BURIANI KIKO
NA MAMA NASR
SADIKI GOGO
Nilimfahamu marhum Bro. Idd
S.Kikong'ona tokea 1996 kupitia gazeti la An-nnur akiandika mashairi na makala
zake zilizokwenda kwa jina la "Kipondo wa Changarawe.’’ Nami pia
nikiandika baadhi ya makala kwenye An-Nuur.
Nilikuja kukutana nae mnamo mwaka
2000, tulikutanishwa na Bro Sadiki Gogo
ambaye nilifahamiana nae mapema 1998 nikiwa Kidato cha Pili pale Kisutu
Girls Secondary School, akinitambulisha kuwa ni ndugu na rafiki yake. Huku Bro
Kiko siku zote akiona fakhari kumtambulisha Bro.Gogo kama mwanafunzi wake.
Kupitia kwao nikaweza kujiimarisha
kitaaluma na kida'wah kwa kujiunga na elimu ya Kiislam kwa posta, vitabu na
machapisho mbalimbali hasa ya akina Harun Yayha, Maududi, Sayyid Qutb, Ahmed
Deedat n.k
Bro. Kiko ametuachia mengi ya
kujifunza kutoka katika umri wake mchache hapa duniani, siku zote akijitahidi
kuakisi mafunzo ya Qur'an na Sunnah katika maisha ya kila siku.
👉Bro Kiko alidhihirisha imani yake ya hali ya juu
katika maisha yake, na alipigania anachoamini kwa hoja za kumshawishi kila
mmoja. Katika mazungumzo yetu mara nyingi ukizuka mjadala namna ya kutekeleza
jambo akituambia kuwa "Dini sio ngumu kiasi hicho" kwa fikra hii aliandika
kitabu "Dini Imerahisishwa".
👉Bro Kiko aliamini katika elimu, nyakati zote ukimkuta
ana kitabu au chapisho mkononi. Alikuwa chachu kielimu kwa vijana wengi nje na
ndani ya familia yake. Nyumbani kwake hapakukauka vijana akiwasomesha na
kuwalea kimaadili na kifikra.
👉Bro Kiko alikuwa mkarimu na bashasha kwa kila mtu.
Alimsaidia aliyemjua na asiyemjua huku akitukumbusha mara nyingi kuwa
"vyote mlivyonavyo vitakwisha itabaki jaza ya mola wako tu (An-Nahl: 96) na
kuwa iko siku mtu atataka arudi duniani sio kuswali bali kutoa sadaqa tu kwa
ule ukubwa wa malipo atakayoona baada ya mauti. Alijenga urafiki na watoto
popote alipokwenda akiwapa zawadi, kuwapiga picha, vichekesho, akiwaelekeza
namna nzuri ya kusoma Qur'an na kufanya hesabu, akiwaburudisha kwa katuni
kutoka kwenye computer yake. Daima akisisitiza kuwa watoto amana Allah katupa
tuwalee vyema.
👉Bro Kiko aliipenda kazi yake, alichapa kazi usiku na
mchana akikariri usemi wake "Tutapumzika kaburini"! Hata gari yake
aliigeuza ofisi akipenda kuendeshwa huku akiweka meza ndogo akiendelea na kazi
zake akiwa safarini. Siku za mwisho za uhai wake pamoja na ugonjwa kumzidi
kiasi cha kutoweza kukaa tena alikuwa akiomba
tulete computer yake kitandani pembeni yake japo aiguse tu.
👉Bro Kiko alikuwa mvumilivu na subra ya hali ya juu mno.
Hakupenda migogoro na alikuwa tayari kwa gharama yoyote kusuluhisha penye
mgogoro nje na ndani ya familia. Siku zote akituusia subra na uvumilivu katika
kuamiliana na watu.
👉Ni ngumu kueleza yote kutoka maisha ya Bro Kiko, itoshe tu kuwa ibra kwetu
sote.
Buriani Kiko. Tulikupenda sana nawe
ulitupenda sana. Pale uliposisitiza tusikuache na tuwaangalie watoto kumbe ulikuwa
ukituaga!
Buriani IDD SULEIMAN
KIKONG'ONA.....kaka, rafiki, mwalimu, mshairi, mwanafikra, mwanadaa'wah na
msanifu mahiri.
TUNAMUOMBA ALLAH (S.W) amghufirie
mapungufu yake, alitie nuru kaburi lake na kumruzuku Jannatul Firdaus.
Amiin
Mwapwani d/o Mohammed
(Mama Nasr Sadiki Gogo)
No comments:
Post a Comment