’’ na ‘’art’’
yenyewe ya uchezaji mpira.
Kilambo
Alipata siku moja kuniambia kuwa wao Yanga walikuwa wanawataka sana wachezaji
wawili kutoka Sunderland waje Yanga kuongeza nguvu - Arthur Mambeta na Hamisi
Kibunzi. Lakini alikuwa akinambia, ''Tuliwataka sana wale waje Yanga lakini
wale watoto wakipenda sana Sunderland hata kama tungefanikiwa kuwachukua
wasingeweza kucheza Yanga kama wanavyocheza Sunderland.''
Kilambo
akimuusudu sana Arthur. Alikuwa akisema Arthur akiwa katikati Simba na Yanga
wakicheza, mpira unapendeza sana. Halikadhaika Kilambo akiniuliza, ''Hivi
nyinyi Simba kwa nini mnampanga yule Bobeya? Yeye ndiyo anaharibu mpira.
Kilambo akiusudu sana mpira kutembea katika majani na Bobeya alikuwa, ''hard
tackler,'' akitumia nguvu katika uchezaji wake.
Kila
siku asubuhi mimi na Kilambo tukinywa chai kwenye mgawa mmoja na huo mgahawa
ulikuwa mashuhuri kwa wachezaji wote wa Yanga na Simba wa zamani na waliokuwapo
kwa wakati ule. Nakumbuka sana Kilambo alikuwa kipenda kunywa chai, chapatti na
ngisi. Mimi toka udogo wangu ngisi hakuwa upepo wangu. Siku moja Kilambo
akaniuliza kama nimepata hata kumuonja ngisi. Nikamjibu kuwa bado. Basi siku
hiyo akanambia hebu muonje. Nikala kipande kutoka katika sahani yake. Kilambo
alicheka sana maana yule ngisi tulimmaliza pamoja. Kutoka siku ile ngisi
akaongezeka katika samaki ninaowapenda.
Mchezaji
wa Cosmo ninaemkumbuka ukimtoa Mustafa Mabuge, aliyekuwa bandarini alikuwa Jamil
Hizam maarufu kwa jina la ‘’Denis Law,’’ mchezaji wa Manchester United. EACHS ilikuwa ikiajiri wachezaji wengi sana wa
mpira. Wakati ule Branch Meneja wa EACHS alikuwa Mzee Thabit Awadh na Principal
Training Officer alikuwa Abdallah Lupatu wote hawa wametanguliwa mbele ya haki.
Lupatu alikuwa Yanga lakini alikuwa habagui akitoa kazi kwa wote na khasa
watoto wa mjini. Ilikuwa yeye ndiye akiwafanyia usaili pale Cargo Training
School iliyokuwa Azania Front (sasa Sokoine Drive).
Arthur
aliingia kazini miaka michache akitokea nadhani East African Airways wakati ule
mimi tayari alinikuta mwenyeji siku nyingi. Baba yake Arthur Mzee Mambeta
alikuwa akifanya kazi EACHS upande wa Medical.
Nakumbuka
siku ya maziko ya Kilambo nilikuwa na Hamisi Kibunzi tukielekea Kisutu
makaburini baada ya kutoka Msikiti wa Manyema tulikomswalia Kilambo, nikamweleza
habari hii ya yeye na Arthur kutakiwa Yanga. Kibunzi akanambia hakuwa anajua
habari hizi.
Ile mechi
ya 1973 Arthur alinieleza kwa kinywa chake kuwa yeye aliamua atacheza na
Kitwana. Kitwana alikuwa mchezaji ambae alikuwa na vurugu kubwa sana kwenye
goli la adui na alihitaji mtu wa kukaanae kumtuliza.
Iko
siku asubuhi tunakunywa chai mimi Arthur, Kitwana na jamaa wengine. Katika
maongezi wakawa jamaa wanahadithia ile mechi ilivyokuwa. Kitwana akawa anacheka
anamwambia Arthur kuwa alikuwa akimchezea rafu hampi nafasi. Arthur akajibu
akasema,'' ''Kitwana lakini si nilikuomba radhi baada ya mechi?''
Nilikutana
na Arthur kama mara mbili tatu hivi ofisini kwa Khalid Abeid na tukizungumza na
kukumbushana mambo ya zamani.
Mtu wa
kwanza kunifahamisha maradhi ya Arthur alikuwa Hamisi Kisiwa kiasi cha kama
miaka miwili iliyopita na mahali tulipokutana ilikuwa Magomeni Mapipa karibu na
ulipokuwa mgawa wa Shomvi ‘’Michuzi Mikali.’’ Michuzi Mikali ulikuwa mgahawa wa shabiki
mkubwa wa Yanga pale Magomeni Mapipa akiitwa Shomvi na likuwa bingwa wa kuku wa
kukaanga kwa ugali au wali. Ukitoa ile kuwa ukienda kula Michuzi Mikali
utakutana na wachezaji nyota wa wakati ule, kilichofanya magahawa huu uwe
maarufu ni ile pilipili aliyokuwa akitengeneza Shomvi kwa ajili ya kulia kuku.
Pale niliposimama na Kisiwa niliweza kuiona nyumba aliyokuwa akiishi Arthur
Mambeta na nakumbuka niliwahi kujanae pale kanipakia katika pikipiki yake.
Kipaji
cha Arthur hakuna asiyekijua kwa wale waliopata kumuona akicheza katika miaka
ya 1960 hadi 1970 mwishoni. Arthur akiwa tayari kapumzika, ''competitive
footbal,'' alikuwa akija kufanya mazoezi Jangwani timu ya Hydra na mimi
nikicheza kunyoosha maungo.
Siku
zile club zote Dar es Salaam zilikuwa na kiwanja cha kufanya mazoezi Jangwani. Hapa
Jangwani nilikuwa namuona Arthur kwa karibu sana na kwa kweli kile kipaji chake
kilikuwa hakina mpinzani wala mfanowe. Mpira akiwanao huwezi kumnyang'anya.
Arthur Mambeta atakumbukwa kwa miaka mingi katika soka la Tanzania.
No comments:
Post a Comment